WANAOREJESHWA NCHINI - TANZANIA
JE, SERIKALI IMEJIANDAA KWA MAISHA YAO BAADA YA REPATRIATION?
Kwa nini kurejeshwa kwa Watanzania kutoka Afrika Kusini kusibaki tu kuwa safari ya kurudi nyumbani, bali iwe mwanzo wa mpango wa ajira, biashara na Reintegration.
Habari rasmi zinaonyesha Serikali ya Tanzania imepanga kuwarudisha kwa hiari takriban raia 669 kutoka Afrika Kusini kutokana na hali ya chuki (xenophobia) dhidi ya wageni. Kundi la kwanza la vijana (karibu 173 kutoka KwaZulu-Natal/Durban) walirudishwa mwishoni mwa Agosti 2026 kwa ndege maalum, na mipango iliyopo ni kuwarudisha wengine kutoka miji ya Cape Town (karibu 300) na Johannesburg kufikia jumla ya raia 669.
Wengi wao walikuwa wameishi huko kwa muda mrefu, baadhi wakiwa na ujuzi, elimu, au biashara ndogondogo. Kurudi kwao si jambo rahisi wameacha shughuli zao za kijamii, wateja, na maisha waliyoyajenga na sasa yamekatishwa ghafla.
Kwenye mitandao ya kijamii, kulionyeshwa video ya vijana wakiwa kwenye ndege wakirejea nyumbani, Tanzania. Kama ilivyo ada ya Watanzania haswa kwenye mitandao ya kijamii, gumzo likawa kubwa, wengi wakaonyesha wasiwasi wao kuwa hao vijana wanaweza kuongeza wimbi la uharifu, mitaani.
Wasiwasi wao una msingi mkubwa na unagusa eneo nyeti la usalama na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kurudi kwa idadi kubwa ya vijana kwa wakati mmoja ambapo baadhi yao walijihusisha na matendo ya kiuhalifu na wengine walikuwa katika sekta isiyo rasmi kunahitaji mbinu za kimkakati ili kuzuia viashiria vya uhalifu na badala yake kuwatumia kama fursa ya maendeleo.
Serikali imeeleza kuwa mpango huo ulitokana na maombi ya wananchi wenyewe waliotaka kurejea Tanzania kwa hiari.
Kwa hiyo, si sahihi kuwatazama watu hawa wote kama "tatizo" au kuwaita wahalifu.
Hata hivyo, ni sahihi kabisa kujiuliza kuhusu maisha yao baada ya kurejea.
Kuna haja ya mpango endelevu lakini si kwa dhana kwamba vijana hawa ni wahalifu. Utafiti unaonyesha kuwa kurudi kwa watu, hasa vijana, kunaweza kuongeza shinikizo kwa jamii na kuongeza hatari ya kurudia makosa. Mataifa mbalimbali yamekuwa yakikabiliana na changamoto kama hii kwa miaka mingi. Kama nchi kuna haja ya kuwa na mpango endelevu wa kuwarudisha na kuwaunganisha vijana hawa, hata kama idadi ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya vijana nchini.
Badala yake, mpango unahitajika ili kupunguza hatari za kijamii zinazoweza kujitokeza baada ya kurejea kwa idadi kubwa ya watu waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa kiuchumi na kijamii kwa muda mrefu.
Kurejea kwa Watanzania kutoka Afrika Kusini ni jambo la kibinadamu na la kitaifa linalopaswa kuungwa mkono. Raia anaporudi katika nchi yake, anapaswa kupokelewa kama sehemu ya jamii yake na kusaidiwa kuanza upya.
Lakini nyuma ya zoezi hili kuna swali ambalo Serikali inapaswa kujiuliza mapema:
Baada ya kuwarudisha nyumbani, tunawafanyia nini?
Swali hili si la kisiasa pekee. Ni swali la uchumi, ajira, ustawi wa jamii na, kwa kiwango fulani, usalama wa taifa.
1. KWANZA: TUSICHANGANYE KUREJEA KWAO NA UHALIFU
Kuna hatari katika mjadala huu ambayo lazima tuepukane nayo.
Kuwa mtu ametoka Afrika Kusini hakumaanishi kwamba ni mhalifu.
Kuwa mtu alikuwa akifanya biashara ndogo Afrika Kusini hakumaanishi kwamba atakuwa mhalifu Tanzania.
Na hata kama baadhi ya waliorejea wamewahi kuwa na matatizo ya kisheria, haiwezi kuwa sahihi kuwahukumu watu wote kwa kosa la wachache.
Kwa hiyo, mjadala wangu si kwamba:
"Vijana hawa watakapofika Tanzania wataongeza uhalifu."
Mjadala sahihi ni:
"Je, mazingira ya kiuchumi na kijamii baada ya kurejea yanaweza kuwaweka baadhi yao katika mazingira hatarishi?"
Hilo ni swali tofauti kabisa.
2. TATIZO LINAANZIA KWENYE MAISHA BAADA YA KURUDI
Fikiria kijana aliyekuwa Durban, Cape Town au Johannesburg kwa miaka kadhaa.
Huenda alikuwa:
Mfanyabiashara mdogo;
Fundi;
Dereva;
Mfanyakazi wa hoteli;
Mfanyakazi wa ujenzi;
Mfanyakazi wa dukani;
Mtoa huduma;
Au mtu aliyekuwa akifanya biashara isiyo rasmi.
Anaweza kuwa hakuwa tajiri, lakini alikuwa na chanzo cha kipato. Sasa anarudi Tanzania.
Anakuta:
Hana mtaji, hana biashara, hana ajira, hana makazi yake mwenyewe, na hana mpango wa kazi.
Hapo ndipo swali la sera linapoanza. Kumleta mtu nyumbani ni hatua ya kwanza.
Kumwezesha kuanza maisha upya ndiyo hatua muhimu zaidi.
3. TANZANIA TAYARI INA CHANGAMOTO KUBWA YA AJIRA KWA VIJANA
Hili ndilo linalofanya suala hili kuwa muhimu.
Utafiti wa Afrobarometer kuhusu vijana Tanzania unaonyesha kwamba asilimia 26 ya vijana walioulizwa walisema hawana ajira na wanatafuta kazi. Aidha, asilimia 66 ya vijana walisema wangependa kuanzisha biashara zao wenyewe. Utafiti huo pia unaonyesha kwamba vijana wanaona uundaji wa ajira kuwa mojawapo ya maeneo muhimu ambayo Serikali inapaswa kuyawekea kipaumbele.
Tanzania pia ina idadi kubwa ya vijana wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka. Afrobarometer ikinukuu makadirio ya World Bank, inaeleza kuwa takribani vijana 800,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Kwa hiyo, vijana 669 (0.083625%) wanaorejea si idadi kubwa ikilinganishwa na nguvu kazi yote ya Tanzania.
Lakini hiyo si hoja.
Tatizo ni mkusanyiko wa mahitaji.
Vijana 669 wanaweza kuwa watu 669 wenye:
Familia;
Watoto;
Madeni;
Mahitaji ya makazi;
Mahitaji ya ajira;
Mahitaji ya mtaji;
Na matarajio ya maisha.
Na kama kundi hilo halitakuwa na mpango wa kuingizwa tena katika uchumi, Serikali itakuwa imekamilisha sehemu ya kwanza tu ya kuwaresha nchini
4. HATARI KUBWA SI LAZIMA IWE UHALIFU INAWEZA KUWA KUKATA TAMAA
Hapa ndipo mjadala wa usalama unapaswa kuwa wa kitaalamu.
Katika jamii yoyote, vijana wanapokosa:
AJIRA + KIPATO + MWELEKEO + FURSA
Huongezeka mazingira ya hatari.
Si kwamba kila kijana asiye na ajira anakuwa mhalifu. Lahasha.
Lakini ukosefu wa fursa unaweza kumfanya mtu awe rahisi kuvutwa kwenye:
Biashara haramu;
Magenge;
Utapeli;
Matumizi mabaya ya dawa za kulevya;
au shughuli nyingine za uhalifu.
Kwa hiyo, kuzuia uhalifu hakupaswi kuanza pale mtu anapokuwa tayari amefanya kosa.
Kuzuia uhalifu kunapaswa pia kuhusisha kuzuia mazingira yanayoweza kuuchochea.
Hii ndiyo maana reintegration ni suala la usalama pia.
5. FURSA KUBWA AMBAYO TANZANIA INAWEZA KUITUMIA
Badala ya kuwaona vijana hawa kama mzigo, Tanzania inaweza kuwaona kama rasilimali watu.
Baadhi yao wameishi Afrika Kusini kwa muda mrefu.
Wameona:
Mifumo ya biashara;
Masoko;
Teknolojia;
Huduma;
Mbinu za ujasiriamali;
Mazingira ya ushindani;
Na namna biashara zinavyoendeshwa katika uchumi mkubwa zaidi wa afrika.
Kwa hiyo, swali lisikuwa:
"Tutawafanyia nini?"
Liwe:
"Tunawezaje kutumia ujuzi na uzoefu walioupata nje ya nchi kuendeleza uchumi wa Tanzania?"
Hapo ndipo tunabadilisha changamoto kuwa fursa.
6. PENDEKEZO: SERIKALI IANZISHE NRRP
Ningependekeza Serikali ianzishe mpango maalumu wa kudumu ambao unaweza kuitwa:
NATIONAL RETURNEE REINTEGRATION PROGRAMME - NRRP
Mpango huu usiwe kwa ajili ya kundi hili pekee.
Uwe mfumo wa kudumu kwa Watanzania wanaorejea kutoka:
Afrika Kusini;
Ulaya;
Mashariki ya Kati;
Asia;
na nchi nyingine.
Kwa sababu suala la kurejea kwa wahamiaji linaweza kuendelea kuwepo hata baada ya tukio hili.
7. HATUA YA KWANZA: "RETURNEE REGISTRATION & SKILLS MAPPING"
Kila anayerejea kwa hiari apewe nafasi ya kusajili taarifa zake za msingi.
Si kwa madhumuni ya kumchukulia kama mshukiwa. Bali kwa ajili ya kumsaidia.
Mfumo unaweza kurekodi:
Elimu
Ujuzi
Kazi aliyokuwa akifanya nje
Uzoefu wa biashara
Mtaji alionao
Eneo analotaka kuishi
Eneo analotaka kufanya biashara
Mahitaji ya ajira
Mahitaji ya mafunzo
Hii itawezesha Serikali kujua:
Tuna watu wangapi wenye ujuzi wa ujenzi?
Wangapi wana uzoefu wa biashara?
Wangapi ni mafundi?
Wangapi wana uzoefu wa hospitality?
Wangapi wanaweza kufanya kazi kwenye logistics?
Wangapi wana uwezo wa kuanzisha biashara?
Hapo ndipo data inakuwa sera.
8. HATUA YA PILI: KUWAPA "RETURNEE STARTER PACKAGE"
Kila mtu anayerejea asiishie kupewa usafiri wa kurudi. Apewe mpango wa kuanzia maisha mapya.
Kwa mfano:
Kwa wafanyabiashara
Mafunzo mafupi ya biashara;
Usajili wa biashara;
Elimu ya kodi;
Huduma za SIDO;
Upatikanaji wa mikopo midogo;
Kuunganishwa na taasisi za fedha.
Kwa mafundi
VETA;
Certification ya ujuzi;
Kuunganishwa na makampuni;
Apprenticeship;
Zabuni ndogo za ndani.
Kwa vijana wasiokuwa na ujuzi
Vocational training;
Digital skills;
Driving/logistics;
Hospitality;
Construction;
Agriculture;
Electrical;
Plumbing;
Welding
n.k
9. HATUA YA TATU: "R. E. F"
Hili linaweza kuwa mojawapo ya suluhisho bora zaidi.
Badala ya Serikali kutoa fedha bila mpango, ianzishe dirisha maalumu la uwezeshaji.
Mfano:
RETURNEE ENTERPRISE FUND
Mfuko huu unaweza kutoa:
Mikopo midogo;
Matching grants;
Vifaa vya kuanzia biashara;
Mafunzo;
Mentorship.
Lakini fedha zisitolewe kwa kila mtu kwa usawa. Zitolewe kulingana na mpango wa biashara. Kijana mwenye mpango mzuri wa biashara apewe nafasi ya kuutekeleza.
10. HATUA YA NNE: PRIVATE SECTOR LAZIMA IHUSISHWE
Hili si jukumu la Serikali peke yake. Sekta binafsi inaweza kuwa mshirika mkubwa.
Serikali inaweza kuingia makubaliano na:
Kampuni za ujenzi;
Viwanda;
Hoteli;
Kampuni za logistics;
Supermarkets;
Kampuni za ict;
Kampuni za kilimo;
Kampuni za usafirishaji.
Badala ya kuwaambia vijana:
"Jitafutie kazi."
Serikali inaweza kusema:
"Tuna vijana wenye ujuzi waliorejea; kampuni zipi zinaweza kuwachukua?"
Hii ni approach ya labour-market matching.
11. HATUA YA TANO: MENTORSHIP YA MIEZI 12
Hili ni muhimu sana. Usalama wa mpango usipimwe siku ambayo ndege imetua.
Upimwe baada ya: Kuanzia Miezi 3, 6 hadi Miezi 12
Je:
Ana kazi?
Biashara yake inaendelea?
Ana kipato?
Ana makazi?
Watoto wake wanaendelea na shule?
Ana changamoto gani?
Anahitaji mafunzo gani?
Hii ndiyo Reintegration Monitoring.
12. POLISI WAHUSISHWE
Wawe sehemu ya mpango lakini si kwa mtazamo kuwa hao vijana ni wahalifu. Polisi wanaweza kushirikishwa katika mfumo wa kuzuia uhalifu.
Lakini kuna tofauti kubwa kati ya:
Security Monitoring na Stigmatization.
Mtu akifika Tanzania na kuambiwa:
"Umetoka Afrika Kusini, wewe ni mtu wa hatari."
Tayari tumemtenga.
Lakini tukisema:
"Umerudi Tanzania; kama una changamoto ya ajira, biashara, makazi au ushauri, hizi ndizo huduma zilizopo."
Tunamrudisha kwenye mfumo wa jamii.
13. SERIKALI PIA IFANYE "EARLY WARNING SYSTEM"
Hii si surveillance ya watu. Ni mfumo wa kutambua matatizo mapema.
Mfano:
Ikiwa katika wilaya fulani vijana 50 waliorudi wamekosa ajira baada ya miezi mitatu, hiyo iwe ishara kwamba:
Mpango haujafanya kazi.
Ikiwa biashara 30 zimefungwa ndani ya miezi sita:
Tatizo linahitaji kuchunguzwa.
Ikiwa vijana wengi wanahitaji mafunzo:
VETA na sekta binafsi zishirikishwe.
Hii inaweza kusaidia Serikali kufanya marekebisho kabla matatizo hayajawa makubwa.
14. JAMBO LINGINE MUHIMU: FAMILIA
Hatupaswi kuwaangalia wao peke yao. Kijana anaporudi nyumbani anaweza kurejea kwenye:
Familia;
Mwenza;
Watoto;
Wazazi;
Ndugu.
Hivyo reintegration ni pia family reintegration.
Familia ipewe elimu kwamba:
"Mtu huyu amerudi baada ya maisha ya nje; anahitaji muda wa kuzoea tena."
Hii inaweza kupunguza migogoro ya kifamilia, msongo wa maisha na kutengwa.
15. JE, KUNA SABABU YA KUWA NA WASIWASI KUHUSU UHALIFU?
Ndiyo, lakini kwa namna sahihi.
Wasiwasi usiwe:
"Vijana 669 ni wahalifu."
Huo ni mtazamo usio na ushahidi. Wasiwasi sahihi ni:
"Je, Tanzania ina mfumo wa kutosha wa kuzuia kundi kubwa la watu wanaorejea bila kipato, bila ajira au bila mtaji kuingia katika mazingira ya kiuchumi na kijamii yanayoweza kuongeza vulnerability?"
Jibu la sera linapaswa kuwa:
Tuanze maandalizi sasa.
Si baada ya tatizo kutokea.
16. KUNA SOMO KUTOKA AFRIKA KUSINI
Hili si suala linalotokea Tanzania tu peke yake. Afrika Kusini imekuwa ikikabiliana na ongezeko kubwa la shughuli za deportation na repatriation. Serikali ya Afrika Kusini iliripoti zaidi ya deportations 109,000 katika miaka miwili ya fedha iliyotangulia hadi Machi 2026.
Na katika 2026, mazingira ya uhamiaji nchini humo yamekuwa magumu zaidi, huku kukiwa na maandamano, vitisho na matukio ya xenophobia dhidi ya wahamiaji.
Hivyo Tanzania haipaswi kuangalia tukio hili kama tukio la mara moja.
Inapaswa kujiuliza:
Je, huu ni mwanzo wa mwenendo mpana wa kurejea kwa Watanzania kutoka Afrika Kusini tu au na nchi zingine?
Ikiwa jibu ni ndiyo, tunahitaji mfumo wa kudumu.
17. TANZANIA ISIFANYE KOSA LA "SHORT-TERM RESPONSE"
Tatizo kubwa la Serikali nyingi Afrika ni kushughulikia tukio, si mfumo.
Ndege imefika.
Raia wameshuka.
Wamepokelewa.
Picha zimepigwa.
Hotuba zimetolewa.
Tunaishia hapo tu.
Tunasahau kwamba Hapo ndipo kazi rasmi inaanza.
Tunapaswa kuhamisha mjadala kutoka:
"Tumewaleta nyumbani."
kwenda:
"Tumewasaidia kujenga maisha mapya."
18. NINAOPENDEKEZA KUWE MPANGO WA MIEZI 12
Mwezi 0-1
Usajili;
Skills Mapping;
Mahali Wanapoishi;
Mahitaji Ya Msingi;
Familia;
Ajira.
Mwezi 1-3
Vocational Training;
Business Training;
Job Matching;
Usajili Wa Biashara;
Mentorship.
Mwezi 3–6
Mikopo;
Vifaa;
Ajira;
Incubation ya Biashara.
Mwezi 6–9
Tathmini ya Kipato;
Biashara;
Ajira;
Changamoto.
Mwezi 9–12
Tathmini ya Mwisho;
Biashara Zinazofanya Vizuri Kuongezewa Mtaji;
Wanaohitaji Msaada Zaidi Kupewa Intervention Maalumu.
19. KIPIMO CHA MAFANIKIO KISIWE "IDADI YA WALIORUDISHWA"
Hili ni jambo muhimu sana. Serikali inaweza kusema:
"Tumefanikiwa kuwarejesha Watanzania 669."
Lakini hicho si kipimo cha mwisho.
Kipimo cha kweli kiwe:
Ni wangapi wamepata ajira?
Ni wangapi wameanzisha biashara?
Ni wangapi wana kipato baada ya miezi sita?
Ni wangapi bado wanahitaji msaada baada ya mwaka mmoja?
Ni wangapi wameingia kwenye mafunzo?
Ni biashara ngapi zimeendelea?
Hapo ndipo tutakapojua kama mpango umefanikiwa.
HITIMISHO
Kurejeshwa kwa Watanzania kutoka Afrika Kusini hakupaswi kutazamwa kama tatizo.
Ni fursa na changamoto kwa wakati mmoja.
Fursa kwa sababu Tanzania inapata watu wenye uzoefu, ujuzi na maarifa kutoka nje.
Changamoto kwa sababu baadhi yao wanaweza kurejea bila ajira, bila mtaji na bila mpango wa maisha.
Na hapa ndipo Serikali inapaswa kuwa makini.
Tusisubiri uhalifu utokee ndipo tuanze kujiuliza maswali.
Tusisubiri mpaka kijana akose kazi miezi sita, mwaka mmoja, ndipo tumkumbuke.
Tusisubiri biashara yake ifungwe ndipo tumwambie Serikali ipo.
Tusisubiri kijana akate tamaa ndipo tuanze kumtafuta.
Kinga bora ya uhalifu wa baadaye inaweza kuwa uwekezaji wa leo katika ajira, biashara, ujuzi na matumaini.
Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba Serikali itumie zoezi hili kuanzisha National Returnee Reintegration Programme yenye ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Kazi, Wizara yenye dhamana ya Vijana, SIDO, VETA, Halmashauri za jiji, sekta binafsi, taasisi za fedha na mashirika ya kijamii.
Kwa watu 669, hili linawezekana kabisa.
Na kama mpango utafanya kazi vizuri, vijana hawa wanaweza kugeuka kutoka kuwa watu tunaowaogopa kuwa wataongeza uhalifu na kuwa wajasiriamali, wafanyakazi, walipa kodi na wazalishaji wanaochangia uchumi wa Tanzania.
Swali la msingi kwa Taifa sasa si:
"Tumewaleta wangapi?"
Bali:
"Tumewaandalia maisha gani baada ya kuwasili?"
HILO NDILO SWALI AMBALO SERIKALI, BUNGE, WATAALAMU WA AJIRA, SEKTA BINAFSI NA JAMII WANAPASWA KUANZA KULIJADILI SASA.





0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?