Yalikuwa ni maneno mafupi, marahisi, na yenye kueleweka yaliyoelekezwa kwa wapiga mishale takribani 50 walioambiwa...
"Lolote litakalotokea, hakikisheni hamshuki juu ya huu mlima huu."
Shetani akawachezea na wakataka kuyaletea ufundi maneno haya. Wapo waliosema alimaanisha tukae hapa kama tukiwa tunapigwa ila kama tumeshinda tunaweza kushuka.
Wengine wakasema hakumaanisha hivyo alimaanisha tukae hapa na tusitoke.
Pakazuka mzozo mkubwa sana juu ya mlima huo uliopelekea wengi wao kuteremka na wachache kubaki. Hii ilipelekea Kamanda wa upande wa pili kupata nafasi ya kujipanga upya na kushambulia tena Jeshi lao.
Wengi walikufa na wengi walidhurika katika vita hii kutokana na watu kutaka kuleta ufundi kwenye maagizo ya wazi kabisa waliyopewa na kamanda wao.
Zimepita karne 14 hadi leo hii, watu wanarudia kosa lile lile. Ufundi umekuwa mwingi...!
Ufundi kwenye maneno ya MwenyeziMungu, Ufundi kwende Hadithi zake Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) Ufundi umekuwa mwingi sana.
Watu wameenda kujadili ayah na hadithi ngumu sana kueleweka huku wakiacha yaliyo mepesi.
Ufundi wao umepelekea Waislamu leo hii kudhurika maeneo mengi sana, watu kuwa na makundi mengi katika dini.
Hatusikii Mijadala ya kuhamasisha Utowaji wa zakah na Sadaka, Hatusikii Mijadala ya Qiyamu Layl, Kusaidia wanafunzi masomo yao wala Hatusikii Mijadala ya kuwasaidia Wajane na Kulisha Mayatima.
Hatusikii Mijadala ya kuwalingania vijana wetu wanao potea katika umalaya, uvutaji wa bangi, sigara na ubwiaji wa unga na ulevi...!
Ufundi umekuwa mwingi mpaka kufikia kukufurishana, ufundi huu ndio umetufikisha hapa tulipo, mpaka tumekuwa hatujielewi tena, wala hatuelewani, kiasi cha kujilimikisha na kugawa Pepo na Jahanam kwa tunao wataka au kuwachukia!
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?