Sunday, 17 April 2016

SIKU YA KWANZA MBONGO KUPANDA NDEGE 

Kupanda ndege sio mchezo ndugu yangu, hebu fikiria katika ukoo wenu watu wangapi wamepanda ndege? Ni wachache unaweza hata kuwataja kwa majina na tarehe ambazo walipanda ndege. Kijijini kwetu kuna wimbo unamsifu mwanakijiji mwenzetu aliyewahi kusafiri na ndege na kutua salama, na hii ni moja ya sifa ambazo ndugu wa ukoo wa jamaa yule huzitaja kama moja ya mafanikio makuu katika ukoo wao kila wanapokuwa wamelewa.

Mbongo wa kawaida akiambiwa atakuwa na safari ya ndege, hasa ikiwa kwa mara ya kwanza, kuna mambo flani ya kimsingi ambayo lazima ayafanye. Baada ya kuhakikishiwa safari ni lazima awataarifu ndugu na jamaa, na anaweza kupiga simu mpaka kwa wazazi wake kuwataarifu kuwa atapanda ndege. Zoezi hili huwa na sababu mbili kubwa kwanza ni kuonyesha furaha ya kwa kupanda ndege na kutaka wazazi na ndugu kujua kuna mwenzao hatimae kafanikiwa kupanda ndege, ili waweze kuanza kujisifu kijijini. Sababu ya pili ni uwoga, unajua kupaa hewani kunatisha, na ukizingatia kila siku tunaona magari yanayotembea ardhini yakianguka sembuse ndege! Basi kupaa hewani kunatisha sana, sasa inakuwa vema kutoa taarifa kwa ndugu na kuomba wakuombee ufike salama uendako. Na pia kuwataarifu wazazi wakaitaarifu mizimu kuwa mjukuu wao anakwenda kupanda ndege.

Baada ya kutoa taarifa kinachofuata ni shopping, hapo lazima mswahili akanunue nguo mpya za kupandia ndege, hata kama safari yenyewe ni ile ya saa mbili tu, kutoka Mwanza kwenda Dar, mtu atagharamia suti mpya, shati na tai, viatu soksi nyeupe na bila kusahau san gogoz. Sanduku jipya lenye matairi, maana ukishuka lazima uwe na sanduku la kuburuza. Na hapo mbongo anakuwa tayari kupanda ndege.

Usiku wa kuamkia siku ya kupanda ndege, Mbongo halali. Usingizi hauji, kila akiwaza kupaa angani haamini, kimoyomoyo anajisemea, ‘Duh hatimae na mimi sasa napanda ndege’, kingine kikubwa kinachomkosesha usingizi ni uoga wa kupitiliza usingizi na kuchelewa ndege. Alfajiri saa kumi na moja inamkuta msafiri wetu kisha amka na anaoga, japo ndege itaondoka saa tisa mchana. Siku hiyo ataoga maji ndoo tatu, maji yakiisha anaongeza tena, nyimbo nyingi za furaha, zile za bafuni, utamsikia anaimba ule wimbo wa Tancut Almasi,’Ninakwenda safari safari yenyewe ya masafa marefuuu’. Bafuni kunakuwa raha tupu. Kufikia saa moja asubuhi kisha kunywa chai, tayari kwa safari ya saa tisa mchana, mwenyewe kisha pendeza na suti na tai.

Unajua Mbongo kama anaenda safari kwa basi huwa hana makuu, ataita Bodaboda au Kibajaji apelekwe kituo cha mabasi, lakini ishu hapa ni kuwa anasafiri na ndege, hivyo itaitwa taxi impelekee mapema uwanja wa ndege, saa nne mbongo yuko tayari uwanja wa ndege, suti ya vipande vitatu bila kujali joto la Darisalama .

Baada ya masaa kadhaa kwenye viti vya kusubiria safari, presha inampanda, presha inamshuka, maana ule muda wa kupanda ndege kwa mara ya kwanza katika maisha yake unakaribia. Na utakuta kichwani kishajipangia akiingia tu kwenye ndege atakimbilia kiti cha dirishani, hii itasaidia mambo mawili, kwanza ataweza kuchungulia nje kuangalia madhari ya miji mbalimbali akiwa hewani, na pili kama kwa bahati mbaya atajisikia kichefuchefu hatasumbua mtu, atafungua tu dirisha na kujisaidia kirahisi unaonae.

Wakati mawazo haya yakiendelea, presha ya msafiri wetu ikapanda ghafla aliposikia, ‘Tangazo, tangazo wale abiria wa kwenda Mwanza tafadhali sogeeni kwenye dirisha la kampuni ya ndege yetu kwa maelezo zaidi’ Jasho likiwa limashamtoka sana kutokana na kuvaa suti na tai kwenye joto, atavuta sanduku lake jipya la magurudumu na kuelekea kule walikokuwa wanaelekea wengi.

Pale wanamkuta binti mmoja kavaa vizuri, analiambia lile kundi la wasafiri, kwa sauti iliyoonyesha kuwa japo anaonekana kama mswahili mwenzetu lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa mmoja ya wazazi wake ni Mmarekani ‘Abiria wetu samahani kwa ntakalowaambia, nimetumwa na menejiment ya uongozi wa kampuni yetu niwaambie kuwa bekozi kutokana na matatizo ya kiufundi ambayo ni tekniko, kwenye ndege yetu, kutakuwa na long dilei na safari yenu imekuwa postponed mpaka kesho saa kumi na mbili alfajiri…!

We are vere vere sori, lakini hii ni wa ajili ya usalama wenu nyinyi abiria wetu ambao ndio wafalme, karibuni msiache kusafiri na ndege zetu kwa usalama na umakini’

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!