Sunday, 11 December 2016

WAISLAMU, TUTAENDELEA KUTUKANANA NA
KUKASHIFIANA MPAKA LINI!?
KWANINI WAISLAMU HATUHISHIMIANI!?

Linapokuja swala la kujadiliana mambo mbalimbali katika Uislamu aidha mambo ya Kisharia au mambo ya Akida na mambo mengine kadhaa wa kadhaa, baina ya Waislamu, mara nyingi kumekuwa na kutawaliwa na Kashfa, Kejeli na matusi baina yetu.

Inafikia mpaka kuitana majina kama vile Makafiri, watoto wa Ibilisi na maneno kadhaa yasiopendeza... Kiasi nakumbuka maneno ya Muislamu mmoja mwenyeji wa Japan akinukuliwa akisema...

Namshukuru Allah niliujua Uislam kabla sijajua matendo ya Waislamu.
Waislamu yahitaji kuzinduka. Tuziache ikhtilafu zetu ndogo ndogo kuwa ndiyo sababu ya kutugawa na kudhoofisha umoja wetu. Kama kulikuwa na wakati ambao Waislamu walihitaji umoja na mshikamano basi huu ndio wakati wenyewe.

Tatizo tulilonalo ni kubwa sana, badala ya sisi kufuata mwenendo mwema wa hao waliotutangulia, kisasi wakatuachia athari njema, sisi tumeamua kuwazidi wao maarifa zaidi kiasi cha sisi kujiona kuwa tuna akili nyingi kiasi cha kushambulia milango ya fahamu zetu n kupelekea kutokuwa na hikma wala busara za kimazungumzo.

Akili zetu upanda na kujiona kuwa sisi ni malaika kiasi tukajikweza na kujiona kuwa tuna haki ya kila jambo na kuwapa watu kile ambacho sisi tunaona kinastahili kwa muda na wakati ule, aidha tutagawa pepo kwa wale tuwapendao na kutuunga mkono au kuwatia motoni wale wasiokubaliana na sisi hata kama wapo kwenye haki.

Sisi tumekuwa zaidi ya maulamaa maana tuna akili sana kiasi cha kushadidia mambo mpaka tunajisahahu kuwa hao tunao washadidia ni Waislam na wanastaili hishma na staha kama zinavyo stahiki nafsi zetu.

Hakika tumefanikiwa katika ili la kutopendana na kuhishimiana, tumefanikiwa kueneza chuki miongoni mwa jamii za Kiislam kiasi tumekuwa mbilikimo wa kifikra (intellectual dwarf), tumefanikiwa katika kugawanyika miongoni mwetu na sasa tupo zaidi Kimakundi, na wale ambao hawapo kwenye makundi au jumuiya yetu basi huyo si mwenzetu.

Tabia hizi kwa kweli zimemea kwenye nafsi zetu na zimendoa mafungamano ya kirafiki na kindugu na kusababisha majadiliano yetu hukosa busara na hikma kiasi cha kupelekea kwenye utengano na uhasama ambao tunaweza kuuepuka.

MwenyeziMungu anatuambia kupitia Qur'an tukufu kuwa:
Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa MwenyeziMungu na Mtume, ikiwa mnamuamini MwenyeziMungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
Qur'an An-Nisaa 4: 59

Na Mtume Muhammad (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) anatuambia kuwa...
"Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuoneana kwao huruma na kusaidiana kwao ni mfano wa kiwiliwili. Kinapopatwa na maradhi sehemu moja basi mwili wote hukesha kwa maumivu na machovu".
(Bukhari na Muslim)
Lakini aaaah! Wapiii yote hayo hatuyataki, tunacho kitaka ni kile tu tukitakacho sisi wenyewe ambacho si kingine zaidi ya kutukanana, kukashifiana na kuvunjiana adabu, huo ndio Uislamu wetu mpya wa zama hizi za Sheikh Gugo Ibn Intanetii Bin Midia Bin Wasab ibn Fasibuk!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!