Sunday, 13 October 2019

TULISOMA NA KULELEWA 

KWA KUCHARAZWA 

BAKORA NA VIBOKO JUU!

Ndio Maana Vijana Sie Tuliozaliwa Miaka 1960 - 1980s Tuna Adabu na Heshima za Kutosha Kabisa.

Kipindi ambacho sie tunasoma kuchapwa ilikuwa kama sehemu ya mtaala wa elimu. Na kuchapwa mtoto haikuwa kesi, na ukijitia umbea kwenda kusema nyumbani, mzazi au mlezi wako naye atakurapua vizuri tu.

Hii ilileta heshima kwa vijana wengi, na ndio maana vijana wa rika lile ambalo limezaliwa Miaka 1960 - 1980s ambao ni watu wazima sasa, tuna adabu za kutosha, kiasi cha kuweza kuzigawa kwa wengine wenye kuzihitaji.

Nakumbuka vizuri sana, kama wewe ni mwanafunzi basi kwa sie tuliozaliwa mjini, siku uanza saa kumi na moja au kumi na mbili alfajiri.

Utaamka na kujiandaa, kisha utawahi namba shuleni, hapo ina maana umefika shuleni saa moja kamili asubuhi, ukiwa na ufagio wako wa chelewa, uliotengenezwa kutokana na makuti ya mnazi..

Baada ya rokoo, unatafuta kiamba chako cha bustani na kukimwagilia maji ya kutosha. Baada ya hapo kuna kufagia kiwanja chako kisha ndio kengere ya mstarini itapigwa na tunajiunga mstarini.

Wataitwa wale ambao wamechelewa rokoo au hawakuwahi namba saa moja na watachapwa mbele ya wanafuzi wote. Hapo inategemea zamu ya mwalimu ataamua ni bakora ngapi ngapi!

Kisha mkiwa mstarini inategemea na siku, mfano shule niliyosoma mimi, siku za usafi wa mwili na mavazi ni Jumatatu na Jumatano au Alhamisi kama nakumbuka vizuri.

Hapo sasa ni kukaguliwa usafi wa nguo za shule, mwalimu atapita uku brasi bandi ya shule ikipiga ule wimbo maarufu wa "Baba paka, alisemaa shimo lile ni la panya..."

Mtakaguliwa sare za shule, kama zmefuliwa na kutakata na kunyooshwa vizuri, nakumbuka tulikuwa tukizipendezesha sare zetu mashati meupe kwa kuziweka wanga, sare imenyooka na uku mgongoni , tumeweka miraba kama mitatu hivi kwa kupindisha shati mgongoni na uku kaputura za rangi ya zambarau zikiwa zimenyooka vizuri na soksi nyeupe.

Wadada nao sketi zao ndefu kupita magoti kidogo na soksi nyeupe ndefu karibia na magoti, na nywele zimesukwa, mtindo wa twende kwa bibi. Wanapendeza wasichana hawana hata wanja wala vipodozi wala nyele za mawigi au kusukwa rasta.

Kivumbi sasa ukutwe ujachana nywele unapitishwa mbele ya mstari, kwa wasichana ambao wana nywele ndefu mtindo ni mmoja tu, kusuka kwa mlazo (Twende kwa Bibi). Zikikutwa zimefumuka fumuka nao wanaletwa mbele na kuadhibiwa, yaani hapo ni mwendo wa bakora!

Kiufupi ukikutwa na kucha ndefu, bakora inakuhusu, ukikutwa na kucha chafu, ukiwa ujakoga, ujapiga mswaki mdomo unanuka, mwalimu kasugua shingo yako katoka na nongo, bakora zitakuhusu.

Baada ya ukaguzi ulioambatana na brasi bendi, hapo ndio kiranja wa zamu ataitwa mbele na mwendo wa gwaride mguu upande na wote tunaitikia, mojaaaaa!!!, Mguu sawaaa, Mojaaa! Nyumaaaz, geuka... !! Moja mbili tatu moja... Kisha mwendo wa mchaka mchaka, tunazunguka aidha kiwanja cha mpira cha hapo shuleni au mnazunguka shule raundi kadhaa, kisha ndio tunaelekea madarasani kwa mwendo wa haraka. 

Darasani nako kuna bakora zinakusubiri, kama ukufanya homu weki ya mwalimu, ni bakora, umefanya homu weki ya hesabu ukakosa, basi mwalimu wako wa hesabu alisha kutaadharisha, kosa moja bakora moja au hata tatu. Ukuudhuria kipindi chake jana yake, bakora! Umechelewa kuingia darasani, bakora...!

Na kabla ya hapo ukute kaingia siku hiyo kachangamka anaanza na mwendo wa tebo. Utasikia unaitwa jina, Sindika Mtakuja! utaitikia... Naam mwalimu, kisha linafuata swali, sita mara nane!  umebabaika au ukikosea utashtukia bakora ya mgongo kama si bakora ya kichwa!

Atachaguliwa mwngine, mwalimu ataita, Mwanshamba Sijali! Sita mara saba, utasikia sauti kali ya kike, ...Arobaini na mbili mwalimu.
Mwalimu atamsifia, Safi sana Mwashamba...!

Ataita jina lingine, Mary Mlekwa, bee! Mwalimu, nane mara tano, arobaini mwalimu....!

Sasa ole wako ukutwe na kikokotozi, wenye lugha yao wanaita kalikuleta au sijui umekutwa na zile saa za kasio zenye kikokotozi ndani yake, hapo ndipo utakapo ipata freshi kwa bakora utakazo charazwa. 

Mpaka kipindi cha hesabu kinaisha, unaweza jikuta una bakora za kutosha.... Bado walimu wa masomo mengine nao awajaingia na kuwacharaza kwa makosa mbali mbali.

Kelele za darasani zilisabisha kuchapwa darasa zima, labda monita wa darasa awe amepeleka majina ya waongeaji darani.

Ukiwa mbishi mbishi kwa kuwa tu ushaanza kubarehe na kujiona umekuwa, hapo utajikuta unapelekwa stafurum ya walimu. Uko ukiingia tu baada ya shikamoo walimu ni kupiga magoti. Na walimu wa makusudi watakuuliza kosa lako nini, utasema na utakuraaa (kwa rafidhi ya Kikurya) mboko za kutosha kwa kila mwalimu aliyeko stafu rumu.

Baada ya hapo utarudi zako darasani na kukuta mwalimu amesha maliza kuandika notsi ubaoni na kaacha homuweki. Hapo sasa ni juhudi zako mwenyewe kuwaomba wanafunzi wenzako ukopi maswali na kutafuta majibu kwa siku ya pili.

Kwa sie ambao tulipitia madrasa za kuhifadhisha Qur'an, tukiita chuoni, uko nako walimu ilikuwa mwendo ni ule ule, ujaifadhi, vizuri ni bakora! Umesoma vibaya Qur'an ni bakora! Sijui umesahau juzuu nyumbani, bakora! Umevaa kofia upande mwalimu ajapenda hapo bakora zitakuhusu.

Miaka hiyo mtoto au mtoto tineja, kuchapwa na walimu au mzazi nyumbani wala haikuwa jambo la kushangaza... Japokuwa tulikuwa na changamoto nyingi za kimaisha, lakini walimu tuliwaheshimu na ukikutana nae aidha asubuhi shuleni au wakati wa kuodoka tukiwabebea mifuko yao.

Ole wako sasa mwalimu anaingia shule au anaondoka na wewe ujamsaidia kubeba mfuko wake, utatia akili siku hiyo, haijalishi ni wa darasa lake au lah. Utaitwa na utachapwa mbele ya wanafunzi mstarini kwa ukosefu wa adabu, umemuona mwalimu kisha ukalala mbele...

Tulinunua kashata zao na bajia na hata kukopa na kulipa pesa siku ya pili yake, kwa wale wa vijijini, kwenda kumlimia mwalimu haikuwa jambo la ajabu na bado pia shamba la shule likiwasubiri.

Tulichapwa na tulinyooka kweli kweli, na wale ambao walishindikana kabisa, waliishia kufukuzwa shule na kiukweli hata maisha yao baada ya shule hayakuwa mazuri hata kidogo.

Shule haikuwa sehemu ya starehe na upuuzi upuuzi, maswala ya kuferi kwenye mitihani ya mwezi, ilikuwa jambo ambalo halivumiliki, na bakora utaziramba za kutosha.

Ndio maana sisi watoto wa enzi hizo, tuna adabu na heshma zetu, ukuti tukitukanana mitandaoni au kuitana majina ya kebehi, si mitaani wala mitandaoni.

Haya maswala ya haki sijui za binadamu, ushoga na usagani, halikuwepo kabisa, kwanza ilikuwa aibu kubwa sana. Leo hii, tumevamia mienendo ya kimagharibi, kiasi watoto waharibike, maana kuna rundo za wana harakati wa kila namna wa kuharibu watoto kwa kisingizo cha haki za watoto sijui binadamu.

Mie nasema hivi, kama shule imeweka sheria ya kutotumia vironga ronga, basi nasema hongera mkuuwa mkoa na hongera rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuunga mkono mkuu wa mkoa. Na tutakuunga mkono na kupigia debe adhabu za kucharazwa bakora kwa wanafunzi na hata watu wazima ambao awana adabu, wafujaji na waarifu mbalimbali, wote hao bakoraaaa zinawahusu.

Nasema hivi, wachapweee tuuuu...


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!