Tuesday, 2 June 2026

 KIZAZI KINACHOTEKETEA

  • Janga la Kubeti Lawamaliza Vijana wa Tanzania
  • Nguvu Kazi Ya Taifa Iko Hatarini Tuchukue Hatua Sasa


UTANGULIZI.

TISHIO KUBWA KWA NGUVU KAZI YA TAIFA.

Karibu asilimia 74% ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 nchini Tanzania wameshishiriki katika shughuli za kubeti.

Katika miaka ya karibuni, kubeti au kamari kupitia michezo ya kubashiri kumeibuka kama moja ya changamoto kubwa zaidi kwa vijana barani Afrika, hususan nchini Tanzania. Jambo ambalo awali lilionekana kama burudani au njia ya kujipatia kipato cha haraka limegeuka kuwa janga la lisilo onekana kwa macho linalotafuna nguvu kazi ya taifa, kuathiri uchumi wa familia, na kusababisha madhara makubwa ya kiafya na kisaikolojia.

Kwa vijana wengi wanaokabiliana na ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama za maisha, na shinikizo la kijamii, kubeti huonekana kama “njia ya mkato” ya kutafuta mafanikio. Lakini ukweli mchungu ni kwamba michezo hii imekuwa mtego unaowanasa wengi na kuwaacha wakiwa wamefilisika, wakiwa na msongo wa mawazo, na wakipoteza dira ya maisha.

Suhala la kuzingatia hapa si kuchukulia kuwa kubeti ni burudani au biashara lahasha bali ni janga kubwa katika nchi yetu na inapelekea kupoteza kizazi kizima bila kuchukua hatua stahiki za kulitafutia ufumbuzi yakinifu.

Makala haya yanakusudia kuwaelimisha vijana, wazazi, na jamii kwa ujumla kuhusu hatari za kubeti ili tuweze kuchukua hatua za pamoja.

SABABU ZINAZOWASUKUMA VIJANA KWENYE KUBETI

Ukuaji wa kasi wa sekta ya kamari nchini haujatokea kwa bahati mbaya. Kuna mambo makuu manne yanayochochea kasi hii.

Vijana wengi hujiingiza katika kubeti kutokana na mambo yafuatayo:

1. Ukosefu wa Ajira, Fursa Rasmi na Kukata Tamaa.

Vijana wengi wanakosa ajira za kudumu au kipato cha kuaminika. Katika mazingira haya, kubeti huonekana kama mbadala wa kupata pesa za haraka, ingawa mara nyingi huishia kuwa chanzo cha hasara.

2. Ukuaji wa Teknolojia na Upatikanaji wa Tovuti.

Simu janja na intaneti vimefanya kamari kuwa rahisi kuliko wakati mwingine wowote na mahali popote. Kwa “click” chache tu, kijana anaweza kuweka dau hata akiwa darasani, kazini, au nyumbani. Tena hata bila kufikiria matokeo yake.

Programu kama Aviator na betting za michezo ya soka zimeenea sana.

3. Matangazo Yenye Ushawishi Mkubwa (Mbinu Chafu)

Kampuni za kubeti hutumia matangazo makubwa kwenye runinga, mitandao ya kijamii, mabasi, na hata kushirikiana na watu maarufu (wasanii wakubwa, wanamichezo mashuhuri) kama ndio mabalozi wao, ili kuaminisha jamii kuwa kubeti ni jambo la "kijanja" na lenye hadhi. Matangazo ya kuvutia, na ofa za “bonasi” yakionyesha ushindi mkubwa, maisha ya kifahari, na ndoto za mafanikio, zinazowashawishi vijana kuamini kuwa ushindi uko karibu na kushinda ni rahisi. Mara nyingi matangazo haya hayataji hatari zilizofichika.

4. Tamaa ya Utajiri wa Haraka

Kuna imani potofu kuwa kubeti kunaweza kumtoa mtu kwenye umaskini mara moja. Vijana wengi huingia kwenye mtego huu wakiamini “bahati” itawageukia, bila kutambua kuwa mfumo wa kamari umeundwa ili kampuni ndiyo ishinde zaidi.

Dhana potofu kwamba “leo nashinda milioni” inaenea sana. Hii inatokana na hadithi za watu wachache walioshinda, huku kushindwa kwa wengi kukifichwa.

MADHARA YA JANGA LA KUBETI KWA VIJANA.

Madhara ya kubeti ni makubwa na ya muda mrefu. Athari za kubeti hazishishii kwenye kupoteza fedha pekee; zinagusa kila nyanja ya maisha ya kijana na taifa kwa ujumla.

1. Uraibu na Afya ya Akili.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 23-31% ya wanaobeti huwa na uraibu.

Kubeti husababisha utegemezi wa kisaikolojia unaofanana na uraibu wa pombe au dawa za kulevya. Kupoteza fedha mara kwa mara huleta msongo wa mawazo, sonona, kukata tamaa, na wakati mwingine hata mawazo ya kujiua.

2. Kufilisika na Kuporomoka kwa Uchumi wa Familia.

Vijana wengi hupoteza akiba zao, mitaji ya biashara, fedha za matumizi ya kila siku, na hata ada za shule (Wanafunzi wa vyuo vikuu wamekuwa wakibeti kwa kutumia fedha za mikopo ya masomo (Boom) au ada, na kuishia kufukuzwa chuo).

Familia nyingi zimevunjika kwa sababu ya madeni na matumizi mabaya ya fedha kwenye kamari.

Kila mwezi, wanaopoteza takriban kati ya TZS 50,000 hadi 100,000 au zaidi.

3. Kuporomoka kwa Maadili na Uaminifu.

Ili kupata pesa za kubeti, baadhi ya vijana hujikuta wakiingia kwenye wizi, udanganyifu, uongo, na tabia nyingine zinazoharibu uhusiano wao na jamii. Kamari imekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia na kijamii.

4. Kupotea kwa Nguvu Kazi ya Taifa.

Badala ya kutumia saa 8 hadi 10 kwa siku kujifunza ujuzi mpya, kufanya kazi za uzalishaji (kama kilimo au ujasiriamali), au kusoma, vijana wengi hutumia saa nyingi wakichambua mikeka, kufuatilia uwezekano, au kutafuta dau la “kurejesha hasara”. Taifa hupoteza nguvu kazi yenye uwezo wa kuzalisha na kuleta maendeleo.

5. Athari kwa Familia na Jamii.

Migogoro ya kifamilia na hata ndoa, huongezeka kutokana na madeni, kutokuaminiana, na kushindwa kutimiza majukumu ya kifamilia.

UHALISIA USIOSEMWA
Ni muhimu kuelewa kuwa mfumo wa kubeti umejengwa ili kampuni zipate faida.
Kwa kila mshindi mmoja, kuna waliopoteza wengi zaidi.
Hii ina maana kuwa kubeti si njia endelevu ya kujipatia kipato ni mchezo wa hatari unaoweza kumwangamiza mshiriki.

NJIA ZA KUKABILIANA NA JANGA HILI.

Kushinda janga hili kunahitaji juhudi za pamoja kutoka serikali, jamii, na vijana wenyewe:

1. Marekebisho ya Sera na Sheria

Serikali inapaswa kuimarisha udhibiti wa michezo ya kubashiri, ikiwemo:

  • Kupunguza au kudhibiti matangazo ya kubeti

  • Kupunguza upatikanaji wa vituo vya kubeti karibu na shule, vyuo na makazi.

  • Kudhibiti matangazo yanayolenga vijana.

  • Kuweka ukomo wa umri na mifumo madhubuti ya uthibitishaji.

  • Pia, kuongeza kodi na kutoa sehemu ya mapato kwa programu za kuwasaidia vijana.

2. Elimu na Uhamasishaji.

Kuendesha kampeni kubwa kupitia mitandao ya kijamii, shule, vyuo, na nyumba za ibada kuhusu hatari za kubeti. Elimu ya fedha (financial literacy) iwe sehemu ya mtaala ili vijana wajifunze kuwekeza badala ya kubahatisha.

Jamii inahitaji kuelimishwa kuhusu:

  • Hatari za kamari.

  • Umuhimu wa kuweka akiba.

  • Njia salama za kuwekeza na kujenga uchumi binafsi.

Elimu hii inaweza kutolewa kupitia shule, vyuo, Misikiti, Makanisa, na Mitandao ya Kijamii.

3. Kuongeza Fursa za Ajira na Ujasiriamali

Serikali na sekta binafsi ziongeza fursa za ajira, mikopo midogo, na mafunzo ya ujasiriamali. Vijana wanapokuwa na njia halali za kupata kipato, hawatahitaji kubeti.

Serikali na sekta binafsi zinapaswa:

  • Mafunzo ya ujuzi wa ujasiriamali na ubunifu (skills training).

  • Kutoa mikopo nafuu na rafiki kwa vijana.

  • Mazingira rafiki ya kuanzisha biashara ndogo.

  • Kuwekeza katika ajira za kidijitali na viwanda vidogo.


Kadri fursa halisi zinavyoongezeka, ndivyo utegemezi wa kubeti unavyopungua.

4. Msaada wa Kisaikolojia na Kurekebisha Tabia

Kuwepo kwa vituo vya ushauri nasaha, vikundi vya msaada, na wataalamu wa afya ya akili kutasaidia vijana waliokwishaathirika kurejea katika maisha ya kawaida.

Pia, familia zifundishwe namna ya kutambua dalili na kutoa msaada.



5. Wajibu wa Familia na Jamii
Wazazi wafuatilie shughuli za watoto wao mtandaoni na kuwafundisha maadili ya kazi na uvumilivu. Vijana wenyewe waunde vikundi vya kusaidiana na kuepuka kubeti.



Wazazi, walezi, na viongozi wa jamii wanapaswa:

  • Kufuatilia mienendo ya vijana.

  • Kujenga mazungumzo ya wazi kuhusu fedha na maamuzi ya maisha.

  • Kutoa mifano bora ya matumizi ya fedha.

NINI KIFANYIKE KUKABILIANA NA JANGA HILI?

Kutokomeza janga hili kunahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa serikali, wazazi, viongozi wa dini, na wadau wote wa maendeleo kupitia hatua zifuatazo:


Sekta

Hatua ya Kuchukua

Serikali na Sera

Kuweka sheria kali za kudhibiti matangazo ya kamari kwenye vyombo vya habari (hasa nyakati za mchana), kuongeza kodi kwenye sekta hiyo, na kupiga marufuku vituo vya kubeti karibu na shule au makazi.

Taasisi za Fedha & Jamii

Kuanzisha kampeni za kitaifa za Elimu ya Utambuzi wa Kifedha (Financial Literacy) ili kuwafundisha vijana jinsi ya kuweka akiba, kuwekeza kwa usalama, na kuelewa hatari za kamari.

Uwezeshaji Kiuchumi

Kuongeza kasi ya ubunifu wa fursa za ajira na kurahisisha upatikanaji wa mikopo isiyo na masharti magumu (kama ile ya 10% ya Halmashauri) ili vijana wapate mitaji ya kufanya shughuli halali.

Afya na Jamii

Kuanzisha vituo vya ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia (Rehabilitation Centers) mahususi kwa ajili ya kuwasaidia vijana waliathirika na uraibu wa kamari ili kuwarudisha kwenye mstari.



WITO KWA VIJANA
Kijana, thamani yako si tiketi ya kubeti.
Ndoto zako haziwezi kujengwa kwa bahati nasibu, zinahitaji juhudi, maarifa, na uvumilivu.

Chagua kujifunza ujuzi.
Chagua kujenga kesho yako.
Chagua kujithamini zaidi ya dau.

HITIMISHO

Janga la kubeti si suala la mtu mmoja, ni changamoto ya kijamii, kiuchumi, na kimaadili inayohitaji nguvu ya pamoja. Vijana ndio nguvukazi ya taifa; wakipotea, taifa linapoteza mustakabali wake. Ni wajibu wa wazazi, walimu, viongozi wa dini, serikali, na vijana wenyewe kusimama kidete kupambana na wimbi hili.

Kubeti si njia ya mafanikio. Ni mtego unaovunja ndoto, unaopoteza muda, na unaoharibu maisha. Taifa lenye vijana wenye dira, nidhamu, na ujuzi ndilo taifa lenye matumaini.

Ni wakati wa kuchukua hatua. Serikali viongozi wa dini, wazazi, na jamii tuungane kukabiliana na janga hili kabla halijaharibu kizazi kizima.

Ni lazima vijana wa Tanzania watambue kuwa "Kampuni ya Kubeti Haishindwi Kamwe" (The house always wins).

Kampuni hizi hazipo kwa ajili ya kuwaondoa vijana kwenye umaskini, bali zipo kwa ajili ya kutengeneza faida kubwa kutokana na upotezaji wenu.

Tuwekeze katika akili na mikono yetu, si katika bahati nasibu.

Wakati wa kuchukua hatua ni sasa.

Ssmbaza makala hii kwa vijana wengi iwezekanavyo. Pamoja tunaweza!

Tanzania yenye nguvu inaanzia kwa vijana wenye maamuzi sahihi.

#KataaKamari #ChaguaKaziSioKamari #OkoaNguvukaziYaTaifa #VijanaNaUzalishaji #TanzaniaBilaKubeti #BettingNiJanga #NguvuKaziYetu #AchaKamari




---

SOURCE

  1. NASAHAZETU
  2. Qur'an2:219.Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri
  3. Qur'an 5:90 - 91 Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha?

  1. TheBetting Industry in Tanzania December 7, 2025
  2. Casestudy of Gallapo ward in Manyara Region


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!