Monday, 31 May 2021

WAMAREKANI WEUSI NA HARAKATI ZA KUREJEA AFRIKA

Back-to-Africa Movement (BlacExit)

Miezi kadhaa nyuma, nilikuwa nimevutiwa na vipindi vya Runinga vya kwenye Mtandao, haswa video zilizoko Youtube. Video zilizonivutia zilikuwa ni za Wamarekani Weusi, waliorudi na kukaa Barani Afrika, wakielezea furaha walizonazo, kwa wao kukaa kwa amani na buraha katika nchi za Afrika, haswa nchi ya Tanzania, Ghana, Namibia na Rwanda.

Kuna idadi kubwa ya Waamerika wenye asili ya Kiafrika wanaohama kwa sababu kubwa moja, "Ubaguzi wa Rangi" na wengi wao wanaona Afrika ndio mahali salama na sehemu yenye amani zaidi na kusiko kuwa na ubaguzi wa rangi, wengine wanasema wanahama kwa sababu ya usalama wao na wa watoto zao.

Na Nchi inayo ongoza kuwapokea Wamarekani wenye asili ya Afrika ni nchi ya Ghana. Nchi ya Ghana Inawapa Uraia Wamarekani Wengi Wenye Asili ya Kiafrika Bila Masharti Magumu na hata Umilikaji wa ardhi kwa masharti Nafuu.

SIWEZI KUPUMUA - I CAN'T BREATH

I can't Breath, ni maneno ambayo yalitamkwa na Mmarekani mwenye Asili ya Kiafrika Eric Garner, aliyekabwa na kuawa na polisi mwaka 2014.

Wamarekani wengine wenye asili ya Afrika waliokumbana na maswahibu hayo ya kupoteza uhai kwa kukabwa koo na polisi wa Kimarekani, baadhi yao ni Javier Ambler, Manuel Ellis, Elijah McClain na hivi karibuni George Floyd.

Kuuawa kwa Floyd, kuliamsha hamasa na hisia kali sana na kupelekea kutokea kwa maandamano makubwa sana nchini Marekani na Duniani kwa ujumla, kiasi cha kupeleka kuwepo kwa kauli mbiu ya Black Life Matters.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2020 iliyotolewa na gazeti la New York Times, kumekuwa na matukio yasiopungua sabini (70) ya raia weusi kukabwa na Polisi, nchini Marekani.

USULI WA HARAKATI ZA KUREJEA AFRIKA

Wamarekani wenye Asili ya Kiafrika Wakiondoka Nchini 
Marekani, Kuelekea Nchini Liberia March/21/1896

Vuguvugu za harakati za Waafrika waishio Marekani kurudi Afrika, hazikuanza hivi karibuni. Zilianza mwishoni mwa karne ya 18 na kushika kani mwanzoni mwa karne ya 19.

Watumwa walioachwa huru, hawakukubaliwa kuishi ncnini Marekani, ususiaji ulikuwa mkubwa haswa toka kwa wazungu, Wamarekani weupe awakutaka kabisa kuchanganyika na Wamarekani wenye asili ya Afrika, wakiwaona kama watu wasiofaa kuchanganyika nao. Ndio Baadhi ya Wabaguzi wakaanzisha mpango wa kuwarejesha Wamarekani Wenye asili ya Afrika, kuwarejesha Afrika.

Hali ya kuwarejesha Waafrika barani Afrika, ilichochewa zaidi Mnamo tarehe 18 Novemba 1803, pale Waafrika Walioko nchini Haiti walipofanya uhasi na kufanikiwa kukamata nchi ya Haiti na kujitawala.

Hii ikapelekea miaka iliyofuata, kuanzishwa kwa taifa la Liberia na uko wakapelekwa Waafrika wengi walio huru kutoka utumwani nchini Marekani. Mpango ulifadhiliwa na kupangwa na shirika moja la Kimarekani lililojulikana kama Jumuiya ya Ukoloni ya Amerika (The American Colonization Society - ACS).

Kulikuwa na kampeni kadhaa wa kadha za kuwashwishi na kuwahakikishia usalama wao kuwa wafikapo uko Afrika watamiliki Ardhi na maisha yao yatakuwa bora mara dufu.

Wahamiaji wengi waliopelekwa Liberia walipoteza uhai. Kiwango cha vifo vya wahamiaji kilikuwa cha juu sana katika historia, Kati ya wahamiaji 4,571 ambao walifika Liberia kati ya mwaka 1820 na mwaka 1843, waliobahatika kufika salama ni watu 1,819 tu ndio walionusurika.

Kwa ujumla, harakati hizi hazikufanikiwa sana; ni watumwa wachache tu ndio walitaka kuhamia Afrika. Idadi ndogo ya watumwa walioachiliwa huru kutoka utumwani walikubali kuhamia Afrika, wengine wengi walilazimishwa.

Wengi wao waliopelekwa Liberia na Sierra Leone walikabiliwa na hali mbaya sana. Wengi wao hawakukubaliwa na wenyeji na wengi walifariki kutokana na magonjwa kadhaa haswa Malaria.

VUGUVUGU JIPYA LA KARNE YA 20

Katika karne ya 20, mwanaharakati wa kisiasa na Mwamerika mweusi, mwenye asili ya Jamaika, mwasisi wa vuguvugu la Rastafari, Marcus Garvey, aliunga mkono harakati za weusi kurudi Afrika, na Waamerika wengine wa Kiafrika waliunga mkono wazo hilo, lakini ni wachache waliokubali kuondoka Marekani.

Kulikuwa na Idadi kubwa ya Waafrika waliokuwa huru ndani nchi ya Amerika, wengi wao walianza kutafuta fursa, haki na usawa. Wamarekani wengi weusi walioachiliwa kutoka Kusini mwa Amerika, walihamia Kaskazini, maeneo yenye viwanda ili kutafuta ajira viwandani.

Wengi wao hawakutakiwa mahali popote, walibaguliwa na kufukuzwa; walionekana kama wageni, wahamiaji haramu ambao walitishia ajira za Wazungu. Wazungu awakuwaona watu weusi kama wanahaki ya kuajiriwa zaidi ya kuwa watumwa.

Mtu mweusi hakuwa na thamani wala hakuwa na nafasi nchini Marekani. Kuna matukio mengi sana ya kibaguzi, kuanzia polisi mpaka raia wa kawada, ukiondo matukio ya kibaguzi, nchi ya Marekani inakabiriwa na idadi kubwa sana ya jinai na uharifu, kwenye vitongoji vya Waafrika nchini Marekani.

Hali hii imechangia sana kwa baadhi ya Wamarekani weusi kufikia maamuzi ya kuhamia Afrika na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya na Asia.

Mnamo 2006, mwigizaji mwenye asili ya Afrika na Amerika Isaiah Washington alikubaliwa kwenye ukoo wa Wamende na akapewa jina la mkuu wa GondoBay Manga. Mnamo 2010, akatunukiwa uraia wa Sierra Leone, hii ni baada ya kupima vinasaba Asili (Genealogical DNA) na vipimo vyake kuonyesha kuwa yeye anatokana na kabila la ukoo WaMendes.

Hii ilikuwa mara ya kwanza ambapo upimaji wa Vinasaba Asili ulitumika kumpatia mtu uraia katika moja ya taifa la Kiafrika.

UVIKO 19 NA WAHAMIAJI WEUSI TOKA MAREKANI

Kuna mengi yenye kupelekea Waafrika weusi wa Kimarekani, kuhama nchini Marekani na kuhamia Afrika, wengi wao ukiondoa hali ya kiubaguzi na kutothaminiwa nchini mwao, wengi wa Afrika hao, uishi kwa wasiwasi wakiogopa polisi na jamii ya wabaguzi na hata weusi wenzao.

Ukizingatia pia miji yenye makazi ya weusi, imekuwa ni vichaka vya uhalifu, uuzwaji na uvutaji wa madawa ya kulevya, wizi na ujambazi wa kutumia siraha, vimekuwa ni vitendo vya kawaida sana.

Wale waliobahatika kuingia kwenye nchi za Kiafrika, wamekuwa mabalozi wazuri sana, wakijirekodi na kutuma video kadhaa wa kadha kwenye mitandao ya kijamii, haswa Youtube, Facebook, Instagram na Twitter. Wakisifia hali ya kiusalama kwenye nchi walizofikia. Urahisi wa maisha, vyakula vya kiasili wanavyokula na ujirani wa kweli kutoka kwa wenyeji.

Wakagundua kwamba yale yote yanayo onyeshwa  kwenye vipindi vya Runinga kuwa Afrika ni nchi yenye Ukame, njaa, magonjwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe si vitu vya kweli.

Wazungu Wakiwashambulia Waafrika, Mauaji ya Atlanta 7/Oct/1906

Hii imepelekea wengi wao, kuondoka Marekani na kuelekea nchi ya ahadi, Afrika. Hata wale waliokuja likizo, baadhi yao au wengi wao wamejiwekea ahadi ya kurejea tena aidha nchi ile ile waliokuja mwanzo au kuendelea kutembelea nchi zingine za Kiafrika kwa lengo la kutafuta nchi ambayo wanahisi wanaweza kuanza maisha mapya.

Wengi wanakwenda Ghana, Nigeria, Benini, Togo, Tanzania, Rwanda, Namibia na Kenya. Wapo walioingia Tanzania kati ya miaka ya 60 na 70, kipindi cha harakati za kujikomboa mtu mweusi, haswa wale wanachama wa Black Panther, ambao wachache wao bado wanaishi Arusha, Tanzania hadi leo.

Kipindi hiki cha uwepo wa Korona, kumepelekea Wamarekani weusi wengi, kuikimbia Marekani, wakikimbia Karantini ya Kufungiwa ndani ya majumba yao. Nchi nyingi za Afrika zilikuwa zimefunga mipaka yake, kuogopa Korona, kasoro nchi ya Tanzania peke yake.

Hali hii ya Tanzania kutofunga mipaka, kilisaidia sana kwa wao kubadirisha tiketi zao za ndege ili waweze kwenda Tanzana badala ya nchi walizodhamiria kwenda, maana Tanzania haikuwa chaguo lao la kwanza.

Wakagundua kuwa ni Tanzania pekee, ambayo haikufunga mipaka yake mwaka 2020. Na wananchi wa Tanzania, wanawapokea kwa mikono miwili. Wakajikuta wanakaribishwa kwa bashasha na furaha.

USUNGO NA USULUHI

Wengi wao wanajifunza mila na utamaduni mpya wa Kiafrika, mfano nchini Tanzania, wengi wao wanaishi vitongojini au kule tunakokuita Uswahili, uko wanajifunza mila na utamaduni mpya wa Mtanzania. Utamaduni wa kuishi kijamaa na kwa Upendo mkubwa na ujirani mwema.

Wanashangaa jinsi watu wasiojuana wakisalimiana asubuhi, Mchana na Jioni, wanashangaa jinsi watoto wa Kitanzania jinsi walivyo na heshima na adabu, wanshangaa wakiona watoto wa shule za msingi wakipanda mabasi wenyewe kwenda na kurudi, bila ya wazazi wao, wanashangaa jinsi Watanzania wanavyo saidiana kwenye shida na raha, wanashangaa kuona wingi wa vyakula vya asili kama matunda na mboga za kila aina, fukwe za bahari zenye maji yaliyo masafi kama kioo.

Wanashangaa kuona kuna fursa za kila aina za kujiongezea vipato, wanashangaa kutosikia milio ya risasi, wanashangaa wakikaribishwa majumbani na watu wakitembeleana bila mialiko, wanashangaa kwenye kila hatua wanayopiga...

FURSA KWAO NA KWA NCHI

Je Tanzania Kama Nchi, Imejiandaa Vipi Kuwapokea na Kuwapatia Uraia?

Hili ni swali hata hao wahamiaji wapya wanajiuliza, kwa sasa hivi sheria zilizoko wahamiaji wengi wanakuja kwa kutumia VISA ya utalii. VISA inayowawezesha kuishi nchini Tanzania kwa miezi mitatu na baada ya miezi mitatu kwisha wanatakiwa watoke kisha waingine tena. Jambo hili limekuwa ni kero kubwa kiasi chake. Hii inapelekea kupata usumbufu kwa wale wenye mapenzi ya kutaka kuishi ndani ya nchi na kuwa raia wa kawaida kama raia wengine.

Na hata suhala la uwekezaji kwenye nyanja mbalimbali limekuwa ni jambo la usumbufu kiasi chake, kuna haja kwa serikali kuangalia upya sheria yake ya uhamiaji na urahia pacha na haswa kwa wale ambao wanataka kuwekeza hata kama mitaji yao si mikubwa sana.

WANAKARIBISHWA NCHINI GHANA BILA MASHARTI

Ghana inawapa Waafrika wa Kimarekani nafasi ya kuhamia nchini Ghana, huku kukiwa na kauli mbiu kutoka serikalini "Warudi Nyumbani" na waiache nchi ya Marekani ambayo hawatakiwi.

Nchi ya Ghana ambayo ipo magharibi mwa Afrika kihistoria ilikuwa kitovu kikuu cha biashara ya watumwa, kwa nchi zilizoko Magharibi mwa Afrika.

Na Mwaka 2019, Ghana iliendesha kampeni ya kubwa sana ya utalii iitwayo "Mwaka wa Kurudi", Kampeni ambayo ilikuwa lengo la kuadhimisha kutimia miaka 400 tangu meli ya kwanza ya watumwa kufika kwenye mji wa Virginia, Nchini Marekani.

Serikali ya Ghana kupitia serikali za mitaa wamezitaka kutenga ekari 500 za ardhi kwa wageni, ikitoa nafasi ya kutosha kwa familia zipatazo 1,500. Awatozwi ada ya usajili kwa diaspora wa Kiafrika.

Mnamo mwaka 2019 Idadi ya wageni kutoka Marekani, Uingereza na nchi zingine iliongezeka sana, kuanzia Januari hadi Septemba ilifikia watu 237,000 ni ongezeko la asilimia 45%, hii ni kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Utalii ya Ghana.

Serikali ya Ghana wana mpango wa miaka 10, wa kuwawekea mazingira rafiki kwa Wamarekani weusi, mpango huo uliozinduliwa mnamo mwezi Juni 2019.

Wanakadiria kupokea watalii wasiopungua milioni 1.5 wakiwemo watu mashuhuri, wanasiasa , viongozi na watu wa kawaida, wanatarajia mpaka kufikia mwisho mwa mwaka kuingiza dola bilioni 1.9 Pesa ambazo zinatarajiwa kupatikana katika mapato kama matokeo ya shughuli za "Year of Return" Mwaka wa Kurudi.

Sekta ya utalii pia imetoa takwimu ya ongezeko kubwa la watalii kwa asilimia 18% kwa wanaowasili kutoka Amerika, Uingereza, Karibiani na nchi zingine muhimu, wakati jumla ya idadi ya watu wanaowasili kwenye uwanja wa ndege wameongezeka kwa asilimia 45% kwa mwaka.

Makadirio ya uduma kwa watalii yameongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka dola $1,862 kwa mtalii mmoja mnamo 2017 hadi dola $2,589 kwa kila mtalii, na athari ya ongezeko la mapato yanayotokana na utalii inakadiriwa kuwa karibu dola bilioni $1.9 

Katika moja ya kampeni ambazo inasimamiwa vema na kuwaonyesha kuwa weusi wanakaribishwa na Afrika ndio nyumbani Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo Kwenye Mzishi ya George Floyd, alituma salamu za rambirambi na aliwapatia familia ya Floyd kitambaa cha jadi maarufu kama Kente, baada ya mazishi yake huko Houston.

Na baadaekukafuatiwa na waombolezaji jijini Accra, wakiimba maneno yake ya mwisho ya George Floyd, "I Can't Breath - Siwezi Kupumua."

Nchini Ghana kuna program zisizopungua 21, zenye lengo la kuwavutia Waafrika weusi kutoka marekani, kuanzia zile za utalii, uwekezaji na hata za uraia tu wa kawaida.

SWALI LA KUJIULIZA

Je Serikali ya Tanzania, wanalichulia vipi hili la Wamarekani Weusi kurejea Afrika, na ikiwezekana Kuishi Tanzania na kuwa Raia kamili? Maana miongozi mwao kuna wasomi wa kila aina ambao kwa njia moja au nyingine wanaweza kuwa ni hazina kubwa na chachu kwenye kuendeleza uchumi wa Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!