KUTENGANISHA ELIMU NI JANGA
Elimu Dunia (Sekyula) na Elimu Akhera (Dini)
Ni utenganisho wenye kuonekana kuwa na faida sana kwenye jamii haswa jamii ya Kiislamu. Ni maneno mazuri ya kuzingatiwa, lakini... Kuna jambo ambalo linatajwa hapo kimantiki na hatujui kuwa limewekwa ndani ya Uislamu bila Waislamu wenyewe kujuwa.
Ni pale tulipotenganishiwa elimu na kuzigawa mapande mawili makubwa, yaani Elimu ya Dini (Kusoma elimu za Fiqh, Sharia, sira Tarekh n.k) na upande mwingine Elimu ya Sekyula (Elimu dunia) kama vile kusomea biashara, uhasibu, fizikia, saikolojia, baiolojia microbiology, chemia n.k.
Huu ni msiba kwa sababu tukiangalia historia (Tarekh) kwenye Uislamu hatukuti hayo mapande hayo mawli ya kielimu. Kwa utenganishi huo tumejizika kwenye kaburi lenye kina kirefu kiasi cha kutupoteza fahamu zetu.
Ajabu tunashindwa kufungua bongo zetu na kujuwa kwanini sura ya kwanza kushuka (surat Alaq - sura ya 96) ilisisitiza sana kusoma, kwa maana ya kujifunza na haikueleza nini cha kujifunza zaidi ni kujifunza kile ambacho hatukijui.
Na hata baba yetu Adam (as) alipoumbwa alifundishwa elimu kama tunavyofahamishwa kwenye Qur'an tukufu:
Surat Baqara 2:31
Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.
Surat Adh-Dhaariyaat 51:56
Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.
Kumuabudu MwenyeziMungu ndio lengo kuu la kuumbwa kwa binadam na majinni, tumepewa akili na utashi ili tuweze kujiamualia mambo yetu, aidha kufata na kutekeleza kile ambacho ndio lengo la kuumbwa kwetu au kukitupa.
MwenyeziMungu kutupatia akili na maamuzi, akatupatia elimu ambazo zitatusaidia kumjua yeye kwa viwango tofauti tofauti kulingana na uwezo wa mtu binafsi.
Surat Fussilat 41:53
Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
Ishara za uwepo wa MwenyeziMungu ni nyingi na miongoni mwa ishara hizo ni elimu mbalimbali tuzisomazo ambazo kwa namna moja au nyingine zinatusaidia kutuweka karibu na Muumba wetu.
Surat Al-An'aam 6:97
Na Yeye ndiye aliye kuwekeeni nyota ili mwongoke kwazo katika kiza cha bara na bahari. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanao jua.
Surat Az-Zumar 39:9
...Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili.
Surat Faatir 35:27
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana.
Surat Faatir 35:28
Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni (Wasomi). Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
Katika ayat hizi tunajifunza kuwa wenye kumcha Allah (s.w) ipasavyo na katika kiwango cha juu cha unyenyekevu ni wale waumini waliobobea katika taaluma mbali mbali za kielimu.
Na hapo hawakutwajwa maulamaa waliobobea kwenye hizo elimu zinazoitwa za dini au akhera tu yaani elimu kama vile Sharia, Sirah, Fiqh, au Hadith tu.
Maulamaa waliopigiwa mfano katika aya hizi ni wale waliozama katika fani za Hali ya Hewa (Meteorologist), uchunguzi wa wanyama (Zoologist), mazao kama mbogamboga (Vegitables), maua (Flowers) na matunda (fruits) na vinavyofanana navyo kwa ufupi hao wanajulikana kwa jina la Kiingereza kama Horticulturist.
Vilevile wametajwa wale ambao wana utaalamu wa jiolojia kama vile Madini (Geologists). Na kuna ayat nyingi tu ambazo zinasisitiza kwenye Qur'an zinazo sisitiza binadamu kuyafanyia utafiti mazingira ya anga na ardhi ili kumtambua Mola wake na kumuabudu ipasavyo.
Kwa Ayat hizo chache tutosheke kuwa elimu zote zenye manufaa kwa binadamu atakazo zisoma mja ziweze kumuweka au kumsogeza karibu na MwenyeziMungu.
Kujuwa Kusoma Qur'an, kujuwa fiqh, sira, tarekh au Sharia vyote hivyo vinaweza kuwekwa na zikaenda sambamba na hizo elimu zilizopewa jina elimu ya sekyula. Kwa sababu elimu hizo ni elimu za msingi (Basic) kwa kila Muislamu.
Ukisomea masomo ya sayansi na ukajifunza bailojia na ukajuwa vipi viungo mbalimbali vya mwili wa binadamu vinavyofanyakazi kama vile moyo, maini, figo, ubongo n.k kwa Muislamu mwenye kumuhofu MwenyeziMungu basi kwa elimu hizo umfanya aweze kumshukuru MwenyeziMungu kwa nehma kubwa tuliyonayo binadamu.
Kama elimu za Sayansikimu zinatuambia tule chakula bora, tuwe wasafi kimwili na kiakili hata Uislamu unatufunza hivyo hivyo.
Kama elimu ya uhasibu inaweza kutuwezesha kutunza mahesabu yetu na hata Uislamu unatufunza hivyo hivyo, maana linapokuja swala la pesa Uislamu unasisitiza kuweka kumbukumbu zake za matumizi na zile zinazo ingia, maana pesa bila daftari upotea bila habari.
Kama elimu ya biashara inatufundisha jinsi ya kufanya biashara kati ya mtu na mtu au kati ya mji na mji au kati ya kampuni na kampuni, tujuwe kuwa hata Uislamu unatufundisha jinsi ya kufanyabiashara kati ya pande mbili.
Kinachotakiwa kwa hao waliobahatika kuzipata elimu hizo ni kungalia na kuziandika upya hizo mitaala (syllabus) ziendane na vile Uslamu unafundisha.
Kama Muislamu kasomea medicine, basi akiwa mahabara, atakuwa na hofu ya MwenyeziMungu na atatumia hofu yake hiyo kutafiti na kutengeneza dawa ambazo zitakuwa faida kwa viumbe na si kutengeneza madawa ya kudhuru viumbe.
Alkadharika kwa wale wengine ambao watakuwa wamesomea, masomo mengine kama Uhasimu (Accountant) nazo zitamfanya awe na hofu kwa kujuwa mizani yake siku ya malipo nayo itakuwa kama vile daftari la uhasibu maana kama kwenye uhasibu kuna kuingiza na kutoa, kuna mali na thamani yake n.k Basi hata maisha yetu ni hivyo hivyo.
Kuna kuingiza na kutoa kwa maana unapotenda jambo jema ni sawa na kuwekeza na unapotenda jambo baya ni sawa na kutoa, na ndio maana tunaambiwa kuwa mwisho wa maisha yetu ya dunia ni pale tutakapo simama mbele ya Muumba wetu na daftari zetu kufunuliwa mbele yetu na tutayaona yale yote tuliyo yatenda.
Sawa na kuwekeza kwenye mabenki, maana kila unapoweka unaongeza kwenye fungu lako na kila unapotoa ni sawa na kutoa kwenye fungu lako la siku ya mwisho.
Uislamu ulipokuwa kwenye utukufu wake, ndipo walipopatikana wanasayansi makini waliogundua mambo mablimbali muhimu vipaji vya watafiti wa Kiislam na wasomi, wanafalsafa na waandishi wa kiislam walioongeza hamasa katika elimu ya sayansi na fasihi, na kuzivuta fikra za watu wa Magharibi.
Uislamu sio tu uliwavutia wanasayansi, bali pia viongozi wa Mashariki na wa Magharibi kutoka Hispania na wa Kirusi na Makhan wa Kihindi pia walivutiwa na taaluma kadhaa ndani ya watafiti wa Kiislamu.
Vituo vyya uchunguzi wa anga vilianza kujengwa katika kila mji maarufu katika Himaya ya Kiislam. Vile vya jiji la Baghdad, Cairo, Cordova, Toledo na Samarkand vilijipatia umaarufu sana duniani.
Chuo cha Baghdad kiligundua kuwa maeneo ya juu ya mwezi hayafuati kanuni maalum. Pia walitabiri kuwepo kwa vituo vya jua, kupatwa kwa mwezi na jua na kuwepo kwa vimondo na madude mengine angani. Walitafiti na kubaini kuwepo kwa mzunguko wa dunia kwa jua. Pia walikuwa watafiti wa kwanza kugundua Copernicus na Kepler.
Ali Ibn Younis, mgunduzi wa (pendulum) timazi au mizani ya saa na vipimo vya jua, ambaye Khalif Al-Haken aliyetawala mnamo miaka ya 990 - 1021, alimwekea kumbukumbu kwa kujengewa kituo cha utafiti wa anga katika Mlima Mucaddam, anaaminika kuwa mmojawapo wa waanzilishi wa Chuo cha Cairo.
Katika hesabu, mpaka leo bado tunatumia tarakimu na njia za kufanyia hesabu zilizogunduliwa na Waislamu. Uvumbuzi wa Aljebra unahusishwa moja kwa moja na Waislam.
Wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Maarifa, Khalif Al- Mamun alimteua Mohammad Bin Mussa Bin Khwarizimi kuwa Mkuu wa Kituo hicho.
Tasnifu yake katika aljebra inaitwa: "Al-Gebr Wal-Muqabala (yaani Hesabu kwa njia ya Alama)". Ni kutokana na sehemu ya kwanza ya kazi yake hii tulipopata jina la hesabu za "algebra" na kutokana na jina lake pia tumepata "algorithm".
Kazi hii, kama ilivyotafsiriwa na Mzungu aitwaye Gerad mwenyeji wa Cremona, alisema:
"Baada ya kuwa msingi wa jumba la hesabu lililojengwa na Waislamu waliomfuatia baadaye, alikuwa na wazo la kuanza kuwafundisha watu wa Magharibi juu ya ubora wa kutumia aljebra katika kufanya hesabu za ukokotozi (algebraic calculus) pamoja na desimali."
"Mojawapo ya mawazo bora ya kisayansi toka kwa wasomi wa Kiislam, Al- Khwarismi bila shaka ni mtu aliyetoa mchango bora katika maendeleo ya somo la Hisabati wakati wa zama za karne za Kati na hata sasa." kama anavyodhani Philip Hitti.
Kazi yake iliendelezwa na Thabit bin Gharrah, aliyefasiri Almagest, kazi ya Ptolemy, aliyegundua matumizi ya algebra katika hesabu za changanuzi (jiometri au geometry).
Hadith
Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Muislamu.
Ibn Maajah.
MwenyeziMungu Anasema Kwenye Qur'an: Surat Az-Zumar: 39:9
Je wanalingana wale wanaojua na wale wasiojua?
Al-Mujaadalah: 58:11
...Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu.
Kwa kuhitimisha makala hii fupi, tunapaswa kuzingatia jambo moja ambalo wengi wetu halitulitii akilini, jambo lenyewe ni kuwa kama pangelikuwepo na mgawanyo wa elimu na kuwa elimu ya lazima kutafutwa na Waislamu ni ile iitwayo "elimu ya dini" kwanini Mtume (saw) aliwaamuru Waislamu kuwa kutafuta elimu ni fardhi na hakusema elimu gani kwa sababu anajuwa kuwa elimu zenye faida ndizo zitakazotukurubisha kwa MwenyeziMungu.
Kwa kuhitimisha makala hii fupi, tunapaswa kuzingatia jambo moja ambalo wengi wetu halitulitii akilini, jambo lenyewe ni kuwa kama pangelikuwepo na mgawanyo wa elimu na kuwa elimu ya lazima kutafutwa na Waislamu ni ile iitwayo "elimu ya dini" kwanini Mtume (saw) aliwaamuru Waislamu kuwa kutafuta elimu ni fardhi na hakusema elimu gani kwa sababu anajuwa kuwa elimu zenye faida ndizo zitakazotukurubisha kwa MwenyeziMungu.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?