MUHARRAM MWAKA MPYA WA KIISLAM BILA MAAZIMIO
Baada ya kumaliza kuswali swalah ya Maghrib, nikakaa na familia yangu, tukiongea na kucheka na uku tukitafakari siku ilivyopita. Mara nikakatizwa na mlio wa simu ya mkononi. Triiii! Triiii! Triiii...! Kuangali kumbe zilikuwa ni meseji zikiingia mfurulizo. Nikawa najiuliza kuna nini tena mbona meseji nyingi kiasi hiki!?
Nikaamua kuzisoma moja baada ya moja, na meseji zote zikinitakia salamu za mwaka mpya wa Kiislam wenye amani na maisha mema. Kuna meseji zingine zikinialika kwenda kwenye sherehe walizo ziandaa na wapo wale waliotaka tu kunisalimia.
Nikashangaa kidogo, sababu uko nyuma sikuwahi kuletewa meseji nyingi kama hizi, nikashukuru na nikajibu meseji moja baada ya moja.
Lakini hata hivyo akili yangu ikajishughulisha kiasi, nikajiuliza haya mambo ya kutumiana meseji nakutakiana kheri ni mambo mazuri, japokua uko nyuma hatukuwa tukitumiana meseji wala uko mitaani hatukuwa tukitakiana mwaka mpya mwema, haya mambo yanashamiri sana siku hizi.
Kwa uzoefu wangu, watu wenye tabia ya kusheherekea siku ya kuingia mwaka mpya, ni wale wenye kufuata kalenda ya kalenda Gregorian (Gregorian Calendar) wengi upatwa na furaha na kuingiwa na kiwewe cha kuiona siku na mwaka mpya, kwa kujiona kuwa wamefaulu kuuona mwaka mwingine.
Lakini tunasahau kuwa miaka inakwenda, na umri ndio unapungua.
Binadamu anapopitisha miaka yake haina maana kuwa hasiwe na furaha bali ahesabu kuwa siku zake zinazidi kupungua na kukaribia kuingia kaburini, anapaswa asikitike na sio kufurahi na khaswa kwa yule ambaye hakujishughulisha kufanya mambo mazuri kwa jamii yake!
Katika maisha ya Muislam, kila mwaka unapo isha anapaswa kukumbuka kuwa anawajibika kulipa zakah haswa kwa wale wenye uwezo na zakah ni nguzo ya tatu ya Uislam na imefaradhishwa katika Qur'an tukufu na katika mafundisho ya Mtume (saw), na kwa sababu ya umuhimu wake, MwenyeziMungu ameitaja mara themanini na mbili katika Qur'an kwa kuifuatanisha pamoja na Swalah.
Kwa wale wote wenye uwezo wa kutoa zakah watakuwa ni wenye kufaulu watakapoweza kutimiza wajibu wao huu na wakawa ndio sababu ya kuondoa au kupunguza umasikini katika jamii zao.
Ili jambo, sijapata kulisikia wala hakuna ambaye ameweza kutuma meseji za kukumbushana kuhusiana na hii faradhi ya kutoa zakah.
Wengi wetu upenda kuweka maazimio na matarajio yaani kuweka malengo kama vile kukusanya pesa kidogo kidogo ili kwenda hijjah na mambo mengine, lakini sijawahi kusikia mtu akijitahidi katika matumizi yake ili siku moja katika uhai wake aje kutoa zakah pale mwaka mpya wa kiislam unapojili.
Waislam tunapaswa kuwa na malengo ya kila siku, tena malengo yenyewe yawe ni malengo ya kujirekebisha kuwa bora kuliko siku iliyopita.
Masaa yamepita, Siku zimepita na hali za Waislam wengi hazibadiliki kuwa bora kwa sababu wengi wetu tumejiweka mbali na Uislam na akidah yetu imekuwa chafu kuliko huo uchafu wenyewe.
Waislam tunaongoza kwenye mambo mengi ya kipuuzi, utakuta waimbaji wazuri kwenye miziki ni Waislam, kwenye uhuni wa kuvuta bangi, madawa ya kulevya na ulevi mwingine, waislam tunaongoza, kiasi hata kufanyiwa istizahi kuwa mbona mwezi wa ramadhani mabaa na maeneo yanauza nyama ya nguruwe (kiti moto) uwa yanakosa wateja na hayajazi kama miezi mingine. Mbona tunapomaliza mfungo ndio mabaa na majumba ya kufanyia ngono ndio yanafurika!?
Tangia kuingia kwa Mitandao ya kijamii, basi Waislam sisi ni kutafuta sifa, kujiona kuwa tunajuwa zaidi kuliko wengine, hatutaki ushauri wa aina yoyote. Kazi tuliyonayo ni kuchafuana tu na kutukanana.
Sheikh fulani hivi, Sheikh Fulani vile, tunagawa pepo kama mali yetu, na wale tusiokubaiana nao tunawahukumu kwenda Jahanam. Tunasahau kuwa wakati sisi tukijishughulisha na kutukanana, wale wa upande wa pili wanaendelea kuwa wenye maisha bora zaidi kuliko sisi.
Ni Waislam wachache sana ambao ni mifano katika familia zao au ndugu na jamaa na marafiki zao na hata mitaani kwao ni mfano wa kuigwa, lakini kama atatokea Muislam mwenye tabia hizi, sisi Waislam wengine ndio tutamkebei na kumtia midomoni kwa kumshusha hadhi yake na kumuona kuwa si chochote zaidi ya kujitafutia sifa tu.
Haya ndio tunayo Waislam wa sasa, na hakuna wa kutuonyesha njia kama hatutakubali ndani ya nafsi zetu kuwa tuyafanyayo sio na tunapaswa kubadirika, laah basi tutaendelea hivi hivi kuishia kutumiana salam za mwaka mpya bila ya kuwa na maazimio yoyote ya kujikomboa, Kitabia, Kiuchumi na Kihali. Sina maana kuwa nakataza watu wasitumiane salamu na kupongezana, lah hasha.
Lakini salamu hizi ambazo hazina kukumbushana wajibu wetu na zisizo na maazimio yoyote zina faida gani katika jamii ya kiislam?
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?