Tuesday, 24 April 2018


UISLAMU UNASEMAJE JUU YA UGAIDI?
 Uislamu, Dini ya Rehma, Hauruhusu Ugaidi. 

Kwa hakika kila mwadilifu anapoangalia historia ya ulimwengu tangu mwanzo mwa wanadamu atatambua kwamba haifai kwa njia zo zote kunasibisha ugaidi kwa dini, madhehebu, taifa au hata nchi, kwa sababu dini hazikuteremshwa isipokuwa kwa kueneza usalama, amani na upendo baina ya wanadamu wote. 

Tukiangalia kwa makini vile vyanzo vya ugaidi tutagundua kwamba ugaidi una misingi mbali mbali lakini kuna vitenda kazi mbili kuu ambazo ni:
  1.  Kuwa  na misimamo mikali kujiunga kwa dini, madhehebu au taifa fulani, 
  2.  Chanzo cha pili ni:  kutozingatia hali za vijana kifikra, kimafundisho, na kijamii kwa ujumla ambapo vijana ndio lengo kuu la makundi ya kigaidi, na wakiwa na maandalizi mazuri watapata ukinga dhidi ya ugaidi na mawazo makali yanayoenezwa na makundi ya kigaidi.
Basi kuwa na misimamo mikali na kutowakinga watu hasa vijana ndizo sababu mbili kuu za kuzuka ugaidi unaopelekea jinai za maangamizi na kupoteza amani ya watu wote bila ya kuangalia dini zao.

 Wazo jingine  linalojitokeza katika makala hii ni kwamba ugaidi sio Uislamu wala hakuna uhusiano na dini ya Kiislamu, bali ni maradhi na balaa iliyoenea ulimwenguni kote; mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

Kwa kweli ugaidi ni maradhi ya kijamii kabla ya kuwa hali au changamoto inayosababisha maangamizi na wasi wasi mkubwa zaidi duniani.

Kwa hiyo tunawahotubia wale wanaosisitiza kuutuhumu Uislamu kuwa ni dini ya kigaidi wakaijaribu kufungamanisha dini na jinai wanazozifanya baadhi ya wafuasi wake bila ya kujali kwamba wahusika wa jinai hizo ni wachache wasiomathilisha Uislamu na wanaojiweka nje ya mipaka ya dini wakavuka misingi yake kwa halifu zao.

Kwa kweli aghalabu ya watu hao wanaopendelea kuunganisha baina ya ugaidi na Uislamu hutafuta maslahi yao hasa kama vile, kuzidisha chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, kupitia kwa kudhihirisha dini hiyo na wafuasi wake katika sura ya dini ya vurugu na ukatili.

Bila shaka hayo ndiyo mawazo batili kwani Ugaidi sio hasa kwa Waislamu tu, bali kinyume kuna magaidi wengi wasio Waislamu, vile vile hasara na waathirika wa jinia za kigaidi ni wanadamu wote wakiwemo Waislamu wenyewe, zaidi ya hapo Waislamu wanapata hasara kubwa zaidi kuliko wengine kutokana na ugaidi ambapo wanapata hasara ya kimada kati ya nafsi, nyumba na pesa pamoja na hasara nyingine ya kimaana kwani wanatuhumiwa wakati wote kwa kuhusika juu ya maangamizi yanayosababishwa na ugaidi huo, ilhali wao ni wahanga miongoni mwa wahanga wa jambo hilo.

La kuzingatiwa hapa ni kwamba dini ya Uislamu imekuja kwa ajili ya kuwaongoza watu kwenye njia sawa na kuwaokoa kutoka kila linaloweza kuwasababishia madhara, Je, dini kama hiyo inawezekana kuhimiza mauaji na kuwafanyia watu jinai za kikatili?!

Jambo la kukumbukwa hapa ni kwamba ugaidi hautokani na wWaislamu peke yao, bali anayeangalia hali ya mambo hasa siku hizi atatambua kuwa baadhi ya vitendo vya kigaidi vimefanywa na wasio Waislamu.

katika hali zote haifai kuituhumu dini yo yote kuhusika ugaidi. Ikiwa wazo hilo linaweza kukubalika basi, tunaweza kuutuhuma chama cho chote kuwa ni chama cha kigaidi kama vile; vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali kwani wafuasi wa vyama hivyo hufanya uadui wakifuata mtindo wa kuwahofisha wengine wakati wote.

Pia, kuna baadhi ya makundi yasiyofuata Uislamu kama vile kundi la Anti-Balaka  nchini Afrika ya Kati linalotekeleza jinai mbaya dhidi ya waislamu na kuwasabibisha mauaji makubwa.

Pia kuna kundi la  "Lord's Resistance Army"  huko Uganda ambalo linatekeleza makosa ya kikatili dhidi ya wanadamu na linalengea kuondoa utawala wa Uganda na kuanzisha hukumu ya kidini ya kikristo, na huku Ujerumani kuna harakati ya  "Pegida"  linalotekeleza mashambulizi makali dhidi ya Waislamu.

Na inasisitizwa kwamba kuituhumu dini ya kiislamu kwa ugaidi inalengea kuwasha moto wa uadui baina ya waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo. Zaidi ya hayo yanayotokea katika Afrika ya kati kuwa ni  "Ugaidi wa Kikristo"  kwa sababu dini ya Ukristo haikuamrisha kwa kufanya mashambulizi hayo japokuwa wanaofanya uadui huo ni wakristo.

Wakati huo huo tunasisitiza kwamba wanayoyafanya wanachama wa makundi ya kigaidi yanayojiita makundi ya kiislamu kama vile  Daesh  (ISIL, ISIS) , Boko Haram, Al-Shabab, Taliban  na makundi mengineyo hayamaanishi kuwa Uislamu umewaamuru kufanya jinai hizo, bali kinyume Uislamu umesisitiza sana kuheshimu nafsi hata ikiwa nafsi ya mnyama.

Kwa hakika makundi haya yanatekeleza mikakati ya kiadui na hao hao wanao nyooshea vidole Waislamu wakisababisha maangamizi kwa wananchi kwa ujumla ambapo waislamu na wasio waislamu hupatwa na athari mbaya na maumivu kutokana na taharuki za makundi hayo. Hapo ndipo tunataka kutoa baadhi ya maswali kwa wale wanaofungamanisha Ugaidi na Uislamu.

 • Je, Nchi ngapi zisizo za kiislamu zinateseka kutoka ugaidi kulingana na nchi za kiislamu zinazoharibika kutokana na hali hiyo?
 • Je, idadi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi wengi zaidi ni Waislamu ama wasio Waislamu?
 • Makundi hayo ya kigaidi  yanalengea wasio waislamu tu ama wanalengea wanadamu wote bila ya kujali dini wala taifa?

Katika Qur'an, MwenyeziMungu Amesema:
"MwenyeziMungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika MwenyeziMungu Huwapenda wafanyao uadilifu." Qur'an, 60:8 

Mtume Muhammad  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akiwakataza askari dhidi ya kuwaua wanawake na watoto,[1] na alikuwa akiwashauri:  ...Msisaliti, msizidishe sana, msimwue mtoto mchanga.[2]

Alisema pia: Mwenye kumuua mtu aliye katika mkataba na Waislamu, hataipata harufu ya Peponi, ingawa harufu yake hupatikana mpaka katika umbali wa mwendo wa miaka arubaini. [3]

Kadhalika, Mtume Muhammad  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amekataza kutoa adhabu ya moto.[4]

Kuna wakati aliorodhesha dhambi ya kuua kuwa ya pili miongoni mwa madhambi makubwa,[5]

Hata akatahadharisha hilo juu ya Siku ya Hukumu, Kesi za mwanzo kuhukumiwa baina ya watu ka tika Siku ya Hukumu zitakuwa ni zile za umwagaji damu.[7]

Waislamu huhimizwa hata kuwa wakarimu kwa wanyama na wamekatazwa kuwadhuru. Mtume Muhammad  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alisema siku moja:

Mwanamke aliadhibiwa kwa sababu alimweka paka kifungoni mpaka akafa. Kwa minajili hii, aliangamiziwa Motoni. Wakati alipomweka kifungoni, hakumpatia paka chakula wala kinywaji, wala hakumwacha huru ale wadudu wa ardhini.[8]

Pia alisema kuwa kuna mtu alimpatia kinywaji mbwa aliyekuwa na kiu kikali, hivyo MwenyeziMungu Alimsamehe madhambi yake, kwa kitendo hiki. Mtume  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa:

 "Ewe Mjumbe wa MwenyeziMungu! Je, sisi hulipwa kutokana na ukarimu wetu kwa wanyama?" 

 Alijibu: Kuna malipo kwa ukarimu kwa kila mnyama hai au mwanaadamu.[9]

Zaidi ya hayo, wakati wa kuchinja mnyama kwa ajili ya chakula, Waislamu wameamrishwa kufanya hivyo katika namna inayopelekea hofu ndogo na mateso madogo sana kwa mnyama, kadiri itakavyowezekana. Mtume Muhammad  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

Mnapomchinja mnyama, fanyeni katika njia iliyo bora zaidi. Mchinjaji akinoe kisu chake kwa ajili ya kupunguza mateso ya mnyama.[10]

Kutokana na mwangaza wa haya na mafundisho mengine ya Kiislamu, kitendo cha kuchochea khofu katika nyoyo za raia wasio na ulinzi, uharibifu wa majengo na mali, ulipuaji mabomu na kuwalemaza wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia, yote haya yamekatazwa, tena ni matendo ya kuchukiza kwa mujibu wa Uislamu na Waislamu.

Waislamu wanaifuata Dini ya amani, huruma na msamaha, na wengi hawahusiani na matukio ya vurugu ambayo baadhi yamehusishwa na Waislamu. Ikiwa Muislamu mmojawapo atajihusisha na kitendo cha kigaidi, mtu huyo atakuwa katika hatia ya kukiuka sheria za Uislamu.

Mwishoni tunapaswa kuutambua ugaidi kuwa ni janga la kibinadamu linalowajibika kushirikiana baina ya wanajamii wote kwa viwango tofauti kwa ajili ya kupambana nalo kupitia kwa mapambano ya kifikra na pengine mapambano yenye kutumia nguvu.

Pia haikubaliki kuzingatia kwamba msingi ya ugaidi na chanzo chake ni dini, kwani kuna magaidi wengi mno hawajui cho chote kuhusu dini ambapo wakiwa waumini wa kweli hawakujiunga na makundi haya wala hawakujipoteza katika njia zile.

Jamii ya kimataifa kwa kiwango cha kirasimu ambapo serikali, jumuiya za kimataifa n.k, ina majukumu mengi kupigania vita ugaidi lakini sisi pia tuna wajibu katika vita hiyo dhidi ya adui hatari zaidi siku hizi.

Basi badala ya kubadilishana tuhuma kuhusika juu ya kuzuka ugaidi lazima tushikamane ili tufanye juhudi za kupambana nao bila ya kusimama mbele ya madai ya kufungamanisha dini na ugaidi ambayo ni batili kabisa.


 [1] Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 1744, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 3015
 [2] Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 1731, na At-Tirmidhiy, Na, 1408
 [3] Imeandikwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 3166, na Ibn Majah, Na. 2686
 [4] Iko ndani ya Abu Daawuud, Na. 2675
 [5] Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 6871, na Swahiyh Muslim Na. 88
 [6] Hii inamaanisha kuua na kujeruhi
 [7] Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 1678, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 6533
 [8] Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 2422, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 2365
 [9] Hadiyth hii ya Mtume Muhammad  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) imeelezwa kwa kirefu hapo nyuma. Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim Na. 2244, na Swahiyh Al-Bukhaariy Na. 2466
 [10] Imeandikwa katika Swahiyh Muslim, Na. 1955 na At-Tirmidhiy, Na. 1409

---
Huu ni mkusanyiko wa makala mbalimbali kutoka vyanzo kadhaa, umehaririwa upya ili kuweza kueleweka kwa wepesi na kwa urahisi kwa wasomaji.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!