Monday, 18 May 2015



Assalamu Alaiykum wa rRahmatullah wa Barakatuh

Kuharibika kwa jamii, kupoteza upendo na kuhadimika kwa mapenzi kati yetu ni jambo lililoanza taratibu na limechukuwa zaidi ya miaka 30 au zaidi, kwa sababu tuliaza kuwa wabinafsi na kujikumbatia wenyewe na kuacha kukumbatia ndugu, jamaa marafiki na majirani wanaotuzunguka.

Zamani nakumbuka kam miaka takribani 30 - 40 tu iliyopita ilikuwa si jambo la ajabu kuona kipindi cha mwezi wa Ramadhani watu wakifuturu nje na kila aliyepita akikaribishwa kukaa na kufuturu.

Hayo yalifanyika si kwamba watu walikuwa matajiri, la hasha, bali ule upendo na kujaliana kulikuwepo kwenye mioyo ya Waislam. Lakini hivi leo Waislam sisi tumekuwa tu mahodari sana kwenye media, haswa vyombo vya habari, Luninga, radio, magazeti, kwenye mitandao, uko ndiko Tunaonyesha Uslam wetu na kila mwenye kutusoma anaona ama kweli sisi ni Waislam haswa na Uislam ndio vazi letu, lakini ukija kwenye maisha halisi ni kinyume kabisa, tumekuwa matapeli wa kutupwa, haturejeshi amana, tunadhurumu mpaka pesa za sadaka misikitini.

Waislam sisi ndio tunaongoza kwenye kila maasi, angalia waimba taarabu ni sisi, vibaka ni sisi, waimba bongo flava ni sisi, matapeli ni sisi, yaani mpaka imefikia sasa Wakristo wanatufanyia istizai, kuwa Mwezi wa Ramadhani biashara ya kiti moto, inadoda kwa sababu walaji wakubwa wapo kwenye mfungo, mabaa nayo yanakosa wateja, sababu wateja wanaona haya kunywa kipindi cha mfungo na mengine mengi.

Na hii yote sisi tujiitao Waislam, Uslam wetu ni wa Kuigiza tu, yaani Uislam wa Ukasuku, sisi tu mahodari sana wa kukariri Ayat na Hadith mbalimbali na kuona kila asiyekubaliana na sisi ni kafiri, yaani hatuoni ubaya wa kuwatoa Waislam wenzetu kwenye Uislam, kama mtu jambo alielewi basi atakwita kafiri, kama ukubaliani naye atakwita kafiri. Njoo basi siku uone hayo maisha yake uko mtaani, utakuta yeye huyo huyo ndio, mwizi wa sadaka za msikiti, watoto zake ndio hao hao waimba taarabu, vibaka na kila balaa analo yeye kwenye familia au jamii inayo mzunguka.

Ukiona Muislam anampenda Muislam mwenzie basi ujue hapo kila mmoja yupo kimaslahi zaidi, yaani kila mmoja anampenda mwenzie kinafiki, kwa sababu anafaidika kwa namna moja au nyingine. Kama mmoja ni masikini na mwingine ana uwezo kidogo basi utakuta tajiri anajipendekeza kwa masikini ili haonekane kuwa anapenda watu kumbe lengo na madhumuni ni kumtumia kwenye maslahi yake na masikini naye alkadharika, yupo pale kutumika na kujidharirisha ili apate mradi wake.

Ni Waislam wachache sana ambao ni mifano katika familia zao au ndugu na jamaa na marafiki zao na hata mtaani kwao ni mfano wa kuigwa, lakini kama atatokea Muislam mwenye tabia hizi, sisi waislam wengine ndio tutamkebei na kumtia midomoni kwa kumshusha hadhi yake na kumuona kuwa si chochote zaidi ya kujitafutia sifa tu.

Haya ndio tunayo waislam wa sasa, na hakuna wa kutuonyesha njia kama hatutakubali ndani ya nafsi zetu kuwa tuyafanyayo sio na tunapaswa kubadirika, laah basi tutaendelea hivi hivi na tutatawaliwa mpaka tunaingia makabaurini mwetu, na hata hayo makaburi nayo yatatawaliwa mpaka siku tunafufuka, tunajikuta tunafufuka na wasio Waislam, maana ndio tulio waiga na kufuata tabia zao.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!