Thursday, 21 April 2016


Binadamu tumekuwa na mipango mingi sana kuhusiana na maisha yetu ya kila siku na ya siku zijazo. Tumekuwa tukipanga na kupangua kuhusiana na maisha yetu ya kila siku, tukiyafanya hayo na tunaendelea kuyafanya kila leo.

Hii yote ni dalili kwamba hapana budi kuwepo kwa siku nyengine tofauti na siku hii ya leo. Iwapo mtu anaishi peke yake au pamoja na wenzake, ushahidi ulio na dalili kuwa hapana budi kuwepo kwa siku nyingine ni mkubwa kwa sababu maisha ya mtu peke yake, mtu yeyote miongoni mwetu, bila ya kuwa na imani juu ya siku inayofuata maisha hayata kuwa maana tena, kwa sababu hakuta kuwa na ile chanagamoto ya kimaisha.

Mawazo hayo yote yalinijia “SIKU NILIPOTEMBELEA MAKAZI NA NYUMBA ZETU ZA BAADAYE”

Kila mmoja wetu mwenye kujitambua miongoni mwetu, hana budi kuyafikiria maisha haya na kuyazingatia kisha akajiuliza; Je Nitakufa? Baada ya taabu yote hii ya miaka 40 au 60 au zaidi miaka 70 ukibahatika kisha nife?

Mimi! Mwenye Akili, Mimi Mwenye Elimu, Mimi Mwenye Ufalme, Mimi Mwenye Fedha Nyingi, Tajili Mwenye Kutajika.

Mimi Nisikiaye na Kuona, Mimi kweli Nife Kisha Nigeuke Kuwa Udongo, Watu Waukanyage Kwa Miguu Yao? Mwisho Gani Huu Unaoumiza?

Wasioamini Mungu, wamelifikiria sana jambo hili na chunguzi nyingi zimefanywa kiasi wakawa na Falsafa kadhaa wa kadha.

Wanasema: "Uhai una maana gani, tunamalizika kwa kufa? Nini faida ya kuishi wakati uhai huu umekwisha andikiwa tangia unapoanza? Kwa hivyo sisi tunapambana mapambano ya kushindwa katika maisha haya, kwa sababu tokea pale tulipoandikiwa kuishi tulikwisha andikiwa kufa."

Kwa hivyo uhodari wako ewe Daktari unafaa nini? Unaruka ruka miaka 40 au 70 kisha? Unakufa?

Wataalam wa akili na mambo yasio ya kawaida (paranormal) wanatufahamisha kuwa, watu wengi wanaokaribia kufa, upata maono ya kutembelewa na ndugu au marafiki na jamaa walikwisha kufa kabla. Hali hii uweza kuwatokea kwenye ndoto au kuwa na mawazo mengi kiasi mwingine kuwaona ndugu au jamaa waliokufa wakiwapungia mikono au hata kuwaita.

Tafiti nyingi ambazo zimewashirikisha wagonjwa walio mahututi au wanaotarajiwa kufa, wamekuwa wakisema kuwa mara nyingi 'wamekuwa wakitembelewa kimaono na jamaa au marafiki zao waliokwisha kufa zamani.

Na kila mtu anapozidi kukaribia kifo chake basi hali hii ya kuwaota au kuwaona ndugu na jamaa waliokwisha tangulia uwa kubwa kiasi cha kujirudia mara kwa mara kiasi ya kuwa kama jambo la kawaida kwa muhusika.

Hali hii imekuwa ikijitokeza kwa watu wengi, japokuwa wengi wao wamekuwa ni waoga kuielezea na wengine ufikia mahala wakatumia vileo kama vile pombe ili kujisahaulisha.

Wanasayansi kutoka Canisius College, jijini New York waliwahi kuwafanyia uchunguzi wagonjwa wasiopungua 66 ambao wanapata uduma za kiuangalizi wa maisha yao ya mwisho kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi (hospice).

Watafiti waligundua kuwa wagonjwa wengi wamekuwa wakipata maono hayo angalau mara moja kwa siku.

Wagonjwa wengi walisema kuwa wamekuwa wakitembelewa na jamaa zao waliokwisha kufa na ugeni huo si kwenye ndoto yaani wanapokuwa usingizini la hasha, wamekuwa wakiwaona dhahiri kabisa.

Watafiti hao wamesema kuwa mtu ambaye anakaribia kufa upata ndoto nyingi na za mara kwa mara zinazowahusu ndugu, jamaa na marafiki wa karibu waliokwisha kufa.

'Maono haya yanaweza kutokea miezi, wiki, siku, au saa chache kabla ya kifo na kwa kawaida uweza kupelekea hofu au faraja kwa muhusika.

Binadamu tunapaswa kujiandaa na safari yetu hii, ambayo kila mmoja wetu ataipitia. Ukikumbuka kifo na wewe upo katika hali njema kabisa basi juwa kuwa wadudu wa ardhini wanakusubiri watatembea juu ya mwili wako mzuri huku wakishiba kwa kula matumbo yako.

Kwa hivyo tunasema kwamba, maisha haya hayana maana bila ya Imani juu ya siku ya mwisho, dunia hii ni njia ya kuelekea katika Makazi ya Akhera na kwamba baada ya makazi haya pana makazi mengine yenye kudumu, matumaini yetu yanapaswa kupanuka na kutengenea, na si kukata tamaa, kila tunaposikia neno KIFO.

Tumekuwa ni watu wenye mapambano na migongano ya kifikra kila tunapo ona mmoja wetu ametutoka, hii yote ni kwa kuwa hatuna uhakika wa maisha yetu yajayo. Na yanapotajwa mauti, anakuwa ametajwa mbomoaji wa raha, na utawaona wale wasioiamini Siku ya Hesabu wanaharakisha ili kila mmoja aweze kustarehe kiasi kikubwa zaidi katika muda huu mfupi.

Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu. (Al-'Imraan, 5: 185)

Tokea kuumbwa kwa Nabii Adam hadi leo hii na mpaka siku ya Kiyama hakuna kiumbe kitakachobakia isipokuwa Mwenyewe Mola Mtukufu, basi na tujiandae na safari yetu hii ya kuelekea kwenye MAKAZI NA NYUMBA ZETU ZA BAADAYE NA ZENYE KUDUMU.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!