Rununu, Tarakilishi na Kipakatalishi, Runinga na Kitenzambali
Kuna faida nyingi na kubwa sana, inapatikana kwenye vifaa janja (smart) vilivyotiwa Akili Bandia (AI) na haswa vikitumika vizuri na walengwa. Lakini hapo hapo kama vikitumika vibaya kwa ukiukwaji mkubwa wa haki ya mmiliki wa vifaa hivyo basi kutakuwa hakuna tena faragha wala usiri (Privacy) kwa mtumiaji wa vifaa janja.
Yatakapo tokea haya yote basi ile nadharia ya NWO (New World Order), ndipo itakapofanyakazi kiuhakika zaidi.
Kwa sababu uduma za kijamii zitakapokuwa zinaendeshwa na AI Technologies na kufikia mpaka magari na majumba yetu kukawa na vifaa tunavyo vitegemea kila siku kama Runinga janja, Jokofu janja, Jiko janja, vitanda janja na hata milango na mageti ya majumba yetu kupandikizwa akili bandia (Artificial Intelligence) na kuwa janja, kwa lugha ya walami wanita smart, basi hapo sasa ndipo tutakapo tawaliwa vizuri zaidi na hao wenye umiliki wa hivyo vifaa.
Hakuta kuwa na usiri wala faragha (privacy) kwenye majumba yetu na sehemu zote za mikusanyiko hata ile ya ndani ya kifamilia.
Kwa sababu, hivi vifaa ambavyo vipo sasa kama vile Rununu au simujanja (smartphone) tayari tutake tusitake zinaangaliwa kwa saa ishirini na nne, hata ukizima data, lakini wakitaka kujuwa wapi ulipo wanajua, maana ile app ya ramani ya google au zile Tomtom Rider kwenye vipando, vyote vimewekea kitu kinaitwa GPS (Global Positioning System) ambayo inatambua wapi ulipo na wapi umeingia, duka gani au nyumba gani upo kiuhakika zaidi kwa aslimia 95% kama si 100%
Hivi karibuni mitandaoni kulikuwa na mijadala kuhusiana na Runinga janja (Smart TV) kuwa kuna uwezekano wa mtu alie upande wa pili kuona upande wako kwa kutumia ile kamera iliyoko kwenye Runinga janja yako, kama vile wanavyoweza kuingilia mawasiliano ya Tarakilishi (kompyuta) au Kipakatalishi na kuweza kuona kile kilicho mbele ya kamera.
Basi vifaa vyenye akili bandia (AI) vitakapokuwa vimeenea kila sehemu, hapo ndipo binadamu atakapojikuta kuwa hana tena faragha, japokuwa kuna faida tele, kama vile nadharia ya kuweka Kibanzi (chip) kwenye miili ya watu kwa kisingizio cha kiusalama.
Ni kweli kuna faida kubwa kuweka vibanzi kwenye miili kama zinavyo onyesha kwa wanyama kwa sababu Kibanzi zinapowekwa kwenye miili licha ya kujuwa mahala gani ulipo pia zina ambatana na taarifa zako zote binafsi zilizo muhimu, kama vile jina lako, umri wako, utaifa wako, magonjwa yanayo kusumbua, aina ya damu yako kama ni A, B, AB au O, vyote hivyo vinakuwepo.
Kwa maana hiyo basi, inakuwa ni rahisi kukuhudumia pale unapopata ajali au unaposumbuliwa ghafla na ugonjwa na hata kama umepotea ni rahisi kukutafuta na kujuwa wapi upo.
Na hata mpango wa kutembea na pasi za kusafiria unaweza kuondoka kwa kuwa watu watakuwa na vibanzi kwenye miili yao, kiasi wakipita forodhani uhamiaji mipakani ni rahisi kwa mashine zenye akili bandia kutambua kuwa wewe ni raia na huitaji VIZA na pia kama unatafutwa basi ni rahisi kutambulikana.
Vilevile uhakika wa kuwatafuta watu waliopotea unaweza kurahisishwa kwa sababu unaweza kumfatilia mtoto au mtu aliyepotea kiurahusu zaidi, kama vile unavyotafutwa simu iliyopotea kwa kutumia utaalam wa GPS.
Google tayari wana gari linalojiendesha lenyewe, na mtu haitaji kuwa na leseni tena, maana gari unaliambia tu au kuandika wapi likupeleke, mtaa gani au mahala gani na linakupeleka bila tatizo.
Kuna Majokofu janja, yenye kutambua umeweka nini kwenye jokofu na kukushauri vyakula gani ule na vyakula vipi uviepuke.
Runinga janja, uliyokuwa nayo, inatambua vipindi gani unapendelea, kiasi ya kukutafutia vipindi vinavyo fanana na vile unavyo vipenda.
Milango ya majumba yanayofunguliwa aidha kwa sauti au kwa kuona sura yako tu, leo hii kuna viatu ambavyo vina weza kunakiri kasi ya mwendo wako, umbali uliotembea, hatua ulizotembea na kujirekebisha kulingana na umbo la mguu wako.
Na taarifa zote kutumwa kwenye Rununu yako au kwenye Tarakilishi au Kipakatalishi chako na kupendekeza namna ya utembeaji wako kulingana na migandamizo ya miguu yako.
Wanadamu tunapojivunia maendeleo ya vifaa tunavyo vitumia kila siku, vilevile tutambue kuwa hata wadukuzi (Hackers) nao hawapo nyuma kimaendeleo, kama wanavyoweza kudukua Rununu na Tarakilishi au Kipakatalishi, basi hata hivyo vifaa janja vingine pia vina uwezekano mkubwa wa kudukuliwa.
Magari yanaweza kuzimwa na kuwashwa na mtu aliyeko mbali zaidi ya kilomita 20,000, nyumba yako yenye milango janja inaweza kufunguliwa na kufungwa na mtu aliyeko nchi nyingine kabisa, kama vile haitoshi kukuona na kunakili (Record) kila unacho kifanya pia anaweza kuzima viyoyozi na vifaa vya joto kwa muda anaotaka mdukuwaji.
Gari lako janja, linaweza kibiwa bila ya mtu kuliendesha, likaendeshwa kwa kutumia Kitenzambali (Remote) na ukaamka asubuhi usilikute.
Ndipo hapo serikali itapoweza kuwafuatilia kila mtu aidha kwa uzuri au kwa ubaya, japokuwa kuna wana harakati ambao wanayapinga haya yote kwa kusema kuwa yanakiuka haki za binadamu, lakini watawala wanayataka yaje hata leo kwa sababu yatawarahisishia kutawala raiya na mali zao.
Haya yote yapo na yashafanyiwa majaribio na kuonyesha mafanikio makubwa kimatumizi, kinachofanyika hivi sasa ni kuyaleta kidogo kidogo kwa raia, nasi bila ya utambuzi tunayapokea na kuyatumia bila ya kujua nyuma ya pazia kuna zimwi gani linalosubiri kutupanda kichwani.
Kuna siku mwanangu mdogo aliwahi kuona Runinga zile zenye kichogo na kuniuliza ni kitu gani, siku moja nilimuonyesha simu zile za kuzungusha, akaniuliza sasa hii ukitaka kuzogoa (Chating) unatumaje meseji, hayo yote hivi sasa ni historia.
Basi na tujiandae kukabiliana na hayo yote, maana leo hii hakuna ambae aliweza kujuwa picha za kutumia filamu za negativu hazitakuwepo tena na kuzitupa kwenye kabati la sahau.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?