Watu wengi wakiwemo baadhi ya waislam, hawaelewi nini maana ya Msikiti. Na hii ndio usababisha mabishano na kutoelewana aidha ndani ya misikiti au nje ya misikiti. Ikiwemo vijiweni, kwenye majukwaa ya siasa na bila kusahau wachangiaji wa kwenye tofuti jamii mbali mbali.
Misikiti ni taasisi mama na muhimu sana katika Uislamu, na ndiyo maana Mtume (saw) alipohamia Madina kitu kwanza kabisa alijenga Msikiti, kwani mambo yote ya Uislamu uanzia na kumalizika Misikitini na si kwenye majukwaa.
Misikiti wakati wa Mtume (s.a.w.) ilikuwa si mahala pa kuswalia tu, bali shughuli zote za kijamii zilifanyoka hapo. Msikiti ni Kituo cha kudhihirisha nembo na nguvu ya Uislamu.
KAZI ZA MSIKITI NI ZIPI?
• Kwanza kabisa misikiti ni Nyumba ya IBADA, ninaposema neno ibada waislam wanaelewa nina maana gani. Na kwa nini sikutumia neno swala. Ibada katika uislam ukusanya mambo mengi sana ikiwemo swala ndani yake.
• Pili Misikiti ni sehemu ya kupitisha mashauri yote ya kijamii. Kwa maana ya Baraza la Shura na bunge la umma linaloamua na kupitisha mambo na mikakati ya umma na kusimamia utekelezaji wake.
• Tatu Misikiti ni kituo cha elimu au taasisi ya kielemu. Ikiwemo Madrasa, shule za msingi na sekondari vyuo kwa maana ya university. Taasisi itakayotoa elimu ya malezi ya kiroho sambamba na ile ya mazingira kwa wanajamii.
• Nne Misikiti ni kielelezo cha usawa baina ya wanajamii ambamo humo wote hulingana katika sharafu ya uja wao kwa Allah. Mkubwa na mdogo, kiongozi na raia, tajiri na fakiri (Masikini), mweupe na mweusi wote hawa husimama katika safu moja, bega kwa bega, nyayo kwa nyayo kumuabudu Mola Mmoja wakielekea sehemu moja.
• Tano misikiti ni Kambi ya mafunzo na maandalizi ya jeshi la haki linalopigana dhidi ya batili. Misikiti ndio Idhaa ya wanajamii na taasisi ya kupashana khabari mbali mbali. Hapa ndo information centre.
• Sita misikiti ni Makazi ya wasiojiweza miongoni mwa wanajamii. Kunapatikana Hospitali itoayo matibabu kwa kila mwana jamii. Vile vile ndio Ikulu au makao ya kiongozi wa jamii ya Kiislamu. Na haya tunayapata kwenye tarekh ya kiislam (Historia). Mtume (saw), alipokuwa kule Madina alijenga nyumba yake, ndani ya eneo la Msikiti. Hii inatuonyesha kuwa msikiti si jengo moja tu la kuswalia basi. Bali ni kituo (Centre) ambacho kimekusanya majengo mengi yanayo itajika ndani ya jamii husika.
HITIMISHO
Lazima ikumbukwe kuwa ni baada ya Msikiti kutumika kwa shughuli hizi, Uislamu uliweza kustawi. Lakini leo hii ni kinyume cha mambo. Sio tu kwamba shughuli hizi hazifanyiki tena Misikitini bali hata Waislamu hawajui kama haya yanatakiwa yafanyike Msikitini.
Hivi ni baadhi ya vielelezo vya vitendo vya mpendwa wetu Mtume (s.a.w.), na ndiyo sunnah zenyewe hizo. Ni muhimu kwetu kufuata vitendo hivyo. Msikitini ndipo mahali pa kufanyiwa hayo na mengineyo yaliyo mema na mazuri ya kumpendeza Allah (s. w.).
Misikiti si sehemu ya kuswalia tu, kama ilivyozoeleka na wengi msikiti ni kituo (centre) hivyo tunaposema mathalani "Masjid Nuur" tuna maanisha kituo chenye mambo mengi sana. Sehemu ya kuswalia, kituo cha elimu au taasisi ya kielemu kwa maana ya education centre, zahanati (kama sio hospitali kamili), kumbi, hosteli, baraza la Shuura au bunge, Information centre kwa ufupi ni kituo (centre) cha mambo ya kijamii na mengineyo na ni kielelezo cha usawa baina ya wanajamii.
QUR'AN SURAT AT-TAWBA: 18
Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao muamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika waongofu.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?