Friday, 18 November 2016

LEO NDIO NIMETIBIWA

Mwanadada mmoja ambaye alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kutokwa na damu sehemu za siri mara kwa mara alichukia sana suala la kwenda hospitali. Kila mara alipokuwa akienda anapewa dawa lakini haponi na anahitajika arudi tena.

Baada ya kumuona haendi kwa muda mrefu na bado anaendelea kuniambia anaumwa, nilimuuliza kwa nini haendi. Alizunguka zunguka kunijibu ila mwisho wa siku akanambia "NIMECHOKA KUCHUNGULIWA" maana sioni kama kuna matibabu.

Mwingine ambaye alihudhuria hospitali kwa muda wa mwezi mmoja akiwa anatibiwa na dokta wakiume, siku alipohudumiwa na Daktari wa kike alimwambia mumewe kuwa, "LEO NDIO NIMETIBIWA" akimaanisha siku za nyuma zote hapakuwa na matibabu.

Wanawake wengi wa kiislamu wanaojitambua suala la kwenda Hospitali kupata matibabu kwao limekuwa gumu na mtihani mkubwa sana.

Mbali na hali zote hizi kuwa kwenye jamii zetu, bado mtu (aidha bila kujua au kuathiria na pressure ya kundi lake analoitakidi lina mtazamo sahihi) anasimama kwenye dar’sa zake na anapita mashuleni kuwaambia watu kuwa masomo ya Secular (Kwa mujibu wao) kuwa ni ya Kikafiri na wanahamasisha watu wasiyasome au kuyatilia mkzo.

Kwa kuwa bado tunaendelea kupumua, basi nafasi ya kutubia kwa kauli hizi bado tunayo. Vinginevyo tujiandae kutoa majibu yatakayomridhisha MwenyeziMungu siku ya Kiyama kwa kuufanya Umma kuingia kwenye matatizo tunayoweza kuyatatua kwa mikono yetu.

Narudia tena kusema kuwa kusomea Udaktari, Madawa (Medicine), Uhandisi (Engineering), Elimu (Education), Sheria (Law), Uhasibu (Accounting), Fedha (Finance) na masomo yote ambayo yanaitwa ya sekula kwa Muislamu anayejitambua napo ni kusoma dini na kwake hayo yatakuwa ni masomo ya dini pia, kwa sababu Dini si FIQ'HI, SIRA, HADITH, NAHAU au BALAGHA tu bali kila somo ambalo litaweza kuwaondolea matatizo Waislamu.

Leo hii Waislam badala ya kuangalia mustakabri wao wamekalia kukufurishana na kutukanana, wakati hao tunao waita makafiri wanaendelea kukamata kila nyanja za kiuchumi na kielimu.

Waislam tunapaswa kubadilika, maana Mwenyezi Mungu awezi kubadilisha hali zetu mpaka sisi wenyewe tuchukue hatua za makusudi kabisa na kufanya jitihada za dhati ndipo naye Mwenyezi Mungu atatufungulia milango yake ya Rehma na Uislam utasimama tena.

Ili tufike uko tunakotaka kufika, tunahitaji watu wenye fikra na mtazamo wa uhakika na watakaoiangalia hii dini katika jicho lile linalopaswa kutazama, narudia tena na kusisitiza kwani Uislam si hayo tuliyo yazoea tu, bali ni kila lenye manufaa na faida katika maisha ya Mwanadamu, hapa duniani na kesho Akhera.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!