Wednesday 6 July 2022

UTAMADUNI WA KUSHANGAZA 
(CULTURE SHOCK)

NA KUWASHANGAZA WAGENI WENGI HUKU UGHAIBUNI

Kwa wale waliobahatika kusafiri haswa nje ya nchi, ikiwa ndani ya bara la Afrika au nje ya bara la Afrika watakubaliana nami kuwa, kuna mengi ya kushangaza katika Maisha ya kila siku ya jamii ile ngeni.

Kuna hili neno la Kiingereza, Culture Shock, utumika mara nyingi kuelezea mshtuko wa mshangao wa mambo mapya ambayo mtu huyaona haswa anapokuwa kwenye nchi ngeni au ukutokea ilihali huna uzoefu nalo.

Mshangao wa mambo mpya, ni uzoefu ambao mtu anaweza kuwa nao wakati mtu anahamia kwenye mazingira mapya ambayo Mila na Utamaduni ni tofauti na mazingira aliyo yazoea.

Utamaduni huo mpya wakati mwingine unaweza kumpelekea mtu kuchanganyikiwa au kuto elewa au kuona kuwa jambo ilo halina maana kwa sababu tu uko alipotoka aidha awalifanyi au linafanyika tofauti na hapo alipo hivi sasa.

Kwenye nchi ngeni, kuna mengi ya kushangaza, makubwa kwa madogo, kuanzia Mazingira, Hali ya Hewa, Lugha, Majukumu ya Kijamii, Tabia za Watu na Maadili, Mahusiano na Watu na kimapenzi au Kirafiki na hata Sheria na Kanuni za Kimaisha ya kila siku. Yote haya uchangia kukupa mshangao wa kiutamaduni.

Kwa ufupi naweza kusema kwamba kuna tofauti kubwa ya Mila na Utamaduni kati ya Waafrika na wasio Waafrika, hapa naamanisha weyeweji kutoka bara la Yuropa yaani Wazungu, watu kutoka Bara Hindi (Asia), Marekani na kadhalika.

UZOEFU WANGU NDANI YA NCHI NGENI.


Licha ya uzoefu wangu wa kusoma sana vitabu vya hadithi/Riwaya (Novels) za Kingereza,  bado nilijikuta napatwa na mishangao ya hapa na pale, haswa nikianzia na mazingira ya hizi nchi za ulaya.

Nakumbuka mwaka 1996, nilipata nafasi ya kutembelea nchi mbili za bara la ulaya, Switzerland na Poland, na baadae nchi ya Uingereza na Ireland.

Nilipokuwa huko Ughaibuni kwa mara ya kwanza, kitu cha kwanza kabisa ukiondoa baridi na theruji, ambayo ilimshangaza sana mmoja wa rafiki zangu, kuanguka kule kwa theruji, yeye alidhani ni mawingi yanadondoka, kiasi ikamtia sana hofu akijuwa ndio mwisho wa dunia.

Binafsi kilicho nishangaza yalikuwa ni mazingira ya nchi. Nchi ni safi, hakuna takataka barabarani, wala kuona mtu akitupa hata karatasi ndogo tu, au kichungi cha sigara. Kila umbali wa mita kadhaa kuna pipa maalum la kutupia taka ndogondogo, kama vile chupa za vinywaji haswa vile ambavyo umenunua ukiwa njiani kisha ukanywa na kumaliza, basi utaitupa humo, karatasi za tiketi za bus au treni, na kadharika.

Hapa unapaswa ufahamu kuwa taka zinazotupwa kwenye hayo mapipa ya mitaani si zile takataka za majumbani, yaani si kutoa taka nyumbani ukazirembea kwenye hayo mapipa, utashtakiwa.

Jambo lingine, haswa nchini Switzerland, lilikuwa machweo ya jua, nilishangaa mpaka kufikia saa nne usiku, jua lilikuwa halijazama bado, yaani kulikuwa kweupe pepepe. Ila sasa nje kulikuwa hakuna watu, wengi wao walisharudi majumbani mwao kujipumzisha. Ila sasa ilipofika saa nane na nusu usiku ndio kama vile alfajiri ya saa kumi na moja, kwa sisi Waislamu ndio ulikuwa muda wa Kusali Sala ya Asubuhi. Kiufupi mchana ulikuwa ni mrefu sana kwa saa karibia ishirini. Nikaja kujuwa kuwa kumbe kipindi cha majira ya joto (summer) jua uchelewa kuzama.

Ilipofika majira ya baridi (winter) napo pia, ulikuwa mshangao mkubwa, maana usiku ulikuwa mrefu sana kuliko mchana, jua likizama mapema tu, saa tisa na nusu jioni ilikuwa machweo, yaani Magharib ishaingia.

Bila kusahau kuwa wafanyakazi na wanafunzi wengi wao ubeba vyakula vyao (haswa sandwich) na kwenda navyo kazini au shuleni/vyuoni. Na ikitokea Rafiki yako kakualika mtoke out au hata kukwambie mwende kwenye Mgahawa au take away, hiyo haina maana kuwa yeye ndio atalipa, hapo juwa kabisa kuwa ukikubali maana yake kila mtu atajilipia.

MAHUSIANO, No Means NO!



Jambo lingine ambalo uwashangaza wengi ni kuhusiana na mahusiano ya kijinsia, ukiondoa haya ya mabaradhuli kuoana yaani ndoa za jinsia moja, ambayo hata Watoto wa chekechea wanafundishwa kuwa si ajabu kuishi na wababa wawili au wamama wawili walio kwenye ndoa ya jinsia moja kama mke na mume.

Kwenye suhala la mapenzi haswa kwenye kutafuta mwenza, usishangae ukajikuta unatongozwa na mtu wa jinsia yako, ila hii inategemea na maisha uliyo yachagua, ukiwa mtu wa mitoko kwenye kunywa pombe kwenye Pub (Bar) basi si ajabu ukatongozwa na mtu wa jinsia yako kwa maana ikiwa wewe ni mwanamme basi ukatongozwa na mwanamme mwenzako na kama wewe ni mwanamke basi ukatongozwa na mwanamke mwenzako na pia si ajabu hata mwanamke akatongoza mwanamme.

Jambo la kuzingatia hapa, kama wewe umetokea kumtongoza mwanamke, kwa bahati akakataa akasema "No" hapo anamaanisha HAPANA, "No Means NO”. 

Kinyume na hapo ukiwa king’ang’anizi itachukuliwa kuwa ni unyanyasaji wa kijinsia (sexual harassment) na wewe mwanaume unaweza ukaingia matatani.

Tofauti na huku kwetu Afrika haswa Bongo, kutongoza na kukataliwa mara ya kwanza haimaanishi kuwa binti hakutaki bali tunachukulia kuwa ni aibu tu ya kike hataki kujirahisisha yaani ni ile sitaki nataka.

Kwa desturi zetu Wabongo kukataliwa mara ya kwanza kuna mfanya mwanaume ahamasike zaidi kuendelea kuwa king’ang’anizi. Sisi tunachukulia kwamba mwanamke kukubali anapotongozwa mara ya kwanza inaweza kuwa ishara mbaya kwake na kuchukuliwa kuwa amejirahisisha au ni malaya. Hivyo, mwanaume ataendelea kumfatilia hata mara mia kidogo mpaka atakapo kubaliwa au kukataliwa kwa mara zote hizo, ndio hapo sasa upepo unaweza kubadili mwelekeo.

Jambo lingine la kuzingatia huko makazini, kama unafanyakazi na mashoga, basi hupaswi kuwanyanyapaa au kuonyesha kuwa uwaungi mkono (japo ni haki yako kutowaunga mkono). Viongozi wako wakijuwa kuwa wewe ni mmoja wao mwenye kupinga ushoga na ikaonekana wazi kabisa bila chenga, kuna hatari ya kusimamishwa au hata kufukuzwa kazi.

UDUMA ZA KIJAMII, UJIRANI NA MAISHA MITAANI.

Uduma nyingi za kijamii zinafata sheria, hakuna tabia za kutoa au kuombwa rushwa, ukiambiwa lete karatasi hii na ile basi kama unazo hizo karatasi, bora uziwasilishe, lahasha hakuna kuzunguka mbuyu.

Watu wanawajibika sana na kufata sheria kikwelikweli, kama umeajiriwa basi wanataka kukuona unafanyakazi kwa saa zote ulizotakiwa kufanyakazi, mapumziko yako ni muda ule tu wa mapumziko.

Kwenye uduma za usafiri watu wanapanga mistari aidha kwenye kukata tiketi au kwenye kupanda usafiri, ni mara chache sana watoto wa shule kupisha wazee ili wakalie viti, ila kuna viti maalumu vimetengwa kwa ajili ya wasio jiweza, walemavu, wajawazito na wzee.

Kwenye kununua bidhaa madukani hakuna kudai kupunguziwa bei, kama tufanyavyo huku kwetu Bongo, bei uliyoikuta ndio hiyo hiyo, labda kuwe na pungozo maalumu la bei.

Ni jambo la kawaida sana mtu kuingia supermarket na mifuko yake au mabegi yake bila kusimamishwa au kuchunguzwa na mlinzi, kama ilivyo huku kwetu Bongo. (Nadhani huku Bongo wizi wa madukani ndio sababu).

Kuna ndugu zetu kutoka Afrika Magharibi haswa Naijeria, wao huwa hawaelewi somo au wanafanya makusudi, nishawahi kumuona mmoja wao akijibishana na muuzaji, aking’ang’ania apunguziwe bei.

Tena basi ndugu zetu wale wa kutoka Magharibi mwa Afrika wana tabia ya kuongea kwa sauti kubwa, tofauti na sisi wa kutoka Mashariki mwa Afrika hatuna hizo tabia. Hata mimi ilinipa tabu kidogo kuwaelewa kwanini hata wakiongea na simu wanapaza sauti, unaweza kumsikia Mnaijeria akiongea akiwa mita mia moja, kwa jinsi anavyopaza sauti yake…

Jambo lingine, sisi Waafrika tushazoea sherehe zetu kufanyika mpaka usiku wa manane, huku tukupiga miziki kwa sauti kubwa, bila kujali kama tunawabughuzi majirani zetu mpaka mtaa wa tatu kwa kushereheka kwetu. Au hata hizi Bar zilizo mitaani kupiga miziki kwa sauti kubwa, tunaona ni jambo la kawaida sana.

Huku ughaibuni ni tofauti sana, kwenye mikusanyiko, muziki hupigwa kwa sauti ya chini ili kutowabugudhi wasiohusika na sherehe hiyo. Kama kunahitajika sauti kubwa basi shughuli au kama ni mwanamuziki anaburudisha basi shughuli hiyo itafanywa kwenye viwanja cha mpira au kwenye viwanja maalum na viwanja hivyo vipo mbali na makazi ya watu.

Ikitokea ukapiga mziki mtaani kwa sauti kubwa, basi mara moja askari polisi wataitwa na hawachelewi kufika. Uzuri wa polisi wa huku si wakorofi na hawatembei na bunduki, wanakuwa tu na Radio ya Upepo (Walk talk) vichupa vya piripiri (Pepper Spray), kirungu, Pingu na wakati mwingine wanakuwa na Bastola za umeme (Stun guns - Tasers).

Wakifika eneo watawasihi kwa upole na unyenyekevu muache kupiga muziki kwa sauti kubwa na baada ya hapo watasogea mbali kidogo ili kuwatazama mwenendo wenu endapo mtakuwa watiifu au lah. Mkiwa watiifu wanaondoka zao. Lah mkileta kiburi hapo sasa ndio wanarudi, mara hii wakiwa kikazi zaidi nanyi mtaisoma namba.

Jambo lingine ambalo haliruhusiwi kabisa kufanywa mtaani au hata uwani kwako ni kuchinja Wanyama, kama vile Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo, Nguruwe au Farasi.

Kuna Rafiki zetu waliwahi kuingia matatani, walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kuchina Kondoo.

Walishtakia kwa kumsababshia mnyama maumivu, mateso na majeraha yasiyo ya lazima.

Sheria ya Umoja wa Ulaya na ya kitaifa kuhusu uchinjaji inalenga kupunguza maumivu na mateso ya wanyama kupitia matumizi ya njia zilizoidhinishwa kisheria za kutumia kumdunga sindano ya kumpumbaza mnyama kabla ya kumchinja.

Walijitetea kuwa kuwa ni Mila na Utamaduni wao tangia huko Afrika kuchinja haswa kama kuna sherehe za kiutamaduni na wao hawakujuwa kuwa hairuhusiwi mtu akiwa mtaani kuchinja.

Maeneo pekee yanayoruhusiwa kisheria ni machinjioni tu.

Walisamehewa ila walikuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja, walitakiwa wasifanye kosa lolote lile, lah sivyo watafungwa jela kwa kipindi kisichopungua miezi sita.

Bucha nyingi za huku hawauzi vichwa vya wanayama, au ubongo au Maini au Utumbo haswa ule wa bomba, kama Ng'ombe, Mbuzi au Kondoo. vinatupwa eneo maalum la kutupia mabaki ya kutoka machinjioni. Ni Bucha chache mno unaweza kupata baadhi vitu kama hivyo, lakini vinakuwa vimeshafanyiwa utaratibu fulani hivi.


MALEZI YA WATOTO, UMBEA, KUCHUNGUZANA KWA MAJIRANI, WAZEE KUISHI PEKE YAO MAJUMBANI.

Wageni wengi wamejikuta matatani haswa kwenye suhala zima la kulea Watoto. Watoto wa huku hawagombezwi wala kusemwa, uambiwa tu, usishangae kumsikia mzazi akimkataza mwanawe kwa kumwambia Mfano; “Sean stops it, stop it please” hakuna kumchapa mtoto, tena Watoto wanafundishwa na kuhamasishwa mashuleni, kuwa wakichapwa au kukaripiwa karipiwa na wazazi basi wakaseme kwa walimu shuleni. Na ikitokea mtoto amesema kwa mwalimu kuwa mzazi au mlezi wake kamchapa, basi hiyo ni kesi kubwa sana. Tena inaweza kukupelekea mzazi au wazazi/walezi wa huyo mtoto kunyang’anywa haki ya kumlea huyo mtoto.

Na ikitokea umenyang’anywa mtoto kwa makosa ya kuchapa, pia itakuathiri kwenye baadhi ya kazi za kijamii kazi ambazo zinawahusisha Watoto, hutopata hizo kazi.

Watoto wadogo wote ukiwapakia kwenye gari, basi wanapaswa wawekwe kwenye viti maalum Baby/Child car seat au Booster seat

Ukiachana na wavulana na wasichana wa vyuo vikuu, si ajabu kuwaona watoto wa shule za msingi na sekondari kuwa na urafiki wa kingono, aidha wa jinsia tofauti au jinsia moja.

Tena hata walimu wanaweza kujuwa na wala si jambo baya kwao, hata wakikutwa wanatembea huku wameshikana mikono na kupigana mabusu, hakuna watakachofanywa, tena wakiwa ni jinsia moja ndio kabisa watahamasishwa kuwa wanacho kifanya ni jambo zuri la kishujaa, kwa kuwa tu linawapa furaha na wanapaswa kujivunia (Pride).

Wengi wa wakaazi wa huku ambao ni wazawa haswa wenyeji, wanapenda sana kuchunguzana na haswa kuwachunguza wageni wahamihaji.

Wala si kitu cha ajabu ukiwa wewe ni mgeni, habari au taarifa zako zikajulikana mtaa mzima kama si nusu ya watu waishio kitongojini hapo.

Siku za kwanza utasalimiwa na kujuliwa hali na watakuuliza maswali kadhaa wa kadha, jina lako, unatokea wapi, sababu zilizokuleta nchini mwao, jeutarudi nchini kwenu au ndio utaseleleka hapo Maisha yako yote.


Wengi wao udhania kuwa Afrika ni nchi na si bara lenye nchi zadi ya 52, Zaidi wanacho kijuwa kuhusu Afrika ni yale matangazo ya utalii (Safari Tour), kuwa Afrika ni nchi moja ambayo binadamu na wanyama pori wanaishi pamoja, kama vile sinema ya Tarzan.

Kiustarabu sisi Waafrika haswa kutoka Afrika Mashariki (Tanzania), kama mtu kutoka mtaani anakusimamisha na kukuuliza maswali binafsi, tunachukulia kuwa ni dalili za urafiki na uwenda mkawa na uhusiano wa karibu wa kirafiki. Basi kama utafikiria hivyo juwa hilo ni kosa kubwa. Yule aliyekuuliza hayo yote uwenda kesho ukikutana nae hasikusalimie, tena akakupita kama vile hajawahi kukuona.

Unaweza kumsalimia hasihitikie au akakushangaa tu, japo wapo wenye kuendeleza urafiki japo wa kusalimiana tu, ila wengi wao si majirani wa kusalimiana na haswa ukiwa mgeni.

Kuna wakati ilinishangaza sana, baada ya kusikia kuwa kuna wazee wenye umri wa miaka 80 na kitu, wakiwa wamekutwa wamefariki majumbani mwao, bila ya Watoto zao kujuwa au hata ndugu zao wa karibu.

Wazee wengi uishia kwenye majumba ya kulelea wazee, Watoto zao hawana muda nao, wapo kwenye kuangaika na ulimwengu. Hali hii ni tofauti na Afrika haswa Tanzania, wazee wengi wanaishi na Watoto zao au ndugu zao wa karibu.

Unaweza kumkaribisha mtu nyumbani kwako, akaona kabisa watu wanavua viatu, na hasivue viatu vyake, mpaka umwambie kuwa vua viatu vyako.

Ukichelea anaweza kuingia navyo mpaka ndani na wala si ajabu akapandisha miguu kwenye makochi yako na isimpitie akilini kuwa anacho kifanya ni makosa.

Ikitokea umekaribishwa nyumbani kwa mtu (Kama ni Mzungu), si ajabu akakutembeza na kukuonyesha nyumba nzima jinsi mikato ya nyumba ilivyo.

Ikitokea kuwa unahitaji kutumia choo (kwenda msalani), basi itakulazimu uombe ridhaa kwa mwenyeji wako (ni ustaarabu wao tu) kwa kusema “May I use the bathroom please?” Au “May I go to the restroom please?” hapo sasa utaonyeshwa choo kilipo...

Huku kwetu Bongo, hali ni tofauti, mgeni atamuuliza mwenyeji “Choo Kipo Wapi au Jamani Msalani ni Wapi”, na sio kuomba ruhusa kama wafanyavyo Warami.

Sasa basi uwende vyoo vya mitaani (Public Toilets) hata kama ni vya kulipia, si ajabu ukaona miguu ya mtumiaji. Maana chini usawa wa magoti kupo wazi na juu hakujafunikwa, utajuwa tu kama kakaa au kasimama. Huku kwetu hali ni tofauti kwani choo kinamficha mtu kabisa, yaani, total privacy.

Huku Ughaibuni maji ya kunawa utayapata kwenye sehemu ya kunawia mikono na si chooni, uko ni wendo wa karatasi tu (Toilet paper).

Kwa raiya na wageni wenye sheria za ukaazi, ambao hawana kazi au vipato vya kuwatosha kulingana na ukubwa wa kaya, wengi wao upata usaidizi wa pesa za kujikimu kutoka serikalini. Utapata matibabu bure na utalipiwa baadhi ya pesa za kodi ya nyumba na hata masomo watakulipia.

Ila ukiwa na kazi, basi vyote hivyo utavilipia kwa pesa yako mwenyewe.

Tatizo moja kubwa ambalo linawasumbua wengi ni kupata nafasi (appointment) ya kuonana na wataalam wa matibabu. Ugonjwa kama si wa dharura, basi unaweza kujikuta unapata mihadi ya kuonana na mtaalamu wa ugonjwa wako hata baada ya miezi tisa au mwaka mmoja.

Ila kama una mudu na uwezo unao wa kulipia mwenyewe, haita kukuchua muda mrefu wa kusubiri kuonana na mtaalamu wa maradhi yanayo kusumbua.

Kina mama wengi wa huku ughaibuni, wanawasuka Watoto zao wenyewe majumbani, na hata kwa baadhi ya wavulana haswa wa Kiafrika wanaopenda kukata nywele, basi wanatafuta utaratibu wa kukatana nywele wenyewe kwa wenyewe, saluni za huku ni ghali haswa saluni za wanawake.

Nakumbuka mara ya mwisho kukata nywele salun, ilinigharimu €15, wastani wa shilingi elfu 35 za Kitanzania.

KAZI ZA NDANI

Mara nyingi nimekuwa nikiulizwa na baadhi ya marafiki wa mtandaoni, haswa kwenye WhatsApp, wakinitaka niwaulizie na hata kuwatafutia kazi za ndani, kama zile zinazopatikana nyumbani au zile
zinazopatikana kwenye nchi za Kiarabu.

Na mie agharabu uwajibu kuwa hakuna hizo kazi, na hata kama zipo basi watakaopewa ni wale raia waliosomea kozi maalum ya mafunzo ya awali ya malezi ya watoto (Child Care) na kwa elimu walioyosomea wanaweza pia kuajiriwa kwenye vituo vya chekechea na tena baada ya kufanyiwa uhakiki kwa maana ya kufanyiwa uchunguzi makini wa kiPolisi, ili kujuwa tabia ya mwenendo wake kama anafaa kuzifanya hizo kazi.

Kuna wengine wamesomea kozi ya Wasaidizi wa Kazi (Support Worker), na wengine kozi ya Usaidizi wa Huduma ya Afya (Healthcare Support Assistant), hizi ni kozi ni za miezi 12 kwa kozi ya cheti cha shahada ya awali na kuendelea mpaka cheti cha Shahada ya uzamili.

Na hao wafanyakazi wanapatikana kupitia wakala wa kazi na wengine wameajiliwa moja kwa moja kwenye vituo vya kulelea watoto au Nyumba za Uuguzi na vituo vya huduma maalum kwa wazee.

Wafanyakazi wote hao wanalipwa vizuri tena kwa viwango vilivyopangwa vema na serikali kwa kila saa watakayokuwa wakifanyakazi.

Huwezi sikia wamenyanyasika kutoka kwa waajiri wao, ikitokea mfanyakazi amenyanyaswa basi huyo mnyanyasaji atashitakiwa na kufukuzwa kazi au kufutiwa leseni yake.

Kuna mambo mengi ya kimaisha ya kushangaza, mambo ambayo wengi wetu hatukuwahi kuyaona au hata kuyasikia.


JE, NDUGU MSOMAJI, NI MAMBO YEPI UMEYAONA NA YAKAKUSHANGAZA JAPO KIDOGO, TUPE UZOEFU WAKO KUHUSIANA NA CULTURE SHOCK!


0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!