JAMHURI YA WATU WA TWAWAWEZA
Ndoto ya Kumbukumbu Iliyopotezwa.
Simulizi hii inatokana na msukumo ule uliotoka kwenye ufunuo wa ndoto ya kweli ya maisha yangu, kabla na baada ya kuzaliwa.
NCHI YA TAWANYIKENI, MWANZO HUSIO NA MWISHO
Hapo zamani kabla ya wewe na mimi hatuja julikana kuwa tutazaliwa, kulikuwa na nchi moja kubwa, iliyobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi sana. Ikiwa imezungukwa na Maziwa na mito yenye kutiririka maji yaliyo matamu, uku ikiwa na aina nyingi za FAUNA mbalimbali, zilizokusanya wanyama wa kila aina.
Wale waliojikuta kuwa wamezaliwa kwenye nchi ile ya TAWANYIKENI, walijiona kuwa kweli wamejaaliwa na kupendelewa sana na Muumba wao, aliyewaumba wakiwa na maumbo mazuri ya kuvutia, na wengi wao walikuwa ni wenye rangi ya Kahawia, iliyokoza na iliyofifia.
Licha ya nchi ya TAWANYIKENI kuwa na makabila mengi sana, yasiopungua mia mbili na utofauti wao wa rangi zao za Kahawia iliyokoza na kahawia iliyofifia, makabila yote hayo yaliweza kuishi kwa amani kwa kuhishimiana na mapenzi na umoja na uelewano mzuri sana.
Kutokana na utajiri wa rasilimali wa nchi ya TAWANYIKENI, nchi ikajikuta inatembelewa na wageni wenye rangi manjano na manjano kibichi, kutoka nchi za mbali sana uko UGHAIBUNI.
Wageni wa kwanza kabisa kufika kwenye nchi ile walikuwa wanatoka nchi ya BUNI, hawa walikuwa wakivaa nguo ndefu zilizoshonwa kutokana na MELIMELI, kuanzia kichwani mpaka miguuni, wakijulikana kwa jina la nchi yao, wakaitwa WABUNI.
Wabuni walikuwa wanaotoka nchi yenye mchanga mwingi sana, na inasemekeana uko kwao, jua ni kali sana, kiasi wengi wao wakajikuta wanapanda nyumba zinaelea majini, na kufunga safari za kibiashara nchi za mbali.
Wabuni ni wafanyabiashara na wachuuzi, wao haswa waliweka makao ya makuu kwenye visiwa vya SIWANZA. Na uko waliweza kujihimarisha kwa bidhaa mbalimbali kutoka nchi zao.
Wabuni walipoingia kwenye nchi ile, walileta bidhaa mbalimbali kama vile Mausuli, Mautuli, Shanga, na Fedhaluka, na kwenda nazo TAWANYIKENI na wao wakachukua rasilimali za kwenye FAUNA wakiwinda wanyama mbalimbali kama vile chui, ndovu na faru.
Wabuni hawa si kuwa walifanya hivyo peke yao, lahasha, bali walishirikiana na watawala wa makabila na wakapata na wapagazi wa kuwabebea bidhaa zao mbalimbali, mpaka pwani ya nchi ya TAWANYIKENI.
Na uko pwani waliuza hizo bidhaa kwa WALAMI hawa Walami walikuwa wanatoka mbali zaidi, nchi zao ni nchi zenye theruji nyingi sana, hao ndio walishirikia na wabuni katika biashara na uchuuzi wa bidhaa mbalimbali na hata kuwanunua raia wa Tawanyikeni na kuwapeleka ughaibuni kwenda kufanyakazi kwenye mashamba yao makubwa.
Biashara na uchuuzi haikufanywa na Wabuni na Walami tu lah, walikuja walowezi kutoka mataifa mbalimbali kama vile Wafurushi, hawa walijulikana kwa uvaaji wao wa viremba vingi kichwani, kulikuwa na Wahinda na uhodari wao wa kula piripiri, Wapotogiza kwa ukatili wao na Wahuna, Wahuna wao walisifika kwa kula kila kitu kinachotembea ardhini, na wengi walishindwa kuwatofautisha kwa jinsi walivyofanana.
Walami ni wale wanaotoka nchi yenye barafu nyingi sana, ni watu wenye rangi ya Manjano, hawa wapo tofauti kidogo na Wabuni. Wao umanjano wao ulikuwa umekoza, labda kwa kuwa nchi yao ilikuwa ni nchi iliyozungukwa na barafu.
Inasemekena Walami wamevuka mabonde na milima, walisafiri na kuzishinda zile bahari kuu saba, uku wakitumia nyumba zinazo elea, mfano wa safina kwenye maji kama vile Wabuni, mpaka kufika kwenye nchi ya TAWANYIKENI.
Walami walipo ona kuwa wenzao Wabuni wanafaidika kwa biashara ile, wakahamua na wao kuwatuma WADADISI wao kwenda kuidodosa nchi ya TAWANYIKENI.
Walami waliposhuka kutoka kwenye nyumba zao zinazo elea majini mfano wa safina, wakawapekea viongozi wa ukoo zawadi mbalimbali kama vile shanga na vifaa vya taswira za kujionea na kuandikishiana mikataba ya ardhi.
LUGHA YA KIHILIKI
Kutokana na muingiliano ule wa watu kutoka ughaibuni na Watawanyikeni haswa kwenye masuwala ya uchuuzi wa bidhaa, kukazaliwa lugha moja adhimu sana, lugha ya KIHILIKI. Lugha iliyowaunganisha Watawanyikeni na walowezi waliotoka ughaibuni.
Lugha ya Kihiliki iliwezesha ule muingiliano wa kibiashara kati ya makabila na makabila pamoja na Walami kuwa mkubwa, na waliweza kuwasiliana na wenyeji kwa kutumia lugha hii.
Kiasi lugha ya Kihiliki hiitwe lugha chotara hisiyo na hati miliki ya kabila moja. Ni lugha ilojegwa kwa mchanganyiko wa makabila mbalimbali ya TAWANYIKENI, lugha kutoka kwa Wabuni, Wafurushi, Wahinda, Wapotogiza, Walami. Kiasi ya kwamba ni rahisi sana kwa mtu kuzungumza bila kujiona kuwa anajipendekeza kwa kabila fulani.
Walami japokuwa walikuwa na lugha yao ya Kilami, lakini waliona kuna umuhimu mkubwa sana kuendelea kutumia lugha ya Kihiliki, kwa sababu ndo lugha pekee ambayo wenyeji wa TAWANYIKENI na wale wa visiwa vya SIWANZA waliweza kuwasiliana wao kwa wao, licha ya kuwa na makabila zaidi ya mia mbili.
Lugha ya Kihiliki iliendelea kutumika kwenye mambo mengi ya wenyeji na kusomesha kwa lugha ya Kihiliki, Ghafimadharika, nchi ilipokuwa chini ya usimamizi wa Malikia wa Kilami, lugha ya Kihiliki iliendelea kutumika kama ndio lugha ya mawasiliano kwenye kila nyanja, kuanzia serikalini, maofisini masokoni na sehemu mbalimbali za kijamii.
HARAKATI ZA KUMUONDOA MLAMI
Watawanyikeni walipokuja kushtuka na kutaharuki wakajikuta wanatawaliwa na Walami. Walami waliwakuta wenyeji wakiishi kwa fauwa na usawa, walipo fanikiwa kuwatawala tu wakawagawa na wengine wakawa fawidhisha kiasi cha kujiona kuwa
MAFAWAISHI waliojiona bora kuliko wengine ambao wengi wao walikuwa MAKABWELA.
Baada ya Karne na MUONGO kadhaa za utawala wa Walami na haswa baada ya kumalizika kwa ugomvi ule mkubwa wa nchi zilizozungukwa na barafu nyingi. Baadhi ya Watawanyikeni, waliopelekwa kusaidia na kuongeza nguvu kwenye ule ugomvi mkubwa kabisa duniani kurejea nchini mwao. Wakajikuta wanahamasika kutaka kujitawala wenyewe na kuwaondoa Walami na Wabuni kwenye nchi yao.
Vuguvugu za kutaka kumuondoa Mlami zilianza nyuma kidogo kabla ya ugomvi ule mkubwa wa Walami, na zikaendelea kwa mapanga, marungu na mikuki na mishale.
Kumbukumbu kubwa ni ile vita vya mvua na radi, vita ambavyo wenyeji wa kusini mwa TAWANYIKENI waliamini kuwa watakapo nyeshewa na mvua, kabla ya kupambana na Mlami kutawafanya wasionekane na risasi za Mlami. Ushujaa na uhodari wao ule hakuna aliyeweza kuurithi hata mmoja, mpaka hivi leo.
Harakati zilishika kani zaidi kadri muda ulivyokwenda harakati hizi ziliongezeka na kuwa maarufu haswa walipomkaribisha kijana mmoja aliyemsomi kama wasomo wengine waliobahatika kusomeshwa na Walami.
Ghulamu GHAMIDHA aliyejulikana kwa jina la Hambiliki, wazee wakamweka mbele ili awe kiongozi na si mtawala aliyekuwa RAMBUKA, kutoka kabila dogo la Kana, hodari wa kuimba na kucheza ngoma, kwa jina maarufu akiitwa Manju mwasisi wa fikra ya Mangazimbwe.
Huyu ndio wananchi ya TAWANYIKENI WAKAMKADIMISHA kuwa Kiongozi wao.
Kipindi kile cha vuguvugu za kiharakati, watu hawakuwa waoga kueleza kweli, vijana kwa wazee, wake kwa waume, walijitolea kwa hali na mali ili kufikia malengo ya kupatikana kwa uhuru kamili katika kujitawala na kujiamulia mambo yao wenyewe.
UHURU WA NCHI YA TAWANYIKENI
Jitihada na harakati zile zilizaa matunda na hatimae nchi ya TAWANYIKENI ilipata uhuru wake.
Japokuwa wachunguzi na wajuwaji wa mambo yale yaliofichika wanasema kuwa uhuru wa nchi ya TAWANYIKENI haukuwa na shaka, lazima tu Walami wangeondoka, tena hata bila ya harakati zozote zile kwa kuwa eti umoja wa dunia ulikuwa umesha weka maazimio ya kuwapatia uhuru.
Hata hivyo hakika ilikuwa furaha ilioje kwa wazalendo haswa wale wanaharakati GHUBARI, waliojitolea kupigania uhuru wa TAWANYIKENI.
Wakati wa uhuru watu WAKARAMISIKA kwa Furaha uku wakifuatana RAMRAMU kwa RAMSA chereko, nderemo na vifijo bila ya RANGAITO za vurugu na ghasia na uku kina mama wakipiga vigereregere vikiendana na vifijo na nderemo za furaha zilizofanana na GHARADA za sauti za ndege waimbao vizuri nyakati za macheleo ya asubuhi jua linapochomoza na kuangazia uhai mpya kwa viumbe wa duniani na kuwapa TEREMA .
Kulikuwa na FASHFASHI hewani watu walivalia Maleba yaliopendeza na wote wakiwa na matumaini kuwa nchi imeachwa ikiwa FAKA, kiasi cha wana TAWANYIKENI wakitegemea kuishi kwa furaha na buraha daima dawamu.
Ni dhahiri kuwa usiku ule adhimu wakati ilipokuwa inashushwa bendera ya Walami na kupandishwa ile ya TAWANYIKENI, iliyokuwa na rangi ya Kahawia Kijani Kibichi, wengi walitokwa na machozi ya furaha kila aliyeshuhudia alikuwa na yakini kuwa ule ulikuwa ndio mwanzo wa maendeleo ya nchi ya TAWANYIKENI.
Raia wa TAWANYIKENI wakawa na hamu na ghamu ya maendeleo ambayo yangekuja kuonekana katika hali bora zaidi za kiuchumi kwa taifa na mtu mmoja mmoja, nyumba bora zaidi, kilimo cha kisasa zaidi, usafiri bora zaidi na juu ya hayo elimu bora zaidi kwa watu wote.
MAISHA BAADA YA UHURU NA UONGO BORA
Baada ya uhuru ule watawala wa TAWANYIKENI walifanya mengi wakidhani kuwa wanaendeleza nchi.
Hali ya kimaisha iliyotarajiwa na raia wa TAWANYIKENI, si vile walivyoitegemea. Kiasi baadhi ya wazee wamesikika wakisema kuwa "Lahiti tungalijuwa kuwa Uhuru ule ungetuletea mashaka haya nina ukakika kabisa washujaa wetu wasingetumia mali zao na muda wao kuondoa ubaguzi wa Walami na hata ingekuwa tumepewa uhuru bila ya harakati basi hakuna ambaye angesheherekea kama ilivyokuwa siku ile ya uhuru".
Lakini basi hakuna mtu yeyote aliyekuwa na mashaka siku ile ya uhuru wa nchi ya TAWANYIKENI na juu ya uhusiano mkubwa uliokuwepo baina ya kuondoka kwa Walami, yaani kupata uhuru na kukaribisha aina mpya ya ukoloni ambao kwa jina jingine la kizalendo zaidi yaani NAIZESHENI, yaani kuwapatia raiya wachache nafasi za kutawala wengine na uku wakikumbatiwa na watawala wa nchi.
Miaka ikasonga mbele, hali za raia hazikuweza kuhimarika sana, wengi wa wale waliokuwepo na wale waliokuja kuzaliwa nyuma, wakawa na wakati mgumu wa kubainisha tofauti za wakati ule wa utawala wa Walamii na ule wa Manaizi, ni utawala upi ni bora kwao.
Baadaye watawala wa TAWANYIKENI na wale wa kule SIWANZA wakaamua kuunganisha nchi mbili ambazo kwa simulizi za wahenga wenye elimu ya mithiolojia na Visasili wanatuhadithi kwamba, kabla ya Gharika kuu, iliyoikumba dunia, hizi nchi zilikuwa ni nchi moja, ila baada ya ile zahma ya gharika, nchi iliyokuwa moja ikajikuta imegawanywa mapande mawili.
Mapande hayo ya ardhi baadae sana, yaani baada ya kupita karne nyingi sana zikaja kujulikana kwa majina ya TAWANYIKENI na SIWANZA.
Ndipo mwaka mmoja watawala wale shupavu kwa jeuri zote wakaamua kuzirejesha nchi zile mbili zilizotengenishwa na gharika kuu na kuziunganisha tena na kufanya Muungano ulizaa jina la TWAWAWEZA.
MAAZIMIO MBALIMBALI YA NCHI YA TWAWAWEZA
Watawala wa nchi mpya ya Twawaweza hawakuishi kuziunganisha nchi hizi tu, maana maazimio yao yalikuwa mengi sana, miaka michache baadae wakaona si vibaya kuchukuwa kwa nguvu mali, majumba, mashamba na mashirika waliyo yakuta na kuyafanya kuwa ni mali ya kila raia.
Kwa ufupi walinyang'anya mali za watu binafsi na kuzifanya za taifa zikisimamiwa na viongozi wachache. Jambo lile lile la kuchukua mali za watu lilipewa jina la AKUMAU yaani Azimio la Kurudisha Mali kwa Umma.
Viongozi wa nchi ya Twawaweza wakiongozwa na mtawala mpya Manju Hambiliki, awakuishia hapo tu, fikra zao sahihi zikazaa mazimio kadhaa.
Moja wapo ya maazimio hayo ni lile la kutoa madaraka ya kila mkoa, matokeo yake azimio lile likaua ushirika ambao uliweza kuwasaidia raia wengi wa nchi ya Twawaweza ushirika ambayo ulianzishwa na wananchi wenyewe.
Muda haukwenda mbali, kukapatikana fikra ya kuongeza walimu wa shule za msingi, na matokeo yake wakachukuliwa wanafunzi waliomaliza standadi seveni na kuwaingia kwenye ualimu.
Uamuzi ule ulikuja kuigharimu nchi ya Twawaweza, maana grafu ya elimu ndipo ilipoanza kushuka kwa kasi sana.
MAISHA NI BAHATI, IFUMBATE
Maisha yaliwafumbata, wakafumbatika haswa, udufu ukawavaa nao ukauvaa. Uroda na udora ukawatia uduwazi, uku wadwanzi wakifaidika. Baadhi yao wakakusanywa katika kutegemea ujamilifu wa kukaa pamoja. Kukaanzishwa maduka ya kaya, elimu bure, kutaifisha majumba, mashamba na kila dhahma.
Manju nao hawakuwa nyuma maana nyimbo nyingi zilitungwa, walidirizi kupongeza na kuhamasisha. Raia wa nchi ya Twawaweza walihishimu sana Manju wao, hivyo moyo wa uzalendo ulionekana wazi wazi machoni mwao, walidirizwa wakadirikika.
La mgambo likilia kuna jambo, mganda ukahitika, amri ikashushwa toka nyumba kuu, waliambiwa nao wakaamini kuwa Twawaweza si nchi huru, hadi wale wote wanaoishi kwenye bara lile kubwa duniani, bara la Ghafima lote liwe huru. Ilikuwa fikra nzuri mno, iliyogusa Mtima wa kila raia, awakujuwa kuwa UTILIFIKU wa mali na rasilimali za taifa lao.
Walitumia kila kitu walichoweza hili kufikia lengo la wale waliobondeni mwa bara la Ghafima nao wawe kama wao. Wakawasaidi kutoka mikononi mwa mahamia walowezi, wakiamini kuwa wale wa bondeni ni ndugu zao haswa. Wapo walipewa hifadhi ndani ya ardhi ya Twawaweza, wao na wajukuu zao. Hakika watu wa Bondeni walifaidi sana msimamo ule.
Manju wakubwa kwa wadogo, awakuchoka maana siyasa ile ya umoja na kutegemeana ilikuwa imeshika kani. Raiya wa Twawaweza walifunzwa mbinu nyingi za kufanya propaganda za oronjo wa kisiyasa na mavanga.
Alfajiri moja iliotulivu, likasikika Parapanda, lililo ondoa upanyavu wa asubuhi ile. Baragumu lililosikika kutoka kwenye kisemeo cha nyumba kuu, kuwa Joka Kubwa lenye vichwa saba, limevamia mifugo yetu, mifugo ambayo ndio lishe ya kuwalisha ndugu zetu waishio Bondeni mwa Ghafima.
Joka ilo hatari limesababisha kuzorotesha harakati za kuikomboa Ghafima. Na lengo haswa la Joka Kuu lile ni kulimeza Bara lote la Ghafima loh! Salalah, Wananchi wa Twawaweza wakaingia kwenye taharuki.
Maana waliambiwa kuwa kule Kasikazini mwa ardhi yao, kumemezwa tayari na hata ile zile tamtamu guru imeliwa yote na Joka lenye vichwa saba.
Raiya wa Twawaweza licha ya umasikini wao, lakini walikubali kujitolea kwa hali na mali na roho zao hili kwenda kulitapisha Joka lile kuu, na ikiwezekana kulirudisha uko lilipotoka au kulikimbiza kabisa liende mbali au lirudi kwa mfugaji wake.
Raiya wa Twawaweza wakalikabiri Joka kuu, waliobahatika kuliona wakanong'ona kwa kusema kumbe ni kama sisi tu, basi wakaingia kwenye shimo lake wakampa adhabu kidogo. Kisha mahala pake wakamweka Nakonda, nyoka mwingine waliomtaka wao. Kwa amri ya Manju mkuu.
Mambo yote yalifanyika, aliyehoji alifungiwa chumbani, pamoja na mahuluku wengine, wakiwemo chawa na kunguni na ndugu zao viroboto.
Basi raiya wakaogopa kuhoji, wakaogopa kuuliza, wakaogopa kusema, wakaogopa kukasirika, wakaogopa kutabasamu, wakaogopa kununa, wakaogopa hata kucheka kwa sauti. Hata kwenye misiba walitakiwa kuto onyesha huzuni wala majonzi na hata kutabasamu ilikuwa ni haramu.
Maana waliambiwa kuwa kwa kufanya hivyo ni katika harakati kuleta maendeleo ya nchi ya Twawaweza.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?