MADARAKA YA UCHIFU NA UFALME
NDANI YA KOO ZA KISIASA.
HAPO zamani, nchi zilikuwa zikiongozwa na Wafalme na zile sehemu ambazo hazikuwa na ufalme, zilikuwa na aina zao za ufalme yaani Uchifu. Hao Machifu nao pia walichukuliwa tu kuwa ni aina ya wafalme katika koo zao, kwa sababu Ufalme na Uchifu hurka zake ni sawa tu.
Binafsi wala sjui ilikuwaje mpaka wakachaguliwa kuongoza. Nahisi tu labda walichaguliwa aidha kwa ushujaa au uchawi wao au walionekana tu wanafaa basi.
Ninacho kijuwa ni kwamba ilifikia mahala wakajiwekea kuwa ni haki yao peke yao kutawala wao na familia zao au ukoo wao tu basi.
Ikitokea baadhi ya familia au ukoo fulani kunung'ung'unika au kuhoji kwanini ni wao tu, hii ilichukuliwa kuwa ni uhasi mkubwa sana na adhabu yake ilikuwa ni kifo.
Wananchi waliendelea kuishi kwa uvumilivu japo waliona kabisa kuwa Mfalme au Chifu wao, zile busara zake na uwezo wake wa kutoa maamuzi umegota na maamuzi mengi ufanywa na wale wanao mzunguka mfalme au chifu huyo.
Lakini hakuna hata raiya mmoja aliyethubutu kusema neno hata wale wapambe wanao ambatana na Mfalme au chifu hawakuthubutu.
Maana hata ikitokea Mfalme au Chifu huyo kufariki, wananchi walijuwa wazi kabisa atakae ingia madarakani atakuwa ni mtoto wa Mfalme au mtoto wa Chifu na si nje ya hapo, na hakuna aliyethubutu kusema kuwa na yeye anautaka Uchifu au Ufalme.
Hali hii iliendelea hata pale yalipokuja mageuzi ya kimfumo, tukaambiwa kuwa sasa hakuna tena Ufalme, wala Uchifu au Usultani wa maisha. Ufalme na Uchifu utakuwa ni kwa kila mtu ambae ataweza kuchaguliwa na wananchi. Vilevile tukaambiwa kuwa kila mtu anao uhuru wa kuingia au kujiunga kwenye ukoo wowote anao uona kuwa unamfaa au kumvutia!
Tukashangilia kweli kweli, tena kwa kucheza ngoma na kuimba, maana tulijuwa kuwa hata kina Kabwela (Walala hoi) nao watakuwa na uwezo wa kuwa Wafalme au Machifu katika koo mbalimbali zilizokubalika.
Harakati zikaanza, watu wakajiunga na koo tofauti na za awali, hata wale waliokuwa hawana koo wakatafuta koo za kujiunga nazo.
Wakajitokeza watu na koo zao walizoziunda upya wakaja wakatuomba tuwaamini, tukawapa amana zetu ili watuwakilishe, wawe ndio Machifu wa koo zetu.
Walipofika uko kwenye baraza la Machifu, wakishirikiana na wafalme wao wakajipandishia malipo, wakaanza kula kwa pupa kiasi cha kuvimbiwa na kufikia wengine kusinzia kwenye vikao Uchifu.
Kila likija swala la Makabwela na shida zao, mjadala uliwekwa pembeni na kuhamishia marupurupu makubwa makubwa kwenye matumbo yao.
Muda ukafika wa kuchagua Wafalme na Machifu wapya... Looh! Wakang'ang'ania waendelee kuwepo hapo hapo walipo, kila wakijitokeza wengine wa kutuwakilisha hawataki na wanakuwa wakali sana eti hao wenye kutaka kuwakilisha watakuwa wametumwa tu si bure.
Makabwela tukajiuliza, iweje tena kazi za Uchifu na Ufalme, zimekuwa si kazi za wito!? Si awa awa walikuja kutuomba, sasa mbona wengine wakitaka kuomba huo Uchifu na Ufalme waonekane kuwa ni waasi!? Au kwa sababu uchifu na ufalme malipo yao ni makubwa?
Wengi wao awa atukuwatuma wala kuwapendekeza watuwakilishe, bali walikuja wenyewe kututaka tuwachaguwe waende kutuwakilisha kwenye huo mkusanyiko wa Machifu, sasa hiweje leo wanapojitokeza wengine waonekane kuwa ni waasi?
Na uku kwenye Koo zetu kuna makabwela wengi wenye uwezo wa kutuwakilisha, mbona miaka nenda rudi ni Wafalme wamekuwa ni wale wale tu, ukigusia tu au wakiona dalili kuwa unautaka Ufalme, basi ujuwe hatima yako kwenye huo Ukoo ipo hatarini!
Najuwa kuwa kila ukoo una mila na desturi zake, lakini tulisha ambiwa tangia mwanzo kuwa, kila mtu kwenye ukoo alio uchagua ana uwezo wa kuwa Mfalme wa ukoo huo kwa muda maalum na kila muda ukifika basi wana ukoo husika watachagua mfalme mpya.
Lakini mpaka leo hakuna tofauti kati ya Ufalme ule kabla ya mkoloni na huu unaoitwa demokrasia, maana koo nyingi wafalme ni wale wale tu.
Je Kwa Mustakabari Huu, Tutafika Kweli, Maana Safari Ni Ndefu Kweli Kweli.
0 comments:
Post a Comment
Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?