Kuhodhika pia ni Maradhi, Ukiulizwa unakiri kuwa kweli uvitumii kwa sasa, ila kuna uwezekano siku ukavitumia, lini haijulikani!
Kuna Siku Nilikuwa Naangalia Kipindi Kwenye Runinga, Walikuwa Wakionyesha Maisha ya Wadudu Mbalimbali. Mojawapo Ya Wadudu Niliovutiwa Nao Ni Nyuki na Wadudu Wengine Wa Jamii ya Chunguchungu.
Kwa kweli nilivutiwa sana na maisha ya hawa viumbe wadogo ambao katika maisha yetu hatuwapi nafasi hata ya kuwatafakari hata kwa sekunde chache. Ni mpaka pale tunapowaona kuwa ni kero ndio tunashtuka na kutambua kuwa wapo duniani.
Wadudu awa kwa kweli naweza kusema kuwa ni wadudu wenye uwezo mkubwa katika kukabiliana na maisha yao ya kila siku, miongoni mwao hakuna kuyuayulika wala yugayuga.
Jambo moja niliovutiwa nalo ni jinsi ya mpangilio wa maisha yao katika ghoba zao na vichuguu vyao.
Kwanza kila mduduke, mdudume na wale Gegenu, wanafata amri bila ya kusita. Jambo ili linastaajabisha kidogo, nikawa najiuliza, ni nini siri yake.
Muda nagundua kuwa, vichuguu hivi vya Mchwa na hata yale makazi ya Nyuki vimejengwa katika hali ambayo inampa nafasi kila mkazi, kufanya kazi zake bila tatizo lolote na bila usumbufu wa hali yoyote ile.
Kamera ya mchukuwaji wa hii vidio naye anastahili sifa na ujasiri na uvumilivu, kwa kweli, mchukuwaji ametuonyesha vyumba mbalimbali kwa kazi tofauti tofauti mfano, Maghala ya chakula ni makubwa na kila mdudu inakuwa ni rahisi kwake kufika hapo bila ya usumbufu wowote.
Kuna vyumba kwa ajili ya kutotolea Mchwa wapya na kuna sehemu maalum kwa ajili ya mawindo mapya na kile ambacho hakina faida au hawakihitaji tena, basi wanakitoa nje kabisa ya kichuguu chao na kukitupa mbali.
Kwa kweli mambo niliyoyaona ni mengi, lakini lengo langu si kuzungumzia maisha ya awa waduduke na wadudume, japokuwa kuna mengi ya kujfunza kutoka kwao. Lengo langu haswa ni kuangalia maisha yetu majumbani mwetu na jinsi tunavyoishi na kukusanya kila chenye uwezekano wa kukusanywa na kuwekwa kwenye majumba yetu.
Hebu angalia kwenye majumba yetu tunamoishi, na jinsi upangaji wa vitu mbalimbali ndani ya vyumba, yaani tuna shindwa na hata na wadudu katika mipangilio.
Utakuta mtu kanunua fenicha mpya, lakini zile za zamani ambazo akizionea aibu na hakutaka hata kuwakaribisha rafiki zake kwenda nyumbani kwake, bado anazitafutia nafasi humo humo ndani.
Kuzitupa au kuzigawa anaona tabu au siju anaona hasara, kwa kweli hakuna anayejuwa!
Zile nguo ambazo hazikutoshi tena, zingine tangia utoto, kuna zingine ulipewa zawadi ulipomaliza kidato cha nne kama si darasa la saba basi ni kwenye kipaimara, ili ukatokezee kwenye mahafari ya shule miaka ishirini kama si zaidi ya miaka thelathini iliyopita, bado unazo tu, nguo hazikutoshi tena, maana ushaongezeka toka kiuno nchi 26 mpaka sasa unavaa kiuno nchi 42, bado unayo tu, ukiulizwa eti kumbukumbu kutoka kwa mjomba ako.
Ukiingia uko kunakoitwa utaa na stoo, ni mazalia ya Panya, Mende, Dambamwiko na wadudu wengine wanaoishi bila ya kulipa kodi ya nyumba.
Godoro tangia ukisoma shule ya bweni, miaka kadhaa na lile uliloanzia maisha ulipomaliza JKT ukahama nalo, bado unalo tu, japokuwa sasa ni mtu na familia yako na umekwisha nunua magodoro mapya, lakini yale ya zamani zamani badala ya kugawa umeviringisha na kuyaweka juu ya kabati, maana kule stoo hakuna nafasi tena.
Ukiulizwa unakiri kuwa kweli uvitumii kwa sasa, ila kuna uwezekano siku ukavitumia, lini haijulikani!
Uko kabatini kwako kuna nguo ambazo ulivaa ukiwa sekondari mpaka leo bado unazo, ukiulizwa eti ni ukumbusho au utazivaa ukipungua, sasa utapungua lini, ulikuwa ukivaa kiuno 26 mpaka leo una kiuno 42 plus...
Uko jikoni ndio shida iliposhika hatamu. Mivyombo ya plastiki imepaukiana vingine vimeyayuka na moto, vipo tu eti vyombo vya watoto, maana ukiwanunulia vya udongo awachelewi kuvunja, watakutia hasara.
Hotpot zote zimekata roho maana plastiki za nje zimepeana taraka na sufuria lake la ndani, lakini bado unalo tu. Kila ukibahatika kununu chupa za maji basi utahakikisha chupa zake huzitupi, vidoo vya sadolini, kila mahala hata hazitumiki zipozipo tu, hata maua hazifai kupandia we unazo tu hutupi, na kuzihitaji wala huzihitaji.
Ukiangalia vyombo vya udongo vina mapengo na magego kama barabara iliyopigwa mabomu ya Urusi, na kila kimoja na dizaini yake havifanani kwa sababu seti zote zimesha vunjika vunjika hivyo ndio vimebakia.
Ukija ndani kwenye hiyo meza ya kujipambia, wenyewe mnaita Dressing table, ni hatari kwa kweli, maana imejaa vikopo na viboksi havina hata kazi, chupa za manukato za tangia mwaka elfu moja mia tisa na… zimekwisha malizika, wewe kopo/chupa zake unazo tu, ukiuliza eti ukumbusho wa zawadi, ulipewa na dalingi wako, ulipokuwa chuo.
Uko stoo ukiambiwa uingie mwenyewe unaogopa, unahisi kama kuingia dambo, sababu stoo imekuwa mji wa Panya na jamaa zao mende, Nge na Tandu, stoo imejaa vitu visivyo hitajika, stoo imekuwa ghetto la panya, maana vilivyokuwemo humo ni vile ambavyo huvihitaji tena, lakini kuvigawa au kuvitupa unaona hasara.
Sasa na lile pale nje ni nini, unaambiwa lile ni gari, unajuliza sasa mbona limebakia sikrepa tu, si uwape wanao kusanya vyuma chakavu, wakavipeleke kwa resaiko. Hutaki kisa ni gari la urithi la kutoka kwa baba yake na babu yako, alikuwaga dereva wa DC enzi Mjerumani akitawala Tanganyika. Lipo tu hapo limekuwa makazi ya paka shume na wadudu wengine.
Kutupa vitu visivyo hitajika hamtupi eti hasara na kuvigawa haviwezekani tena maana havina hadhi tena ya kupewa mtu, vimekosa ile uhalisi wake, hakuna hanaye vitaka wala kuviulizia.
Ndio maana kila siku hamuishi kupishana mahospitalini, mara leo kikohozi kesho kifua kizito, mara, tumbo, mafua ndio kitu cha kawaida kabisa. Sasa kwanini msiumwe hali ya kuwa mmeamua kuigeuza nyumba yenu kuwa jalala kama si dampo!?
Tumewaambukiza mpaka watoto wadogo, maana wanajuwa kuwa nyumbani kwao hata kikopo cha shikirimu au kopo la plasitiki la siagi havitupwi vinaoshwa vinawekwa hapo.
Halafu bado unaendelea kumuomba Mungu akupe, akupe uweke wapi na kwako pameshajaa au uoni!?
Kitaalamu huu ni ugonjwa wa akili ambapo mtu hushindwa kabisa kutupa vitu ambavyo havitumii.
Huu ni ugonjwa ndio! Na wengi tumehathirika na haya maradhi ya kutopenda kutupa au kugawa tusivyo vitumia wenye lugha yao wanaita "Hoarding Disorder".
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?