Thursday, 4 February 2016

WABONGO NA MAISHA YA ULAYA


Baada ya kuzamia Ulaya jamaa yangu mmoja kutoka kusini, kijiji chao kikiwa jirani kabisa na kijiji chenu, hatimae akawa anaishi Uswisi. Lakini maisha yake yalikuwa ya kujifichaficha maana alikuwa hana vibali vya kuishi Uswisi. Washikaji wenzie wakamtonya kuwa dawa kubwa ya kuishi Uswisi kwa raha ni kufanya chini juu kuoa mwanamke wa Kiswisi na hapo lazima baada ya muda mfupi unapata uraia.

Katika sakasaka hatimae mama mmoja mzee mzee akaingia mkenge na kudhania anapendwa ile mbaya na jamaa yangu, akakubali kuolewa. Kuendeleza uwongo, Mbongo akawa kajitambulisha kuwa eti yeye Mzulu anatoka Afrika ya Kusini, si unajua Wabongo mishen taun walivyo. Ndoa ikafanyika bibi kizee wa Kizungu kajua kaolewa na Mzulu, kumbe jama Mngoni tu kwisha kazi, tena wa Matimila.

Siku moja mama wa Kizungu karudi kwa mumewe akiwa na furaha sana, ‘Mume wangu leo nimekutana na Mswisi mwenzangu nae kaolewa na bwana Mzulu kama wewe, nimewakaribisha Jumapili waje kwa chakula cha mchana ili mkumbushane mambo ya kwenu”

Jamaa yetu mkojo ulimbana ghafla, akajua kuwa sasa mambo ndio yameharibika, alikuwa anaiona laiv safari ya kurudishwa Bongo kwa kosa la utapeli. Hata harufu ya Komonyi na ulanzi akaanza kuisikia.

Usiku wa Jumamosi alikesha mimacho imemtoka akawa anajaribu kukumbuka hata neno moja la Kizulu alilowahi kusikia, hakukumbuka, miji ya Sauzi aliyoikumbuka ilikuwa Soweto na Johannesburg, Cape Town na pia akakumbuka Kwa Zulu Natal, akaona jamaa akifika atang’ang’ania kuwa katoka Kwa Zulu Natal, basi mengine atajifanya bubu.

Jumapili ikaingia siku yake ya kuumbuka ikawa imefika.

Hatimae wageni wakaingia, kina mama wa kizungu wakawa katika furaha za kuwa na waume Waafrika tena wote Wazulu. Akina mama wakasema wao wanaenda jikoni ili jamaa waongee kikwao. Jamaa yangu akawa anamuangalia mwenzake kichwani anajiuliza huyu Mzulu namuanzaje ili asiharibu mambo? Si akaanza kujisema kwa nguvu, ‘Sasa huu msala huu mi Kizulu nakijulia wapi?’ Hee ghafla yule mgeni akarukia, ‘ Aise unajua Kiswahili?’

‘Ndugu yangu kwanini nisijue Kiswahili? Nihifadhi ndugu yangu mi Mngoni natoka TZ, nimezaliwa Matogoro huyu demu nimemdanganya mi Mzulu’. Mgeni nae akajibu, ’Aise Mungu ashukuriwe na mimi nilidhani we Mzulu, maana mie natoka Mfaranyaki, nilimdanganya huyu wangu kuwa natoka Sauzi, hapa nilikuwa sina raha najua we Mzulu, na huyu mama akijua nilikuwa namdanganya atanishtaki na safari ya kurudi Bongo itakamilika’

Hapo hapo jamaa zangu wakaanza kuongea Kingoni, Tukuwoni Bambo…, zikomo, Yeo, za kunyumba... Zabwina, za Magono…, za Maluku.. Vana wayimwiki…? Hongera wa muyangu, wa kunyumba mewa… kumbe na wewe wa nyumbani.

Wakaanza mpaka kuimba nyimbo za Kingoni. Msengilwe malongo vangu… Nami nakumanya… Nilipokuwa mwenyewe wenzangu amunisemi, nikiondoka kidogo nyuma mwanisengenya… Chilangondo... Chilangondo... Jambooo Jamboo lile... Umeweza yeye, Umeweza yeye, umewezaaa, kaka, umeza mwenzetu...

Wazungu kusikia nyimbo za furaha, wakarudi sebuleni kuangalia kulikoni. Kwa furaha jamaa wakajidai eti wamegundua kuwa wananatoka kijiji kimoja kusini kidogo ya Kwa Zulu Natal.

Mwengaaa, Usengwili....!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!