Sunday 10 December 2017

WAISLAM UISLAM UMETUSHINDA!?

Hatutaki Qur'an Wala Hadith.

Linapokuja swala la kujadiliana mambo mbalimbali katika Uislamu aidha mambo ya Kisharia au mambo ya Akida na mambo mengine kadhaa wa kadhaa, baina ya Waislamu, mara nyingi kumekuwa na kutawaliwa na Kashfa, Kejeli na matusi baina yetu.

Inafikia mpaka kuitana majina kama vile Makafiri, watoto wa Ibilisi na maneno kadhaa yasiopendeza...!

Je Waislam sisi wa zama hizii, tunajuwa zaidi ya wale waliotutangulia mbele ya haki? Kiasi leo hii yoyote yule ambaye hakubaliani na madhehebu au itikadi tunazo zikubali sisi basi huyo ni wa kutiwa motoni na peponi tunawapeleka wale tuwapendao na kuwatupa motoni tunaotofautiana nao kifikra!?

Hii yote inasababishwa na nini kama si kudumaa au kuto baleghe Kiakili na Kiroho, na ilo ndilo linako pelekea wengi wetu kukosa kuhishimiana katika majadiliano yetu na haswa tunapotumia mitandao ya kijamii.

Kwa kweli Waislamu sisi wa sasa tuna tabia ambayo ni mbaya kabisa, tabia iliyo ondoa mafungamano ya Kindugu na kirafiki na umoja katika jamii kiasi tumekuwa hatusikilizani tena, tumekalia kubezana, kutukanana kukebeihana, ugomvi ndio umekuwa dini yetu na kuacha dini tuliopewa na MwenyeziMungu na kukumbatia tulioibuni wenyewe.

Mtume (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) anasema hivi:
"Uislamu ulianza katika hali ya ugeni, na utarudi katika hali ya ugeni kama ulivyoanza."

MwenyeziMungu anatuambia kupitia Qur'an tukufu kuwa:
Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa MwenyeziMungu na Mtume, ikiwa mnamuamini MwenyeziMungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
Qur'an An-Nisaa 4: 59

Lakini Waislamu sisi, hatuyataki hayo, hatufati Qur'an wala Hadith, tunachokitaka wala hakijulikani zaidi ya kutukanana mitandaoni.
Huo ndio Uislamu wetu mpya wa zama hizi za Sheikh Gugo Ibn Intanetii Bin Midia Bin Wasab ibn Fasibuk!

Afadhali basi ushabiki wa Kimadhehebu tungelikuwa tunashabikia maendeleo ya Uislam na Waislam husika ili kukuza elimu zenye kuweza kuwakwamua Waislam Kielimu, kiuchumi na kimawazo na kujitambua, lah hasha, ushabiki umejikita kwenye Maswala ya hitima, maulidi kujuwa kama Qur'an ni kiumbe au si kiumbe, Qunuti au tusiqunuti, sheikh fulani hivi, sheikh yule vile...!

Tunafumbia macho yale yanayoigusa na kuiharibu jamii yetu... Ndio tunaona kila pembe wacheza kamari ni watoto zetu, walevi watoto zetu, mashoga na liwati na wavuta bangi watoto wetu, mambo ya kikubwa watoto wetu, na kila baya Waislamu sisi tunahusika.

Hatusikii Mijadala ya kuhamasisha Utowaji wa zakah na Sadaka, Hatusikii Mijadala ya Qiyamu Layl, Kusaidia wanafunzi masomo yao wala Hatusikii Mijadala ya kuwasaidia Wajane na  Kulisha Mayatima.

Hatusikii Mijadala ya kuwalingania vijana wetu wanao potea katika umalaya, uvutaji wa bangi, sigara na ubwiaji wa unga na ulevi...!
Lakini aaaah! Wapiii yote hayo hatuyataki, tunacho kitaka ni kile tu tukitakacho sisi wenyewe ambacho si kingine zaidi ya kutukanana, kukashifiana na kuvunjiana adabu.

Na Mtume Muhammad (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) anatuambia kuwa...
"Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuoneana kwao huruma na kusaidiana kwao ni mfano wa kiwiliwili. Kinapopatwa na maradhi sehemu moja basi mwili wote hukesha kwa maumivu na machovu".
(Bukhari na Muslim)

Uislamu ni dini iliyojengea katika misingi ya umoja. Ndiyo maana tukaona hata ibada zake zimelenga zaidi katika kuleta umoja baina ya Waislamu. Kwa mfano, mtu anaweza kusali sala ya faradhi peke yake; lakini sala ya jamaa Msikitini ina daraja 27 juu ya sala ya mtu peke yake. Kuna saumu nyingi za sunna, lakini saumu yenye fadhila kubwa ni ile ya faradhi ya funga ya Ramadhani, ambayo Waislamu wote duniani huifanya pamoja.

Tukija katika ibada ya Hijja tutaona kuwa kuna Umra, ambayo ni Hijja ndogo mtu anaweza kuitekeleza peke yake, wakati wo wote; lakini Hijja yenyewe ambayo ndiyo yenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.) lazima itekelezwe na watu wote, kwa pamoja na kwamuda maalum. Tutaona lengo kubwa la ibada kufanywa hivyo ni kwa ajili ya kuwafanya Waislamu wawe na umoja.

Qur’an na Sunna zimesisitiza sana juu ya umoja na kutahadharisha juu ya utengano.

Wahenga walisema: "Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu".

Lakini inaonekana sisi Waislamu hatuna habari na hayo kabisa. Tuko tayari tutengane na tuwe dhaifu kwa ajili tu ya kuendekeza ikhtilafu zetu.

MwenyeziMungu anatufahamisha kupitia kwenye Qur'an kuwa...

Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu.
Qur'an Surat Al I'Mran [3]110

Ufundi umekuwa mwingi mpaka kufikia kukufurishana, ufundi huu ndio umetufikisha hapa tulipo, mpaka tumekuwa hatujielewi tena, wala hatuelewani, kiasi cha kujilimikisha na kugawa Pepo na Jahanam kwa tunao wataka au kuwachukia!

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!