Wednesday 25 April 2018


JAMHURI YA MUUNGANO YA
TANGANYIKA NA ZANZIBAR
TANZANIA

JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIA

Tanzania ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki. Imepakana na Uganda na Kenya upande wa kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki, Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa kusini, Kongo, Burundi na Rwanda upande wa magharibi.

Eneo lina kilometa za mraba 947,303 (nchi ya 31 duniani); maji ya ndani yanachukua asilimia 6.2. Idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 walikuwa 44,928,923 (nchi ya 30 duniani) kutoka 34,443,603 waliohesabiwa katika sensa ya mwaka 2002.
Msongamano ni wa watu 47.5 kwa km2 (nchi ya 124 duniani).

Tanzania ni nchi kubwa zaidi kati ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Mji mkuu ni Dodoma (wenye wakazi 410,956), lakini rais bado yupo Dar es Salaam, jiji kubwa zaidi, lenye watu zaidi ya milioni 4,364,541.

Miji mingine ni kama vile Mwanza (706,543), Arusha (416,442), Mbeya (385,279), Morogoro (315,866), Tanga (273,332), Kahama (242,208), Tabora (226,999) na Zanzibar (223,033).

JIOGRAFIA

Nchi iko katika eneo la Maziwa makubwa ya Afrika, hivyo maziwa yanafunika km2 61,500, yaani 6% za eneo lote la nchi.
Pia ina mito mingi ambayo inaelekeza maji yake katika Bahari ya Hindi mashariki mwa nchi, lakini mingine inachangia Mto Zambezi kupitia Ziwa Nyasa, michache Bahari ya Kati kupitia Ziwa Victoria na mto Naili, mingine tena Bahari Atlantiki kupitia Ziwa Tanganyika na mingine inaishia katika mabonde kama ya Ziwa Rukwa.

Karibu thuluthi moja ya nchi inalindwa kwa namna moja au nyingine: kuna Hifadhi za Taifa 16, mbali ya Hifadhi Teule, Hifadhi za Mawindo, Mapori ya Akiba n.k.

HISTORIA FUPI

Jina "Tanzania" limeundwa kutokana na majina ya TANganyika na ZANzibar (pamoja na athira ya jina la kale la "AzanIA").
Nchi hizo mbili zilikuwa zote chini ya utawala wa Uingereza hadi kupata uhuru lakini hazikuwa makoloni ya kawaida.
Zanzibar ilikuwa na hali ya nchi lindwa kutokana na mikataba kati ya masultani wa Zanzibar na Ufalme wa Muungano (Uingereza).
Tanganyika iliwahi kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia halafu ikawa chini ya Uingereza kama eneo la kudhaminiwa kutokana na azimio la Shirikisho la Mataifa lililoweka Tanganyika katika ngazi "B" ya maeneo ya kudhaminiwa.

Tanganyika na Zanzibar zilikuwa nchi mbili tofauti hadi 1964, zilipoungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapo kiongozi wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kuwa Rais wa kwanza na kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar Abedi Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Tanzania, chini ya Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania na kuanza mpango wa kurekebisha uchumi kuendana na masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (1995-2005) aliendeleza mfumo wa uchumi wa soko huria ambapo mashirika ya umma yanabinafsishwa.
Tarehe 21 Desemba 2005 Jakaya Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa nne wa taifa (2005-2015), naye aliendeleza sera za watangulizi wake akitokea chama hichohicho cha CCM.

Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa rais wa awamu ya tano, John Magufuli (wa CCM vilevile).

MIUNDO YA MUUNGANO

Tangu muungano wa Tanganyika na Zanzibar kufanyika mwaka 1964 Tanzania imekuwa na miundo ifuatayo:
• Nchi inatawaliwa na serikali ya muungano ikitekeleza sheria zinazotolewa na bunge la Tanzania.
• Tanganyika au Tanzania bara haina serikali wala bunge la pekee.
• Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) ina serikali na bunge lake vinavyoratibu mambo yasiyo ya muungano.

MAMBO YAFUATAYO YAMEKUBALIKA KUWA SHUGHULI ZA MUUNGANO:

• Mambo ya Nje
• Jeshi
• Polisi
• Mamlaka ya Dharura
• Uraia
• Uhamiaji
• Biashara ya Nje
• Utumishi Wa Umma
• Kodi ya Mapato, Forodha
• Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu.

UTAWALA

Muundo wa uongozi na utawala katika kipindi cha ukoloni ulizingatia mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola yaani utawala, bunge na mahakama.

Mgawanyo huu umeainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 4(1).

Tangu uhuru, mgawanyo wa madaraka na uhusiano miongoni mwa mihimili hiyo uliimarishwa ipasavyo kwa kuzingatia wakati, mahitaji ya demokrasia na misingi ya utawala bora.

Mgawanyo wa kiutawala wa Tanzania unafuata Katiba ya nchi I 2.2. Tanzania imegawiwa kwa mikoa 31. Kila mkoa huwa na wilaya ndani yake. Jumla ya wilaya ni 169, ambazo kati yake 34 ni miji.
Ndani ya wilaya kuna ngazi za tarafa (division) na kata (ward).
Chini ya kata kuna vijiji na wakati mwingine ngazi ya chini tena ambayo ni vitongoji.

WATANZANIA

Watu wa Tanzania hawaenei sawasawa. Katika maeneo makavu sana, kwa wastani kuna mtu mmoja tu kwa kilomita ya mraba (1/km²), lakini sehemu zenye rutuba za bara, kuna watu 51 kwa kila kilomita ya mraba. Hatimaye huku Unguja kuna watu 134 kwa kilomita ya mraba na katika Mkoa wa Dar es Salaam ni 3,133 kwa kilomita ya mraba. Asilimia 70 hivi huishi vijijini.

MAKABILA YA TANZANIA

Jamii nyingi za watu zimeishi na kushirikiana katika eneo la Tanzania bara kwa milenia nyingi. Kati ya jamii hizo, nyingi zilikuja kutoka maeneo mengine ya Afrika.

Nyingi katika jamii zilizohamia sehemu hii ziliingia katika makundi madogomadogo kwa amani, ingawa ziko zilizoingia kwa njia ya uvamizi na vita. Baadhi ya jamii zilizovamiwa zilijihami na kuwazuia wahamiaji wasiendelee kuteka maeneo mengine.

Kufikia mwaka 1884, wakati Wajerumani walipoanza harakati za kufanya sehemu hii ya Afrika kuwa koloni lao, kulikuwa na makabila zaidi ya 120 katika eneo la Tanzania bara.

Kuna makabila 125 hivi. Makabila yenye watu zaidi ya milioni moja ni Wasukuma, Wanyamwezi, Wachaga, Waha, Wagogo, Wahaya, Wajaluo na Wamakonde.

Jambo la pekee kuhusu jamii zilizoishi na zinazoendelea kuishi Tanzania ni kwamba wakazi asili wanawakilisha makundi yote makuu manne ya lugha barani Afrika.

1. Idadi kubwa sana ya Watanzania ni wa jamii ya Wabantu (k.m. Wazaramo, Wagogo, Wasukuma, Wahaya, Wachaga, Wapare na Wapogoro).
2. Nje ya hao, kuna Waniloti, kwa mfano Wamasai na Wajaluo ambao wengi wao zaidi wanaishi Kenya.
3. Kundi lingine ni makabila ya Wakushi wanaoishi kaskazini mwa Tanzania; hao ni makabila ya Wairaqw, Wafiome na Wasi.
4. Kuna vikundi viwili vya Wakhoisan wanaofanana na makabila ya Botswana na Namibia; majina yao ni Wasandawe na Waburunge.

Hatimaye kuna Wahadzabe wachache ambao utafiti wa DNA umeonyesha hivi karibuni wana uhusiano wa asili na Watwa wa nchi za Afrika ya Kati.

Pia kuna asilimia ndogo ya watu wenye asili ya nje ya bara la Afrika, kwa mfano Wahindi, Waarabu, Waindochina, Wafarsi, Wachina na Waingereza. Hii ilisababishwa na karne za mchanganyiko wa mahitaji ya biashara yaliyofanywa na mabara ya Ulaya na Asia hapo Afrika.

LUGHA

Nchini Tanzania kuna lugha za kikabila zaidi ya mia moja na ishirini, kwa kuwa kila kabila lina lugha yake.

Kiswahili ndiyo lugha ya taifa na inazidi kuwa lugha mama kwa watoto wengi, hasa mijini. Walau asilimia zaidi ya 90 za wakazi wanakitumia walau kama lugha ya pili. Kiswahili ni mojawapo kati ya lugha za Kibantu: hii imesaidia sana kukubaliwa kwa Kiswahili nchini, kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania ni wasemaji wa lugha za Kibantu. Kiswahili kinatumika kama lugha baina ya watu wa makabila mbalimbali na kwa mambo rasmi; kwa hiyo ni lugha rasmi ya dhati.

Baada ya uhuru, Kiingereza (iliyokuwa lugha ya kikoloni kabla ya uhuru) iliendelea kutumika kwa mambo kadhaa rasmi na kwa elimu kuanzia sekondari ingawa sera mpya inataka Kiswahili kishike nafasi yake hadi chuo kikuu; kwa hiyo ilichukuliwa kama lugha rasmi ya dhati pamoja na Kiswahili. Lakini utumizi rasmi wa Kiingereza umepungua katika milongo iliyopita, na sasa utumizi huu karibu umekwisha. Kwa hiyo siku hizi ni kawaida zaidi kuchukulia Kiswahili kama lugha rasmi ya dhati pekee.

Sera mpya ya elimu inakusudia kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote kufikia mwaka 2024.

DINI

Nchi haina dini rasmi na katiba ya Tanzania inatangaza uhuru wa dini kwa wote. Mara nyingi idadi ya wafuasi wa dini hutajwa kuwa theluthi moja Waislamu, theluthi moja Wakristo na theluthi moja wafuasi wa dini za jadi. Lakini tangu uhuru swali la dini ya wananchi halijaulizwa tena katika sensa, kwa hiyo kadirio la theluthi-theluthi inawezekana ni zaidi azimio la kisiasa. Kwenye visiwa vya Zanzibar idadi ya Waislamu huaminiwa kuwa takriban 97%

URITHI WA DUNIA

Mahali pafuatapo katika Tanzania pamepokewa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia".
(mwaka wa kukubaliwa - jina la mahali)
1979 – Hifadhi ya Taifa Ngorongoro
1981 – Hifadhi ya Serengeti
1981 – Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara
1982 – Hifadhi ya Taifa Selous
1987 – Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro
2000 – Mji Mkongwe wa Jiji la Zanzibar / Unguja
2006 – Michoro ya Kondoa

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!