Wednesday, 30 September 2015


Waswahili tunasema akukatazae kukomba mboga, anataka ushibe... Apasuaye nguo basi lazima awe fundi wa Kushona.

Ukiona mtu anatapika matapishi tena anatapika mpaka nyongo, kisha badala ya kufuta na kupiga deki, anayageukia matapishi yake na kuyaramba tena uku akiyafurahia na kisha kukukaribisha ukae ule nae, basi ujuwe mtu huyo ana matatizo ya akili.

Binadamu sisi ni sawa na kurasa za kitabu, ukitaka kumjuwa usiangalie jarada lililo nje, unatakiwa ukifungue kitabu na kukisoma. Juzi kati tumesikia mengi kuhusiana na viongozi wetu ambao walituhamanisha kuwa kuna nyoka tena ni mwenye sumu kali, wananchi tukaamini na kukamata magongo ili tuwe tayari kuuwa nyoka aliye hatari kutoka kwenye shimo lake.

Lakini kwa ghafla bin Vuu, walio tutangazia kuwa nyoka yu karibu kutoka ni nyoka tu wa maigizo na si yule aliyekuwa kabla ya kutoka pangoni, nyoka huyu hana sumu na hata ukimpa mtoto wako mchanga awezi kumdhuru, japokuwa nyoka huyo ni swira (Cobra), lakini tunaaminishwa kuwa ni nyoka mpenda watu.

Binafsi sina hofu na wabongo, kwa sababu nimeona wabongo ni kabila moja la ajabu na la kipekee. Kwa kawaida watoto wote duniani wana nyongo. Ukiwafinya wanalia, ukiwatekenya wanacheka.

Lakini wabongo wao huwa hawana nyongo, hawajui kulia. Ukiwatekenya wanacheka, ukiwafinya wanacheka, ndio maana watu wanaweza kufanya lolote waliwezalo ili wapate wanayoyataka, hata kwa rafu, na wao wakahamaki lakini wakacheka tu.

Wagombea fanyeni lolote muwezalo mpaka vyama vyenu vishinde. Wabongo hawana nyongo. Ukiwatekenya wanacheka, ukiwafinya wanacheka.

Wabongo ni viumbe wa ajabu kama nilivyosema hapo juu... Mfano ukiona mtoto anamwambia mtoto mwenzie kwa jambo la kitoto, watu wazima tutasema kuwa watoto wanacheza, na hata mtoto akimwambia baba yake kuwa gari ile ni langu au ndege ile ni yangu, baba awezi sema kuwa wewe mtoto wacha uongo, atakacho sema baba ni kumtia moyo mtoto, kuwa ndege ile ikitua nitakuletea, huyu ni mtoto anakua. Lakini tunaposikia maneno ya kitoto anaambiwa mtu mzima, basi ujuwe hapo kuna walakini.

Ili tulilonalo sasa miezi hii michache ni dogo sana kuliko ilo linalokuja kwa sababu linalokuja tutakaa nalo si chini ya miaka kumi.

Lengo langu hapa ni kuwanasua wale wanaojiona kuwa wapo katika harakati za kidemokrasia zenye lengo la kuwapatia Watanzania wote fursa sawa wasije kuingia katika mtego huu. Pia ni kuwajulisha wanaharakati hao kuwa mabadiliko hayawezi kuja kwa kumwondoa mtu mmoja tu, bali kwa kuuong'oa mfumo wote na pahala pake kuchukuliwa na mfumo mwingine.

Neno ili “NINGEJUWA” Siku zote huja mwisho wa safari... Na majuto ni mjukuu!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!