WAISLAMU hodari kumi tu waliolinda nchi
Huo ni mmoja ya misemo mashuhuri katika enzi za Yuam nchini China ikiisifu juhudi ya Waislamu kutokana na uhodari wao wa juu katika “wushu" (sanaa ya mapigano “Wushu"ya Waislamu wa China na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao.
HIVI leo huwezi ukaizungumzia historia ndefu ya sanaa ya mapigano ya Uchina na ikawa kamili bila kutaja mchango wa Waislamu katika kuiboresha fahari ya taifa hilo (martial art), ambayo kwa sasa imeshatoka nje ya mipaka ya nchi hiyo ya Asia na kuendea kote duniani.
Ujasiri wa kutenda, nidhamu iliyokomaa (si nidhamu ya woga kama walivyo baadhi ya Waislamu). Afya njema, utoaji wa hoja zenye mashiko, umoja, hekma, na nguvu inapohitajika ni miongoni mwa sifa za msingi za Waislamu wa China zinazoinawirisha sanaa ya kisasa ya mapigano ya nchi hiyo.
Mapambano ya kutumia mikono kwa kubadilishana makonde sura kwa sura, mtu na mtu au mtu na watu ni moja ya aina za wushu ya Waislamu.
Kutumia ala nzito na nyepesi, fupi na ndefu, kali na butu ni sehemu nyingine ya Wushu ambayo Waislamu wa China wanajivunia kuwa nayo.
Tukirejea katika ngumi (makonde) moja ya aina mashuhuri za ngumi ambazo Waislamu wanatumia toka katika utajiri wao mkubwa wa “Wushu" ni makonde ya “cha" yaliyoanzishwa katika zama za Ming na kuimarika vyema wakati wa Qing.
Mwanzilishi wa makonde hayo ni kijana mbichi aliyeitawala Chamir, aliyetokea China Magharibi.
Kwa mujibu wa historia ya Waislamu China kijana huyo mwenye moyo thabiti wa kimapindizi na nia ya kujifunza, alikuwa katika wito wa mfalme wa kuwatimua wavamizi wa Kijapani katikati ya enzi za Ming ambapo alijivuta hadi kijijini Zhangyin Zhuang wilayani Guan mkoani Shandong alipopata maradhi ya homa ya matumbo.
Hapo alipokelewa na Waislamu waliomuuguza vyema hadi kupona kwake. Ni wakati huo kijana Chamir alipowafunza Waislamu hao staili moja ya makonde kama shukrani ya kumkirimu.
Kwa heshma na kumbukumbu yake, Waislamu wa Zhangyin Zhuang wakayaita makonde hayo jina la Chamir kwa kifupi “Cha". Na tangu hapo aina hiyo ikavuka mipaka ya Guan na kuendea katika maeneo mengine ya nchi.
Historia inatufuhamisha kuwa kwa ujumla Wushu ya Waislamu wa China ina tabia ya Wushu ya kabila la Wahan na tabia nyingine ya kabila la Wahai ambayo ni miongoni mwa makabila 56 yanayofuata Uislamu ipasavyo nchini China, yakiwa na jumla ya Waumini wasiopungua milioni 14 na misikiti isiyopungua 30,000 mikoani kote.
Katika maandiko yake kuhusiana na Uislamu nchini China, msomi mashuhuri wa Kiislamu nchini humo Bw. Feng Jinyilan katika kile alichokiita: “Marejeo teule juu ya Uislamu Uchina" pamoja na Bw. Li Xinghua wakieleza historia ya jamii hiyo, wanaonisha wazi kwamba nyakati za mwisho za zama za Ming, sanaa ya mapigano (martial Art) ilikuwa mashuhuri na kutandawaa nchi nzima.
Mnamo mwaka 1642 Bw. Li Zicheng kiongozi wa Mapinduzi ya Wakulima alizunguka mji wa Chengzhou.
Miongoni mwa wapiganaji alio watumaini mno, ni wale mastadi wa Wushu wa Kiislamu wasiopungua 300 waliokuwa chini ya imamu katika kambi maalumu. Pia alikuwapo jemedari wa Kiislamu aliyeitwa Ma Shaouying aliyeongoza kikosi cha Waislamu kilichojiunga na mapinduzi ya mwishoni mwa enzi yautawala wa Ming uliong’olewa mamlakani na madarakani mapema mwaka 1644. Huo ni ushahidi wa wazi wakuonyesha mchango wa Wushu ya Kiislamu katika kuleta mageuzi nchini China.
Historia inatufahamisha kwamba mnamo mwaka 1616 hadi 1911 (Enzi ya Qing) dhulma, unyanyasaji uliopea toka kwa watawala wenye mamlaka na madaraka katika jamii iliogubika jamii ya Waislamu.
Hivyo basi Waislamu hawakuvumilia uonevu huo dhidi yao, wakaanzisha mapambano makubwa ya mfululizo dhidi ya madhalimu.
Waislamu walitambua kwamba wakitaka kulinda dini yao, iliwabidi kuwa na afya njema, kwa hiyo hulka za ujasiri, umoja na kuto ogopa watu wenye mabavu zikalelewa na kuimarishwa. Katika misikiti ya kila pahala zilitengwa nyanja za kufanyia mazoezi ya Wushu kila saa za asubuhi, jioni na baada ya sala, watu wote (waumini wote) walijikusanya pamoja kufanya mazoezi ya kuinua ustadi wa Wushu (sanaa ya mapigano).
Katika hali hii ya mazingira ya kijamii, wushu ya Waislamu iliendelea kwa upesi na wakatokea wanafunzi hodari wa Wushu kizazi kwa kizazi.
Rejea Feng Tinyuan kwenye Uislamu katika China, wushu ya Waislamu Uk. 71-72. Foreing language press Baiwanzhuang – Beijing.
Tarehe inaonyesha wazi kwamba mwaka 1911 hadi 1949 (zama za Jamuhuri ya Uchina) kabila la Wahui (ambalo ni moja ya makabila ya Waislamu) kulikuwa na mabingwa wengi mno wa Wushu ukimuacha bingwa mashuhuri Bw. Liu Baonii.
Miongoni mwao ni Chan Zhengfang, muumini mzuri wa Kiislamu kijijini Zhanyying Zhuang, wilayani Guan huko Shandong.
Bwana huyu alihamia Honan mbeleni. Uhodari wake wa sanaa ya mapigano uliwaacha wengi vinywa wazi.
Matunda yake ni pamoja na mabingwa mashuhuri hivi leo nchini humo na duniani kiujumla kama kina Zhanga Xitai, He Zhengquan, Ma Zhenbag na wengineo wengi walioendea hasa katika mikoa ya Shanzi, Hebei, Shandong, Honan, Shaanxi, Jiangsu, Shanghai na hata Hubei.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni za kile kinachojulikana kama “China mpya", asili ya wanawushu wa Kiislamu wa kabila la Hui, imepata maendeleo maradufu.
Mnamo katikati ya karne hii, waumini wa Kiislamu wa Shandong na Hebei wameasisi taasisi muhimu ya kuchunguza kwa undani zaidi sana ya mapigano ya Kiislamu toka kabila la Wahui.
Chama cha sanaa ya mapigano ya Kiislamu katika misikiti kikaasisiwa kuendeza fani hiyo kwa ummah.
Wakawataka mastadi wa Wushu ya Kiislamu kuzama chini mno katika sanaa hiyo azizi hivyo kurejesha utaalamu wa Wushu wa kale ili usipotee.
Hivi sasa wanataaluma hiyo wenye ubingwa wa hali ya juu sana katika umma wa Kiislamu Uchina, wananza kupokea kwa wingi wanashule wa rika zote (wazee, watoto kwa vijana, wake, kwa waume) kuwafunza wushu; na mkazo mkubwa umewekwa kwa kizazi kipya, na matunda yake yanaendelea kuonekana.
Kwa mujibu wa mtafiti mashuhuri wa Kiislamu, Feng Jinyuan, wushu ya Kiislamu ya kabila la Wahui inatabia zake mahsusi, ameainisha baadhi yake kama ifuatavyo:
Waislamu wa Kihui wanahistoria ndefu ya uchezaji wa wushu. Kila kizazi kilikuza na kinaendelea kutoa mastadi ambao wametoa mchango mkubwa mno katika kuiboresha na kuitajirisha sanaa ya mapigano (wushu) ya China.
Fani hiyo iliasisi kwa nyakati za Ming na kustawishwa sana enzi za Qingna ikawa ni jambo la lazima kujifunza mbinu za kujihami ili kulinda maisha ya jamii katika zama za udikteta na ukandamizaji wa kitaifa. Sanaa hiyo ilifanya kazi isiyosahaulika katika jamii hususan kuimarisha afya, kujenga kuta imara za hulka ndani ya jamii ya Kiislamu hasa za kuvumilia shida na kusaidiana.
Aidha, kutoogopa kufanyiwa ukatili, kuwa wakarimu na kusaidia wengine na kutetea kwa nguvu zote haki katika jamii.
Sanaa hiyo ina taaluma nyingi, ambazo ni matokeo ya maendeleo ya mfululizo juu ya msingi wa kupokea vilivyo bora toka kwa wengine, kufafanua na kurekebisha kizazi kwa kizazi hata kufikia sasa.
Sanaa hiyo inatazamana na kipindi kipya cha maendeleo, imeshakuwa harakati za kawaida za nadharia za kuimarisha afya za watu na umoja wa makabila toka haja za kulinda kabila, dini na kujilinda katika jamii ya kimwinyi. Sasa Wushu imeenea zaidi.
Kiuhakika sanaa hiyo ya Kiislamu inayopendwa kote duniani hata sasa bado haijatiliwa uzito na jamii nyingine za Kiislamu hasa za Afrika ya Mashariki kama Tanzania, kinyume chake inawafaidisha watu wa jamii nyingine wasio na asili nayo kuwakandamiza Waislamu!
Ukiacha wenzetu wa China wanaozifuata kwa vitendo sunna za Bwana Mtume (saw) si kwa kumpigia dufu na kula pilau tu, Waislamu wenzetu wa Afrika Kusini wanaikaribia Uchina katika nyanja hiyo.
Baadhi ya taasisi za Kiislamu zimelifanya somo la sanaa ya mapigano (Martial art) kuwa ni moja ya masomo muhimu kabisa kwenye shule zao, kuanzia madrasa za mitaani, shule za watoto wadogo hadi vyuo vya elimu ya juu.
Zipo baadhi ya madrasa zimefikia hatua ya kuwarudisha darasa (kurudia mwaka) kwa wale wanafunzi waliofeli vibaya somo hilo. Miongoni mwa mitindo niliyowahi kuiona ikitumiwa sana nchini humo na baadhi ya taasisi za Kiislamu ni pamoja na Carate ya Kijapan maarufu sana kwa jina la ‘Goju lau’ mtindo ambao unafunza mbinu ngumi na staili za kujihami.
Mitindo mingine ya mapigano ni pamoja na Judo, Kungfu, Shaolin, Taiji na Taiji Boxing, na hata shotokan na Tiechi (inner structure na outer structure).
Mitindo hiyo pamoja na Tao na Yoga wameirekebisha kidogo na kuiweka katika sura ya Kiislamu. Hivyo kama Uchina ni mbali tunaweza kujifunza mengi kwa ndugu zetu karibu.
Wapo vijana wengi wa Kiislamu East Afrika ambao ni mabingwa katika sanaa ya mapigano, hata hivyo ustadi wao unawasaidia (unawanufaisha) madhalimu. Ni vyema tukiitafuta njia nzuri ya kuwarejesha mastadi hawa wausadie Uislamu na Waislamu wenzao. Itakuwa vizuri Waislamu na taasisi zao hasa misitiki mwashule na madrasa za mitaani wakianza programu hiyo sasa.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?