Wednesday, 2 September 2015


Kuoana si huchukuana tu mke na mume, Bali mnachukua ulimwengu wenu mzima. Kuanzia hapo mpaka maisha yenu yote mke/mume wako atakuwa mwenzio, mwandani wako, na rafiki yako mpenzi.

Atashiriki katika nyakati zako nzuri, siku zako, na miaka yako. Atakuwa pamoja nawe katika furaha na shida, katika mafanikio na tabu, katika ndoto zako na katika wakati wa hofu. Ukiumwa, atakupa huduma bora kabisa. Wakati unapohitaji msaada atafanya vyovyote awezavyo kwa ajili yako. Wakati una siri, ataitunza siri yako, wakati unahitaji ushauri, atakupa ushauri mzuri kabisa.

Atakuwa na wewe utakapoamka asubuhi kitu cha kwanza ambacho macho yako yataona ni macho yake. Wakati wa mchana, atakuwa na wewe, kama kuna wakati mchache hatokuwa na wewe kwa kimwili, atakuwa anakufikiria wewe, anakuombea dua kwa moyo wake wote, akili yake yote, na roho  yake nyote.

Ukienda kulala usiku, kitu cha mwisho macho yako kuona itakuwa ni yeye, na ukilala bado utakuwa unamuona katika ndoto zako. Kwa kifupi atakuwa ni ulimwengu wako mzima na wewe utakuwa ulimwengu wake mzima.

Inasikitisha sana katika jamii zetu kila nikizungumza na wana ndoa utasikia matatizo tuliyonayo yanafanana. Ni matatizo tanayowapata kutoka kwa waume zao au wake zao.

Ni hali ya kutisha sana na inafaa tuzingatie sana na wala tusiidharau, kwani utakuta hata watu waliosoma dini au kuelimika kwenye elimu mbali mbali pia wanaongozwa na jazba kwenye kutoa maamuzi. Sio vibaya kutofautiana kimawazo lakini iwe kwa njia ya kusomeshana au kukatazana pale pindi mtu anapotaka kukosea lakini utakuta sio hivyo kabisa.

Baadhi ya majumba yetu wanawake wengi wako hatarini kwa kukosa uongozi mzuri wa waume zao. Furaha inatoweka ndani ya nyumba kwa wanaume kukosa imani kwa wake zao na kujiona wao ni mabwana hawapaswi hata kutoa msaada mdogo unapohitajika. Je, nyumba kama hiyo itakuwa na mapenzi kweli au watu wataishi tu kuendeleza maisha kwa kuwa wamezaa, au kwa kuwaogopa viongozi wao wa dini na wazee wao?

Nilikutana na mama mmoja na katika mazungumzo naye, alikuwa akilia kwa uchungu na kusema:
Sisi tumeolewa kwa ajili ya kuwa na furaha au kuwa ni wafanyakazi wao wa ndani hawa wanaume?

Anasema yeye kazi yake ni kufua, kupiga pasi kulea watoto na kupika. Mume akiingia ni kula kulala na kutoka kwenda kwa marafiki tu, hana mapenzi hata ya kumwambia mkewe:

Mke wangu leo chakula kizuri au mke wangu umependeza” 

Ni neno dogo sana lakini lina athari kubwa sana ndani ya moyo wa mke wako.

Kwa upeo wangu naona yote haya yanasababishwa na ukosefu wa elimu na ubinadamu na kuto kuwa na huruma kwa mwenzi wako. Wanaume hawapewi mafunzo ya kutosha wanapotaka kufunga ndoa jambo ambalo ni muhimu sana wafunzwe vipi kuishi na wake zao.

Kwa mwanaume inaonekana kama vile ni kutawaliwa pale mwanaume anapokutwa anaosha vyombo, kupika, kufua na kuogesha watoto nyumbani.

Jambo hili limeghafilikiwa kwa viongozi wa dini na hata wazee ambao aghlabu wao wanatoa mawaidha na mahubiri mengi kuwaonya wanawake zaidi kuliko wanaume kiasi ambacho kinawafanya wanaume wasitambue makosa yao na waache kufanya ihsaan na wawe na Rehma kwa wake zao. Siku zote nyumba ikivunjika anashutumiwa mke tu ilhali pengine ukorofi unaaza kwa mwaname mpaka kufikia hali ya kuachana.

Tuna jukumu ya kulifikiria jambo hili hasa wale ambao wanaishi nchi za nje (Ulaya na Marekani) kwani wanawake wanazidi kuwa wajeuri na kukosa nidhamu kwa vitimbi vya waume zao majumbani mwao.

Daima jaribu uwezavyo kuwa mtu mzuri kwa mkeo/mumeo kwa njia ya maneno na vitendo. Ongea nae, mchekee, tafuta ushauri wake, muulize juu ya mawazo yake, tumia wakati maalum na yeye na daima kumbuka kwamba mume/mke bora ni yule anaye jali familia yake.

Ni kawaida kwa wanandoa kuahidi kuwapenda na kuwaheshimu mwana ndoa mwenziwe mpaka mauti yawatenganishe. Naamini kwamba ahadi hii ni nzuri au ni bora kabisa, lakini haitoshi! Haitoshi kumpenda mkeo/mume tu. Lazima upende anachokipenda pia. Familia yake, anaowapenda yeye uwapende pia. Usiwe kama mwenzangu mmoja ambaye hakufurahiwa kuja kwa wazazi wa mke wake kukaa kwa wiki chache.

Alimwambia wazi mkewe “Mimi siwapendi wazazi wako”. Bila ya kusita mkewe alimtazama machoni kwa hasira na kusema, “Na wako pia siwapendi”.

Mapenzi yasiishe hapa duniani tu, tunaamini kuna maisha baada ya mauti ambapo wale ambao walifanya wema katika dunia hii wataungana na wanandoa wenzio uko mbinguni (Peponi).

Basi ni jukumu letu sote kuziangalia tena na tena ndoa zetu na kuondoa tofauti ndogo ndogo zinazo jitokeza kila leo.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!