Watu wengi linapokuja swala la Mwalimu Nyerere na Kiswahili, wanashindwa kuangalia hali halisi ya nchi na watu wake, makabila na mahusiano yao kwa maana ya kabila na kabila, kabla na baada ya uhuru.
TANGANYIKA:
Tukiangalia nchi ya Tanganyika, tunaona kuwa si nchi ya ukabila kama zilivyo nchi jilani, kama vile Kenya, Uganda, Burundi au Congo-Kinshasa. Wengi wanashindwa kuelewa kwanini nchi hizo zimegawanyika kiukabila, lakini kwa nchi ya Tanganyika, jambo ilo hata kama lipo basi ni chini ya aslimia 1 (-1%) Sababu ni nini basi tumekuwa hatuna ukabila na lugha kubwa imekuwa ni Kiswahili. Ili ni swali wengi wanashindwa kuchemsha akili na kujiuliza sababu yake.
KENYA:
Tukiziangalia nchi nilizo zitaja hapo juu, tukianza na nchi ya Kenya tunakuta makabila makubwa ni Matano, ambayo ni Wakikuyu 22% Waluhya 14%, Waluo 13%, 12% Wakalenjin na 11% Wakamba, Wakisii na Wameru kwa ujumla wao ni %12, waliobakia ni makabila mengine. Kwa hiyo ni rahisi sana kwa makabila makuu matatu ya mwanzo kuingia kwenye mgogoro wa matumizi ya Lugha na kimadaraka na hata kisiasa.
CONGO-KINSHASA:
Ukija kwenye nchi ya Congo-Kinshasa, tunakutana na wazungumzao lugha kuu nne Kimongo, Kiluba, Kikongo na Kiswahili, japokuwa katika hao wenye kuzungumza hizo lugha kuna makabila madogo madogo mengi lakini wanaunganishwa na Lugha kuu hizo nne, ukiondo Kifaransa.
Kwa ujumla maelezo ya hapo juu, inakuwa ni rahisi kuwagawa watu kimatabaka kwa lugha zao kwa sababu lugha zote hizo zina wazungumzaji wengi karibia sawa. Linapokuja swala la kisiasa na kiuongozi, mara zote utaona kwenye nchi zenye makabila machache yenye watu wengi kunakuwa na migogoro ya kisiasa.
BURUNDI:
Tukiangalia nchi ya Burundi tunakuta mgawanyiko ambao unatisha kidogo. Nchi ya Burundi Wahutu ni 85% wanafuatia Watutsi ambao wapo 14% na kisha kuna kabila dogo la Watwa lenye watu asilimia 1% tu. Na kama tunavyosikia kwenye vyombo vya habari, kuhusiana na nchi ya Burundi na mapigano yao ya kikabila, yote ni kugombea madaraka ya kiutawala kupitia ukabila kwa sababu, kabila lenye watu wengi kwa miaka mingi walijikuta wapo nje ya madaraka kisiasa na kitawala, wakitawaliwa na Watutsi ambao inasemekena asili yao si Burundi, lakini kutokana na sababu za kikoloni, Watutsi wengi ndio waliokuwa wakipendelewa na Serikali ya mkoloni na ndio waliotayarishwa kuja kutawala nchi na kuachwa wenye asili ya Wahutu, ambao ni wengi kuwa nyuma kimaendeleo. Hapo utaona kuwa kabila lenye watu wengi haliwezi kukubali kutawaliwa na walio wachache, lazima wataleta ukorofi na ukizingatia nafasi nyingi za kisiasa zinagawiwa kiukabila.
UGANDA:
Kwa nchi ya Uganda ukiangalia sensa ya mwaka 2002 kulikuwa na mgawanyiko wa idadi ya watu kiukabila kama ifuatavyo 16.9% Baganda, 9.5% Banyankole, 8.4% Basoga, 6.9% Bakiga, 6.4% Iteso, 6.1% Langi, 4.7% Acholi, 4.6% Bagisu, 4.2% Lugbara, 2.7% Bunyoro 29.6% makabila mengine madogo madogo.
Kwan chi kama hii pia kuna uwezekano mkubwa sana wan chi kutawaliwa kiukabila.
TANZANIA:
Nchi ya Tanzania, kuna jumla ya makabila yasiopungua 120, hii ni idadi ambayo tunafundishwa mashuleni, lakini ukiangalia kwenye encyclopedia tunakuta kuna makabila yapatayo 210. Hayo makabila yote yameungwanizwa na lugha moja ya Kiswahili. Unaweza kuona ajabu ni vipi makabila yote hayo kuweza kuunganishwa na lugha moja ya Kiswahili? Jibu ni rahisi sana.
Kwanza kabisa, muingiliano wa kibiashara kati ya makabila na makabila ni mkubwa, na walipokuja wafanyibiashara wa kutoka mashariki ya kati, waliweza kuwasiliana na wenyeji kwa kutumia lugha zao na za wenyeji, na kuzaa lugha moja ya Kiswahili, tunaweza kusema Lugha ya Kiswahili haina mwenye hati miliki nayo, kwa maana si ya kabila moja. Ni lugha ilojegwa kwa mchanganyiko wa makabila mbalimbali ya Kibantu, Kiarabu, Kifursi, kihindi, Kipotogizi (Kireno), Kiingereza, Kidachi na hata Kichina. Kiasi ya kwamba ni rahisi sana kwa mtu kuzungumza bila kujiona kuwa anajipendekeza kwa kabila fulani.
Ulipokuja utawala wa Kijerumani, wao waliendeleza kutumia Lugha ya Kiswahili kwenye mambo mengi ya wenyeji na kusomesha kwa lugha ya Kiswahi, alikadharika, nchi ilipokuwa chini ya usimamizi wa serikali ya Uingereza, lugha ya Kiswahili iliendelea kutumika kama ndio lugha ya mawasiliano kwenye kila nyanja, kuanzia serikalini, maofisini masokoni na sehemu mbalimbali za kijamii.
TAWALA ZA JADI
Wakati wa vuguvugu la kumkataa mkoloni na haswa kipindi cha utawala wa Mjerumani, tunaona kuwa makabila mengi yaliweza kujiunga pamoja katika kupiga vita utawala wa Mjerumani, kwa mfano, Mkwawa aliweza kuunganisha makabila yote ya Iringa, Mtemi Mirambo wa Tabora, aliweza kuunda jeshi alilo liita, Warugaruga, ili ni jeshi ambalo lilikusanya vijana kutoka makabila mbali mbali kama vile, Wangoni, Wahehe, Wanyanyembe, Wanyamwezi n.k
Chief Mirambo, mtawala wa kabila la Wanyamwezi mwaka 1870-1881 alikuwa ni mtawala mwenye nguvu sana, utawala wake ulienea kuanzia Urambo, Tabora, Pwani ya ziwa Tanganyika, Iramba, Mwanza Mpaka mipaka ya Uganda. Na kwa upande mwingine alikuwa akisaidiwa na Sultani wa Zanzibar, Utawala wake ulikuwa na nguvu kiasi cha Wakoloni kumwita kwa jina la Napoleone wa Afrika ya Kati, lugha iliyo waunganisha ilikuwa ni Kiswahili.
Mwimbo maarufu wa chama cha Tanu, ...Eeeh TANU yajenga nchi! Umetokana na Wimbo wa Jeshi lake, Ukiimbwa Eee Chuma Chavunja Vichwa. Askari hao wote waliunganishwa na lugha moja ya Kiswahili.
Ukija kwenye vita vya Majimaji July 1905 - July 1908, tunakuta hali ni ileile tu, makabila ya kusini mwa Tanganyika yaliunganishwa na Kinjikitile Ngwale "Bokero" kupambana na serikali ya Mjerumani. Makabila ambayo yanajulikana kwa majina ni Wamatumbi, Wangoni, Wangindo na makabila mengine ya kusini mwa Tanganyika. Uhasi huu wa kumpiga Mjerumani ulikuwa mkubwa kiasi cha serikali ya Mjerumani kuagiza askari wa ziada kutoka kwenye koloni lao linguine uko New Guinea. Makabila haya yote yaliunganishwa na lugha gani, kama si Kiswahili?
Vilevile tunapaswa kuelewa kwamba, watawala wote walopata kuitawala Tanganyika, hawakuwa na nia ya kuitawala milele, labda Mjerumani alikuwa na nia hiyo, lakini aliponyang'anywa Tanganyika kutokana na kushindwa kwake vita kuu ya dunia. Nchi ilikabidhiwa kwa Muingereza, kwa maana itapofikia mahala Watanganyika wanaweza kujitawala basi wapewe nchi yao.
Hii pia ilichangia sana kwa Muingereza kutowekeza sana katika nchi kwa kuwa alijuwa si muda mrefu utawala wake utakoma, kwa jinsi hiyo hakuwalazimisha wenyeji au wakaazi wa Tanganyika kuzungumza Kingereza au kuwalazimisha kama zilivyo nchi nyingine zilizotawaliwa na Muingereza.
Mfano mmoja wapo nchi kama Nigeria, Kenya, Zimbabwe, Ireland, na nyingine ambazo Muingereza aliondolewa kwa mapigano alikuwa na nia ya kuzitawala milele nchi hizo ndio maana utakuta lugha kuu ni Kiingereza, hii ni tofauti na Tanganyika, kwa sababu Muingereza dhamira yake ilikuwa si kutawala daima au kwa muda mrefu sana, tofauti na zile nchi ambazo alikuwa na nia ya kukaa muda mrefu kama sio milele kwa hiyo alikuwa anawaandaa wananchi kuijuwa lugha ya kiingereza ili iwe rahisi kwao kuwatawala, hii ni tofauti na Tanganyika, maana waliendelea kukitumia Kiingereza kidogo na Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano.
Na hata tulipo pata uhuru, mwendelezo ulikuwa ni huo huo, haikuwa rahisi, kukiwacha Kiswahili na kukumbatia Kiingereza pekee au lugha za Makabila, kwa sababu hakuna kabila ambalo lingeweza kuwa kubwa kiasi cha kuweza kuwekeza katika lugha za kimawasiliano zaidi ya Kiswahili. Na hata mkoloni hakuweza kuandaa baadhi ya makabila kuja kutawala kwa manufaa yao kwa sababu hakuna kabila kubwa kiasi cha kutosheleza Nyanja zote za kitaifa zaidi ya kukitumia Kiswahili.
Kwa hali hiyo Kiswahili kikabakia kuwa ndio Lugha kuu pekee ya mawasiliano mpaka leo hii.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?