Walikaa Siku 40, Mchana na Usiku, Hakuna kutoka Nje
Maandiko yanatufahamisha kuwa Nabii Nuhu na Familia yake, waliweka kukaa siku 40 mchana na usiku, Wakiwa ndani ya Safina _( Meli)_, wakizungukwa na Maji na uku mvua kubwa ikinyesha.
Waliweza kustahimili madhira yote yale, wakimtegemea MwenyeziMungu tu.
Hakukuwa na Internet kwa ajili ya kujliwaza au kuwasiliana na walio nje ya Safina.
Hakukuwa na Facebook wala WhatsApp kuwazeshesha kuzogoa na ulimwengu wa nje.
Hakukuwa na Youtube wala Instagram, wakaweza kujiselifisha na kuwajuza walio nje ya safina wala wao kujuwa inacho endelea nje ya Safina.
Hakukuwa na Mawasiliano ya simu wala Runinga, ili kuweza kusikiliza na kutazama taarifa za habari ya yale yanayojiri uko nje ya Safina.
Hakukuwa na Netflix wala Amazon Prime wala Disney plus, wakaweza kupoteza wakati na kujiliwaza kwa filamu mbalimbali.
Sauti pekee walizozisikia ni sauti za wanyama walioko wenye Safina, sauti zao wenyewe na sauti ya matone ya mvua tu.
Hakuna walichoweza ukitegemea zaidi ya Rehma za MwenyeziMungu, wakitarajia huruma zake peke yake.
Walichoweza ufanya ni dua na sala na kuwa na imani kubwa kwa Muumba wao, ndiye aliyeweza kuwa kinga na balaa lile la gharika kuu.
Basi sie wa karne hii ya 21, inatushinda nini kumtegemea MwenyeziMungu na uku tukifata ushauri wa Matabibu na Madaktari wa Afya?
Basi tuzingatie ushauri wa Wataalamu wa tiba, bila usahau sala na dua ndio vitu pekee vitavyoweza kutusaidia kwenye kipindi hii kigumu cha ugonjwa huu wa mripuko wa Virusi vya Korona.
MwenyeziMungu, Aliyetukuka Hakuleta maradhi/ugonjwa isipokuwa Ameteremsha na dawa yake, basi nasi tutarajie faraja kubwa hivi karibuni kutoka kwa Wataalamu ambao mchana na usiku wapo wakijitahidi kutafuta dawa na kinga ya tatizo hili.
Imani yetu ikiwa thabiti na uku tukitarajia kwake, basi siku si nyingi tutasikia tiba na kinga ya virusi hivi imepatikana nasi tutaweza kushuka kwenye safina uku tukiwa na faraja na furaha kwa matumaini mapya.
Tunashauriwa na hata kualiamriwa tupande katika jahazi (Safina) la kujikinga na Korona uku tukitaraji Rehma zake MwenyeziMungu.
Maana uko nje kumeshateremshwa mvua ya Korona na kila ardhi (Nchi) ya dunia hii wapo kwenye Majahazi (Safina) zao, kila nchi inakwenda kwenye mawimbi kama vile kwenye Safina ya Nabii Nuhu.
Na kwenye kipindi hii cha gharika ya Korona, hawakosekani mfano wa mtoto wa Nabii Nuhu, wapo watakaodharau na matokeo yake watagharikishwa na hata kuwasababishia wengine kukumbwa na hii gharika.
Sina maana kuwa waliopata korona wamefanya makusudi au ukahidi, lahasha, ninachosisitiza ni kwamba tusiwe sisi ndio sababu ya kueneza huu ugonjwa kwa wengine, tufate ushauri wa wataalamu ili kuepukana na madhara ya Korona.
Na tukiweza hayo, basi tutarajie baada ya muda ardhi iliamriwa kuimeza Korona yote na mbingu nazo zikaamriwa zizuie kama vile zilipo amriwa kuacha kuteremsha mvua.
Na mwisho Jahazi (Karantini) letu ilisimama kwenye Mlima Judi kama lilivyosimamam Jahazi la Nabii Nuhu, na sote tutaweza kutoka katika jahazi (Karantini) na kuendelea na maisha yetu kama kawaida.
Ee MwenyeziMungu, hakika sisi tunajikinga Kwako kutokana na mambalanga na umajnun (Wazimu na Maradhi ya Akili), na ukoma na maradhi yote mabaya, pamoja na virusi vya Korona.
Aamiyn
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?