Lakini Hatuwaoni
Siku moja baada ya miangaiko yangu ya mchana kutwa, nilihamua kuingia mgahawani ili nitulize njaa kidogo kabla ya kurejea nyumbani kwangu.
Nikaagiza pilau yangu na kujiweka vizuri ili nikishambulie chakula kile, kwa jinsi njaa ilivyokuwa imenikamata.
Kabla sijakata tonge aliingia kijana mmoja wa makamu yangu, akaja na kukaa meza karibu na ya kwangu. Akaagiza chakula kama kile nilicho agiza mimi.
Wakati mimi na wengine tukiendelea kula, nikashangaa yule jamaa akiashiria kitu, nilipo mtazama kumbe alikuwa anawaita watoto wawili, wa kike na wa kiume, wakiume anaonekana ni mkubwa kuliko Yule wa kike. Makisio ya umri wao wapata umri wa miaka saba na kaka mtu kama miaka 12 hivi.
Wale watoto walikuwa wakiangalia ndani ya ule mgahawa uku wakionyesha wazi kuwa wana hamu na wao wapate ule mlo na si hamu tu, ni dhairi kabisa walikuwa na njaa haswa.
Yule jamaa alipoona kuwa hawaji, nahisi walikuwa wanaogopa, akanyanyuka na kutoka nje na kuwashika mkono na kuingia nao mgahawani na akaketi nao. Kisha akawauliza wanataka kula nini, nao bila kusita wakaashiria kuwa wanataka kula kama kile anachokula yeye.
Jamaa akawaagizia chakula, sisi wengine tukimwangalia tu kwa jicho la pembeni kila mtu na lake.
Kilipoletwa chakula yaani sahani mbili za pilau, wale watoto wakakivamia uku wakiwa na shauku kubwa kwelikweli. Kusema ukweli walionyesha wazi kuwa walikuwa na njaa haswa.
Nilipo mtazama yule jamaa alikuwa naye anawatazama tu wale watoto jinsi walivyokuwa wakikishambulia sahani zao za pilau. Hata dakika kumi hazikutimia walikuwa wamesha maliza chakula chote mezani.
Wakamshukuru mfadhili wao kisha hao wakaondoka wakiwa na nyuso za furaha kwa kupata mlo ambao nina uhakika kama waliwahi kula basi hawana hata kumbukumbu ni lini waliwahi kula mlo kama ule.
Jamaa naye akamaliza chakula chake na kumwita weita akamwomba bill ya chakula chake pamoja na wale watoto wawili mtu na mdogo wake.
Bili ya chakula ilipokuja kumwamgalia jamaa, alikuwa kama kapigwa na bumbuwazi la mashangao, mimi kwa kimbelembele changu nikamuuliza vipi kaka, kwani bili ni kubwa sana au…!? Akaniangalia kisha akameza fundo la mate na kuiangalia tena bili yake na kisha akatabasamu na mara nikamuona akitokwa na machozi kiasi.
Nikazidi kushangazwa na yule mtu, nikazidi kupatwa na hamu ya kujuwa kinacho endela, yeye naye bila ajizi akanionyesha ile bili aloletewa.
Nikaikamata ile karatasi na kuisoma, nikakutana na jambo ambalo hata mimi nililengwalengwa na machozi kidogo.
Jambo ambalo hatukulitegemea kuweza kutokea haswa kwenye hizi nchi ambazo kila mmoja anajali mustakabari wa maisha yake na uku akiweka mbele kujirimbikizia ili awe na pesa nyingi zaidi.
Nikafikicha macho yangu na kuisoma tena, nikakutana na maneno yaleyale niliyoyasoma sekunde chache zilizopita… “Hatuna mashine ambayo inaweza kumlipisha mwenye ubinadamu kama ulio uonyesha wewe leo, MwenyeziMungu akujaalie kwenye mambo yako”
Maneno haya yakajirudia tena na tena kwenye kichwa changu, kiasi nisahau kumrejeshea karatasi yake.
Ile karatasi ya jamaa, ilikuwa kama imefungua ukurasa ambao siku zote nilikuwa nauona lakini kwa namna moja au nyingine sikuutilia maanani, japokuwa nilikuwa nauona, na ili si kwangu mimi tu, msiba huu umeikumba jamii zetu haswa sisi ambao tuna vipato kiasi cha kuweza kula milo angalau mitatu kwa siku.
Tukijitazama haswa sisi Waislamu wa leo hii. Utakuta ndio matajiri na pesa zetu zipo kwenye mabenki yenye kutoa riba. Hatuwaangalii watoto yatima, kiasi tumewapa majina kama vile Machokoraa au watoto wa mitaani, mimi binafsi sijawahi kuona mitaa ikizaa watoto, lakini ndivyo tunavyo waita.
Dunia imetukamata kwelikweli, kwenye majumba yetu tunakula na kusaza na tukitoka nje, tunawanyooshea vidole hao watoto wa mitaani/Machokoraa kuwa wanatusumbua sana kwa kutuibia vitu vyetu, ilihali tunajisahau kuwa, kuwatunza na kuwalea ni moja ya majukumu yetu, lakini tunafikiria kuwa majukumu yetu yanaishia ndani ya familia zetu tu, hapo ukiondoa kazi za kujitafutia riziki, baada ya hapo basi.
Tunasahau kuwa kwa kutoweza kuwaangalia na kuwapatia mafunzo hao watoto wasio na walezi ndio na wao kwa kuwa ni binadamu wana mahitaji yao, lakini kwa kukosa kwao jinsi ya kujiwezesha ndio wameingia kwenye tabia ambazo athari yake imeikumba jamii nzima.
Ayat za Qura’n zenye kusisitiza kuwasaidia masikini, mayatima na wasio na uwezo ni nyingi, lakini wengi wetu tunazisoma tu na wala hatuzingatii kile tunacho kisoma.
“Muabuduni MwenyeziMungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri.” Q4:36
Mtume ﷺ amesema kuwa, amemdhamini Pepo mleaji yatima, kwa sababu kulea mayatima siyo kazi rahisi lakini ni kitendo ambacho amekijaalia MwenyeziMungu (swt) kiwe na thawabu na malipo makubwa kesho Akhera. Katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira (ra) na kutolewa na Muslim kasema:
“Mleaji yatima wa karibu yake (kwa ujamaa) au wa mbali (siyo katika jamaa), mimi na yeye kama hivi (vidole) viwili (yaani pamoja naye) Peponi.”
Mleaji yatima maana yake ni kumwangalia yatima katika mambo yake; kumlisha na kumvisha, na ikiwa kama ana mali aifanyie biashara ili iongezeke na pia ipatikane masurufu katika mali hiyo ya kununulia chakula na vitu muhimu vya kutumia.
Na pia Mtume ﷺ kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbaas (ra). na kutolewa na Ttirmidhi:
“Atakaemdhaminia yatima miongoni mwa Waislamu kwenye chakula chake na kinywaji chake mpaka MwenyeziMungu amjaalie ajitegemee, Mola amemdhaminia Pepo, ila akifanya dhambi (kubwa) isiyosameheka.”
Ukitaka ulainike moyo wako mkaribishe yatima kwako na umpapase kichwa chake na umlishe katika chakula chako. Kwa hakika (mambo) haya yatalainisha moyo wako na utapata haja yako.
“Kumsimamia mjane na maskini kwa matumizi na malezi ni kama vile mwenye kujitahidi katika njia ya MwenyeziMungu au kama yule ambaye anafunga (mchana kutwa) na anaamka usiku (kucha kusali).”
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?