Thursday, 17 June 2021

Vaccination or zombilification, Ghafla Kukawa Kiza Totoroo

Uko mitandaoni, kumekuwa na taarifa kadhaa zinazohusu chanjo, zipo taarifa hasi na chanya, zenye kuogopesha na zenye kutia matumaini.

Serikali za mataifa mbalimbali Ulimwenguni kote watu wanahimizwa kupokea chanjo za UVIKO 19 (COVID-19) ili kujilinda na kupambana na janga la virusi hivyo. 

Hata hivyo wapo wale ambao wana mashaka na hizo chanjo na haswa baada ya kupatikana kwa habari mbaya kwa baadhi ya watu kupata matatizo baada ya kupatiwa chanjo haswa chanjo ya Oxford-AstraZeneca.

Awali Jamuhuri ya Ireland ilichukua uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya Oxford-AstraZeneca kwa kuhofia hatari ya watu kuganda damu

Taifa hilo sio pekee ambalo limetilia shaka usalama wa chanjo hiyo ya Oxford-AstraZeneca kwani nchi nyingine zilizofanya uamuzi huo ni pamoja na Uholanzi, Denmark, Norway, Bulgaria, Iceland na Thailand. Kwa nchi za Afrika ni Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda, japo wanasua sua...

Kupitia taarifa ya watengenezaji wa AstraZeneca wamesema kuwa hakuna ushahidi kwamba kuna ongezeko la kuganda damu miongoni mwa watu waliochanjwa.

Habari hizi na nyingine kadhaa, ndizo zimeongeza hofu na taaruki kwa baadhi ya watu, kiasi cha wanaharakati wengine kuanzisha kampeni za kupinga usambazaji wa chanjo.

Uko mitandaoni ukifuatilia mijadala, utaingiwa na hofu kubwa sana, kama hofu niliyoipata mie kuhusiana na hizi chanjo.

HOFU ILINIJAA KWA KUTOONA TENA

Hofu ilinijaa, kiasi cha kutengeneza hofu kwenye ubongo wangu, kiasi nikisikia tu habari za chanjo, basi mapigo ya moyo uongeza kasi bila ya mimi mwenyewe kuyaamrisha.

Sikutaka kabisa kusikia eti natakiwa nami niweke mihadi (Appointment) mtandaoni ya kwenda kupata chanjo, japokuwa kazi ninayoifanya ni hatarishi, maana nakutana na watu wengi na miongozi mwao wana maambukizi tayari. 

Nilitamani niwe wa mwisho kabisa kupatiwa chanjo, baada ya raia wote wasiopungua milioni nne nchini hapa Ireland kuchanjwa, nilitaka nishuhudie chanjo zikiwakigeuza Mandondocha au Misukule (Zombies) hali uku mimi nikiwa si miongoni mwao.

Nilidhamiria hivyo na nikatamani iwe hivyo, lakini haikuwa kama nilivyotaka.

Juzi hapa, daktari wangu (GP), kupitia muuguzi (nurse) alinipigia simu, nikaipokea nikiwa nipo kazini.

Muuguzi wa zamu akaniuliza kama muongeji ni mimi, na baada ya kumthibitishia kuwa ndiye, akanipa taarifa ambayo sikuipenda kabisa kuisikia masikioni mwangu.

Alinipa taarifa iliyopasua moyo wangu na kusababisha mapigo ya moyo kuongeza kasi, nilihisi kwa mbali kinywa kikijaa mate machungu mdomoni kisha bila ridhaa yangu, yakarudi tumboni.

Taarifa ilisikika wazi na ilipasua ngome ya masikio yangu bila chenga, kuwa natakiwa siku ile mida ya alasili, niwe nimefika kwa daktari wangu kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya UVIKO 19 kwa kudungwa chanjo ya Pfizer/BioNTech.

Akili yangu ikafanyakazi maradufu ya kawaida yake, ikiwaza ili na lile na mambo kadhaa kwa sekunde na wakati mmoja, picha na maelezo mbalimbali yakanijaa pomoni. Habari mbaya na nzuri zote zikapita akilini mwangu kama umeme wa radi. 

Nikataka kukataa, lakini nikakumbuka kuwa hapa kazini, wafanyakazi wote tunatakiwa tuwe tumekwisha pata chanjo ya Korona kwa hiyari ya lazima.
Mwishowe nikajitia ushujaa, nikajiambia kuwa "Kifo cha Wengi Harusi". Nikapiga moyo konde, nikamjibu kuwa hapa nilipo nipo kazini, je awawezi kuhairisha mpaka siku nyingine?

Nikajibiwa hapana, ninapaswa niwepo kituoni kupata chanjo bila kukosa, na sababu kuu mbili zikatolewa kuwa umri wangu na kazi nihifanyao ndio imepelekea kuwa miongoni mwa watu wa mwanzoni kupatiwa chanjo ya UVIKO 19.

Sikutaka kubishana tena, nikamkubalia kwa shingo upande kuwa nitaudhuria bila kukosa, maana sikutaka kupoteza ajira yangu, tena baada ya kukaa nyumbani mwaka mmoja na nusu bila kazi.

Nikaomba ruhusu kwa kiongozi wa zamu, kuwa naelekea kwenye kituo cha chanjo, naye bila ajizi akanipa ruhusa na kunipongeza kuwa nimefanya maamuzi ya busara sana kwenda kupatiwa chanjo.

Nikamwangalia na kutabasamu tu, uku ndani ya mtima wangu naugua kwa mashaka niliyonayo moyoni, maana woga na hofu vilikuwa vimenijaa, kiasi cha kunichanganya akili.

Kwa shingo upande, nikaelekea zangu kwa daktari wangu, nikakuta kuna mtu mmoja kanitangulia. Nikapewa fomu ya karatasi na kutakiwa kujaza kama nina tatizo lolote lile la kiafya, kama vile shinikizo la damu, mzio _(allergy)_ au damu kukataa kuganda pale inapotoka kwa kutobolewa na sindano na maswali mengine kadhaa wa kadha kuhusiana na afya yangu kiujumla. Majibu yote yakawa HAPANA.

Nikarudisha fomu yangu kwa muuguzi wa zamu, uku akitabasamu na kuniambia kuwa nisubiri kidogo, dakika si nyingi nikaitwa na muuguzi niingie ndani kwa ajili ya kupatiwa chanjo.

Muuguzi akanitazama, kisha kama aligundua kitu kwenye fikra zangu, akanihakikishia usalama wangu na kunieleza kuwa nisiwe na wasiwasi wala kuwa na hofu kila kitu kitakuwa sawa tu na hata wao walisha patiwa chanjo kabla...

Mie mapigo ya moyo, kwa mbali yakaanza kuongeza mwendo, japo nilijikaza kisabuni... Akachukua dawa na sindano na kunitaka nichague bega, nikamwambia bega la upande wa kushoto, maana mie natumia mkono wa kulia kwa kazi zangu zote.

Baada ya kupandisha shati nililovaa, muuguzi akanisogelea uku mkono mmoja kakamata sindano na mkono mwingine ana pamba yenye sipiriti, akapangusa bega langu nami nikajikuta nafumba macho uku moyoni nikisoma dua kadhaa wa kadhaa.

Nikashtuka ananambia kuwa tayari kesha maliza, na nikatakiwa nipumzike kwa dakika 15 na baada ya hizo dakika ndio naweza kuondoka zangu.

Nikatoka zangu na kukaa kwenye viti kwa ajili ya kupumzika, kwa mbali nikaanza kusikia kama kichwa kinaniuma, nikalisikia na tumbo nalo linaita, ngruuuu! Nikajiuliza nitatizo au woga, nikajikuta nabanwa na haja ndogo ghafla, nikajisemea moyoni, sasa mambo yeshaanza, ili kojo limetokea wapi ghafla hivi?

Nikanyanyuka na kuingia zangu msalani uku taa ya mle ndani ikijiwasha yenyewe... nikapunguza maji mwilini na kuyaangalia jinsi yalivyo ya njano _(nikasahau kuwa saa mbili zilizopita nilikunywa orange Squash)_ na rangi ile inatokana na ile sharubati niliyokunywa... Hofu ikapanda, baada ya kujisafisha, nikawa nimesimama kwenye kioo mule mule msalani. 

Nawaza na kuwazua, kichwa nacho kama kinauma, macho kama sioni vizuri (nikasahau kabisa kuwa sikuvaa miwani yangu ya macho), ghafla kukawa kiza.

Tobaa! Yailahi... nikajisemea moyoni kuwa nishakuwa kipofu, mbona ghafla hivi sioni, akili ya binadamu inafanyakazi kwa haraka sana, nikawaza mambo kadhaa kwa mara moja (Familia yangu, mke na watoto, ndugu na marafiki, kazi yangu, michezo ninayoipenda kwenye Runinga, vyote vikaja kichwani), wakati nawaza hayo ilikuwa kidogo nianguke kwa hofu, nikajipiga kwenye mlango wa kutokea, na ghafla tena kama ilivyotokea mwanzo, mwanga ukaangaza mule msalani...

Kumbe kilichotokea ni taa kujizima tu na si macho yangu yameingia upofu, nikakumbuka kuwa mle ndani msalani taa yake inatumia sensa maalum, kama kukiwa hakuna harakati zozote taa inajizima na kukiwa na harakati taa inawaka, nikakumbuka nilivyoingia sikuwasha taa, bali taa iliwaka yenyewe...

Nikatabasamu, kisha nikatabasamu tena, kisha nikacheka, nikajicheka kwa kuwa na hofu ambayo haipo, hofu ambayo ilikuwa imepandikizwa kwenye mioyo na akili zetu kutoka mitandaoni na haswa tovuti jamii...

Nikajisemea moyoni hama kweli hofu usababisha madhara na hata kifo... Sina maana kuwa ukichanjwa hutakufa au usipochanjwa hutokufa lahasha, kinachotakiwa ni kile kinachoitwa "Kinga ni Bora Kuliko Kuponya."

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!