Monday, 1 February 2021

SI KATIKA UISLAMU 

KUANIKA AIBU ZA WATU MITANDAONI.

Na Si Maadili Mazuri Katika Jamii

Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.
Surat An Nah'l 16:90

Assalamu'alaikum warahmatullahi wabarakatuh.

Miaka hivi karibuni kumezuka Masheikh wengi wa kwenye mitandao ya kijamii na haswa vijana, ambao licha ya changamoto za kimaisha lakini kwa namna moja au nyingine wameweza kujifunza Uislamu wao, na kuelewa mawili matatu. Kwa kweli ni jambo la kuwapongeza sana vijana wenzetu.

Nawapongeza kwa sababu wameweza kushinda vishawishi kadhaa na kuamua kujitolea kutafuta elimu ili iwafae wao na jamaa zao hapa duniani na kesho akhera, Alhamdulillah.

Pamoja na kuwapongeza uko, pia nieleze masikitiko yangu makubwa kwa vijana wenzangu, ambao wamejawa na hamasa na msisimko mkubwa sana kwenye mambo kadhaa yahusuyo dini ya Kiislamu, na haswa kwenye kufutu na hata kwenye kutafuta suluhu za masuhala kadhaa kwa Waislamu na jamii kwa ujumla.

Hivi karibuni kumeonekana video ya Sheikh, akisuluhisha kashfa ya ugomvi wa Mama na mtoto wake, Kashfa ya aibu kubwa katika familia ile.

Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na kupelekea kuadhirika na kuvunjiwa heshima ya hao walio peleka kesi ile, mama na mtoto wake, pamoja na sheikh aliyekuwa ndio msuluhishaji wa kadhia ile, sidhani kama ingemtokea yeye au mke wake au hata mtoto wake angefurahia kwa kurekodiwa na kisha kuadhiriwa adharani, kwenye mitandao ya kijamii.

Bila kumung'unya maneno, nadiriki kusema kuwa; kutumwa kwa video ile Sheikh, umefanya makosa makubwa sana, umeeneza fitna kwenye mitandao ya kijamii.

Ni jambo zuri sana kusuluhisha ugomvi na kutoelewana kwa Waislamu na familia zao, tatizo lililo jitokeza ni uvunjifu wa maadili ya usikilizaji wa kesi kama zile umevunjwa, haikupaswa aidha wewe au yeyote yule kurekodi kwa video na kuisambaza video ile ya aibu, aibu ambayo wewe ulipaswa ubaki nayo mwenyewe moyoni na si kuisambaza kwenye mitandao ya Kijamii.

Ofisi za Kadhi na Masheikh wengine, wanapokea kesi za kila aina na zipo zinazofanana na hiyo na kubwa zaidi ya hiyo, lakini hatujawahi kuziona mitandaoni, zinabakia siri kwa wale walio husika tu.

Hizi tabia za kutumia mitandao ya kijamii kuwaonyesha watu wenye kuhitaji misaada au wenye kesi kama hizi, zimeenea kwa wengi.

Utakuta mtu yupo radhi kuanika aibu zake au za mwenzake kwenye group za mitandaoni na kila mmoja akaona au akasoma aibu zile kisa eti atafuta majibu aweze kurekebisha aidha ndoa yake au mahusiano yake na wazazi wake au na mwenza wake au hata ndugu yake.

Ndio utaona mtu anakwenda kwenye familia ya watu wahitaji kama vile; Wagonjwa Wajane, Mayatima, walemavu na wahitaji wengine, kisha baada ya kuwapa alichokusudia au wakati anawasaidia na hapo hapo anawarekodi kwa video na mapicha kisha, shwaa sekunde tu, habari zishasambazwa mitandaoni.

Hizi ni fitnah za shubuha ambazo zinamuingiza mtu katika madhambi na kuharibu yale yote mtu aliyo yafanya na haya mambo ni mapya na ni ukhuraafi ambayo yanaharibu amali za mtu.

Hakika tumeshafanya makosa na tunaendelea kufanya makosa, tunajitenga na tabia za Kiislam na tunarithisha mambo mabaya kwa kizazi chetu kwa maana ya watoto zetu. Hakika tunakitenga kizazi na Uislam.

Tuweni hadhari kwa hili enyi watu, na tusubiri katika Dini ya Allah na tushikamane nayo bila kujali mitihani itakayotufika ya watu. MwenyeziMungu anatufahamisha kupitia kwenye Qur'an kuwa;

Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu...
Qur'an Surat Al I'Mran 3110

Na Mtume Muhammad (salla Allahu 'alayhi wa-sallam) anatuambia kuwa:

"Yeyote atakayeishi baada yangu ataona tofauti nyingi; hivyo shikameni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifah wangu waongofu baada yangu; shikamaneni nazo, na ziumeni kwa magego yenu. Na jihadharini na mambo ya kuzua, kwani kila uzushi ni upotevu".

"Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuoneana kwao huruma na kusaidiana kwao ni mfano wa kiwiliwili. Kinapopatwa na maradhi sehemu moja basi mwili wote hukesha kwa maumivu na machovu". Bukhari na Muslim

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!