Ni unafuu wa kimaisha kwa walalahoi na si faraja ya kuona baadhi ya wachache wakiwajibishwa.
Wakati mwingine utendaji wa mtu unaweza kuwa ni uwakilishi wa ukweli wa mawazo yako yakiwakilisha jamii ya watu wa aina fulani, aidha kitabaka, kijinsia au hata kiimani.
Kiongozi yoyote yule, anapotoa mahamuzi fulani na kulifuatilia ili kutatua tatizo ambalo kwa namna moja au nyingine linaigusa jamii moja kwa moja au kwa njia mbadala, basi wananchi wanaoguswa na jambo ilo aidha watakuwa wanayaangalia maamuzi hayo kwa jicho la bashasha au mashaka, na hii ni kulingana na hali halisi ya jamii hiyo kihistoria na hapo ndipo kunaweza kuzua maswali mengi vichwani mwa wadadisi wa mambo mbalimbali ya kijamii na kisiasa.
Viongozi wetu wanapaswa kuwa makini sana kwa kila hatua wanayochukuwa kwenye maamuzi yao ili yale ambayo yaliwahi kutokea uko nyuma yasijirudie tena.
Unaweza kujiuliza nakusudia nini kwa utangulizi huo. Kwa kuendelea kunisoma unaweza kuelewa kusudio langu ni nini.
Hii nchi imepata uhuru wake mwaka Desemba 1961, mpaka ikifika Desemba 9 2015 ni miaka 54 tangia tujitawale. Tanzania ni nchi iliyopitia kwenye hali na maazimio balimbali ya kisiasa na kiuchumi.
Haya Maazimio yalikuwa mengi tu, moja katika Maazimio ni lile la Arusha. Azimio ambalo lilitoa azimio la kutaifisha Mashamba na Mashirika na Makampuni ya watu binafsi na kuyafanya kuwa ni mali ya Taifa (Umma). (sina uhakika hapa kama kweli zilikuja kuwa mali za umma au za viongozi wachache). Mambo hayo yalijiri mwaka sitini na saba (1967) na tukaipa jina - Azimio la Arusha.
Hawakuishia hapo fikra zao sahihi zikapelekea azimio lingine la madaraka mikoani hii ilikuwa mwaka1971... (siyasa hii ilikuja baadae kuuwa co-operatives zote zilizo anzishwa na wananchi, usiniulize tafadhali ilikuwaje kuwaje... sitaki udaku).
Tanganyika ilipotaifisha, mashamba, Mabenki na baadhi ya mashirika... Ilionekana kuwa ni jambo jema na litawainua mpaka makabwela, lakini tukasahau kuwa hayo makampuni na hayo mashamba tuliyoyanyang'anya wenyewe ndio hao hao walioshika soko la ulimwengu wa bidhaa mbali mbali, na ndio hao hao wenye kutengeneza hizo mashine za viwandani....!
Hayo makampuni na hayo mashirika pamoja na mashamba tuliotaifisha, tukawapa ndugu jamaa na marafiki zetu, ili waziendeleze matokeo yake kila mtu anayajuwa... Hakuna hata mmoja aliyesimamishwa mbele ya wananchi kuulizwa kulikoni?
Zikatumika akiba zilizoko, zilipokwisha basi tukabaki tunatizamana tu. Tukaambiwa tufunge mikanda miezi kumi na nane (18), na kweli tukaifunga nikanda mpaka viuno vikawa kama nyigu. Matokeo yake yakatushinda tukaamua kuwarudishia walewale tulio wanyang'anya...!
Nadiriki kusema kuwa hii nchi ni ya wachache sana, ni wale wenye uwezo wa kuuza na kununua, wenye uwezo wa kupata matibabu, wenye uwezo wa kula na kusaza, wenye uwezo wa kutobanana kwenye madaladala na si kwa wale waishio uko vijijini, ambako kwao kuwaona viongozi ni mpaka kipindi cha kampeni.
Wazalendo wale ambao enzi zile walijulikana kama Makabwela, yaani watu wa kipato cha chini, leo hii tunajulikana kwa jina la Walala Hoi, na haswa wanaoishi mikoani wanaweza zaidi kuona kile ninacho kizungumza... Si ajabu uko mikoani na haswa ukitembea siku ya soko au gulio ukamwona dalali akiuza kitanda cha kamba... karne hii.
Miaka ile ya themanini Tanzania iliingia kwenye nngwe nyingine, tilishuhudia aliyekuwa waziri mkuu Marehemu Edward Moringe Sokoine, akitoa maagizo ya kuwafilisi wale wote waliokuwa wakionekana kuwa wana hujumu uchumi wa nchi hii. Walalahoi tukafarijika kiasi kwa kuona sasa hali zetu zitakuwa bora zaidi ya jana.
Matokeo yake yakawa ni kinyume na matarajio yetu. Nchi ikaingia kwenye kizaa zaa kingine kwa wafanyabashara wengi wakajikuta wamepoteza biashara na mali zao, kuanzia majumba, Magari na hata mashamba. Tukajikuta kwa mara nyingine tena nchi haina bidhaa muhimu, kama vile Unga wa Mahindi, Ngano, Sukari, Mchele, sabuni, Mafuta ya kula na ya taa, hizi zote tukaziita bidhaa adimu.
Serikali ilipoona kuwa hali si nzuri, tukaanzishiwa maduka ya kaya, yaani kila familia ilikuwa na resheni yake ya kununua bidhaa kulingana na idadi ya watu wa kwenye familia husika. Mtu alikuwa haruhusiwi kununua bidhaa ambazo tukiziita adimu zaidi ya kiwango kilichopangwa.
Lakini yanini kujikumbusha hayo yote, si wazee wetu walituambia kuwa yaliopita si ndwele tugange ya jayo...? Ah wakati mwingine kukumbuka yaliopita, kunaweza kusaidia tusijikwae pale tulipojikwaa na kudondoka kwa mara ya pili. Kwa sababu aliyeumwa na nyoka akiguswa na unyasi ushtuka, tena anaweza kupiga yowe likawashtua wengi.
Watanzania tulishaumwa na nyoka, na madhara yake bado yapo mpaka hivi leo tunauguza donda. Japokuwa hali inavyo onekana sasa kama vile kuna dalili za furaha na matumaini labda hali inaweza kuwa nzuri kwa jinsi rais Magufuri na timu yake wanavyozikabiri kero chache katika nyingi ambazo wananchi wengi wanaamini zikiondoka basi tunaweza kuwa na nafuu ya kimaisha.
Wakati mwingine ni unafuu wa kisaikolojia tu, kwa kuona kuna watu wanawajibishwa kulingana na utendaji wao kuwa si wa kuridhisha.
Watanzania tuna matatizo mengi yanayotukabili, matatizo ambayo kila kukicha yanaongezeka na kukosa utatuzi yakinifu. Uduma nyingi zimekuwa hazipatikani mpaka kwa kujuana au kwa kutoa rushwa. Japokuwa tunajuwa kuwa rushwa ni uchafu na kama vile mwili mchafu usababisha harufu mbaya na kuwakera walio jilani nawe, hivyo hivyo uduma mbaya za kijamii zinazo ambatana na utowaji wa hongo ukera na kuathiri jamii ya Watanzania kwa kiwango kikubwa sana.
Hali inavyokwenda si kwamba sote tutakuwa matajiri au wenye uwezo kama hao walio na uwezo kifedha, lah! Tunacho tarajia ni kuona kuwa uduma za kijamii kama vile Hospitali, Usafiri, Elimu na hata upatikanaji wa uduma za maji safi na umeme bila kusahau chakula, mavazi na malazi, nakadharika vinapatikana na vikiwa katika hali bora zikiwakilishwa kwa utendaji mzuri na kila mwanachi awe na uwezo wa kuvipata na kunufaika navyo.
Hatutaki kufarijiwa kisaikolojia, kwa kuona tu baadhi ya wafanyabiashara au kwa baadhi ya wahusika wa uduma za kijamii wakiwajibishwa tu, bali tunataka kuona tunapata unafuu wa maisha na kila raiya akajivunia kuwa Mtanzania.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?