Wednesday, 20 March 2019

Ule Uhasama Kati ya CCM na CUF, Usije Ukawa wa Vyama Vitatu, CCM, ACT na CUF

Kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, historia inaonyesha kwamba, uko Zanzibar kulikuwa na mizozano mikubwa ya kisiasa baina ya vyama vikubwa vya kisiasa, yaani ASP na ZNP (Hizbu).  Mizozano hii ilijiri kati ya miaka 1955 mpaka1964, ilipoamuliwa kuwa na chama kimoja tu cha siasa uwamuzi ambao ulizima migawanyiko ya kisiasa ndani ya visiwa vya Zanzibar baada ya mapinduzi.

Makovu yale yaliotokana na chuki kati ya Wazanzibar wenyewe si kwamba yalikuwa yamepona kabisa, lahasha, ndani ya makovu yale kulikuwa na vidonda vibichi, vilivyokuwa vikifukuta kama shaba iliyoyayushwa.

Mfumo wa vyama vingi uliporuhusiwa tena na 1995 uchaguzi ulipo fanyika na CCM kuchukua ushindi, makovu yale ambayo yalizaniwa kuwa yamepona kabisa, yalitumbuka upya na kuwa vidonda vipya, uhasama mkubwa ukarejea upya kiasi cha kusababisha chuki kubwa baina ya ndugu wa familia moja kutoshirikiana katika shughuli za kijamii, kama harusi na misiba na mambo mengine kadhaa.

Hali ilikuwa mbaya zaidi kisiwani Pemba, maana walibaguana katika misiba, sherehe, vyombo vya usafiri na biashara, jambo ambalo lilidhorotesha maendeleo visiwani humo.

Matukio ya watu kuvamiwa na kupigwa, wananchi kususa kununua bidhaa za wafuasi wa chama kimoja, mabasi kukosa abiria au abiria kushushwa kwa sababu ya tofauti za kiitikadi, kususia kushiriki katika maziko na harusi yalitawala kwenye kisiwa hicho ambacho ni moja ya visiwa vikubwa viwili vinavyounda Zanzibar.

Mpaka kufikia mwezi Julai 31 ya mwaka 2010, baada ya kura ya maoni ya kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa, uhasama na chuki baina ya wapenzi wa CUF na CCM, ukawekwa kando.

Hizi zilikuwa ni juhudi za viongozi wawili, aliekuwa rais wa Zanzibar Amani Karume na katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamadi walipohamua kuwa sasa inatosha na kwa kupitia vyama vyao (CCM na CUF) waamua kuwe na Maridhiano na Serikali ya umoja wa kitaifa ikaundwa.

Tukashuhudia utulivu, amani na upendo vikirejea tena miongoni mwa Wazanzibar wenyewe na maisha yakawa yenye utulivu, japokuwa si wote walilifurahia hili, maana kulikuwa na matukio ya hapa na pale kuonyesha kuwa si shwari kama inavyo onekana.

Nakumbuka vurugu kubwa zilizotokea mwezi May mwaka 2012, pale Jumuiya ya Uamsho ilipohusika na kuwachochea vijana kukusanyika na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma moto gari, kupanga mawe barabarani na kufanya hujuma mbali mbali kinyume cha sheria.

Chanzo cha vurugu zile zilitokana na wanaharakati hao kufanya maandamano makubwa ya kushtukiza ambayo yalizistua mamlaka za usalama visiwani humo, lakini baada ya kutawanyika jioni yake baadhi ya viongozi wa maandamano hayo walitiwa mbaroni.

Hayo twaweza sema yalishapita, maana kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema hivi; "Yaliopita si ndwele, tugange yajayo".

Wasiwasi wangu ni huu mgawanyiko uliotokea hivi karibumi, kwa baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF, walipoamua kujiunga kwenye chama cha ACT, baada ya upande unao ongozwa na Pro. Lipumba kushinda kesi iliyokuwa inawakabila baina ya wanao unga mkono upande wa Seif Sharifu na upande wa Pro. Lipumba.

Nachelea ule uadui uliokuwa baina ya CUF na CCM, ukawa baina ya ACT, CUF na CCM kwa mbali, binafsi naamini kwa dhati kabisa kuwa lolote litakaloamuliwa na viongozi hawa wa CUF na ACT wanachama watalifuata.

Tunarajia, ule uhasama uliokuwepo baina ya wanachama wa CUF na CCM kiasi cha kutoshirikiana katika shughuli za kijamii, usihamie kwa wanachama wa CUF na ACT na wala usibakie CCM, vyama vya kisiasa hisiwe sababu ya kuharibu udugu, urafiki na ujamaa baina ya wanachama wa pande zote.

Tusisikie tena wanachama wa chama kimoja aidha ACT, CUF au CCM, wanashushwa kwenye daladala au kutouziwa bidhaa ya aina yoyote wanapokwenda markiti au dukani.

Tusisikie tena mashamba kuvamiwa na mazao kuharibiwa kwa sababu za itikadi za kisisas au kufukuzwa kwenye nyumba au kuchomeana nyumba kwa kuwa tu, fulani ni CCM/CUF/ACT.

Tusisikie tena, habari za kupopolewa kwa mawe kwa viongozi wa kisiasa kama ilivyowahi kutokea walipo popolewa mawe Maalim Seif Hamad na Dk  Mohamed Shein. Nakumbuka misafara yote miwili ilishambuliwa jioni ambapo baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Naandika haya kwa sababu, kugawanyika kwao kisiasa kunawafanya Wazanzibari wasiweze kukubaliana kuhusu masuala nyeti yanayohusu mustakbali wao na wa vizazi vyao vijavyo...

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!