Wednesday, 10 August 2016

Kuna mambo mengi sana kwenye ili jambo, ila kwa uchache naweza kusema katika mazungumzo yanayopendwa basi mazungumzo ya ngono au kuridhishana kimapenzi baina ya jinsia mbili ndio yanaongoza sana, wengine huita Hot Night

Kwa kweli ili ni janga kubwa sana kwa vijana au niseme watu wengi wenye kushiriki mijadala kwenye mitandao na haswa makundi (groups) zenye michanganyiko ya kijinsia.

Ukizunguka kwenye mitandao ya Kijamii, habari nyingi zinazojadiliwa na vijana ni mahusiano ya Kijinsia (Kingono). Na ufikia mpaka kuambiana ni jinsi gani unaweza mfanyia mwenzio hivi au vile mpaka akaridhika.

Maswala ya simulizi za Ngono kwa Kisingizio cha Kuimarisha Ndoa za watu au mahusiano yamekuwa ni gumzo kubwa sana na kufikia mahali hata mtu akisema kuwa haya maswala si vema kuyaweka kwenye mijadala hii ya wazi, utaonekana kuwa wewe umepitwa na wakati au mshamba.

Ili limekuwa ni tatizo moja kubwa sana na kwa bahati mbaya sana limewakumba hata wale wenye kujionyesha kuwa wameshika dini.

Waislamu nao hawakubakia nyuma wameiga mazungumzo hayo na kuyapa majina kadhaa wa kadha tena wakiambatanisha na Hadith za Mtume (saw), kwa lengo la kuhalalisha kile ambacho kimeharamishwa.

Kuzungumzia Maswala ya ngono na namna ambavyo unaweza kumstarehesha Mke/Mume kwa kuandika kila jambo hatua kwa hatua na kutaja viuongo husika kwa majina yake halisi ni sawa na kuangalia picha za uchi au picha chafu za Ngono.

Katika Imani ya Kiislamu ni haramu kwa Muislamu kusoma au kutazama filamu za ngono ambazo kwayo huamsha hisia na ashiki. 

Kwa sababu zozote zile haifai katika Uislamu. Hili hata kimantiki haliingii akilini kwani wale ambao utakuwa ukiwasoma au kuwaangalia watakuwa katika hali ya uchi ambayo imekatazwa na Uislamu.

Simulizi hizi ujenga taswira kwenye ubongo wa msomaji na kuchochea zile kemikali zenye kuamsha hisia za kufanya jimai na zinamtia Muislamu hawaa na ashki ya bure na hivyo kumkaribisha yeye na zinaa.

Utakuta mtu anajionyesha kama ustadhi/ustaadha mzuri, lakini linapokuja swala kama ili ndio uwa mstari wa mbele kutetea na kushadidia kuwa inafaa kwa sababu itaimarisha ndoa na kuwafunda wale wenye kutarajia kuingia kwenye ndoa.

Tena uona sifa kubwa kwa kule kubandika maswala ya ngono na kujionyesha kuwa yeye ni mahiri sana na mwenye ujuzi wa maswala hayo.

Haya ni matokeo ya kuzarau mafunzo ambayo zamani wazazi wetu waliweza kuwakusanya vijana balekh na kuwapatia mafunzo tena kwa siri na haswa wale waliotarajiwa kuingia kwenye ndoa na kuwafahamisha kinaga ubaga nini kinapaswa kufanywa kwenye ndoa na yapi hayafai.

Tulipoanza kuyazarau mafunze yale kwa kisingizio kuwa yamepitwa na wakati, matokeo yake ni kuwepo uwanja huru mwenye kila lake kulirembea kwenye mtandao, bila kuzingatia maadili ya kijamii, dini wala kabila.

Hii naweza kusema ni sawa na kufundisha uchawi kisha ukawaambia wanafunzi wako wasiwaroge watu kwa kuwa si jambo zuri.

Matokeo yake ni hodi zisizokwisha kwenye inbox, wataanza na salamu na kuelezeana matatizo ya hapa na pale. Watajifanya kuombeana madua na maneno mazuri mazuri.

Siku ya pili utapigiwa simu na mazungumzo yataendelea na kupelekea kuombana picha na matokeo yake ni kupeana ahadi za kukutana na mwishowe ni kungonoana.

Waislam, tumewacha mafundisho ya dini na kila mtu siku hizi amekuwa ni ulamaa mwenye kutoa fatawa na wajuzi wa fiqh, ule utaratibu na nidhamu ya kukaa chini ya Masheikh imepitwa na wakati na siku hizi Ulamaa mkubwa mwenye kutegemewa ni Sheikh Gugol Ibn Intanetii.

Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atusamehe kwa makosa yetu mbali mbali tunayofanya mchana na usiku.


Aamiyn

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!