Tuesday, 25 April 2017

Mwezi wa ramadhani unakaribia, hii imenipelekea kutafakari kiasi, na kujikuta nawaza ili na lile na kujiuliza… Kwanini kila mwaka tuwe kwenye ugomvi kwenye swala la mwandamo wa mwezi!?

Nikajikuta natabasamu badala ya kusikitika liliponijia wazo kama mamlaka haya ya kutangaza mwandamo wa mwezi wangekabidhiwa wanasiasa, jasho lingetutoka, maana kwenye Magazeti tungesoma yafuatayo…!

Sisi hatukubaliani na hao wanaojaribu kutafuta umaarufu kuwa wameuona mwezi, dunia nzima inajua kuwa  chama chao kina misingi iliyojaa ufisadi.

Tunaenda mahakama ya wananchi kushtaki ili tupate ruksa ya wananchi kutangaza kuonekana kwa mwezi.

Mkitupa uongozi wa nchi hii tunawahahakikishia tutakuwa na mwezi wetu ambao umetokana na jasho la Watanzania wanyonge.

Tunaenda mahakamani kuzuia kutangaza kuonekana kwa mwezi kwa kuwa hawa waliotangaza wamekiuka sheria mama.
• Mahakama yazuia kutangazwa mwezi kuonekana mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Chama cha naniliu kimetangaza kuwa kimepata taarifa za kiintelijensia kuwa mwezi utaonekana kesho.

Uongozi wa juu kuwashughulikia waliotangaza kuonekana kwa mwezi kwenye mitandao ya kijamii.

Kuanzia kesho chama chetu kinaziba masikio, pua na midomo kupinga kuweko kwa naniliu kwenye kamati  ya kuangalia mwezi.

Wananchi wa vijiji vingi wachukua sheria mkononi na kuuona mwezi bila kupewa ruksa na vyombo husika.

Mheshmiwa spika naomba muongozo kabla ya kutangaza kuonekana kwa mwezi…

Maelezo haya yaweza yasitokee kweli kwenye jamii yetu, lakini bado hatujaepuka migogoro inayotokea kila unapokaribia mwezi wa ramadhani. Maana hao Masheikh zetu hawana tofauti na viongozi wa kisiasa, kwa sababu kila mtu ana angalia maslahi yake...!

Tumekwisha shuhudia, kila mwaka, Waislamu sisi wa Afrika Mashariki kutofautiana masiku ya kufunga, kuna wanaofunga mwezi ukionekana Saudia, kuna wanaofunga mwezi ukionekana kwenye nchi zao na kuna wanaofunga kwa kutangaziwa na Masheikh zao.

Na hii imepelekea nchi moja kuwa na ramadhani mbili, kiasi cha kupelekea hata sikukuu ya Iddi kuwa mbili…!

Na kwenye Qur’an tunasoma maneno haya, japo hatuyapendi kuyafuata: 

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka.
Qur'an Surat Al I'mran [3]:103

-TARAJUMA-
Nyote nyinyi shikamaneni na Dini ya Mwenyezi Mungu, wala msifanye jambo litalo leta mfarakano baina yenu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlivyo kuwa wakati wa ujahili nyinyi kwa nyinyi maadui. Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zenu kwa Uislamu, mkawa mnapendana, na ilhali kwa sababu ya ukafiri wenu na kufarikiana kwenu mlikuwa juu ya ukingo wa Moto, akakuokoeni kwa Uislamu. Kwa mfano wa bayana kama hii ya pekee Mwenyezi Mungu anakubainishieni daima njia za kheri, ili mdumu katika uwongofu.

Vilevile Mtume (saw) alisema,
"Msitofautiane, kwani waliokuja kabla yenu walitofuatiana wao kwa wao, na kisha waliangamizwa."
(Al-Bukhaariy)

 "Yeyote atakayeishi baada yangu ataona migogoro mikubwa"

Na ni kweli... Maana hapa ndipo tulipo, tunaishi katika zama za mikinzano na kutokubaliana, kutokubaliana katika iymaan, Fiqh, Aqida Faradhi na Sunnah na hata siasa, hali ni mbaya, inatisha na inasikitisha. Lilikuwa kundi moja na jamii moja, sasa tuna makundi chungu nzima, na kila moja linalingania misingi yake yenyewe.

Tunasoma kuwa Muislam ndugu yake Muislam, halikutajwa Dhehebu au Kabila au Taifa, umetajwa Uislam, sasa vipi dhehebu au kabila au taifa liwe bora zaidi ya Uislam wenyewe?

Na tunapokuwa na mgongano wa mawazo baina ya Waislamu, maadui zetu wanapiga makofi mengi na kufanya kila hila uendelee ugomvi baina yetu.

Wahenga walitufunza kwamba; Panzi wakipigana, kunguru hupata ulaini wa kitoweo cha siku hiyo. Ndivyo hali yetu Waislamu wa kizazi cha sasa.

Tunafarikiana huku maadui zetu wanapata mwanya mzuri wa kuendeleza dhulma.

Hii ni Nasaha tu kutoka kwangu binafsi kwenda kwa Waislam wote, ni hiyari ya kila nafsi kuikubali au kuikataa.

 "Ewe Mwenyezi Mungu, nitosheleze kutokana na wao kwa unachotaka"
Aamiyn.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!