Monday 27 February 2017

HASWA WATUMIAJI WA WHATSAPP, FACEBOOK & FORUMS

Miaka Hivi Karibuni Kumezuka Masheikh Wengi wa Kwenye Mitandao na Haswa Vijana, Ambao Licha ya Changamoto aa Kimaisha Lakini kwa Namna Moja au Nyingine Wameweza Kujifunza Uislamu Wao, na Kuelewa Mawili Matatu. Kwa Kweli ni Jambo la Kuwapongeza Sana Vijana Wenzetu.

Nawapongeza kwa sababu wameweza kushinda vishawishi kadhaa na kuamua kujitolea kutafuta elimu ili iwafae wao na jamaa zao hapa duniani na kesho akhera.

Pamoja na kuwapongeza uko pia nieleze masikitiko yangu makubwa kwa vijana wenzangu ambao wamejawa na hamasa na msisimko mkubwa sana kwenye kupapia mambo kadhaa yahusuyo dini ya Kiislamu na haswa kwenye kufutu masuhala kadhaa kwenye Uislamu.

Wengi wao wamefikia mpaka kuweza kutoa fatwa na kufutu na ata kuwa radd Maulamaa na Masheikh wakubwa, Maulamaa na Masheikh ambao wametumia robo tatu ya maisha yao kusoma elimu ya dini na wakajitahidi kwa kadri ya uwezo waliojaaliwa na MwenyeziMungu, katika kufikisha na kutufafanulia mambo kadhaa ambayo wengi leo tunafaidika nayo.

Kuna makundi (groups) mengi kwenye mitandao ya kijamii haswa Facebook, WhatsApp, Telegram na tovuti baraza kadhaa. Makundi ambayo yanasimamiwa na vijana wasio na utambuzi na ufahamu katika Dini, japo wanajiona kuwa wamesoma.

Vijana wengi ambao aidha wamemaliza Juzuu au Masahafu au niseme wamekaa darasani si zaidi ya miaka saba na baada ya hapo basi wameingia mitaani na kujivika usheikh wa kutoa fatwa na kufutu masuala kadhaa ya kielimu.

Wengi wao wanajuzisha yaani wanahalalisha na kuharamisha mambo tena bila woga, na wengine wanafikia mpaka kutoana kwenye Uislamu na kuitana majina kama vile Makafiri, pote potovu, watoto wa Ibilisi, Mbwa wa motoni na maneno kadhaa yasiopendeza. Na uku wakibishania urefu wa ndevu zao na wengine wanafikia kutukanana kisa huyu anasema kuwa Qur'an ni kiumbe na mwingine anasema si Kiumbe!

Na hii yote ni kutokana na utumiaji mbaya wa mitando ya kijamii, mtu kaka nyuma ya kompyuta au simu yake na kutumia google kutafuta maswala kadhaa na kujifanya kuwa yeye ndiye anayefutu hayo maswala na wengine kufikia mpaka kuwatukana matusi makubwa Maulamaa na Masheikh, waliotangulia mbele za haki na hata walio hai.

Na hata wasomaji, ambao asilimia kuwa ni vijana, nao wamekuwa si wenye kupenda kuwafata Masheikh na kupiga goti kwa ajili ya kutaka kusoma au hata kuuliza maswala mbalimbali ya kijamii.
Utakuta mtu yupo radhi kuanika aibu zake au za mwenza wake kwenye group za mitandaoni na kila mmoja akasoma aibu zile kisa eti atafuta majibu aweze kurekebisha aidha ndoa yake au mahusiano yake na wazazi wake.

Tumeufanya Uislamu kama soko la nguo za mitumba, kila mtu chagula chagula anachagua nguo anayotaka nyingine anaacha. 

Ajabu wengi wanafikiria kuwa wanaweza kujifunza Uislamu kupitia group za Facebook, WhatsApp, Telegram na tovuti baraza.

Kwanini vijana hawataki kwenda kusoma kwa Mashekh na kung'ang'ania kukufurishana kwenye mitandao?

Binafsi sijawahi kuona mtu akaitwa Profesa au kupata degree kwa kuuliza kiujanja ujanja kupitia Facebook, WhatsApp au Telegram.

Kama elimu ya sekula tu, mtu anasoma miaka saba, ikaitwa elimu ya Msingi, kisha akaongeza miaka minne na kumaliza form Four, na akaendelea tena miaka miwili ili kumaliza form six na kama ameweza kuendelea basi atasoma chuo kikuu si chini ya miaka miwili kwa uchache. Na jumla ya miaka yote hiyo si chini ya miaka 15 kwa uchache na kutunukia shahada ya kwanza, na bado anaonekana kuwa ni wa kawaida tu na si wa kufutu maswala ya kielimu.

Vipi leo mtu asome miaka yake miwili mitatu na kuuliza uliza kwenye mitandao, kisha leo awe tayari naye ni sheikh au ulamaa wa kufutu maswala kadhaa kwenye Uislamu?

Hivi tumefanya jitihada ngapi kuwafikishia Waislam wenzetu ambao kila kukicha wapo kwenye majumba ya ufuska kama vile mabaa, vilabu vya usiku, wapo ambao kazi yao ni kubeti kwenye kamari, wapo wauza na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Wote hawa wanahitaji kunasihiwa ili wapate kuepukana na hayo matatizo na si kukaa kwenye kompyuta au kutumia simu zetu kuwatukana Masheikh na Maulamaa.

QUR'AN SURATUT TAWBA 9:71
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

MAELEZO
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake, wao kwa wao ni wapenzi wa kupendana na kusaidiana, kwa mujibu wa Imani. Wanaamrisha yanayo amrishwa na Dini yao ya Haki, na wanakataza yanayo katazwa na Dini. Wanatimiza Sala kwa nyakati zake, wanatoa Zaka kuwapa wanao stahiki kwa wakati wake. Na wanat'ii anayo waamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wanayaepuka anayo yakataza Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hao ndio watakao kuwa chini ya Rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwalinda kwa Rehema, na Mwenye hikima katika upaji wake.

Na Mtume Muhammad (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) anatuambia kuwa...
Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuoneana kwao huruma na kusaidiana kwao ni mfano wa kiwiliwili. Kinapopatwa na maradhi sehemu moja basi mwili wote hukesha kwa maumivu na machovu.
(Bukhari na Muslim)

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!