MZEE FARAJA FOROJO GANZE
Wengi wetu tumebahatika aidha kushiriki au hata kuchangia mbio za Mwenge wa uhuru wa Tanganyia (Tanzania), lakini ni wangapi kati yetu tunajuwa asili haswa ya huo Mwenge!?
Ipo siri kubwa kuhusu Mwenge wa Uhuru ambao hukimbizwa nchi nzima. Wapo wanaodhani kwamba aliyeleta mabadiliko katika nchi kwa kuanzishwa kwa mwenge huo ni Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere lakini kiukweli haswa Mwalimu Nyerere si mwanzilishi wa Mwenge wa Uhuru.
Mnajimu maarufu ambaye sasa ni marehemu, Sheikh Yahya Hussein aliwahi kusema na ikaandikwa kwamba mvumbuzi wa wazo la kuwa na Mwenge wa Uhuru ni Forojo Ganze ambaye alikuwa ni mmoja kati ya wazee waliotumwa kufanya zindiko la nchi baada ya uhuru mjini Bagamoyo mkoani Pwani.
Forojo Ganze aliyezaliwa mwaka 1902 alifuatana na wazee wengine kwenda kwenye zindiko Bagamoyo ili Mwalimu Julius Nyerere aweze kutawala vema.
Wazee hao na miaka yao ya kuzaliwa kwenye mabano ni Mzee Ramadhan (1920), Ally Tarazo (1929), Komwe wa Komwe (1918) na Sheikh Yahya Hussein (1925).
Wazee hao walipewa kazi hiyo na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam enzi hizo kuhakikisha rais aliye madarakani hapingwi na mtu yeyote, zindiko hilo lilifanyika Bagamoyo katika moja ya mashimo yanayopatikana wilayani hapo na baadaye Mwalimu Nyerere alipelekwa Bagamoyo, akachinjwa mbuzi na Nyerere akaambiwa atambuke (aruke damu) baada ya kutokula kutwa nzima (alifunga), jambo ambalo aliwahi kukiri hadharani katika moja ya hotuba zake.
Sheikh Yahya Hussein alinukuliwa akisema hata hivyo, katika mashimo yale Forojo Ganze ndiye mtu pekee aliyeingia katika moja ya shimo kwa ajili ya kuuliza mizimu na aliwaacha wenzake nje wakimngoja ili kujua atakuja na jibu gani ili wakampatie rais na wazee wa Dar es Salaam.
Utamaduni wa rais kuongea na wazee wa Dar es salaam unaendelea hadi sasa na wamekuwa na maamuzi ya kitaifa na husikilizwa sana wanachokisema, zindiko la Bagamoyo linafanya kazi.
Kilichoshangaza, alisema ni mtu huyo kuingia shimoni na kukaa siku kumi na siku ya kumi na moja alipotoka alikuwa hoi hajiwezi akiwa kama mtu aliyepigwa, na alikuwa akiongea lugha hisiyojulikana.
"Tulimchukua akiwa hoi hadi Ikulu Dar es Salaam na tulimfikisha mbele ya Mwalimu Nyerere na akatamka maneno yanayotumika au yanayohusu Mwenge wa Uhuru kwa Kiswahili kisha akanyoosha juu mkono wake wa kulia ambao tayari ulikuwa umeandikwa namba hii 115, kisha akakata roho," alisema Sheikh Yahya.
Akinukuu maneno hayo Sheikh Yahya alisema Forojo alimwambia Nyerere:
"Baba, sisi tunataka kuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini mahala pasipo na tumaini, faraja palipo na huzuni, tumaini pasipo na tumaini, upendo penye chuki na heshima palipo na dharau."
Baada ya kutamka hayo mbele ya Mwalimu Nyerere, Ganze alikata roho na siku chache baadaye Mwalimu Nyerere akayafanyia kazi maneno yake na kuanzisha Mwenge wa Uhuru ambao ulipandishwa Mlima Kilimanjaro na Kapteni Alexander Nyirenda aliyekuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)," alisema Sheikh Yahya.
Hata hivyo, mtaalam huyo wa unajimu alisema kilichowashangaza wengi ni maneno yaliyoongozwa yasemayo "UMULIKE NJE YA MIPAKA YETU ULETE TUMAINI" akahoji ina maana ndani ya nchi tubaki gizani? Sheikh Yahya Hussein alisema anashangazwa kwa nini Forojo Ganze hakutangazwa kama mwanzilishi wa Mwenge wa Uhuru kwani baada ya mazishi ya Forojo, ulianzishwa ambao ulikimbizwa nchi nzima mara tu baada ya uhuru mwaka 1961 na unaendelea kukimbizwa hadi sasa.
Nyerere alimuagiza Sheikh Yahya Hussein atafsiri maana ya ile namba 115 aliyokuwa ameiandika mkononi Forojo akamwambia:
"Namba 115 maana yake utakufa ukiwa na umri wa miaka 77 na Taifa la Tanzania kwa kipindi hicho litakuwa na umri wa miaka 38," na ndivyo ilivyokuwa.
Mwaka 1999 Mwalimu Nyerere alikufa akiwa na miaka 77 na taifa lilikuwa na miaka 38 ya uhuru na 77+38 =115, namba aliyoiandika Forojo Ganze mkononi.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?