MPANGO KINA WA MIAKA 5 YA KUREKEBISHA VIJANA - Panya Road
An Extensive 5 Year Reforms Program for The Youth - Panya Road
- Hata Wafungwa Wanaweza Kufaidika Kwenye Programu Hii.
- Tuwatumie Panya Road, Kuimarisha Uchumi kwa Kutoa Mafunzo ya Uzalishaji, Ufundi na Kazi za Amali, Mila na Utamaduni na Uzalendo.
Haya Matukio ya Panya Road, yananikumbusha tukio moja
lililonitokea miaka mingi nyuma, zaidi ya miaka 40 hivi. Nakumbuka kushuhudia
jamaa ninaye mfahamu, akikimbizwa na umati watu, wakimtuhumu kukwapua pochi ya
mama mmoja, huku wakipiga kelele za mwizi.
Yule kijana alinipita mbio na huku akivua shati lake na
kuingia kwenye jalala la taka, na kujifanya kichaa huku akigaagalika kwenye
taka. Halafu aliniambia, “wakija waambie mwizi amepita.” Anamaliza kusema tu,
waliokuwa wakimfukuza walifika pale, wakitweta.
Kuna waliokuwa na mawe na vipande vya tofali, wengine
mapanga, marungu na silaha nyingine. Nilijua yule kijana alikuwa ni mwizi na
miaka ile kulikuwa na vikundi vya vijana wahalifu wakisumbua sana watu kwa
tabia zao za kukwapua kwapua watu.
Kidogo niwaambia wale watu, mwizi wao ndiye huyo hapo jaani.
Lakini kitu fulani kiliniambia niache, sikumbuki kama ni woga au huruma tu
iliyonijia, sikuwapenda wezi na pia sikupenda kuona wakiadhibiwa kwa kupigwa
mawe au kuchomwa moto.
Walipo niuliza nikawaongopea huku nimejawa na hofu kwa mbali
“Karuka huo ukuta, kadondokea upande wapili, kaacha shati lake hapa.”
Lile kundi hata sijui ilikuwaje, waliniamini, japo walikuwa
na wasiwasi kidogo kwa yule kijana aliyepo jaani, lakini walinisikiza na kuamua
kuondoka.
Yule kibaka, alinishukuru sana huku akinitaja kwa jina
langu, kumwangalia vizuri kumbe tunafahamina, tukiishi mtaa mmoja, japo yeye
alinizidi umri na hatukuwa marafiki, lakini kwa kule kutomchongea kwa wale
watu, kulimfanya anione kuwa mimi ni jirani mwema.
Yule kijana alikuja kuhama, sijui walihamia wapi, ila
ninachojuwa baba yake alikuwa ni mtumishi wa serikali, nadhani mzee wake
alipata uhamisho mkoani.
Baada ya miaka isiyopungu ishrini, nilikuja kukutana na yule
jamaa, mkoani Kigoma, keshakuwa mtu mzima, mwenye familia yake na uzuri zaidi
ni mfanyabiashara mkubwa tu, akimiliki duka la spea za magari na boti za uvuvi.
Alinikumbuka nami nikamkumbuka, akanikaribisha nyumbani
kwake, tukaongea mengi, akanambia kuwa hasingeweza kunisahau kwa sababu
niliokoa maisha yake, na tangia siku ile aliyokimbizwa nami nikamsaidia ilikuwa
kama ndio dawa, maana aliacha wizi, akajishughulisha na biashara na sasa
anajitegemea na ana familia ya watoto wawili.
Lengo hapa si kuwahadithia tukio la kibaka mmoja aliyepata
bahati ya kuokolewa miaka 40 nyuma, lahasha, ila nimekuwa najiuliza hivi awa
vijana tunao waita Panya Road, ni kweli hatuna suluhisho la kudumu? Maana wengi
wao ni vijana walio kati ya umri wa miaka 12 na 20 au 25 tu.
MPANGO WA KUWAWEZESHA PANYA ROAD
Binafsi natamani badala ya kuwafunga jela, tuwe na mipango
maalum ya kuwarejesha Panya Road kutoka kwenye maisha ya kudhuru watu, uraibu
wa dawa za kulevya na wizi na kuwageuza kuelekea kwenye maisha ya kawaida
kupitia mafunzo maalum.
Kuwafundisha Panya Road kulihudumia Taifa lao na kuwatumia
vijana hao katika kuwapatia mafunzo ya msingi ya kujiendeleza katika shughuli
za kilimo, viwanda, uvuvi, ufundi na kazi za amali. Kuwafunza elimu ya uraia,
Kuwafunza na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kijamii na utamaduni.
Mpango huu uwe wa miaka mitano (5), huu mpango utaratibu,
kusimamia na kuendesha mafunzo endelevu hivyo basi kupitia mpango huu vijana
hawa watajengeka kiuzalendo, wataweza kujitegemea na kujiamini.
Nakumbuka miaka ile kuanzia 1964 mpaka katikati ya miaka ya
70, serikali ya Tanzania ilikuwa mikakati ya kuwapeleka watu kwenye vijiji vya
ujamaa.
Najua kuwa kulikuwa na matatizo ya kiutendaji, ndio maana
jambo lile halikufanikiwa kama lilivyotarajiwa, lakini tunaweza kuchukua lile
wazo kisha tukawashirikisha wasomi na wanaharakati wakalikarabati na
kuliwasilisha tena, kisasa zaidi.
Kama vile serikali ilivyoanzisha JKT na baadae JKU kuwa ni
vyombo vya kuelimisha na kuandaa vijana wa Kitanzania kiuzalendo, kimaadili,
kinidhamu na kuwafanya raia wema wanaopenda kutumikia na kulinda nchi yao. Basi
kwa nia ileile na uthubutu uleule, tunaweza kuanzisha "MPANGO KINA
WA MIAKA 5 YA KUREKEBISHA VIJANA - PANYA ROAD" (AN EXTENSIVE 5 YEAR
REFORMS PROGRAM FOR THE YOUTH - PANYA ROAD), kiufupi MKKV-Panya Road
WIZARA ZA SERIKALI ZITOE WATAALAMU.
Mpango huu wa miaka mitano, MKKV-Panya Road, unaweza
kusimamiwa na wizara kadhaa, wakiongozwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya
Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo n.k.
Kwenye hizo kambi za kudumu, vijana wapewe mafuzo ya Stadi
za Maisha ya kujitegemea kinadharia na kivitendo, Kusoma, Kuandika, Kuhesabu na
utoaji wa elimu ya Msingi na Sekondari kwa ujumla wake.
Programu hii ya MKKV-Panya Road, pia ijumlishe kuwaandaa awa
vijana Kisaikolojia, Kuwapatia Elimu za Mafunzo ya Kilimo, Viwanda, Uvuvi,
Mapishi, Elimu ya Uraia na Uzalendo, Ufugaji, Ujenzi, Ufundi wa aina mbalimbali
kama vile Uashi, Useremala na Ukarabati wa magari, elimu za dini, utamaduni na
michezo.
Vilevile kuwepo wataalamu wa saikolojia na ushauri nasaha watakao
weza kuwashauri na kuwasaidia awa vijana katika masuala ambayo yamewafanya wawe
na tabia mbaya, ili kuwasaidia kuepukana na kurejea tena kwenye maisha ya
uhalifu. Na kuwabadirisha kuwa raia wema, wanaojiamini, wanaojituma, wenye
uzalendo na kuipenda nchi yao.
Kwa kushiriki katika programu hii ya MKKV-Panya Road, vijana
watapata fursa ya kupata ujuzi unaohitajika katika maisha yao na kuwa na
ujasiri na ushindani kwa taaluma yao baada ya kuhitimu.
Mbali na ujuzi wa kujifunza ili kuwa na nguvu kitaaluma,
vijana watajengeka kiuwezo na kujiamini na kuweza kuanzisha miradi yao wenyewe.
Vilevile itasaidia kuwabadirisha na kuwa raia wema,
wanaojiamini, wanaojituma, wenye uzalendo na kuipenda nchi yao.
NB:
Kama kutakuwa na kesi ya mauwaji kwenye uhalifu wa hao vijana, basi Sheria ichukuwe mkondo wake.Hili wazo ni kwa wale tu ambao hawana kesi za mauwaji.