Tuesday, 16 June 2015


Mke wa pili! Ni maneno yaliyorindima na kutoa mwangwi katika kichwa changu. Nilimuuliza: “Kwa nini? Je mie sio mrembo? Abadan! Kamwe sitakubali suala la mke wa pili. Kama unataka mke wa pili waweza kwenda kumchukua lakini utambue kuwa ukirudi hutanikuta hapa!” 

Hayo yalikuwa maneno yangu niliyomwambia mume wangu miaka kadhaa iliyopita aliponitamkia kuwa anakusudia kuoa mke wa pili. Alinieleza kuwa ni mwanamke ambaye alikuwa ameachika muda si mrefu na alikuwa na watoto 4. Yuko katika wakati mgumu na hajui mahali anapoweza kupata chakula au hana uhakika wa kuwahudumia wanaye. 

"Baba yao yu wapi?" Nilimuliza. "Huyo baba hawezi kuwatunza wanaye? Kwa nini wewe mtu wa mbali ubebe mzigo wa mwanaume mwingine? Kuna njia nyingine za kumsaidia kiuchumi bila kulazimika kumuoa! 

Nilikuwa sipati picha kuwa katika ndoa ya wake wengi. Kuchangia mume na mwanamke mwingine; kuchangia penzi lake, tabasamu lake, utani wake na mwanamke mwingine. Nilikuwa sipati picha nikiwaza kuwa mume wangu atakuwa akimkumbatia na kumnong'oneza maneno matamu ya mahaba. 

Ni jambo ambalo kwangu halikubaliki. Nilikasirika na kusema: "nimemfanyia mangapi? Hana hata shukrani? Nimekuwa mkewe, daktari wake na mlezi wa nyumba yake. 

Nimemzalia watoto 3 wazuri. Ni kama tusi dhidi yangu kwenda kuoa mwanamke mwingine. Kwani mimi si mrembo? Kwani mimi sina nguvu?" 

HAPANA! Sikuweza kulikubali hilo kabisa na niliweka wazi msimamo wangu. Huyo mwanamke akiingia, basi mie nitaondoka! Sikutaka kuzunguka mbuyu katika msimamo wangu. Akitaka kuihatarisha ndoa yetu, maisha yetu, na watoto wetu kwa sababu ya mwanamke mwingine, basi aendelee na mpango wake huo. 

Sitamzuia! 

Sasa inaonekana miaka mingi imepita. Nilidhani kuwa maisha yatadumu milele na kwamba hakuna kitakachobadilika. Lakini yalibadilika... 

Mume wangu hakuoa mke wa pili. Baada ya maonyo na vitisho vyangu aliachana na wazo hilo. Sijui kilichompata mwanamke yule na watoto wake. Nahisi walihamia mji mwingine. 

Mume wangu hakuthubutu tena kuzungumzia mke wa pili, na hilo lilinifurahisha. Niliweza kumzuia mume wangu lakini sikujua kuwa muda ulikuwa ukikimbia.

Kauli yake ya mwisho aliniambia kuwa anahisi maumivu ya kichwa na anaenda kujipumzisha mpaka wakati wa swala ya 'Isha. Usiku huo hakuweza kuswali 'Isha kwa sababu hakuamka tena. 

Nilichanganyikiwa mno kwa kifo hicho cha ghafla. Ndani ya sekunde nimenyang'anywa mume niliyeishi naye. Niliomboleza kwa muda mrefu kifo cha mume wangu kipenzi. Punde nilianza kuondokewa na kitu kimoja baada ya kingine. Kwanza gari, duka na kisha nyumba. 

Tulihamia kwa kaka yangu aliyekuwa na familia. Mimi pamoja na wanangu 3 tulisongamana katika nyumba yake. Punde wifi yangu akaanza kukereka kwa uwepo wetu. Nilihitaji kutoka, kufanya kazi na kutafuta sehemu yetu wenyewe badala ya kuishi kwa kula masazo ya watu wengine. Lakini sikuwa na stadi na utaalamu. 

Mume wangu alipokuwa hai tuliishi kwa raha mustarehe. Sikuhitaji kwenda nje na kujipatia utaalamu. Maisha yakaniwea magumu mimi na wanangu. Sikuwa kijana tena, umri ulikuwa umenibadilisha. Kila mara nilimkumbuka na kila moyo unapodunda. Mambo yanawezaje kubadilika namna hii? 

Siku moja kakangu aliniambia kuna mtu anayejuana naye anatafuta mke. Ni mtu mzuri, mwenye akhlaq nzuri na mwenendo mzuri sana. Ananifaa, lakini anataka niwe mke wa pili. 

Ni mara ya pili katika maisha yangu ninatajiwa neno hilo la MKE WA PILI lakini katika mazingira tofauti. 

Alikuja nyumbani kwa kakangu. Tulionana moja kwa moja. Nilimpenda na nilipenda kila kitu kuhusu yeye. Aliniambia kuwa mkewe wa kwanza anajua kuwa anataka kuoa mke mwingine lakini anaonekana wazi kuwa haungi mkono wazo hilo na kwamba hajui atajibu nini atakapomweleza kuwa amepata mtu. 

Akasema kuwa jibu lake litategemea iwapo mkewe atashawishika na hoja ya ndoa ya matala. 

Usiku huo nilianza kuswali Istikhara. Pia nilikuwa nikiomba kwa shauku jambo hilo lifanikiwe. 

Nilikumbuka miaka mingi iliyopita pindi maisha ya mwanamke mwengine yalipotegemea uamuzi wangu na jinsi uamuzi huo ulivyokuwa. Niliumia sana. Nilihisi kuwa kwa sababu sikumpa mwanamke mwenzangu nafasi katika maisha yangu basi ni zamu yangu kuadhibiwa na Allah. 

Nilijuta na kutubu. Wakati wa uhai wa mume wangu dhamiri haikunisukuma kutubu kwa nilichokuwa nimemfanyia mwanamke mwenzangu, kwa sababu akili yangu ilikuwa ikiniambia kuwa sina kosa kwa dhana kuwa nilikuwa nikilinda mali yangu. Sasa nikiwa katika hali hii nilitambua ukubwa wa kosa nililolifanya kwa kumkatalia mwanamke mwenzangu fursa ya kuwa na mume. Niliomba sana mwanamke huyu akubali. 

Siku kadhaa baadaye alinipigia simu kunitaarifu kuwa mkewe alikuwa na wakati mgumu kulikubali lakini anataka kuonana nami. 

Nilikuwa na jakamoyo juu ya siku hiyo ya kukutana naye. Siku moja kabla nilisali sana na kumuomba Allah anisaidie. Nilipokutana naye alikuwa kama mimi. 

Alikuwa mwanamke anayempenda mumewe na anayekhofu kumpoteza. 

Aliushika mkono wangu na kuniambia huku machozi yakijaa machoni mwake: "Hili ni jambo zito sana kwangu, lakini ninatumai tunaweza kuwa ndugu". 

Maneno yake yaliupasua moyo wangu. 

Kitu pekee nilichohitaji katika nyakati hizo ngumu ni mkono wenye huruma utakaonipokea na kunikumbatia, mkono utakaonipa tumaini na nguvu ya kusonga mbele. Kwangu mimi, mkewe alikuwa mwanamke wa kipekee na daima nitaendelea kuwa mwenye shukrani kwa hilo. Nilidhani kuwa hakuna mwanamke anayempenda mumewe kama nilivyompenda mume wangu, lakini alinifundisha maana ya upendo wa dhati (unconditional love). 

Huwezi kuijua hali ya mtu mpaka ikufike. Toa uamuzi sahihi kwa mujibu wa Qur'an utaona namna Allah subhanahu wa ta'ala atakavyokumiminka baraka mara dufu.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!