MJUWE MZEE JUMBE MUHAMMAD TAMBAZA
Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, alizaliwa January 1891 ni mmoja katika wapigania uhuru mashuhuri wa nchi hii ambao, historia inawataja kama ni watu waliotoa mchango mkubwa sana katika kufanikisha kumng’oa Mkoloni Mwingereza, katika ardhi yetu tukufu.
Hayati Mzee Tambaza, ambaye alifariki mnamo July 21, 1978. Ikiwa ni miaka 40 tangu kifo chake , anaingizwa katika kundi moja la watu wa mwanzo kabisa waliompokea kwa furaha na upendo kijana Julius Nyerere kutoka Butiama, alipofika jijini Dar es Salaam kwa kumuunga mkono ‘mia kwa mia’, katika harakati zake za kupigania uhuru wa Tanganyika kwenye miaka ya 1950s.
Wanaharakati wengine aliokuwa nao ni pamoja na Mzee Mwinjuma Mwinyikambi wa Mwananyamala; Mzee John Rupia wa Mission Quarters; Sheikh Suleiman Takadir; Sheikh Haidar Mwinyimvua (Kisutu); Mzee Max Mbwana (Kariakoo); Zubeir Mwinshehe Mtemvu (Gerezani) pamoja na familia ya Mzee Azizi Ali (Mtoni) na ile ya Kleist Sykes (Gerezani), Dar es Salaam.
Ukoo wa Diwan Tambaza Zarara bin Mwinyi ndio waliokuwa wenyeji wa maeneo ya katikati ya jiji wakati huo, wakihodhi eneo la ardhi yote ya Upanga, iliyosambaa kuanzia Daraja la Selender kuelekea Palm Beach Hotel, hadi Ikulu ya Magogoni kwa upande mmoja; na kwa upande mwengine maeneo yote kutoka Aga Khan Hospital, Ocean Road Hospital, Kivukoni Front (makaburi ya asili ya wanandugu wengine yako pale Wizara ya Utumishi, Magogoni) kwenda Mnara wa Saa pale Uhuru Street na vilivyomo ndani yake.
Habari zinasema kwamba, katika siku za mwanzo tu za kupambana na Mwingereza, wazee mashuhuri wa hapa Dar es Salaam walikutana na kuamua kumfanyia ‘zindiko’ na ‘tambiko’ la kijadi, pamoja na kumwombea dua maalumu kijana mdogo, Julius Nyerere, ili kumkinga na waovu na pia kuifanya nyota yake ing’are juu ya wote wenye nia mbaya naye; wakiwamo watawala wa Kiingereza, hasa Gavana Twinning.
Katika moja ya hotuba zake za kuaga aliyoitoa mnamo Novemba 5, 1985, Nyerere alilikumbumbuka tukio hilo na hapa chini anasimulia:
“…Mimi nimeanza siasa na wazee wa Dar es Salaam; na wazee wa Tanzania…na mambo makubwa kama haya kama hayana baraka za wazee hayaendi… huwa magumu sana. Wanasema ngoma ya watoto haikeshi! Mimi nilipata baraka za wazee tangu zamani; tangu awali kabisa.
“Sasa siku moja, Dosa akanifuata Magomeni (nyumbani kwake) akasema: ‘Leo wazee wanakutaka. Wapi? Kwa Mzee Jumbe Tambaza. Wanakutaka usiku. Nikasema haya, nitakuja. Nikaenda. Nikakuta wazee wameshakaa wameniita kijana wao kuniombea dua. Mimi Mkristo wao Waislamu watupu. Wakaniombea dua za ubani. Tukamaliza.”
Anahadithia Mwalimu na kuendelea:
“Tulipomaliza wakasema kuna dua pia za wazee wao. Basi wakanitoa nje. Tukatoka. Zilipomalizika… zilikuwa za Korani; sasa zikaja dua za wazee… za jadi, “…walikuwa na beberu la mbuzi… wamechimba shimo. Wakaniambia simama. Nikasimama beberu akachinjwa huku anaambiwa Twinning ‘umekwisha’… nikaambiwa tambuka… nikavuka lile shimo na baada ya hapo nikaambiwa …basi nenda zako kuanzia leo Twinning amekwisha!”
Mwalimu alimaliza kusimulia namna alivyofanyiwa dua na tambiko nyumbani kwa Mzee Tambaza, Upanga jijini.
Kutawaliwa na Wazungu kuliwakera na kuwakasirisha watu wengi sana, kutokana na kule kudharauliwa ndani ya nchi yao wenyewe na watu wengine; hasa pale walipominywa katika kupatiwa huduma muhimu kama elimu bora, matibabu na mahala pazuri pa kuishi.
Pamoja na mambo mengi mengine yaliyokuwa mabaya kutokana na kutawaliwa, yamo pia na yale ya kuwekwa kwa madaraja katika utoaji huduma muhimu. Sisi, wana wa nchi hii, hatukuwa na shule za maana hata kidogo; watu wote sisi tukasomee shule moja tu (Mchikichini) mpaka darasa la nne; kwa nini hasa kama siyo dharau?
Nyumba zetu za kukaa zilikuwa za ovyo zilijengwa kwa miti na kukandikwa udongo na juu ni makuti, tena hapa hapa mjini Dar es Salaam, sikwambii vijijini; umeme uko kwenye taa za barabarani na siyo majumbani mwetu. Tukiwasha vibatari na taa za ‘chemli za Aladin’ kwa wenye uwezo kidogo kila siku.
Hospitali ziliishia kutoa kama huduma fulani ya mwanzo tu (First Aid). Haikuwapo hospitali ya Amana, Temeke, Mnazi Mmoja, Mwananyamala wala Mbagala. Tuliponea kibahatibahati tu kwa mizizi na majani ya porini. Ukiwa na homa kali basi chemsha mwarobaini; tumbo la kuendesha chemsha majani ya mpera au mpapai nani akupe ‘antibiotic wewe’.
Hospitali ya Muhimbili, yenye maabara na vipimo pamoja na madaktari bingwa, ilijengwa mwaka 1957 - ni juzi tu - kwa heshima ya Binti Mfalme Margareth II, aliyekuwa na ziara ya kutembelea makoloni ili aje kufungua rasmi hospitali hiyo. Kiwanja kilitolewa kwa hisani ya familia ya Mzee Jumbe Tambaza, ambapo miembe ile mikubwa inayoonekana mpaka leo pale ilikuwa shambani kwa kina Tambaza.
Kwa hivyo basi, ukiacha labda homa na vidonda, magonjwa mengine yote kwetu ilikuwa ni kifo tu. Umri mkubwa wa kuishi kwa wastani ulikuwa ni miaka 30.
Mzee Jumbe Tambaza, ambaye jina lake linanasibishwa na shule maarufu ya Sekondari ya Tambaza ya jijini - hana uhusiano wowote na shule hiyo - shule ilipewa jina lake kutokana na eneo iliyopo na kwa kuthamini mchango wake katika kupigania uhuru.
Kabla ya hapo, wakati huo wa ubaguzi wa rangi na matabaka, shule hiyo na ile ya msingi iliyo jirani nayo inayoitwa Muhimbili Primary, zilikuwa mahsusi kwa vijana wa Kihindi tu – hasa Ismailia - zikijulikana kama ‘Aga Khan Schools’ na kamwe hawakuwa wakisoma Waswahili na Kiswahili pale.
Shamba la Mzee Jumbe Tambaza pale Upanga, lilianzia mbele kidogo ilipo Shule ya Jangwani Wasichana (ambayo wakati wa ukoloni ilijengwa na serikali wasome watoto wa kike wa Kihindi tu, na ile Shule ya Azania ilikuwa kwa watoto wa Kihindi wa kiume), na kutambaa moja kwa moja mpaka lilipo Daraja la Selender pale baharini.
Eneo la Majengo ya Hospitali ya Muhimbili ilikuwa mali ya Jumbe Tambaza na marehemu nduguze (Msakara, Kudura na Mwamtoro Tambaza). Kutokana na kukosekana kwa hospitali ya maana ya rufaa kwa ajili ya Waafrika (kwa sababu ya ubaguzi tu), hayati Mzee Tambaza alitoa eneo lote lile la Muhimbili ijengwe hospitali ya Waafrika ili kupunguza vifo vilivyotokana na kukosa tiba sahihi.
Kijihospitali kidogo kwa ajili ya watu Weusi kilikuwapo pale jirani na Kituo cha Kati cha Polisi (Central Police Station) jijini, ikiitwa Sewa Haji Hospital, kwa heshima ya mfadhili aliyeijenga kusaidia jamii masikini. Sewa Haji alikuwa mkazi wa Bagamoyo mwenye asili ya Kibulushi kutoka Persia. Baada ya kujengwa hospitali yaj Muhimbili, jengo moja katika yale matatu makuu, likaitwa Sewa Haji kama kumbukumbu yake.
Mjini Dar es Salaam wakati huo wa kibaguzibaguzi, serikali ya kikoloni haikutenga sehemu ya kuzikia watu weusi ambao walikuwa daraja la nne. Yale makaburi mashuhuri ya Kisutu, wakati huo yalikuwa ni ya watu wenye asili ya Kiarabu tu! Mwengine yoyote, ilibidi apelekwe kijijini kwao tu nje ya mji – Kunduchi, Mbweni, Msasani, Bagamoyo, Kisarawe, Maneromango na mikoani pia.
Sasa, ili kuondoa adha hiyo na usumbufu, Babu Mzee Tambaza, alitoa bure sehemu kubwa ya eneo lake itumike kwa watu wenye kuwa na shida ya kuzika ndugu zao jijini. Makaburi ya Tambaza siku hizo yalikuwa maarufu sana kuliko yalivyo yale ya Kisutu kwa sasa. Kamwe watu weusi hawakuwa wakizikwa Kisutu, kama ilivyo wakati huu.
Kufuatia hali hiyo, Jumbe Tambaza aliwashawishi binamu zake wawili, Mwinyimkuu Mshindo na Diwan Mwinyi Ndugumbi na wao wakatoa sehemu watu waweze kuzikana kule maeneo ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa na Ndugumbi, Magomeni Makuti; makaburi ambayo mpaka leo yameendelea kutumika kuzikia watu wote.
Neno, ''Tambaza,'' limetokana na neno ''kutambaa,'' au ''kusambaa,'' eneo kubwa. Diwan Tambaza na nduguze walikuwa watawala wa sehemu mbalimbali za hapa Mzizima siku za nyuma kabla Waarabu, Wajerumani wa Wangereza kufika hapa. Nduguze wengine ni Diwan Uweje; Diwan Uzasana; Diwan Mwenye-Kuuchimba na Diwan Mwinyi Ndugumbi.
Majina hayo walijipachika wenyewe kiushindani, kujigamba na kujitukuza kuliko ndugu wengine; hivyo kimafumbo mafumbo, huyu akajiita hivi na yule akamjibu mwenzake vile; mwengine akajiita naye atakavyo, kutokana na uhodari na tawala thabiti walizoziongoza.
Majina hayo pandikizi, hata hivyo yalikuwa na maana yake kila moja; kama vile mtu aseme mimi ‘Mobutu Sese Seku Kuku Mbenju wa Zabanga’, ikiwa na maana ya ushujaa kwa ‘Batu ba Kongo na fasi ya Zairwaa!’
Sasa Diwan Tambaza alipojiita vile, nduguye Diwan Uweje akamjibu na kumwuliza hata ukiwa umesambaa ndio uweje? Mwengine naye akasema, ‘’Ah! Uliza sana wewe uambiwe.’’ Hivyo yeye akajita Diwan Uzasana. Diwan Mwenye-Kuuchimba, yeye alikuwa akitawala maeneo ya Mtoni Kijichi na Mbagala yake, akasema, ‘’Nyie wote mnacheza tu, ‘mimi ndiye mwenye kuuchimba!’’ Kwa maana ya kwamba ndio kiboko ya wote. Ilimradi hali ikawa ndiyo hiyo; na hizo ndio zama zao, kwani husemwa kila zama na kitabu chake.
Mwandishi wa makala haya, ni mjukuu Mzee Saleh bin Abdallah Tambaza wa Zarara, anakuwa ndugu wa Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, yaani baba zao walikuwa ndugu.
Shamba la babu yangu linasambaa kuanzia Don Bosco, Makao Makuu ya Jeshi, Diamond Jubilee, Msikiti Maamur (kaburi la babu na babake babu yamo ndani ya Msikiti wa Maamur unapoingia mkono wa kulia pale ukutani), kuelekea kwenye Jamat la Wahindi mpaka Mahakamani kule Kisutu.
Miembe, minazi na mizambarau ile ya asili inayoonekana Upanga, ilipandwa na babu yangu kwa ajili ya urithi wa wajukuu zake, itakapofika zamu yao kumiliki maeneo yale.
Kwa bahati mbaya sana, Wazungu Waingereza, wakaona mandhari ile nzuri ya Upanga, hawakustahili watu weusi kuishi pale na wakawaamuru babu zangu wahame wawapishe Wahindi raia daraja pili. Hii ni baada ya wao Wazungu daraja la kwanza kuchukua eneo lote la Oysterbay (sasa Masaki). Maeneo yote hayo mawili yenye upepo mwanana ni karibu kabisa na bahari.
Kitendo cha kumhamisha mtu nyumbani kwake kwa namna ile, halafu kumpa fidia uitakayo wewe, ni dharau, dhuluma na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Wazee wale wastaarabu na wajanja hawakuwa na haja ya kuyauza maeneo yale, kwani ukiyaangalia utaona waliyapangilia ili vizazi na vizazi vya kwao viishi hapo.
Hii haihitaji mjadala wala maelezo marefu, lakini ni ushahidi tosha kwamba inaweza ikawa ndiyo sababu kubwa iliyomfanya Mzee Jumbe Tambaza awe mstari wa mbele kabisa katika kuwachukia watawala wa Kizungu na kumuunga mkono Nyerere kwa nguvu kubwa kama ile.
Mchango wa Mzee Jumbe Tambaza katika ukombozi wa nchi yetu haukutetereka hata kidogo, kwani hata pale rafiki yake mpenzi Sheikh Suleiman Takadir, alipotahadharisha watu kuwa makini na Nyerere maana ameonyesha kwamba siku za usoni angependelea zaidi jamaa zake, Mzee Jumbe hakumuunga mkono na akakubali Sheikh Takadiri atengwe na jamii kwa manufaa ya umoja wa kitaifa.
Jumbe Tambaza pia hakumuunga mkono Zubeir Mtemvu, kwenye suala la Kura Tatu ambalo ilibaki kidogo tu chama cha Tanu kingesambaratika na kuwa vipande viwili; lakini yeye alibaki na Nyerere wake mpaka dakika ya mwisho kule Tabora hadi kukasainiwa waraka wa ‘Uamuzi wa Busara’ ambao uliwapeleka TANU kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu.
Katika picha ya pamoja iliyopigwa baada ya kutangazwa ushindi wa kuingia kwenye Kura Tatu kwa chama cha TANU, anayeonekana nyuma ya Mwalimu Nyerere pale Tabora ni Mzee Jumbe Tambaza. (Rejea kitabu Mohammed Said, ‘’Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes… uk 275).
Kutokana na uaminifu wao usiotetereka kwa chama chao, Mzee Jumbe Tambaza na mwenziwe Mzee Mwinjuma Mwinyikambi; wazee wale wawili wa Kimashomvi kutoka Mzizima, kwa muda mrefu wamekuwa wajumbe wa kudumu (permanent seats) kwenye Kamati Kuu ya TANU bila kupigiwa kura; achilia mbali ule uwepo wao kwenye Baraza la Wazee wa TANU.
Mnamo mwanzo wa miaka ya mwanzoni 1950, Mzee Tambaza alitumbukizwa tena kwenye mgogoro mkubwa na serikali pale ilipokuwa inajenga upya Barabara ya Umoja wa Mataifa kutokea Faya kuelekea Daraja la Selander, ilipoamuliwa kwamba sehemu ya eneo la makaburi iondoke kupisha ujenzi huo.
Hayati Mzee Tambaza, alifungua kesi mahakamani dhidi ya serikali, kesi ambayo inatajwa kama moja ya kesi nzito (landmark cases) sana kutokea hapa nchini na Afrika Mashariki iliyogusa imani ya Dini ya Kiislamu; kwamba je, ni halali au si halali kufukua makaburi ya watu waliokufa?
Kesi ya Makaburi, kama ilivyokuja kujulikana, iliunguruma kwa muda mrefu na kujaza kurasa za mbele za magazeti wakati huo, kutokana na mabishano makali ya hoja (cross examinations) mahakamani baina ya mawakili wa pande mbili hasimu.
Wakati serikali ikiwatumia masheikh wazawa wa hapa waliosema kwamba inakubalika kufukua makaburi, Jumbe Tambaza aliwatumia masheikh wakubwa kutoka Mombasa na Zanzibar, akiwemo aliyekuwa Kadhi wa Zanzibar Abdallah Saleh Farsy kupinga hoja hizo.
Kwa kishindo kikubwa, Mzee Tambaza alishinda kesi ile na ikabidi barabara ile ipindishwe pale kwenye mteremko wa kutokea Faya na kuyaacha makaburi na vilivyo ndani yake kama yalivyo. Haraka haraka, Hayati Mzee Tambaza akafanya maamuzi ya kujenga msikiti ambao haukuwapo mahala hapo kabla ya tukio hili, kuepusha kujirudia.
Huyo ndiye Mzee Jumbe Muhammad Tambaza, mwanaharakati wa kupigania uhuru wa taifa hili wa kupigiwa mfano, aliyetetea na kutoa vyake kusaidia wanyonge wenziwe katika jamii yetu katika kipindi cha manyanyaso ya utawala dhalimu wa Malkia wa Uingereza. Alimfanyia madua na matambiko ya jadi Mwalimu Nyerere ili nuru yake ing’are kama mwezi na jua!
Ewe Mola – ilaze roho ya marehemu mahala Pema peponi- Aamiyn
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?