Tuesday, 16 June 2015


Kama kuna fani inayovamiwa kwa nguvu hivi sasa na watu wengi basi ni fani ya habari. Kwa waliokwenda kujifunza fani yenyewe na wasiopata mafunzo, ambao wamejaribu na kuwa magwiji. Wabunifu wa habari katika aina tofauti tokea kusema, kuandika na kuchora picha na hatimaye kuzipeleka watakako aidha kwa walio waajiri au walio wakusudia tu, ili mradi wazipate hizo habari.

Fani hii pia haina rika, yeyote awezaye hujaribu na hata kama haelewi miiko, adabu za uandishi na upigaji wa picha zenyewe. Vibari vitakiwavyo au hata kujali mishahara. Naandika haya si kwamba naifuja fani hii ya habari bali nasikitika kuwa jahazi ili la kuleta faida kwa jamii limeingia wadau fujo, ambao vibari vyao vimo viganjani na vidoleni mwao.

Tumeyasema na tutaendelea kuyasema na ni wajibu tukumbushane, maana sisi binadamu tuna sifa ya kusahau na kujisahau.  Ni vizuri kusikiliza ulimwengu na maendeleo yake ya kiteknolojia, lakini eh! Mengine karaha maana viumbe sisi wa Mwenyezi Mungu tunapovuka mipaka kwa yale au vile vya kutusaidia vikawa ndio vitendea dhambi vya kiteknolojia.

Ugomvi humohumo, kashfa tele, uongo usio mfano, matusi na kujiona kuwa wajua zaidi ya wengine na wizi wa kimambo leo, umbea wa kisasa kwa njia ya teknolojia na waandishi bila fani wamekithiri.

Ni kweli kabisa maendeleo mapya uzaa tabia mpya na spidi tulionayo inachafua hata mashine za kupimia mwendo au gavana. Si majumbani mwetu, maofisini au hata kwenye mchanganyiko wa kijamii, ni zama hizi za kisasa za kuharakisha maendeleo ya kimaisha, Twitter, Youtube, Skype, Facebook, Whatsapp, Telegram, Talkray, Line, Viber na mitandao mingine kadhaa ya kiajabu ajabu.

Basi hiyo whatsapp kwa vijana ndio mbolea yao ya kimaendeleo na kujuwa mfumo wa haraka wa kurahisisha mambo.
Je viandamizi hivi kama nyenzo za kutusaidia ni vibaya kimadhumuni? Ili si swala linalotaka majibu ya ndio au hapana, bali lina mjadala mfupi sana. Vitendea kazi hivi vimesaidia kiasi gani na vimechafua kiasi gani, basi jawabu lake na ndio la kulijadiri na kutoa nukta ya kweli.

Lakini bado tunaweza kwa hasira tukaangalia maharibiko na tukasema kuwa havifai. Basi hatutakuwa tumetosheleza kukiaminisha kilio chetu. Kwa hiyo tutoe asilimia tustahiki, kisha tukanyane, kwamba ili kwa mitandao hii limefeli na ili limepasi liendelee.

Nadhani haya ni mazungumzo tu, kwani maji yamekwisha kumwagika, tuchukuwe tambara au spongi tupanguse au kukamua. Lakini kama ni farasi keshatoka bandani na anatimua vumbi na mlango kuufunga saa hizi ni kupoteza wakati bure. 

Basi dini bado ipo na itaendelea kuwepo na umma huu moja ya kazi yake kubwa ni kuamrishana mema na kukatazana maovu.

Tutokako kifaa kidogo cha mkononi unachozungumza nacho hivi leo, kiliogopesha mno na aliyenacho basi ni mtu wa idara nyeti kwa lugha ya kileo. Ukiharifu sheria basi utazungukwa kabla ujapepesa, kumbe wa ubavuni mwako kakuchuuza wewe huna habari.

Zana hizi tulizo zitaja sasa zimeenea na tena kwa utaalam mara dufu, na ndio ustaarabu mpya, vizibiti siri vipya na wepesi mpya wa mawasiliano na bado tutaendelea kuunda.

Nasema tunatumia kwa faida gani nzuri? Binafsi sijui maana hata kwa faida mbaya kwa wengine imetosha, maana hoja ni kuwaumbua wenzio na kuifurahisha nafsi yako. Kwa Allah tungojee hesabu.

Facebook, Twitter, Skype, whatsapp, Youtube na vinginevyo kweli ni daraja fupi za mawasiliano, lakini kwa wasiotumia vyema utu na heshima zao ni daraja dhaifu mno la kukuelekeza kwenye ghadhabu za Allah, kwani unasimanga, unakashifu, unazuwa uongo, unafitinisha na unaiba siri za watu bila idhini zao. Vyema kwenye ghafla njema, je kwenye yale yasio pendeza?

Jamani kwanini hata wagonjwa wapo ICU, atokee mtu na umbea wake kwa teknolojia ajidai anakwenda kukagua mgojwa, basi nafasi hiyo ya kipekee ya kusimama na kumuombea dua ndio atammulika na whatsapp huyoo dakika moja mgojwa wa watu kajaa duniani kote ana mipira kohoni, puani na waya za vifuani.
Mmbeya huyu keshakonga roho, kawafurahisha mahasimu wa mgonjwa hata maiti nayo upigwa picha akatangazwa bila ya idhini ya wenyewe.

Njoo kwenye huo mtandao wa Skype, matusi humohumo, wanaonana uso kwa uso, wa Ulaya, Marekani au Arabuni wanasutana kwa mtandao kwa walio Afrika. Kila mmoja anamlaani mwenzie kupitia katika kioo, utadhani jogoo pale aonapo ona jogoo mwingine kwenye kioo, kumbe ni mwenyewe anakiparura kioo, ndio tusi linakurejea.

Tizama mitandao inavyo tuchezea, uko kuchorana na kubadirishana sura na kuvalishwa usivyo vivaa au kuunganishwa na mtu husiye pendana naye, basi usiseme, ufundi wa haya upo kiganjani, tuna umbuana tu.

Nasema, hatutumii nehema vyema, tena na wakati hatuutumii ipasavyo, baadhi yetu hivi sasa hatuwezi kustaamiri dakika tano, tusivute simu zetu, tupigiwe au tusipigiwe, kila mmoja kainamia anapangusa kioo cha simu kama bao la kupigia ramli. Anaandika tu akifuta, si mirihi, si shamsi si kamari.

Ebu tukithirishe ibada, Allah tunamsahau, tunatumia vibaya mitandao, je hatujasoma ile ayah ya 148 ya Surat An-Nisaai, inayosema:

"MWENYEZIMUNGU hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila kwa mwenye kudhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua"

Basi tuyafanyao Allah anatujuwa, yeye ndiye aliyetuumba, tusijidanganye kwa kuwa ufundi sasa unazidi basi tutakufuru. Tunajuwa sasa simu zetu zinafanya kazi hata kwenye pipa la maji. Nyengine zinafunguka kwa kuzipepesea jicho au kupandisha nyusi, mbali ya hiyo miito ya milio ya mbuzi paka na mingine, inayokera hata msikitini.

Lakini kumbuka wewe na mimi tulikuwa nani kama si tone la maji ya uzazi, tushakuwa wajuwaji kwa kuwakera wengine!?

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!