Friday, 12 February 2021


PIA TUJULIKANE KWA MAJINA TULIYOPEWA NA WAZAZI

Maisha ya Ughaibuni, Mitandaoni na Rakabu zetu.

Kila mtoto wa Kibinadamu, anapozaliwa upewa jina pamoja na ubini wake, mtoto ukuwa na kufikia umri wa kujitambua.

Kwenye maisha kila binadamu ukumbana na harakati zake binafsi za Kimaisha, wapo waliotoka vijijini na kwenda mjini kujitafutia maisha na wapo waliowahi kudandia meli na kwenda kutafuta maisha ughaibuni.

Hayo yote ni katika harakati za kujitafutia unafuu wa maisha ili kukidhi mahitaji yetu ya kila siku na kikipatikana cha ziada basi kisaidie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na hata kufanyia matanuzi na kuwakoga wengine. 

Yote hayo ni maisha. 

Jambo moja kubwa na ndio haswa dhumuni la walaka huu, ni pale kijana aidha mvulana au msichana, anapoondoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kujitafutia maisha aidha mkoa mwingine au nje ya nchi.

Na anapofikia uko, akabadirisha jina lake alilopewa na wazazi wake, jina ambalo ndio utambulisho wake kwa watu wake, wakiwemo ndugu, marafiki, jamaa na majirani.

Ni kweli, mtu anapofikia umri wa kujitegemea kisheria ana haki ya kubadirisha jina, lakini unapobadirisha jina lako unatakiwa, uwafahamishe wale unaokaa nao na uko ulikotoka wafahamu kuwa wewe sasa unaitwa fulani bin fulani au unajulikana kwa Rakabu fulani.

Hii ni Karne ya Tovuti Baraza/jamii (Social Media), vijana wengi utumia muda wao mwingi sana kwenye kuperuzi kurasa za tovuti baraza/jamii.

Kipindi chetu sie wengine, tukitumia sana vibaraza, kupiga soga, vibaraza ambavyo vilijulikana kwa jina la Vijiwe/Vijiweni.

Uko pia tulitumia Rakabu tulizo zichagua, badala ya majina yetu halisi, lakini licha ya kutumia Rakabu, bado tulijulikana kwa majina yetu halisi.

Ukimsikia mtu anaitwa kwa jina la Rakabu, tulimjuwa pia kwa jina lake halisi, kwa hiyo haikuwa tabu hata anapopata tatizo au kukutwa na mauti, basi tuliweza kufikisha taarifa hizo nyumbani kwao, tena basi usikute hata nyumbani kwao wanalijuwa jina lake la mtaani.

Siku hizi imekuwa sivyo na haswa wengi wetu tuishio Ughaibuni, tukajitengeneza kurasa kwenye tovuti jamii na kubadirisha majina yetu halisi.

Utakuta mtu ana marafiki zaidi ya elfu nne, mpaka unashangaa, hivi huyu mtu marafiki wote hao anawasiliana nao vipi...!?

Si ajabu katika hao elfu kadhaa, ni watu wanne tu labda, nasema labda ndio wanaweza kumjuwa kwa jina lake halisi.

NASAHA na USHAURI

Ni Muhimu sana kwenye hizi Tovuti Baraza/jamii (Social Media) kuwa na Ndugu na marafiki mnao fahamiana vizuri na haswa wale wenye kutumia Rakabu yaani majina ya utani au waliobadirisha majina yao.

Si kwenye tovuti jamii tu, lahasha, hata kwenye maisha yetu mitaani na haswa wale wanaojiona kuwa wao ni watoto wa mjini na wale waishio ughaibuni.

Kuna haja kubwa sana kwa mimi na wewe, tukawa na marafiki wenye kutujuwa kwa majina yetu halisi na uko nyumbani tuliko toka, wakatujuwa kwa Rakabu zetu na hata kwa majina tuliyo yabadirisha, ili likitokea la kutoke wanao tujuwa wakaweza kupata taarifa zetu kutokana na hayo majina yetu mapya, ya Ughaibuni au ya uko Mjini.

Utakuta mtu anaitwa Nyange Nyaisawa, lakini uko kwenye tovuti jamii au mtaani anajiita Young Neyo, mtu anaitwa Jumanne Karubandika, kule anajihita JayFour Karry

Utakuta Msichana anaitwa Nyasanje Matano mtaani yeye anajihita Neysalious Mtamu

Na wengi wa namna hii, wa kike na wakiume...

Muhimu ni kuwa karibu na watu japo wachache wanaokujuwa vizuri, siku likitokea la kutokea wajuwe wapi wapeleke taarifa. La sivyo ujikubalishe tu, ukiaga dunia uzikwe na manispaa ya mji husika.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!