Tuesday, 27 September 2022

HAYATI ZA UJANA WETU
SIKU YA IDD

Baada ya Mfungo Na Vile Vigoma vya Kula Daku, Jioni Tulielekea Viwanjani

Nimejikuta tu, Naandika, Kumbukumbu Chache Zilizobakia Miaka ya 70 Mpaka 80.

Nakumbuka Nilipokuwa Bado Kinda, Mwezi Kama Huu Ulioisha, Mwezi wa Ramadhani, Ilikuwa Baada tu ya Kumaliza Kufuturu, Basi Wale Matineja, Walikuwa Wakipitapita Majumbani Usiku Wakiimba na Wengine Hata Kucheza, Wakitumbuiza kwa Kupiga Vigoma vya Kula Daku.

Kwa Sie Tulikulia Dizim, yaani Dar Es Salaam Ilikuwa Jambo la Kawaida sana Kuwaona Vijana Wadogo Mida ya Saa Mbili Mpaka Nne Usiku, Wakipita Majumbani na Vigoma Vyao. Wakiwaimbia Watu Mitaani, "Kula Daku, Kula".

Wakati Mwingine Hata Vijana wa Makamo Pia Walitutumbuiza, Ila Hawa Ilikuwa ni Tofauti Kidogo, Wao Walikuwa Wakipita Kuanzia Mida ya Saa Nne Usiku

Hizo ni enzi ambayo Waislamu walikuwa na Imani, ilikuwa ikifika muda wa kufuturu, basi utaona wakitandika Mikeka na Majamvi, nje ya majumba yao. Kiufupi Wanaume Walikuwa Wakifuturu barazani, na kila mpita njia ukaribishwa, japo anywe nusu kikombe cha uji, uji uliokolezwa pilipili Manga (Pilipili Mtama). Na wanawake waliokuwa wakifuturu uwani. Kama ilikuwa ni nyumba yakupanga, basi wote wakaazi wa hiyo nyumba ujumuika na kupata futari kwa pamoja, kila mmoja akileta futari yake aliyopika siku hiyo.

Nimekumbuka baadhi ya maneno ya nyimbo zilizokuwa zikiimbwa.

Muulizeni mzungu alietoka angani bwana x2.

Babu kaungua ndevu kwa uji wa ramazani bwanaa...

Kula daku maneno yangu, kula eeh daku wee, daku kulaaa...

Huyu na huyu kama mtu na nduguye bwana...

Nasema huyu na huyu kama mtu na nduguye bwanaaa...

Ukiwaangalia sana mapua kama nguruwe bwana...

Kula daku maneno yangu, kula eeh daku eeh, daku kulaaa...

Kwa wale tineja, wakimaliza kuburudisha aidha wapewe pesa kidogo, Kuanzia senti 10, 20 au senti Hamsini, (Sumni), nyumba nyingine wakitoa Makoko na Matandu ya wali na maisha yaliendelea kwa furaha na amani tele.

Utoto ule waliweza kuaminiana, senti kidogo zilizokusanywa, masiku ya Ramadhani, waligawana siku ya sikukuu ya Idd Fitri, hazikuwa pesa nyingi, kiasi cha shilingi 10 au 15 au 20 kama mna bahati.

Ilikuwa ikifika jioni kila mmoja alielekea kwenye viwanja vya sikukuu. Na wachache wetu tulibahatika kununuliwa nguo mpya na viatu kwa ajili ya sikukuu.

Haikuwa ajabu ukanunuliwa shati na suruali, ukakosa viatu, au ukanunuliwa viatu ukakosa aidha suluwali au shati.

Tuliobahatika tulipewa na pesa kidogo, nadra sana ukapewa shilingi tano, ni mwendo wa shilingi kuja chini.

Sie tuliolelewa kwenye vitongoji vya Kariakoo na Gerezani, Kisutu, Upanga, Ilala, Magomeni na Buguruni kiwanja chetu Maarufu cha kushehereka, kilikuwa pale Kidongo Chekundu (sasa ni Jakaya M. Kikwete Youth Park - JMK), kiwanja kilicho kati ya mitaa ya Livingstone, Kiungani, Kisarawe na Lumumba, mbele ya shule ya msingi Gerezani.

Hapo Kidongo Chekundu, kulikuwa na Mabanda kadhaa wa kadha ya muda, yaliozungushiwa magunia, mabanda maarufu yalikuwa yale ya vikaragosi, ngoma ya Nachi, (mfano wa chakacha), mieleka na kadha wa kadha.

Nje kulikuwa na uchezeshaji wa korokoro (Kamari) na michezo mingine ya kubahatisha.

Kulikuwa na wachuuzi wa bidhaa wa kila aina, mihogo ya kukaanga na kuchoma, viazi vitamu na mbatata vilivyopondwa na kuwekwa pilipili ya unga kwa juu, vikiliwa na machicha ya nazi, mbwimbwi, ubuyu, juice za ukwaji, togwa, embe za kuchepa, karanga shikirimu za vijiti na kadharika.

Sherehe zilikuwa za siku tatu mfululizo, mabanda yakifunguliwa saa 10 jioni mpaka usiku wa saa nne.

Sie tulikuwa tukikaa karibu na viwanja, ilikuwa burudani tosha, kuona watu wa rika mbalimbali, wakitoka vitongoji vya mbali wakijumuika pamoja wakubwa kwa wadogo, kusheherekea sikukuu ya iddi.

Wengine wetu tulikwenda kutazama sinema kwenye majumba ya kuonyeshea filamu.

Kwa Dar es Salaam Kulikuwa New Chox, Odeon, Cameo, Avalon, Empress, Empire na Drive-inn Cinema kule Msasani, ambayo unaingia na gari lako.

Enzi hizo tulikuwa tukitumiana salamu kwa njia ya Redio, kulikuwa na watu maarufu wa kutuma salamu, yaani karibia vipindi vyote hawakosi hao watu na mwisho wa salamu unaandika ujumbe maalum, kama vile Salamu ni nusu ya kuonana n.k.

Ukibahatika, basi waweza kukutana na gari la RTD, likipita mitaani, na kuwapa watu nafasi za kutuma salamu zao za sikukuu, hapo utatakiwa utume salamu kwa watu watatu na kisha utatakiwa uchaguwe wimbo wa kusindikiza salamu zako.

Kule maeneo ya Posta ya zamani, pembeni ya jiji la Dizim, mkabala na shule ya Forodhani, kulikuwa na eneo ambalo sasa nahisi kumegeuzwa kituo cha feri, tukipaita Bombei. Hapo paliuzwa vitu vya Ubuge ubuge na ilikuwa kila Jumapili utawakuta watu ufukwemi, wakipunga upepo uku wakiangalia Meli na Majahazi yaliyotia nanga.

Kiza kikiingia, wale vijana wadogo wadogo waliokwenda kwenye viwanja vya michezo, wanajikusanya na kurudi majumbani mwao, kuanzia saa moja jioni.

Wale wa nje ya mji, wanasogelea vituo vya mabasi ya UDA hapo utakutana na foleni ndefu ya wasafi wakiwa kwenye foleni za kupanda mabasi. Hakukuwa na fujo za kugombea mabasi kama hivi sasa, watu wakieshimiana na uku pembeni kuna mgambo akichunga usalama wa abiria.

Ndani ya basi hata kama umewahi kukalia kiti, kama kulikuwa na mzee au mama mjamzito, basi alipishwa ili akalie siti ya basi. Ilikuwa kawaida kusikia mtu au watu wakisema, "...Jama Hakuna Muislamu wa Kumpisha Huyo Mama Mjamzito siti!"

0 comments:

Post a Comment

Je Una Nasaha zozote Kuhusiana na Makala hii?

RAMADHAN KARIM

Read

Subscribe to RSS Feed Follow me on Twitter!