Wednesday, 6 July 2022

 

VIJANA NA MATUMIZI YA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU ZA KIUME

Kwanini vijana wengi wa Kitanzania Wanatumia Dawa za Kuongeza Nguvu za Kiume?

Hivi karibuni, nilibahatika kusafari na kutembelea jiji la Dar es salaam Tanzania. Jiji la Dsm ni jiji lililo sheheni kila aina ya biashara. Na moja ya biashara iliyopata umaarufu sana hivi karibuni ni biashara ya kuuza dawa, haswa dawa za kiasili (Kienyeji) na moja ya dawa zenye kuuzika sana ni zile dawa zinazo aminika kuwa zina uwezo wa kuongeza uwezo wa mwanamme kwenye kufanya jimai, yaani Dawa za Kuongeza Nguvu za Kiume.

Kiukweli jiji la Dar, limeshamiri kwa uwepo wa matangazo mbalimbali mengine ni rasmi na mengine sio rasmi kuhusiana na dawa za asili haswa za kuongeza nguvu za kiume.

Utafiti uliofanyika hivi karibuni, umeonyesha kuwa wakazi wengi wa miji mikubwa ya Afrika Mashariki, mf: Arusha, Dar es Salaam, Zanzibar, Kampala, Mbarara, Nairobi na Mombasa, ndio miji yenye kuongoza kwa matumizi ya Dawa za Kuongeza Nguvu za Kiume.

Hizi dawa zipo kwenye mifumo kadhaa tofauti tofauti, kuna vidonge, za unga, zipo za majimaji na hata za kupaka kama mafuta. Kiufupi dawa za kuongeza nguvu za kiume zinaongoza kwa kununuliwa zaidi kwenye maduka makubwa kwa madogo ya dawa kwenye miji hii ya Afrika Mashariki.

Dawa nyingi za kienyeji zimetokana na mchanganyiko aidha wa mizizi au majani ya mimea kama vile; Mzingifuri (Lipstick tree), Mstafeli (Soursop), Mkwamba/Mhina Mwitu (Flueggea virosa), Mpinga/Mkinga waume au Muumbuzi (Cassia petersiana - Senna), Mchunga (Wild lettuce), Mkundekunde Mjohoro (Cassiansiamea), Mshubiri Mwitu (Tree Marigold), Mpepa/Mkalamu (Flagellaria) na mingine mingi. 

Vilevile kuna wachuuzi wa vinywaji kama vile AlKasusi na Supu ya Pweza. Vinywaji hivi vimejipatia umaarufu si Dar es Salaam na Zanzibar tu, bali karibia mikoa mingi nchini Tanzania na hata baadhi ya miji nchini Kenya, kama vile Nairobi na Mombasa. 

Wanaume wengi wamekuwa ni watumiaji wakubwa wa hivi vinywaji, kwa imani ya uongo kuwa ukinywa AlKasusi au Supu ya Pweza au siki ya Mbirimbi au ukila Mihogo mibichi, ukachanganya na Karanga Mbichi na Nazi Mbata basi uimara wako kwenye tendola ndoa uongezeka mara dufu.

Baadhi ya hizi dawa za kienyeji na vinywaji zilifanyiwa uchunguzi wa kimaabara, na kugundulika kuwa zimechanganywa na dawa za kuongeza nguvu za kiume aina ya Sildenafil maarufu kwa jina la Viagra na nyingine kukutwa na Tadalafil (Cialis).

Licha ya wauzaji wa hizi dawa na vinywaji vya kusisimua mwili kwa ajili ya jimai kuwa wengi kiasi cha kila muuzaji kuwa na wateja wa kutosha, lakini baadhi ya vijana nilio bahatika kuzungumza nao katika mitaa ya Dar es Salaam na vitongoji vyake walikanusha kutumia dawa na vinywaji hivi kwa lengo la kuimarisha nguvu za kiume. 

Wao wanadai kuwa wanatumia hizi dawa na vinywaji kwa ajili ya kuimarisha lishe ya mwili na si kujisisimua kwa ajili ya kuongeza uwezo wao kingono ulioshuka.

Kwa utafiti wangu usio rasmi, jiji la Dar es salaam linaongoza kwa matumizi ya hizi dawa, likifuatiwa na Arusha Pamoja na Zanzibar.

Utafiti uliofanywa mwaka 2016 na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, utafiti umeonesha kuwa, takriban takribani katika kila mwanaume mmoja kati ya wanne ana tatizo la nguvu za kiume. 

Utafiti huo ulifanyika kwa wanaume elfu kumi na nane mia nne arobaini na mmoja (18,441) huku umri wa waliochunguzwa ni wastani wa miaka 40.

Sensa ya 2012 ilionyesha kwamba wakazi wa kiume wilayani Kinondoni walikuwa jumla ya wastani wanaume 860,802. 

Sasa ukifanya mahesabu ya kila wanaume wanne mmoja ana tatizo kutakuwa na idadi ya wanaume wapatao 215,200 wana matatizo.

Nakumbuka miaka ile ya 1970 – 80 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, matumizi ya dawa za kienyeji za kuongeza nguvu za kiume yalikuwa zaidi wakitumika na wazee wa makamo, kuanzia miaka 65 kwendaa juu na wale wenye maradhi ya sukari.

Tofauti na sasa, matumizi ya hizi dawa na vinywaji yamekuwa maarufu sana kwa vijana, wengi wao wakiwa kati ya umri wa miaka 17 - 40 na wachache kati ya miaka 40 na 60 na kuendelea.


CHANZO CHA TATIZO NI NINI?

Tatizo hili lina athari nyingi sana zikiwemo za kisaikolojia na kifamilia pia, ikiwemo kupelekea mahusiano kutokuwa imara na mara nyengine kuvunjika kabisa.

Kuna sababu nyingi za kibaiolojia na kisaikolojia kwa watu (haswa vijana) kupelekea kupungukiwa nguvu za kiume, ikiwemo ugonjwa wa kisukari na msongo wa mawazo na mtindo wa maisha ya mtu binafsi. Kama vile kuwa na imani potofu na matarajio yaliyokithiri yanayotokana na kuangalia picha za ngono (ponografia) ambayo hubadilisha mawazo ya vijana wengi kuhusu kile kinachojumuisha 'kawaida' inapokuja suala la “uanaume”. 

Nakumbuka uangaliaji wa picha video za ngono, zilishika kani sana kuanzia miaka 90 haswa kwa vijana wadogo waliochini ya umri wa miaka 20.

Ukiondoa matatizo mengine ya kiasili, athari ya kuangalia sana video za ngono, vimepelekea vijana wengi kujichua kwa ajili ya kujirizisha kingono.

Wapo baadhi ya vijana wa makamo waliosema kuwa, sababu kubwa inayopelekea kwa wao kutumia hizi dawa ni kwa sababu wapenzi wao wa kike kutoridhika pale wanapo jamiiana na waume zao. Ndio inapelekea kwa vijana wengi wa kiume kuanza kutafuta njia mbadala ya kutumia dawa za kuongeza nguvu hili wawaridhishe wapenzi wao. 

Baadhi walijitetea kwa kusema kuwa, wanawake wengi hivi sasa wamekuwa wakitumia sana viungo bandia vya kiume hili kujiridhisha kingono, na hii imepelekea kwa wao kuto tosheka na hali halisi ya mambo.

Wataalamu wa afya wanatuambia kuwa; Chanzo au Vyanzo vya tatizo hili la upungufu wa nguvu za kiume ni vingi ambavyo mara nyingi wengi huvipuuza, hivyo huathiri mfumo wako taratibu sana, uchukua muda mrefu kujitokeza na vyanzo vingine huathiri mwili kwa haraka.

Kuna aina ya Maisha au Mitindo ya Maisha (Lifestyle) inayoweza kukuweka hatarini kupata tatizo la nguvu za kiume hapa nitaorodhesha kwa uchache tu, ila kwa wenye haya matatizo wanapaswa kuonana na daktari husika:

Ulaji wa Majani ya Miraa inayofahamika pia kama 'Mirungi' (Ghat) unazuia ukuaji wa manii. Na hii kumfanya mwanaume hasiwe na hamu ya kufanya jimai.

Aidha ulaji wa kipindi kirefu wa miraa unafanya mbegu za kiume za wanaume kufa haraka pindi zinapowekwa kwenye uke.

Utafiti huu unafatia ule uliofanywa mwaka 2014, na wataalamu kutoka chuo kikuu cha Nairobi kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Konstanz cha Germany na kile cha Minnesota, Marekani uliobaini kuwa ulaji wa miraa licha ya kusababisha uhanithi pia unaathiri ubongo wa walaji wake na kusababisha msongo wa mawazo, mfadhaiko na mahangaiko ya kiakili mbali na matatizo mengine chungu nzima ya Kisaikolojia.

Tabia za kujichua kwa mda mrefu, Ulaji holela wa vyakula vyenye Mafuta mengi na Sukari nyingi, Ulaji mwingi wa Mihogo Mibichi, Ugonjwa wa Kisukari, Kuwa na Lehemu nyingi (Cholesterol) itakayo pelekea kupata Shinikizo la Damu (B.P) au Ugonjwa wa Moyo, Uzito Kupita Kiasi na Unene Uliozidi, Kuvuta Sigala na Unywaji wa Pombe, Matumizi ya Madawa ya Kulevya, Utumiaji wa vinywaji vinavyobadili hali ya mwili, Kuwa na Mawazo Mengi na Wasiwasi Mwingi, Kutopata usingizi vizuri. Umri hasa Uzee, Kuwa na Matatizo kwenye Kibofu cha Mkojo na mwisho kabisa ni matumizi makubwa ya dawa zenye kemikali za kutibia magonjwa kama Saratani (Kansa), Vidonda vya Tumbo, Moyo, Kisukari, B.P, na Magonjwa mengine.

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!