UKIPEWA NAFASI UTAMREJEA AU UTATAFUTA MWINGINE?
Kabla ya kuanza kuandika makala hii, nimekumbuka swali moja ambalo niliwahi kuliuliza kwenye group mbaimbali za whatsapp.
Swali lenyewe niliuliza hivi:
Je ikitokea leo hii, ndoa zote kufutwa na kutakiwa kuanza upya, utataka kuoa/kuolewa na Mume/Mke huyu uliyenaye au utataka mwingine?
Majibu yalikuwa mengi, ila wengi walisema kuwa huyu huyu aliyenaye, wapo wachache walisema itakapo tokea hali hiyo basi uwamuzi wake utakuwa hapo hapo. Kuna wengine waliliona swali lile kama ni upuuzi na kuandika maneno makali kabisa kuwa ni jambo lisilo wezekana na kwa hiyo hakuna haja ya kulijadili.
Huyu aliyekataa sababu zake ndizo hizo kuwa swali halina uhalisia, lakini alishindwa kujuwa kuwa swali ili limeegemea sana kwenye mantiki ya swali lenyewe.
Ni kweli hali kama hiyo haiwezi kutokea, sawa lakini lengo la swali lilikuwa kuwapa wasomaji changamoto na kuziangalia upya ndoa zetu. Je tumeridhika nazo, tupo kwenye furaha na ndoa zetu, je zinakidhi haja na kutupa faraja, kiasi ikitokea kuchaguana upya tutataka tuendelee na hizi hizi au ndio itakuwa mwisho wa safari!?
Baadhi ya majumba yetu ndoa zipo hatarini kubomoka, maisha yao ndoa yananing’inia kwa kushikiliwa na uzi wa buibui. Furaha imetoweka ndani ya nyumba kwa kukosa imani na ndoa husika, kwa sababu ambazo zinaweza kurekebishika.
Wanaume wamekosa imani kwa wake zao kwa kudharauliwa kwa kuondoshewa ile hali ya kuonekana kuwa wao ndio viongozi wa nyumba kiasi ya kwamba mume anaishi tu lakini kiuhalisia ndoa kwake imekuwa kama sehemu ya jela ya kisaikolojia.
Wakati huohuo wanawake nao ujiona kuwa kwa kuwa tu wamepata M/Watoto kwenye ndoa hiyo basi chochote watakacho kifanya hata kama hakipendezi kwenye ndoa, wanaona kuwa hakuna kitakacho haribika kwa sababu wana aidha mtoto au watoto kwenye hiyo ndoa.
Je, nyumba kama hiyo itakuwa na mapenzi kweli au watu wataishi tu kuendeleza maisha kwa kuwa wamezaa, au kwa mmoja kuwa na mali nyingi au kwa kuwa Mume/Mke ana jina linalotajika mitaani au kwa kuogopa wazee wao?
Inasikitisha sana katika jamii zetu kila nikizungumza na wana ndoa utasikia matatizo waliyonayo yanafanana. Ni hali ya kutisha sana na inafaa tuzingatie sana na wala tusiidharau, kwani utakuta hata watu waliosoma dini au walio elimika kwenye elimu mbali mbali ndio wenye kuongoza kwenye migogoro ya ndoa.
Sio vibaya kutofautiana kimawazo lakini iwe kwa njia ya kusomeshana au kukatazana pale pindi mtu anapotaka kukosea lakini utakuta sio hivyo kabisa.
Kukaa pamoja kwa niya Mume na Mke ni kukamilisha furaha na si kumgeuza mmoja kuwa ni kisonoko mfanyakazi wa ndani.
Kazi za kufua, kufagia, kupiga pasi kulea watoto na kupika, hizi ni kazi ambazo wana ndoa wanapaswa kusaidiana, japokuwa kwenye jamii zetu, kazi hizi ufanywa sana na wanawake lakini si vibaya tukasaidiana. Na inapotokea mume kumsaidia Mke, isipelekee Mke kujisahau kiasi cha kuona kuwa huyu mume nimemuweka mkononi, hafurukuti wala hatweti, nitakacho mwambia anafanya.
Waume kiasili wameumbwa kutawala, kuheshimiwa zaidi na kuonyeshwa kuwa wao ndio viongozi na ndivyo hivyo ilivyo. Sasa ikitokea mume kumsadia mke, hisiwe tena mke hata akimuona mume yupo na rafiki zake au ametembelewa na jamaa zake basi ndio kutaka kuwaonyesha kuwa wewe mke unaweza kumwamrisha mume vile unavyotaka. Hapo utakuwa umeharibu, lakini kama mume mwenyewe akitaka kusaidia mbele ya jamaa zake si vibaya na ndivyo inavyotakiwa haswa.
Japokuwa kwa mwanaume wengi inaonekana kama vile ni kutawaliwa pale mwanaume anapokutwa na marafiki, jamaa au ndugu zake anaosha vyombo au kupika au kufua na kuogesha watoto nyumbani.
Haya yanasababishwa na ukosefu wa elimu na ubinadamu na kuto kuwa na huruma kwa mwenzi wako. Wanaume wengi hawapewi mafunzo ya kutosha wanapotaka kufunga ndoa jambo ambalo ni muhimu sana wafunzwe vipi kuishi na wake zao.
Nasaha nyingi zinazohusu ndoa na haswa siku ya harusi uelekezwa kwa wanawake, hata viongozi wa dini nao sana uwatahadharisha wanawake kuhusiana na mambo ya ndoa kuliko kwa wanaume. Hii inawafanya wanaume wasitambue makosa yao na waache kufanya ihsaan kwa wake zao. Siku zote nyumba ikivunjika anashutumiwa mke tu ilhali pengine ukorofi unaaza kwa mwaname mpaka kufikia hali ya kuachana.
Wanandoa wengi ambao wanaishi nchi za nje haswa nchi za Ulaya na Marekani, wanawake zao wanazidi kuwa wajeuri na kukosa nidhamu kwa sababu ya ule uhuru na haki za wanawake zilizopitiliza, nasema zilizopitiliza kwa sababu sisi Waafrika wengi hatujazizoea na tunaziona kuwa zimepitiliza mipaka ya kiutamaduni na imani zetu za dini.
Nao wanawake kwa kuona kuwa wana haki zaidi ya waume zao basi wamekuwa wajeuri kiasi cha kutisha, maana si ajabu kuona mwanamke kumfukuza ndani ya nyumba mume na kumfungashia virago mume wake kwenye mifuko ya taka na kumrembeshea nje, akaokote uko mafurushi yake.
Hai hii imepelekea wengi kuwa aidha na vimada ili kutafuta haueni au wengine kuamua kuoa wake wengine aidha Afrika au uko uko walipo.
Basi ni jukumu letu sote kuziangalia tena na tena ndoa zetu na kuondoa tofauti ndogo ndogo zinazo jitokeza kila leo.
Ili itakapotokea nafasi ya kuchagua kwa mara ya pili tuharakishe kuwachaguwa wale ambao tuliokuwa nao kwenye ndoa zetu za sasa.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?