Friday, 8 April 2022

 NI NANI AMEMUUMBA MWENYEZIMUNGU?

Swali Kutoka Kwa Wasio Amini Uwepo wa MwenyeziMungu:
'Ikiwa Mwenyezi Mungu Ameumba Kila Kitu, Ni Nani Aliyemuumba MwenyeziMungu?'

Moja katika Maswali ambayo hayana maana na swali linalo jipinga lenyewe (nonsensical and self-contradictory).

Ukilichunguza ilo swali, ni swali ambalo halina mantiki na halina maana (very illogical and meaningless). Labda swali linaweza kutafsiriwa kumaanisha, 'Ni Nani Aliyeumba 'Ambaye Hajaumbwa?'

Kuwepo kwa ulimwengu, sayari na viumbe vingine vyenye kutegemeana, hii inaonyesha kuwa viumbe vyote ulimwenguni ni tegemezi, hali hii ni uthibitisho tosha kwamba kuna Nguvu kubwa ambayo imesababisha vyote kuwepo. Nguvu hii ya juu lazima iwe kubwa kuliko ulimwengu na isitegemee chochote ili kujiendeleza. Muumba huyu kwa ufafanuzi hajaumbwa na hivyo kuuliza ni nani aliyemuumba Muumba ni upotofu wa kimantiki.

Ni makosa, ni sawa na mtu akiuliza: Je! rangi ya Buluu au Samawati ina ladha gani?

Sifa hizi haziingiliani kwa jinsi swali linavyo wasilishwa. Wasioamini Mungu wanapenda kuuliza maswali yenye kasoro za kimantiki kwa sababu hawaelewi au kukubali mantiki thabiti ya hoja kuwa ulimwengu na vilivyomo vimeumbwa na Muumba ambaye hajaumbwa.


Kila mwanadamu anajua kwamba kila kitu kilichopo kina sababu na maelezo ya kuwepo kwake. Kuna  sababu ya kutosha ya kueleza tukio lolote katika ulimwengu; haiwezekani kwamba ulimwengu ulikuja kuwapo kwa nasibu bila sababu yoyote.


Je, MwenyeziMungu Anawezaje Kuumbwa Ikiwa Yeye Mwenyewe Anadai Hana Asili ya Kuumbwa?

Swali linachukulia kuwepo kwa huluki ambayo imeundwa/kuumbwa mara moja na haijaumbwa. Kwa ufafanuzi, MwenyeziMungu hajaumbwa. Ikiwa MwenyeziMungu aliumbwa, basi hawezi kuwa MwenyeziMungu kwa sababu atakuwa na muumba mwingine au MwenyeziMungu alie juu yake. Swali linapelekea kudhani kuwa MwenyeziMungu ana mipaka. Wazo la 'MwenyeziMungu kuumbwa' huzalishwa kwenye akili yenye asili ya dhana potofu wa mawazo fifi (a circular fallacy).


MwenyeziMungu hana mwanzo wala mwisho. MwenyeziMungu Hafungiwi na wakati na nafasi (time and space), kama tulivyo sisi viumbe vyake. Yeye ndiye aliyeumba wakati na nafasi, kama vile alivyoumba kila kitu kingine. Inaposemwa kwamba kila kitu kina Muumba, kauli hiyo inarejelea kila kitu kilichoumbwa. 


Ni ulemavu wa kauli kuwa kisayansi, MwenyeziMungu hayupo, kwasababu haijamthibitisha kama wanavyosema wanasayansi. na kwamba maada ndiyo chanzo cha kuwepo kwa uhai, na kubadilika kwa maumbile.


MwenyeziMungu, hata hivyo, hajaumbwa. MwenyeziMungu wetu, Bwana wetu, Muumba Wetu kwa Ufafanuzi Hawezi Kuumbwa.


Yeye ndiye anayefanya Uumbaji, Yeye ndiye Mwenye nguvu. MwenyeziMungu yupo katika umbo lisiloumbwa. Hana mwanzo wala mwisho. Yeye ndiye wa Awali yupo na alikuwepo kabla ya kuwepo mwanzo, na anaendelea kuwepo bila Mwisho, yeye ni wa Milele. Anajitosheleza, Anajitosheleza. MwenyeziMungu anajitegemea. Ikiwa anategemea kitu au vitu au mtu fulani, hawezi kuwa MwenyeziMungu.


MwenyeziMungu hafuati sheria za uumbaji wake, sheria ya maisha, bali Yeye ndiye aliyeziumba sheria hizi hapo kwanza, kwa ajili yetu katika wakati wetu na mahali tunapoishi. Yuko huru kutokana na maada. MwenyeziMungu yuko juu ya wakati na nafasi na anaishi bila kutegemea kitu chochote kile.


MwenyeziMungu, aliyetuumba viumbe, hana budi kuwepo nje yetu. Ikiwa atawekewa mipaka na wakati au nafasi, hawezi kuwa MwenyeziMungu. Kama vile mtu anayeweza kuunda kifaa cha elektroniki, lazima aishi nje yake. Haiwezekani kwa MwenyeziMungu asiye na wakati na asiyezuiliwa na anga kuwepo wakati yeye mwenyewe aliumba wakati na anga. Sheria za uumbaji na maisha hazitumiki kwa MwenyeziMungu.


UTHIBITISH0 WA UWEPO WAKE.

Uthibitisho wa uwepo wake unatokana na viumbe na vitu alivyo viumba. Hebu na tuangalie mfano wa kwanza mmoja mdogo wa MACHO ya viumbe.

Macho yana tabia ya kupitisha mwanga ndani yake (mpaka kwenye retina), na hiyo ndiyo sehemu pekee yenye tabia hii katika miili yetu. Sehemu ya nje kuna ngozi ngumu inayoruhusu mwanga kupita na ndani yake pana ute unaopitisha mwanga pia, na lensi (ya kukusanya miale ya mwanga) iliyo katikati, na kiini kabla ya lensi.



Macho yameumbwa katika mpangilio unaoliwezesha jicho kuona, ambapo ubora wake hakuna msanii yeyote bingwa anayeweza kulirekebisha au kuliunda. Je, hivi ni kweli kwamba muundo huu wa jicho ni matokeo ya bahati nasibu? Yaani tuseme ilisadifu tu kwa jicho likajiumba vile bila ya awali kujua kuwa kuna mwanga na kujua tabia ya mwanga na hivyo likajinasibisha nao katika hali ya kuweza kuutumia mwangaza huo katika kuona?


Tuangalie mfano wa pili, Nyota iliyo karibu na Dunia yetu, ambayo ni JUA.

Umbali kutoka Dunia yetu mpaka kwenye Nyota ya Jua ni Kilomita 149.8 million.


Jua  ni kitovu cha mfumo wa Jua (Solar system) wenye sayari nane, sayari vibete na magimba mengi madogo madogo. Dunia yetu hii ni sayari ya tatu kutoka kwenye Jua, katika mfumo huu. Jua ni nyota iliyo karibu na Dunia yetu kuliko nyota nyingine zote.


Umbo la Jua linakaribia kuwa tufe kamili. Maada yake ni utegili yaani gesi ya joto sana inayoshikamanishwa na nguvu ya graviti.


Kipenyo cha Jua ni takriban kilomita 1,392,684 ambayo ni mara 109 kipenyo cha Dunia yetu. Masi yake ni mara 330,000 ya masi ya Dunia. Kwa ujazo Jua ni kubwa mara milioni moja kuliko Dunia.


Je hatujiulizi ni jinsi gani Jua likawepo kwa umbali huu ulioko sasa, Je hatujiulizi kama ikitokea Dunia au Jua vikasogeleana, hali itakuwaje au vikakimbiana hali itakuwaje, kwanini Dunia ipo hapa ilipo na hisiwe mahala ambapo sayari zingine zipo!


Kwa akili yenye kutafakali kwa uketo, ni dhahiri kabisa kuwa kuna ambaye ni mwenye nguvu ambaye ndie aliye wezesha yote haya.


Hizo zote ni ishara za uwepo wake Muumba ambaye sisi tunamtambua kuwa ndiye MwenyeziMungu kwa wanaadamu kupitia kwa zama zote zikichang’anywa na wahyi Wake kupitia kwa Manabii Wake, wanaadamu wote wamepatiwa fursa ya kumtambua MwenyeziMungu mmoja tu wa kweli, ambaye hakuumbwa na yeyote.


Mambo kama haya, ambayo ni ya kutafakari sana, siku zote yapo na yataendelea katika fikra za binadamu, na kumuashiria ili aamini kuwa lazima kuna MUUMBA, ambaye amefanya yote haya, na bila shaka kila kitu kimo katika nguvu zake, na ni yeye wa kuogopwa.


Vile vile tunafahamu kuwepo kwa akili kwa mwanadamu! Akili ndiyo inayofanya mwanadamu aliyetengemaa atofautiane na kichaa au na mnyama hayawani. Ni kutokana akili alizonazo mwanadamu ndiyo zinazopekea aweze kushitahika pale inapothibiti kukiuka haki za wengine. Na uzoefu unaonyesha kuwa katika hali ya kawaida, hakuna mtu atakayefurahia kuambiwa hana ‘akili’ ila kwa aliyepunguani.


Lakini akili ikoje? Akili si ubongo, haishikiki na hakuna miongoni mwetu ajuae ladha, harufu, umbile wala rangi yake! Hata hivyo, bado tunakubali kuwepo kwake. Tunakubali kuwepo kwa akili kutokana na ishara zinazodhihirisha kuwepo kwake.


Ishara za kuwepo akili ni nyingi mno! Kwa mfano, tunapoona majumba marefu (maghorofa), meli, madege makubwa, treni, magari, viwanda, au kopyuta na namna zinavyofanya kazi, tunakubali kuwa huo ni usanii wa mwanadamu na si kiumbe mwingine katika mimea au wanyama tunaowafahamu.


Lakini, mwanadamu hakuweza kutengeneza hayo kwa maguvu tu aliyonayo. Ni akili ndiyo iliyotoa matunda yote hayo! Kwa maneno mengine, vitu vyote alivyotengeneza mwanadamu vinathibitisha kuwepo kwa akili. Ni ishara na ushahidi kuwa akili ipo hata kama yenyewe haionekani.


Ikiwa kuwepo kwa maghorofa, meli, madege makubwa, treni, magari, viwanda, au kopyuta na namna zinavyofanya kazi kunathibitisha kuwepo kwa akili isiyoonekana, je, kuwepo kwa mwanadamu mwenyewe na akili yake kunathibitisha kuwepo nani? 

Au je, kuwepo kwa wanyama, mimea, ndege, na wadudu wenye maumbile, rangi na sauti mbalimbali kunathibitisha kuwepo kwa nani?


Hakuna lingine ila kuwepo kwa vitu hivyo kunathibitisha kuwepo MwenyeziMungu aliyetengeneza vyote hivyo pamoja na mwanadamu. Kuwepo kwa Jua, Mwezi na Sayari ikiwemo Dunia pamoja na mabadiliko ya usiku na mchana ni ishara na ushahidi kuwa MwenyeziMungu yupo, na kwa kuwepo kwake ndio sababu ya vitu hivyo kufanya kazi katika nidhamu na utaratibu usiotetereka wa usanii huu wa ajabu tunaoendelea kuyashuhudia.


Mwenyezi Mungu Anasema katika Qur’ani:

“Tutawaonyesha Ishara Zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?” 
Qur'an 41: 53


Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana. Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao. 
Suurat Ar-Rum 30:43-44


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!