Friday, 18 May 2018

ASILI YA UVAAJI WA KANGA (KHANGA) LESO
Na Misemo Inayotumika.

Khanga au Leso ni vazi au nguo nyepesi pia ndefu ya rangi mchanganyiko, ambayo hupendwa kuvaliwa na wanawake, hasa nchi za Afrika Mashariki na kati (Maziwa Makuu) pamoja na nchi zinge za Afrka.

Nchi nyingine zenye kuvaa, vazi ili la Khanga ni Zambia na Malawi, Komoro, Madagascar (Malagasi uko zikijulikana kwa jina la Lamba), Ghana na Nigeria.

Khanga ni kitambaa cha umbo la mstatili kilichotengenezwa kwa pamba chenye urefu wa mita moja unusu na upana wa mita moja na sentimita kumi na ambacho hutarajiwa kumfunika mvaaji kutokea kifuani hadi karibu na jicho la mguu.

Kanga, ni kitambaa chenye rangi kama kitenge, lakini nyepesi, huvaliwa na wanawake na mara kwa mara na wanaume wa Afrika Mashariki na katika kanda za Maziwa Makuu ya Afrika.

Kipande cha Khanga au Leso kimegawanywa sehemu tatu, sehemu ya PINDO ambayo uitwa MPAKA kwa pande zote nne, na sehemu kuu, ijulikanayo kwa jina la MJI hapa ndipo penye mapambo na ubunifu. Na sehemu ya tatu ni JINA au sehemu ya UJUMBE.


Kwa kawaida, Khanga huuzwa kwa gora (Jora) au doti, vipande viwili na huvutia zaidi zikitumiwa pamoja. Jora ya Khanga inaponunuliwa huwa imeunganishwa upande wa mapana.

Mnunuzi halafu huikata vipande viwili upande wa mapana na kuzipindisha ili zisitoke au kuchanikachanika nyuzi. Na kutumiwa kwa jinsi mtu anavyotaka, aidha kuvaliwa kama ilivyo au kushonwa vazi lingine.

ASILI YA KANGA - KHANGA -LESO
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali asili ya khanga, mwanzo kabisa zilitengenezwa kutoka kwa aina ya kitambaa cha pamba kilichosafirishwa/kilichoingizwa kutoka Marekani.

Nguo (Kitambaa) kilikuwa kinajulikana kwa jina la MERIKANI haswa kwa upande wa Zanzibar, jina ili la Kiswahili limetokana na kivumishi cha Amerika (kinacho onyesha mahali au asili yake).

Vazi hili mwanzo lilikuwa linavaliwa na Watumwa wa kiume na wa Kike.

Wanaume walijifunika au kuvaa kiunoni na watumwa wa Kike walijifunika kuanzia usawa kifuani (Kwapa).

Kwa watumwa wa kike, wao walitofautiana rangi na kitambaa walichovaa watumwa wa kiume.

Ili kukifanya kitambaa kionekane ni cha kike zaidi, wanawake (mtumwa) mara kwa mara walivaa rangi nyeusi au rangi ya buluu. 

Kitambaa hiki cha Merikani kilichobadirishwa rangi na kuwa cheusi kikajulikana kwa jina la KANIKI.

KUPATIKANA KWA JINA LA KHANGA - LESO (KANGA).
Si watu wengi walipendelea kuvaa vazi hili la Kaniki na wengi walilidharau kwa kuwa tu lilikuwa ni vazi duni na lililo valiwa haswa na Watumwa na kuonekana kuwa ni vazi la kitumwa.

Lakini baadae Wanawake wengi ambao waliachwa huru kutoka utumwani, na hata wale wanawake wakiungwana ambao hawakuwahi kuwa watumwa nao pia walitaka kulivaa na kuwa sehemu ya jamii ya Waswahili, hapo ndipo walianza kuongeza ubunifu na kulipamba vazi ili Merikani, ili lionekane ni la kiungwana zaidi. 

Walichokifanya ni kuondoa ule weusi kwa kupamba wakitumia aina ya kemikali (bleach) ili kuondoa ule weusi, uku wakizizuia baadhi ya sehemu zisipate kemikali na wakati mwingine walitumia mbinu ya uchoraji kwa mkono.

Na matokeo yake kitambaa hiki cheusi aina ya Merikani baada ya kuongezwa urembo huo, kikaonekana kama kina rangi mbili madoa madoa meupe ndani ya weusi na wakati mwingine madoa meupe ndani ya rangi ya Buluu yanayo onekana kama madoa madoa mfano wa ndege aina ya KANGA na kuanzia hapo ndipo kikapata jina ilo la utani kwa kufanana kwake na ndege aina ya Kanga.

Baada ya utumwa kupigwa marufuku na kufutwa mwaka wa 1897, vazi hili la khanga lilianza kupata umaharufu na kutumika na wengi na mwonekano wake ukaanza kubadilika na kuonekana kwamba aliyevaa alikuwa na uwezo wa kifedha.

Kwa wakaazi wa mji wa Mombasa na Zanzibar, wao walifananisha vazi la khanga na vitambaa vya mkono Leso (Lencos ), ambavyo vina asili ya Ureno (Portugal).

Vitambaa hivi vya mkono (leso) vililetwa na wafanyabiashara wa Kireno kutoka nchi za India na Arabuni. Wanawake wa huko Zanzibar na Mombasa, walianza kuviunganisha pamoja vitambaa hivi vyenye umbo la mraba na kuvifanya vionekane kama kitambaa kimoja kikubwa kilicho unganishwa kutokana na vitambaa kadhaa na kupata umbo la mstatili.

Ubunifu huu, ukapata umaarufu katika kanda nzima ya pwani ya Afrika Mashariki, kiasi ukaenea mpaka bara hadi eneo la Maziwa Makuu.

Vazi ili likafanana na lile la Merikani (Kaniki) na hata pia kufanana na khanga, kimatumizi na hata kuitwa kwa jina ilo la Khanga kwa watu wa Bara na hata Zanzibar, ila kwa wakaazi wa Mombasa, wao wanaendelea kutumia neno leso, hata kwa kile kitambaa cha Merikani ambacho kilikuja kubadirika jina na kuitwa Khanga.

Mpaka kufikia katikati ya karne ya ishirini ndipo kukaanza kuletwa vitambaa vilivyochapwa kwa mashine na haswa kutoka nchi za India, Mashariki ya Mbali na Ulaya.

ULIMWENGU WA KHANGA - LESO
Ulimwengu wa kanga au leso ni ulimwengu wa uzuri, rangi za kupendeza, nakshi changamano, mavazi ya kusitiri na papo hapo kupitisha ujumbe fulani kupitia methali, misemo na misimu.

Khanga ina matumizi anuwai ya jamii, ni ya mapambo katika sherehe mbalimbali za kijamii. Khanga ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Mswahili na Mwafrika kwa vile matumizi yake yamepanuka nje ya mwambao wa pwani zilikoanzia.

Siku hizi kuna khanga ambazo ni kubwa zaidi na hujulikana kama khanga za kuswalia miongoni mwa Waswahili kwa sababu hutumika na wanawake kujifunga wakati wa kuswali.

Kanga ni zaidi ya kipande cha nguo, kwa sababu ina matumizi mengi, inaweza kutumika kama sketi au kushonwa gauni, vilevile yawezwa kuvaliwa kama Kilemba na hata kwenye kubebea mtoto mgongoni na wakati mwingine utumika kama Ngata kichwani na kubebea ndoo au mzigo kichwani.

Kama ilivyo zoeleka kuwa Kanga ni vazi la kiutamaduni wa watu wa pwani ya Mashariki ya Afrika, mara nyingi hutolewa kama zawadi kwa siku za kuzaliwa mtoto au matukio mengine maalum. Kama vile Harusi au Misiba na uvaliwa kwenye kuomboleza misiba na hata kutolewa kwa familia iliyofiwa.

Na kubwa zaidi, kwenye ununuzi wa Khanga, mara nyingi mnunuzi wa kanga zaidi ya kuangalia uzuri wa mji wake, lakini pia uzingatia ujumbe ulioko kwenye kanga husika.

Kuna pia kanga zinazo sherehekea matukio ya kisiasa na kijamii ijapokuwa hizi zaidi hutengenezwa nchini Tanzania na Kenya. Masuala ya kitaifa na sera zake pia hutetewa na kupigiwa debe kupitia Khanga kama kampeni za upangaji uzazi na utambuzi wa magonjwa kama ukimwi nakadharika. 

Vilevile kumeshuhudiwa khanga maalum kwa ajili ya kampeni za chaguzi kuu zikisifu vyama vya kisiasa kwa mfano wagombeaji wa urais, ubunge na udiwani.

MANENO KWENYE KHANGA
Baadae kwenye Miaka ya mwanzoni ya 1900 Khanga zikaanza kuandikwa maneno na misemo mifupi yenye busara na hata hata methali na wakati mwingine kuandikwa kauli mbiu zenye kuhamasisha.

Mwanzoni Khanga au Leso hazikuwa na maneno, yaani, misemo na methali au misimu. Inaaminika kuwa Abdalla Kaderdina Haji Essak, aliyejulikana kwa jina maarufu la "Abdulla", ndiye alianzisha mtindo huu wa maneno kwenye Khanga mwanzoni mwa miaka ya 1920, alianza kutofautisha khanga zake alizokuwa akiziuza kwa kuandika "K.H.E. - Mali ya Abdulla". 1920 (Parkin, David 2004:1).

Na mara kwa mara aliongeza Methali za Kiswahili. Maneno yenyewe ijapokuwa yalikuwa ya lugha ya Kiswahili, yaliandikwa kwa hati za Kiarabu. Mwishoni mwa miaka ya hamsini ndipo hati za Kilatini zilitumika wakati matumizi ya Khanga yalipopanuka kutoka kwa watu wa pwanina kuenea kote Afrika Mashariki.

Ilipofika kwenye Miaka ya 1950 Kanga zilianza kutengenezwa nchini Tanzania (Tanganyika) na Kenya na nchi nyingine katika bara la Afrika.


BAADHI YA MANENO YA KWENYE KHANGA
• Ajabu ya kondoo kucheka kioo.
• Akutukanaye hakuchagulii tusi.
• Amekuja kwa meno ya juu.
• Chokochoko Mchokoe Pweza Binadamu Hutomuweza.
• Ganda la mua la jana chungu kaona kivuno.
• Hekaheka nyuma vita mbele.
• Jina jema hungara gizani.
• Kikulacho ki nguoni mwako.
• Kula vya Ndani, vya Nje Husitamani.
• Mahaba yetu asali hayahitaji sukari.
• Mapenzi ya kweli kuishi wawili Kwako mtu hanitoi.
• Mkeka mkalie hata mkinitukana wifi yenu ndie mie.
• Moyoni upeke yako.
• Nakupenda wewe sina mwengine.
• Naogopa Simba na meno yake, siogopi mtu kwa maneno yake.
• Ndfu ndio Tamu, Fupi Zinaekenya.
• Nilikuota wewe.
• Nimepata la Azizi dawa ya roho yangu.
• Nishike Unikande Nikiregea Unipande.
• Panua Paja Mkwaju Waja.
• Pendo letu limoyoni.
• Pendo likipata mjuzi humea mizizi.
• Penzi halichagui rangi.
• Si mzizi si hirizi bali moyo umeridhi.
• Takuenzi uwe wangu maishani.
• Wastara nimestirika mlilolitaka halikunifika

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!