Wednesday 26 January 2022

 POLISI, ACHENI UGAIDI

Raia Tumechoka Kubambikiwa Kesi.

Kumekuwa Na Malalamiko Mengi Sana Kutoka Kwa Raia Wa Kawaida, Wafanyabiashara Na Hata Wanasiasa, Kuwa Jeshi La Polisi Nchini, Kupitia Polisi Wake Wachache Kuwa Wanatabia Mbaya Sana Za Kuwabambikia Kesi Raia Wa Nchi, Tabia Ambazo Hazina Tofauti Na Ugaidi.

Kuna baadhi ya watumishi wa jeshi la polisi wanakiuka miiko ya utumishi wao, malalamiko ya raia ni mengi na hayapaswi kupuuzwa, tabia ya kubabimbikiwa kesi, kuombwa rushwa, na hata kunyimwa haki mbalimbali, limekuwa ni jambo la kawaida sana.

Imefikia mahali bila kutoa rushwa basi polisi hawawezi kushughulia au kutatua matatizo ya wanyonge, hakuna raia anayejivunia kuwa jeshi la polisi ni jeshi rafiki kwa raia wake, HAKUNA.

Inapofikia mahala raia ndani ya nchi yake, raia anayelipa kodi au hata yule ambaye hana uwezo wa kulipa kodi, wakakosa imani na vyombo vya sheria haswa polisi, basi hapo kuna haja kubwa sana ya aidha waziri husika au hata Rais wa nchi kuvitazama/kukitazama upya chombo hicho cha usalama wa raia nchini.

Kumekuwa na matukio mengi sana ya polisi kuwapiga raia pale tu wanapokamatwa na kufikishwa kwenye vituo vya polisi. Vipigo ambavyo upelekea hata ulemavu wa muda au wa kudumu kwa raia hao. Mtu anapokamatwa na polisi anakuwa tu ni mtuhumiwa, ni mahakama tu peke yake ndio yenye uwezo wa kumtia mtu hatiani na ni pale tu ushahidi yakinifu unapo tolewa na kukubaliwa na hakimu, lakini kabla ya hapo huyo si mshtakiwa, bali ni mtuhumiwa tu.

Sasa hizi tabia za askari polisi, kuchukuwa sheria mikononi na kuwapiga watuhumiwa ni kwenda kinyume na haki za kiraia. Raia wengi wamepatikana na hayo maswahibu ya kupigwa pale wanapokamatwa na polisi, na wakati mwingine kwa kubambikiwa kesi, aidha za kuwa na Bangi au wizi na wakati mwingine hata kesi za mauwaji hata ugaidi.

Nakumbuka mwaka 20013, mwezi wa tatu, kituo kimoja cha Runinga kupitia taarifa yake ya habari ya saa 2.00 usiku, walilipoti kwamba Polisi wapatao 20, walivamia nyumba ya mfanyabiashara wa madini wakamuua na kupora na fedha hizo milioni 350, kwa madai ya kuwa walikuja kulipiza kisasi kwa kuwa mfanya biashara huyo alivamia kituo cha polisi na kumjeruhi polisi mmoja kwa risasi.

Tabia ya baadhi ya Askari Polisi kujihusisha na rushwa na ujambazi na hata mauaji ya raia na wafanyabiashara wa dhahabu kwa visingizio mbalimbali, linaonekana kama ni jambo la kawaida sana kwenye chombo hiki ambacho kinapaswa kuwa chombo rafiki kwa raia, lakini ni kinyume chake.

Hivi karibuni tumesikia tena taarifa ya kutisha sana, toka kwa kamanda wao akikiri kuwa askari wake saba wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji ya kigaidi kwa kijana mfanyabiashara na maiti yake kutupwa njiani tu kama maiti ya panya au mende. Kisa cha kuuawa ni kwa raia huyo mlipa kodi na mfanyabiashara ni pale alipothubutu kuwadai askari hao zaidi ya shilingi milioni 33 fedha zake halal, kumbe masikini hakujuwa kuwa polisi wale ni magaidi waliovaa unifomu za polisi, polisi ambao hawakuwa tayari kuheshimu kiapo walichohapa cha kulinda raia na mali zao.

Kwa tabia hii ya jeshi la polisi, kuna haja kubwa sana kuundiwa tume huru ya uchunguzi, ili hata zile kesi ambazo raia kadhaa wametuhumiwa nazo zipate kutazamwa upya, leo ikitokea raia kuamua kujichukulia sheria mikononi kwa kukosa imani na jeshi la polisi, ataitwa gaidi, na hata yale mauwaji ya yule kijana aiyeuwa polisi watatu na mlinzi mmoja binafsi, pia kunahitajika uchunguzi mpya.

Taarifa zilizotolewa hapo awali zilisema kijana yule alikuwa mtu wa kawaida tu katika jamii, sasa kwa ripoti ya polisi kumuita yule kijana ni gaidi kwa kweli ilileta hofu kwa raia, lakini kwa vitendo vya jeshi la polisi dhidi ya raia vinaleta hofu zaidi, maana raia hawana pa kukimbilia, jeshila polsi haliaminiki tena, kwani hatuwezi kujua watu wangapi wamedhurumiwa kimya kimya katika jamii yetu...


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!