HIVI KWELI NILIKUFA AU
NILIUWACHA TU UHAI KWA MUDA!?
- Naamini
Kabisa, Nilikufa Kwa Dakika Kadhaa, Ilikuwa ni Hali ya Kushangaza na
Kustaajabisha Mno!
- Ni Tukio Lililotokea Zaidi ya Miaka Kadhaa Nyuma, Kabla ya Mabasi ya Mwendokasi...
Siku hiyo ilikuwa kama siku zingine tu zisizo na majina, ile hamu ya katembea kwa miguu na ile taswira ya jiji la Dar, ilisawiri barabara kwenye bongo langu.
Kama kawaida ya mitaa mingi ya Kariakoo,
kumejaa watu wa kila aina. Nikapita kwenye mitaa iliyosongamana watu
nikishajika huku na kule, nikakumbuka kufuchama Rununu yangu, kwa kuchelea
wivi, wasijeichukua bila ruhusa yangu, huku sauti za wabeba mizigo kwenye
Rikwama, wakiyosayosa maneno ya kutiana nguvu.
Nikapishana na msukuma rikwama mmoja akanitolea maneno ya kuudhi, sikumjali! Upande mwingine kuna Bodaboda zinafukuzana, nikazikwepa nisipigwe dafrao...!
Huku nikijiwazia, "...hawa waendesha Bodaboda wamekuwa watu wa ajabu sana, ni watu wenye kudhania kuwa wao wana haki ya barabara na hata pembeni ya barabara kuliko mtu mwingine yoyote, na sheria za barabara haziwahusu..."
Ghafla bin vuu..! Nikajikuta napaa hewani, usawa wa futi kadhaa, nikabakia naelea hewani, huku makelele ya watu na kina mama wakiwa kwenye shake kubwa... "Mtumeee...! Kashauwa, Tobaaa yaillahi kijana wa watu..."
Sikumbuki ni nini kilitokea, ila nilicho kiona mpaka leo nikikikumbuka naingiwa na shakawa kubwa yenye kutetemesha mwili wangu na moyo kuingiwa na hofu, kiasi cha kuunyogesha.
Tahamaki nikaona watu kwenye tahanani, huku wametaharuki, wakijikusanya kumzunguka mtu aliyelala pembeni mwa barabara, nikamsikia mdada mmoja akisema, "…Kagongwa na Bodaboda...!"
Kitu cha kwanza kunistaajabisha, ambacho mpaka leo sijui jinsi ya kukielezea wala kuolelezesha, ni ile hali ya utulivu na amani niliyokuwa nayo muda ule. Nilikuwa namuonea huruma kila mtu, kama vile wanapoteza muda wao tu hapa duniani.
Kitu cha pili ambacho kilishtua roho yangu, ni pale nami nilipotaka kujisogeza kuelekea kwenye akhlaki ya ule mkusanyiko... Badala ya kutembea nilikuwa kama mtu anae elea na kujisogeza mzima mzima, sikuwa nakanyaga ardhi, nilihisi wepesi ambao sijawahi kuupata kwenye maisha yangu.
Kuna kitu kilinipelekea nione upande wa machweo ya jua, nikaona viumbe visivyo elezeka, kama vile vinaashiria nisiende huko walipo... Sawia wengine wakiniita nielekee walipo wao, wakiwa upande wa Kaskazini wakiwa na maumbo yenye kupitisha mwanga, mfano wa Jeli...!
Matendo yote hayo yalitokea sanjari...! Nikastaajabia uwezo ule wa kuona pande zote bila kugeukageuka!
Ile hali kwanza haikujisajili kwenye bongo langu, ni mpaka pale nilipojisogeza kwenye lile kusanyiko. Nikapitiliza bila kugusana na mtu yoyote yule, ndipo hapo sasa mshituko mkubwa ulipo nipata.
Nilishuhudia mwili wa mtu ukiwa umelala pembeni karibu na mtaro wa maji, huku mtu mmoja Shaibu mwenye mwili wa ajabu, akijitahidi kushajiishika kutoa huduma ya kwanza, huku akiwazuiya vijana sefule mashakili, wasipenyeze vidole vyao kwenye mifuko ya suruali iliyovaliwa na ule mwili.
Nikamkumbuka yule Shaibu, ni mmoja wa wazee wa mitaa ya kule Gerezani, ni katika jamaa zetu, ananifahamu nami namfahamu, lakini jinsi alivyo kama vile yupo tofauti na watu wengine (Nilikuja Kufahamu Baadae, Kwanini Nilimuona yupo Vile).
Yule Shaibu, alikuwa akinihita kwa jina langu na lababa yangu (Fulani Bin Fulani), huku akishahiri watu wasimamishe gari waupeleke mwili hospitali. "...Simamisheni gari tumpeleke hospitali haraka, huyu bado mzima, mwili ungali moto, si wa ahera huyu..."
Nadhani watu wengine walimuona ni wa kawaida tu, la sivyo, asingesogea mtu karibu yake…!
Nikataka kumwambia kuwa nipo hapa, pembeni lakini sauti haikutoka, maana hata hao watu wengine, wakinipita bila kunikwepa, kama vile mtu anapishana na upepo...!
Ule Mwili Pale Chini, Ulikuwa Ni Mwili Wangu...!
Wakaunyanyua ule mwili na kuupakia kwenye gari la mizigo, Toyota Pickup, ajabu nyingine ni pale nilipo ona ule mwili umeunganishwa na nafsi yangu au sijui niseme ndio roho yenyewe (Wallahi hata sijui ni kitu gani), kimefanana na kama uzi mwembamba hivi wa ajabu, wenye rangi niseme kama nyeupe au rangi ya fedha pamoja na rangi ya Zambarau hivi lakini yenye kupitisha mwanga, kiufupi niseme kama uzi wa kioo wenye kumetameta, wenye kufanana na mwanga au umeme wa radi.
Uzi au kamba ile nyembamba sana ilikuwa imeniunganisha mimi na mwili ule, kupitia kwenye kitovu... Nikajikuta nipo sawia na mwendo wa gari.
Kupitia barabara ya Msimbazi, kisha barabara ya Uhuru, kuelekea hospitali ya Amana.
Yule Shaibu akaweka mkono wake mmoja kwenye kichwa cha ule mwili kwenye utosi, na mkono mwingine akashika vikidole gumba vya miguu wa kulia na kushoto, kisha akatamka shahada (la 'ilaha 'illa-llahu akitaja na majina mengine ya MwenyeziMungu, Ar-Rahmaan, Ar-Rahiim, Al-Aziiz, As-Samii, Al-Basiir, Al-Wahhaab, Al-Baasit, Al-Ghafuur, Al-Hafiidh, Al-Mujiib, Al-Waduud, Al-Ba’ith, Al-Mu’id, Al-Muhyii, Al-Hayy, An-Nur, Al-Barr, At-Tawwab, Al-‘Afuww, Dhul-Jalaali Wal-Ikraam, Mrejeshe… ).
Akabonyeza kwenye chembemoyo, kwenye
mbonyeo ulio baina ya gegedu la mifupa ya mbavu, katikati ya kifua cha mwili
ule (mwili wangu), kwa kidole gumba chake, kwa lengo la kusisimua mapavu na
moyo wa ule mwili, viweze kurejea kwenye kazi yake...!
Kila alipokuwa akikandamiza kifua cha
mwili ule baina ya gegedu na utosi, huku nami nikajikuta naukaribia ule
mwili...!
Ni kama vile alikuwa anavuta ule uzi ulioniunganisha mimi na ule mwili...!
Ghafla polepole nikaanza kuhisi kupotelewa na uwezo wa kuona na kusikia, sikusikia chochote, kama vile ninayepoteza fahamu na kuzama kwenye rima, lisilo na mwisho, macho hayakuona kitu... Huku ule uzi ukinivuta na mimi kwa haraka sana kama mtu anayevutwa na nguvu kubwa kelekea ulipo mwili wangu…!
Nilikuja kushituka nipo Hospitali ya Muhimbili, nilikuja kuambiwa kuwa, baada ya ile ajali, wasamalia wema, walinipeleka Hospitali ya Amana, kisha kuhamishiwa hospitali ya Muhimbili.
Uzuri vipimo vilionyesha kuwa sikuathirika sana, kule kupoteza fahamu ni baada ya kujipigiza kichwa kwenye lami.
Kumbe nilipoteza fahamu kwa siku mbili.
Siku ya tatu, baada ya kutoka hospitali, nilimuulizia yule mzee aliyenisadia (Nikamtaja kwa jina), nikaambiwa kuwa, uwenda nimemfananisha tu, maana huyo mzee mbona, alisha fariki siku nyingi sana, ni zaidi ya miaka kumi sasa tangia amefariki...! Kidogo nizimie tena...!
Ndugu zangu, kweli roho zipo, maana zile dakika kadhaa, niliona mengi sana, niliyaona yasioweza kuonekana kwa macho ya kawaida, MwenyeziMungu alifungua pazia la macho yangu ya rohoni, nikaona yasiyo onekana kwa macho ya kawaida.
Kiukweli wala sijui ni kwa jinsi gani naweza kuyahadithia mambo yale yote...!
Nilipotoka hospitali, nilikuja kutafuta kufahamu maana ya yale maneno ya Shaibu yule... Nikayaelewa...!
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?