MAUAJI MKURANGA, KIBITI NA RUFIJI (MKIRU)
Je ni Ugaidi, Chuki za Kisiasa na Jeshi La Polisi au Ni Uhalifu tu Mwingine!?
1. Je Ni Ugaidi Kama Ule wa Al-Shabab
2. Je Ni Chuki Tu Za Kisiasa
3. Je Ni Chuki za Wananchi Dhidi ya Jeshi La Polisi
4. Je Ni Uhalifu Tu Kama Uhalifu Mwingine!?
Kwa nyakati mbalimbali, viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa wametoa kauli kadhaa kuhusiana na mauaji yanayoendelea huko Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Kwenye makala hii, inayopatikana mtandaoni imejaribu kuainisha dhana za aina nne, kama zilivyo orodheshwa hapo juu.
Kuna maswali kadhaa ya kujiuliza, Je Ni Ugaidi kama ule wa Al-Shabab, au ni Chuki tu za Kisiasa au ni Chuki za Wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi, au yawezekana ikawa ni Uhalifu tu Kama Uhalifu Mwingine!?
Tuanze na dhana kuwa mauaji hayo yanatokana na chuki za wananchi. 'Ushahidi' kuhusu dhana hii ni wa aina mbili. Kwanza, Januari 23, 2013, kulijitokeza vurugu kubwa huko Kibiti zilizolazimu jeshi la polisi kutumia helikopta kuzidhibiti. Vurugu hizo zilitokana na kifo cha mkazi mmoja wa Kibiti aliyefariki Hospitali ya Taifa Muhimbili alikopelekwa kutibiwa majeraha ambayo ilidaiwa aliyapata kutokana na kupigwa na polisi.
Vurugu hizo zilipelekea Barabara ya Kilwa kufungwa kwa zaidi ya masaa matatu, na hivyo kuathiri usafiri kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi; sambamba na wananchi kuvamia kituo kimoja cha polisi na kuchoma moto nyumba moja ya polisi.
'Ushahidi' wa pili wa dhana kuwa chanzo cha mauaji ya MKIRU ni chuki za wananchi dhidi ya jeshi la Polisi ni ripoti maalum ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi iliyochapishwa Mei 26 mwaka 2017 kwa atakayeweza kuipata.
Kwa kifupi, ripoti hiyo inaeleza kwamba wengi wa wakazi wa MKIRU ni masikini wenye elimu duni, na tegemeo lao kubwa la kipato ni kuvuna raslimali nyingi zilizopo eneo hilo na kuziuza.
Biashara kubwa ambayo vijana wanajihusisha nayo ni uchomaji na uuzaji wa mkaa, uvunaji magogo kwa ajili ya mbao, uuzaji wa kuni na mazao mengine ya mashambani kama vile mpunga na mihogo,hii imeajiri vijana wengi katika maeneo hayo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofanywa na mamlaka za mitaa, maofisa wa Idara ya Maliasili, jeshi la mgambo na polisi, kwa muda mrefu sana.
Licha ya mamlaka husika kuweka lundo la vizuizi, pia wananchi hao walilalamikia 'kodi za kukomoana.' Kwa miaka mingi sasa, wananchi wamekuwa wakilalamikia vizuizi hiyo kuwa kitovu cha dhuluma na uonevu mkubwa wanaofanyiwa wananchi na wasimamizi wa vizuizi ambao wamekuwa wakikadiria kodi za kukomoa, kutaifisha magunia ya mkaa na mbao na mali nyingine za wananchi.
Wananchi hao wanadai kuwa uonevu na dhuluma vimechokoza hasira za vijana wengi, ambao "kazi zao ndio mkaa, kuni na mbao au mihogo." Kuhusu matumizi ya silaha, ilielezwa kuwa vijana wengi katika maeneo hayo wana mafunzo ya mgambo na JKT huku wakiwa hawana ajira nyingine zaidi ya kutegemea biashara hizo.
“Si suala la kidini. Ni manyanyaso tu. Leo unadhulumu watano, kesho kumi, hawa wakiji-organise unatarajia nini?” aliuliza mkazi mmoja wa eneo hilo, na kuongeza kuwa ingawa dhehebu moja la kidini lina vijana wengi lakini halina uhusiano na mauaji.
Kuhusu dhana nyingine kwamba mauaji ya MKIRU yanatokana na ugaidi, kuna 'ushahidi' wa matukio mbalimbali kwa takriban miaka mitano sasa ambayo japo serikali imekuwa ikiyaita kuwa ni ujambazi, yana viashiria vya ugaidi.
Moja ya vitu vinavyoleta ugumu katika kutanabaisha ugaidi au lah, ni kasumba iliyoshamiri kitambo ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wepesi kuwatuhumu wapinzani wao wa kisiasa kuwa wanapanga au wanajihusisha na vitendo vya kigaidi kwa minajili tu ya uhasama wa kisiasa.
Baadhi ya wanasiasa wa chama tawala CCM, kwa nyakati tofauti wamewahi kuvituhumu vyama vya upinzani vya CUF na Chadema, na baadhi ya viongozi na wanachama wake, kuwa wahusika wa ugaidi, tuhuma ambazo mara zote hazikuweza kuthibitishwa.
Japo magaidi hupendelea wafahamike kuwa ndio wahusika wa tukio la kigaidi, kunapojitokeza watu wasio na hatia kutuhumiwa kuwa ndio magaidi, hiyo inaweza kurahisisha kazi ya magaidi halisi.
Katika mlolongo wa matukio mbalimbali yenye viashiria vya ugaidi, Julai 2 mwaka 2017, Rais Magufuli aligusia kuhusu 'Mashehe wa UAMSHO' ambao wapo gerezani kwa zaidi ya miaka minne sasa wakisubiri hatma ya mashtaka ya ugaidi yanayowakabili. Katika hotuba yake jijini Dar, Rais Magufuli aliashiria kuwa kuna uhusiano katika ya mauaji ya MKIRU na mashehe hao wa UAMSHO, huku akiibua taarifa mpya kuwa hata sare 500 za jeshi zilizokamatwa jijini Dar zilikuwa na uhusiano na mashehe hao/ 'ugaidi' huko MKIRU.
Kadhalika, Julai 5 mwaka 2017, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa mauaji ya MKIRU yana 'mkono wa nchi za nje.' Kingine cha muhimu katika maelezo ya IGP Sirro ni kubainisha kuwa mauaji ya MKIRU yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka miwili.
Tukio jingine ni pamoja na lile la Mei mwaka 2016 huko Mwanza ambapo kulitokea mapambano makali kati ya askari wa jeshi la polisi wakisaidiwa na wenzao wa Jeshi la Wananchi dhidi ya kilichoelezwa na serikali kuwa ni genge la majambazi.
Mapambano hayo yalielezwa kuwa na uhusiano na uvamizi kwenye msikiti wa Rahman jijini humo, ambapo kulitokea mauaji ya kutisha baada ya watu wasiofahamika kuvamia msikiti huo na kuwauwa kwa kuwachinja Imamu aliyekuwa akiswalisha swala ya Isha, Ferouz Elias (27) na waumini wawili, Mbwana Rajab na Khamis Mponda
Tukio jingine ni lile la Machi 2 mwaka 2015 ambalo lililozua taharuki miongoni mwa Watanzania wengi kufuatia kuibuka kwa video zenye ujumbe ulioashiria uwepo wa kundi linalopambana na jeshi la polisi kwa sababu za kidini.
Mei mwaka 2016, kikundi kilichojitambulisha kama Ahl Kalf Mujahidina kilitoa wito kwa Waislam kuwa wajiunge nacho, ambapo kilieleza kuwa kimeweka makazi yake kwenye mapango ya Amboni huko Tanga.
Kwa ufupi tunaweza kuwa na nukta saba muhimu katika uchambuzi huu.
1. KUMEKUWA na harakati za muda mrefu za kusambaza na hatimaye kuimarisha ugaidi nchini Tanzania. Katika uchambuzi huu, ushahidi uliotumika umeanzia mwaka 2013, miaka minne iliyopita. Hata hivyo, jitihada hizo za kusambaza/kuimarisha ugaidi zimekuwa kama za kulipuka na kufifia (sporadic), japo kama tukiamini kuwa mauaji ya MKURU ni sehemu ya harakati hizo, basi hitimisho linakuwa kwamba harakati hizo zimefanikiwa kujikita.
2. CHUKI ya wakazi wa maeneo husika zinasaidia kufanikisha harakati hizo za magaidi hao. Katika matrix ya pili iliyobakiwa na dhana mbili badala ya nne za awali, kuna 'consistency' katika 'uhusiano' wa dhana ya ugaidi na chuki ya wananchi. Pengine hili limechangiwa na mamlaka husika kutofanyia kazi vilio vya wakazi wa eneo hilo (rejea taarifa ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi kuhusu maujai ya MKIRU).
3. KAULI ya IGP kuwa mauaji hayo yana mkono wa kutoka nje inapewa uzito na matukio mbalimbali yaliyotumika katika uchambuzi huu. Na katika hitimisho langu, natafsiri kuwa mauaji yanayoendelea katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ni ugaidi unaofanywa na kundi lenye asili ya nje ya Tanzania lakini lenye ufuasi wa kutosha nchini humo, na linapatiwa msaada na wakazi wa eneo hilo.
4. KUHUSU 'mashehe wa UAMSHO,' hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kauli ya Rais Magufuli hivi karibuni iliyoashiria kuwa kuna uhusiano kati sare za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni, mashehe wa UAMSHO na mauaji ya MKIRU. Kinachowezekana ni wahusika (magaidi) wanaweza kutumia suala la mashehe hao kama sababu ya kufanya ugaidi wao.
5. TUKIAFIKIANA kuwa mauaji ya MKIRU yanafanywa na magaidi, na tukiafikiana pia kuwa magaidi hao wanaweza kutumia suala la 'mashehe wa UAMSHO' kama moja ya sababu zao, bado ni muhimu kuepuka kulifanya suala hilo kuwa linatokana na masuala ya kidini. Kama ambavyo kuna wanasiasa wanaotumia mauaji hayo kuendeleza chuki za kisiasa na hatusemi siasa ndio chanzo cha mauaji hayo, ndivyo ilivyo kwa wanaoweza kutumia dini kama kisingizio cha kufanya ugaidi. Hili ni muhimu sana kuzingatiwa kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa MKIRU ni Waislamu, na kuhusisha ugaidi huo na Uislamu/Waislamu sio tu itaathiri uwezekano wowote wa ushirikiano baina ya wakazi wa eneo hilo na vyombo vya dola/serikali bali pia inaweza kuzua balaa la machafuko ya kidini.
6. TUKIAFIKIANA kuwa kinachoendelea huko MKIRU ni ugaidi basi itabidi pia tuafikiane kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji uwekezaji mkubwa kweli intelijensia kuliko matumizi ya nguvu. Taarifa kwamba baadhi ya wakazi wa maeneo ya MKIRU wamelazimika kuhama makazi yao kwa "kuhofia vipigo kutoka kwa Polisi" zinafanya uwezekano wa kupata ufumbuzi kuwa mgumu.
7. KWA wanaofahamu vema pwani ya mkoa wa Pwani sambamba na jiografia yake na mikoa ya jirani watatambua kuwa wingi wa "vipenyo" (ambavyo hadi hivi karibuni vilikuwa vikitumika kama 'njia za panya' kuingiza na kutoa bidhaa mbalimbali) na mtawanyiko wa makazi yaliyochanganyika na mashamba, mapori na misitu, vinaweza kuwa mazingira mwafaka kwa watu hao wenye nia mbaya.
Mwisho napenda kutaadharisha kwamba, Uchambuzi sio lazima ukubaliane na hali halisi na matukio yanayotokea hivi sasa uko Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU) Hakuna anayelazimishwa kuafikiana na uchambuzi huu.
Kwa msaada mkubwa kutoka kwa Rafiki Chahali
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?