Sunday 17 May 2015


Nilikuwa nimekaa nikiangalia Luninga, kipindi kiliwa cha maduka ya fashion za nguo aina mbali mbali. Nikaona jinsi watu wanavyo angaika kuchagua aina mbalimbali za mavazi, wapo waliochagua mavazi ya kubana, wapo waliochagua magauni marefu yaliopasuliwa chini, wapo waliochagua vimini, na kadhaa wa kadha. Katika hali ya kutafakali ikanipitia fikra mbalimbali ya hali yetu Waislam wa sasa.

Nikawa najiuliza, hivi Waislam sisi, tuna tofauti gani na wale watu wanao ingia kwenye maduka ya nguo na kujichagulia nguo wanazotaka au kuzitamani!? 

Waislam sisi wa zama hizi mbona tumeacha mafundisho mazuri ya dini yetu, na Kuugeuza uislam kama Duka la nguo za fasheni! Mtu anachagua nguo anayotaka nyingine anaacha. Tumesahau au tunafanya makusudi kukarifu maneno ya MwenyeziMungu yasemayo...!

Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.
Qur'an Surat Baqara [2]:208

Na kwenye surat nyingine amesema: 
Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.
Qur'an Surat Al I'mran [3]:103

Vilevile Mtume (saw) alisema,
Msitofautiane, kwani waliokuja kabla yenu walitofuatiana wao kwa wao, na kisha waliangamizwa.” (Al-Bukhaariy)

Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migogoro mikubwa” Na ni kweli... Maana hapa ndipo tulipo, tunaishi katika zama za mikinzano na kutokubaliana, kutokubaliana katika iymaan, Fiqh, Aqida Faradhi na Sunnah na hata siasa, hali ni mbaya, inatisha na inasikitisha. Lilikuwa kundi moja na jamii moja, sasa tuna makundi chungu nzima, na kila moja linalingania misingi yake yenyewe.

Zama hizi za teknolojia, kunapatikana maulamaa wengi sana, Wapo waliosoma Saudia, Sudan, Pakistan na maeneo mengine mbalimbali, na bila kuwasahau wakina sie wa gugo dot kom. Kiasi imekuwa sasa Waislamu hatujui lipi la kulikubali na lipi na kulikataa! Na linalovunja moyo zaidi ni kuwa tofauti na migongano inapelekea kuangamiza Umoja wetu wa Kiislam.

Maswahaba waliomuona Mtume (saw) wanatufahamisha kuwa “...Mtume (saw) alitutolea mawaidha makali ambayo yalitikisa mioyo yetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allah! Kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga, basi tuusie.” Ndipo akasema: “Ninakuusieni usikivu na utiifu hata kama mtatawaliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu..."

Waislam sisi hayo yote hatuyataki, na kama tunayataka basi tunafanya kama vile wafanyavyo wanunuzi wa nguo uko madukani, twachukua kile tu tukitakacho na vingine twaviacha.

Tumeipa Dunia kipaumbele, Waislam leo tumekuwa na dharau, kibri, jeuri, tunapenda farka, kujikweza, kukashifiana, kutukanana na kuitana majina ya ajabu. Tena basi ukimwambia mtu usimtusi Muislam mwenzio, ndio inakuwa kama umemchochea, ataleta ayat na hadith kuhalalisha matusi yake.

Waislam dunia tumeipa kipaumbele sana, Elimu au rizki kidogo Allah akitupa basi. Hatuna muda tena na Uislam, hatuna muda wa kuwatazama wagonjwa mahospitalini, wafungwa magerezani, uko mitaani kuna mayatima, wajane na mafukara, hawana msaada wowote na sisi. Tumefumba macho kabisa kipaumbele ni farka, na hoja za utengano na umadhehebu ndizo tunazienda na kuzishabikia.

Na ndo umefika ule muda wa Allah kuondoa hofu kwa makafiri juu ya waislam na kuwafanya waislam waogope kufa na wapende dunia. Mtu ukisali swala tano na kufunga na kujifaharisha na umadhehebu, basi tayari unaona umekabidhiwa funguo za peponi. Basi hapo utamtia peponi/motoni umtakaye na kumtoa umtakaye.

Najuwa kuwa mabandiko na makala zenye kusisitiza umoja katika Uislamu, hazipendwi lakini kati ya mimi na wewe hatuna budi kuhimizana katika kheri na kupeana nasaha, hata kama watakaosikiliza na kufuata hawazidi hesabu ya vidole vya mkononi, tusichoke kufikisha mpaka tunaingia Makaburini mwetu.

“Najilinda na maneno ya Mwenyezi Mungu  yaliotimia kutokana na hasira zake na adhabu yake na shari ya waja wake na vioja vya mashetani na kunijia kwao Ewe Mwenyezi Mungu hakika sisi tunakufanya Wewe uwe katika vifua vyao na tunajikinga kwako na shari zao, Hakika Mwenyezi Mungu anatutosheleza, naye ni mbora wa kutegemewa”
Aamiyn

Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao. Na Mwenyezi Mungu anapo watakia watu adhabu hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.
Quran Surat Ar-Raa'd 13:11

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!